JSON Variables

Thursday, May 15, 2025

NCC YAJA NA MFUMO KUSAIDIA SEKTA YA UJENZI


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akifungua mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi ambayo imefanyika leo jijini Dar es salaam.

Mhandisi Tumaini Lemunge kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) akiwasilisha mada  katika mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi ambao umefanyika leo jijini Dar es salaam

.

Baadhi ya washiriki walioshiriki katika mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi ambao imefanyika leo jijini Dar es salaam.

........................

:: Wakandarasi wazembe nao waonywa

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amewataka wakandarasi nchini kutekeleza miradi kwa weledi na kwa kuzingatia viwango, ili kuleta tija kwa taifa.

Akizungumza leo Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi, Mhe. Ulega amesisitiza umuhimu wa wakandarasi kutekeleza kazi zao kwa kuzingatia masharti ya mikataba, maslahi ya wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wake, wakandarasi wana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi. Amesema wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo hukwamisha utoaji huduma kwa wananchi, hivyo kusababisha hasara kwa Serikali.

"Tutawachukulia hatua za kisheria wakandarasi wazembe wanaokiuka makubaliano ya mikataba. Serikali ipo pamoja nanyi kwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora ya kazi, lakini hatutasita kuwawajibisha ikiwa mtakwenda kinuume na makubaliano," Mh Ulega amesema.

Wakati huo huo, Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limebuni mfumo mpya wa uchakataji viwango vya bei za ujenzi na matengenezo ya barabara, lengo likiwa kuisaidia sekta ya ujenzi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akiwasilisha mfumo wa uchakataji wa viwango vya bei za ujenzi na matengenezo ya barabara katika mkutano huo, Mhandisi Tumaini Lemunge wa NCC, amesema mfumo huo umetengenezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi.

Mhandisi Lemunge amesema mfumo huo utaaidia taasisi, wahandisi washauri, na wakandarasi kufanya makadirio sahihi ya gharama.

“Mfumo huu utawasaidia watumiaji kuandaa makadirio ya gharama kwa miradi mbalimbali ya ujenzi na matengenezo ya barabara, pia utasaidia kulinganisha bei ya mzabuni na bei halisi ya soko, ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi unakuwa na tija,” amesema.

Ameongeza kuwa mfumo huo utapunguza changamoto ya utoaji wa bei zisizoendana na uhalisia wa gharama za miradi, jambo ambalo limekuwa likikwamisha utekelezaji bora wa miradi ya ujenzi.

“Natoa wito kwa wakandarasi wote kuwasiliana na NCC ili waanze kutumia mfumo huu kwa ajili ya kupata bei halisi za zabuni, jambo ambalo litawasaidia kupanga kazi kwa ufanisi,” amesisitiza.

  

DIWANI KHIMJI AGAWA TUZO KWA WANAFUNZI PAMOJA NA WALIMU

Diwani Wa Kata ya Ilala Mhe.Saady khimji amegawa tuzo Kwa wanafunzi waliofanya vizuri Katika masomo Yao Pamoja na Kwa walimu wanaofanya kazi vizuri Katika shule ya Mzizima English Medium School Jijini Dare s salaam.


Hafla hiyo Mgeni Rasmi Alikuwa Mhe.Saady khimji ambaye ndo amegawa tuzo Hizo.


Khimji Katika hafla hiyo amewaomba wanafunzi kusoma Kwa bidii Kwasababu wao ndo Taifa la kesho.

Pia amesema ifikapo uchaguzi mkuu Wana ilala wajitokeze Kwa wingi kwenda kumpigia Kura Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muuungano Wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassani Pamoja na Mussa Hassan Zungu.


Amesema Zungu amekuwa kinara wakutatua Changamoto Mbalimbali Katika jimbo lake analoliongoza Ilala Sasa Maendeleo yamekuwa makubwa Kwasababu ya Zungu.

Amemaliza kwakusema ilala Inamafanikio makubwa kwahiyo Ufikapo uchaguzi mkuu Wana ilala wamchague Mussa Hassan Zungu Kwa moyo mmoja.

 

RC KATAVI ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA UMEME TABORA - KATAVI

Mkurugenzi wa Miradi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Frank Mashalo (Pili kulia) akitoa ufafanuzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, kuhusu maendeleo ya Mradi wa Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Katavi unaotekelezwa na Kampuni ya ETDCO ambao umefikia asilimia 96, hayo yamejiri katika  ziara ya Mkuu wa Mkoa huo ya kukagua miradi ya maendeleo iliyofanyika Mei 15, 2025, Mkoani Katavi.

Picha za miundombinu  ya Mradi wa Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Katavi unaotekelezwa na Kampuni ya ETDCO  Mkoa wa  Tabora  hadi Katavi.

.......

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, unaotekelezwa na Kampuni ya ETDCO, ambao kwa sasa umefikia asilimia 96.

Akizungumza Mei 14, 2025, akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Katavi, Mhe. Mrindoko amewataka wananchi wa Mkoa wa Katavi, hususan wa Wilaya ya Mlele, kujitayarisha kupokea umeme kwa kujiimarisha katika shughuli za uzalishaji ili kujiongezea kipato.

Aidha, Mhe. Mrindoko ametoa rai kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kufikiria kuwekeza katika Mkoa wa Katavi, kwani sasa utakuwa na umeme wa uhakika na wa kutosha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Alhaji Majid Mwanga, amewataka wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu ya umeme inayojengwa na serikali kwa gharama kubwa.

Nao wananchi wa Wilaya ya Mlele wameishukuru serikali kwa kuwaletea umeme wa Gridi ya Taifa, huku wakisema kuwa hatua hiyo itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.

Katika ziara hiyo Mhe. Mrindoko ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Alhaji Mwanga, ambapo amekagua ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Tabora, pamoja na Kituo cha Kupokea, Kupozea na Kusambaza Umeme cha Inyonga, kilichopo Wilaya ya Mlele.

Wednesday, May 14, 2025

‘VIWANGO VYA UJENZI WA SHULE ZA SERIKALI KUREJESHA UBORA’


NCC kuhakikisha vinadhibiti utoro, hasara kwa matengenezo ya kila wakati

SERIKALI kupitia Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), lililo chini ya Wizara ya Ujenzi, imetekeleza ahadi yake kwa kuhakikisha viwango na viwango msawazo vya ujenzi bora wa majengo ya shule zake za awali, amali na sekondari vinaandaliwa, ili sekta husika ya elimu ivizingatie au kuvitumia pindi inapoandaa miongozo ya ujenzi wa shule, pamoja na ununuzi wa samani kwa ajili ya shule hizo.

NCC imefanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wataalamu wa ujenzi, wahusika wa uboreshaji na matengenezo ya mifumo ya umeme, maji na huduma nyingine muhimu kutoka katika wizara na taasisi mbalimbali, kwa kuandaa rasimu, baada ya kupitia miongozo inayotumika sasa, kuichambua na kuangalia changamoto au mapungufu yaliyopo, hususan kwenye eneo la viwango na viwango msawazo vya ujenzi wa shule na aina ya samani zinazotumika.

Kwa mujibu wa Mratibu wa maandalizi ya viwango na viwango msawazo hivyo, Mhandisi Heri Hatibu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa NCC, lengo la kuandaa viwango na viwango msawazo hivyo ni kuweka muongozo wa usanifu, ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya shule za Serikali.

“Tunafanya hivyo ili kuhakikisha kunakuwa na viwango na viwango msawazo vya ujenzi wa majengo ya shule vinavyoendana na wakati uliopo wa sayansi na teknolojia, vyenye kuzingatia mahitaji halisi ya watumiaji wa majengo, wakiwemo wenye mahitaji maalum, na vyenye kuzingatia usalama wa wanafunzi, walimu na mazingira” Mha. Hatibu amesema.

Aidha, ameongeza kuwa, viwango hivyo vinavyotarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2025/2026, vitasaidia kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali za nchi, yatakayowezesha kupangwa bajeti za usimamizi wa miradi ya ujenzi, kwa urahisi.

Wakati akifungua kikao kazi cha kuandaa viwango hivyo mjini Morogoro hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa NCC, Mha. Dkt Matiko Mturi amesema, inapaswa viandaliwe viwango na viwango msawazo vitakavyo rejesha ujenzi wa majengo mbalimbali yakiwemo ya shule, kwenye ubora unaotakiwa, unaozingatia usalama na kuendana na thamani halisi ya gharama zinazotumika, kama ilivyokuwa zamani.

Dkt Matiko anasema, ukiangalia majengo yaliyojengwa miaka mingi iliyopita utagundua kuwa ni bora na hayahitaji matengenezo ya mara kwa mara kama yanayojengwa sasa. Amesema ujenzi wa majengo hayo ulizingatia mambo mengi muhimu ambayo miongozo yetu mingi ya sasa haiyaainishi.

“Ukiangalia maabara za shule zilizojengwa zamani utagundua kuwa za sasa zina walakini. Lakini, si maabara tu, bali hata majengo ya shule za zamani za Serikali ni imara. Kwa sababu hiyo, ninasisitiza muandae viwango na viwango msawazo vitakavyosaidia kuandaliwa kwa miongozo ya ujenzi wa shule hizo, itakayo ondoa mapungufu hayo,” amesema.

Mha. Ronald Mwajeka wa Idara ya Maendeleo ya Miundombinu katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ametaja baadhi ya mapungufu yaliyopo katika viwango na viwango msawazo vilivyopo kwenye miongozo inayotumika katika ujenzi wa shule za serikali, ambayo yamepatiwa ufumbuzi kuwa ni

Maeneo yaliyokuwa na changamoto na kupatiwa suluhisho kwa kuwekewa viwango ni pamoja na uchaguzi wa eneo/maeneo ya ujenzi, vigezo stahiki vya kuzingatia katika kutekeleza ujenzi, vielelezo vya kuzingatia wakati wa usimamizi na ukaguzi wa kazi za ujenzi. Mengine ni eneo la ubora na uimara wa vifaa vinavyotumika katika ujenzi, kuwekwa kwa viwango vya chini vitakavyozingatiwa wakati wa ujenzi, kuhakikisha kuwa jengo linaweza kutumika na watu wa hali zote. Amesema awali viwango havikugusia shule za amali lakini vya sasa vimezizingatia.

Mtaalamu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi. Agricia Mtakyawa amesema viwango na viwango msawazo vinavyo andaliwa vitapunguza matumizi ya fedha za Serikali kwenye huduma za maji, umeme na nyingine, kwa sababu vimeelekeza ujenzi utakaoruhusu uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua, pamoja na matumizi zaidi ya nishati ya umeme wa jua.

“Majengo ya shule yatazingatia ukubwa wa madirisha unaoruhusu hewa na mwanga wa kutosha, taa za umeme zinazotumia ‘sensor’ ambapo panapokuwa na mtu darasani zinawaka zenyewe na kujizima pindi wanafunzi na walimu wote wanapotoka darasani, au bwenini, ofisini kwa wanaohusika na maeneo hayo.   

Tuesday, May 13, 2025

NCAA YASHIRIKI WARSHA YA KUHAMASISHA UANZISHWAJI WA JIOPAKI KATIKA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI.


Na Mwandishi wetu, Addis Ababa, Ethiopia 


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inashiriki warsha ya kimataifa iliyolenga kuhamasisha uanzishwaji wa hifadhi za jiolojia (UNESCO Global Geoparks) katika nchi za Afrika Mashariki iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii ya Ethiopia.


Warsha hiyo inayofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia kuanzia tarehe 12 hadi 15 Mei, 2025 imewakutanisha wataalamu wa Jiolojia, urithi wa asili, malikale na watunga sera kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki ambazo ni Ethiopia, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Djibouti, kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuanzisha na kukuza hifadhi za jiolojia katika ukanda wa nchi za Afrika.


Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo, Waziri wa Utalii wa Ethiopia, Bi. Selamawit Kassa, alieleza dhamira ya serikali yake kuanza hatua za awali za kuanzisha jiopaki nchini humo, kutokana na urithi mkubwa wa jiolojia uliopo nchini Ethiopia na kusisitiza kuwa jiopaki ni njia muhimu ya kuhifadhi urithi wa asili na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia utalii endelevu.


Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni hifadhi pekee katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara yenye hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai (Ngorongoro Lengai UNESCO Geopark) kupitia kwa Afisa Uhifadhi Mkuu Dkt. Agness Gidna imewasilisha uzoefu na mafanikio yake katika kuanzisha, kusimamia na kuendeleza Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai ambayo ni jiopaki pekee iliyopo kusini mwa Jangwa la Sahara na ya pili barani Afrika ikitanguliwa na M’Goun UNESCO Global Geopark ya Morocco. 


Akitoa uzoefu wa usimamizi wa Jiopaki ya Ngorongoro Dkt. Agness Gidna ambae ni mtaalam wa Urithi wa Utamaduni NCAA, alieleza wajumbe wa mkutano huo kuwa hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro Lengai upekee wake unatokana na urithi wa kijiolojia, kiikolojia na kiutamaduni unaojumuisha Mlima Lengai wenye volkano hai ya kipekee duniani na eneo la Ngorongoro lenye historia ya binadamu wa kale pamoja na vivutio vya utalii vilivyopo na jinsi unavyosaidia jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.


Kwa mujibu wa UNESCO, hadi sasa kuna UNESCO Global Geoparks 229 katika nchi 50 duniani, Geopark mbili tu kati ya hizo ndio zilizopo Afrika. 


Hali hii inatoa fursa kubwa kwa bara hili kuwekeza zaidi katika kutambua, kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya urithi wa jiolojia, ambayo mengi bado hayajatambuliwa kikamilifu.


Katika warsha hiyo, washiriki wanatarajiwa kuibua mikakati ya pamoja ya kitaifa na kikanda, pamoja na kuanzisha mitandao ya ushirikiano katika kukuza jiopaki kama njia ya kuhifadhi mazingira, kuendeleza elimu, kuimarisha uchumi wa jamii na kuboresha utalii barani Afrika.


Tanzania kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ilitambuliwa na UNESCO kupata hadhi ya Jiopaaki mwaka 2018 imepata fursa ya kuhamasisha nchi nyingine kufuata nyayo zake katika uanzishaji wa hifadhi za jiolojia, ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa na kinara wa uhifadhi endelevu barani Afrika.

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAIMARISHA USHIRIKIANO NA SEKTA BINAFSI KUINUA UTALII NA UWEKEZAJI


Na. Philipo Hassan - Dodoma.


Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha ushirikiano na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika Sekta ya Utalii ili nchini iweze kuchangia katika uchumi na maendeleo ya Taifa.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alipokuwa akifungua mkutano wa Tatu (3) wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa majadiliano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi katika utalii (Ministerial Public Private Dialogue - MPPD) uliofanyika leo Mei 13, 2025 katika hoteli ya St. Gasper jijini Dodoma.


“Wizara inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza utalii ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma, miundombinu ya utalii na utangazaji wa vivutio vya utalii. Aidha, idadi ya watalii imeongezeka na kufikia 5,360,247 ambapo watalii wa ndani ni 3,218,352 na watalii wa nje 2,141,895 huku mapato yatokanayo na shughuli za utalii yakifikia Dola za Kimarekani Bilioni 3.3” alieleza Mhe. Dkt. Balozi Chana.


Kutokana na taarifa  ya World Tourism Barometer ya Januari 2023 imeitambua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizovunja rekodi ya idadi kubwa ya watalii wa kimataifa (best performing destinations January to December, 2024).


Halikadhalika, Tanzania imeshika nafasi ya 12 duniani kwa ongezeko la watalii, ikitanguliwa na nchi kama Uturuki, Qatar, Saudi Arabia, Albania, El Salvador, Colombia, Andorra, Ethiopia, Curacao, Jamhuri ya Dominican na Visiwa vya US Virgin.


Aidha, Mhe. Chana ameweka bayana kuwa Tanzania imeendelea kutambulika kimataifa na kupata tuzo mbalimbali za utalii kwa mwaka 2024. Baadhi ya tuzo hizo ni pamoja na Eneo linalovutia zaidi kiutalii (Africa’s Leading Destination), Eneo linaloongoza kwa utalii wa safari duniani (World’s Leading Safari Destination), Hifadhi ya Taifa Serengeti kuendelea kuwa hifadhi bora duniani, Mlima Kilimanjaro kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika (Africa’s Leading Tourism Attraction na Bodi ya Utalii Tanzania kutajwa kuwa Bodi Bora Afrika.


Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wadau wa utalii kuendelea kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kusimamia na kuendeleza Sekta ya Utalii kwa maslahi mapana ya Taifa.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, alifafanua kuwa malipo ya fedha za kigeni ni kwa ajili ya miamala ya ndani, hivyo malipo ya kimataifa katika sekta ya utalii yataendelea kufanyika kama kawaida.


Katika hatua nyingine, Dkt. Abbasi amewahakikishia wadau wa utalii kuwa hakutakuwa na tozo za ghafla katika kipindi hiki, na kwamba iwapo zitahitajika baadae, wadau wa sekta ya utalii watahusishwa kikamilifu.


Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo, ameiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu katika maeneo ya hifadhi ili kuvutia wawekezaji, sambamba na kuruhusu matumizi ya fedha za kigeni (USD) kwa wafanyabiashara wa utalii wa kimataifa.


Pia Chambulo, aliiomba Serikali kushughulikia suala la bima kwa waongoza watalii na wapagazi, pamoja na kuhakikisha mikataba ya uwekezaji inakuwa na usawa kwa wawekezaji wote nchini.


Mkutano huo ulijumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali, Wizara, Wakuu wa Taasisi za Serikali wakiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Musa Nassoro Kuji, Wadau wa Utalii pamoja na wageni waalikwa waliojitokeza kushiriki mkutano huo.

TRC YATOA TAARIFA JUU YA AJALI YA TRENI YA ABIRIA KUTOKA PUGU KWENDA KAMATA

 


Jumla ya watu 10 wamejeruhiwa baada ya treni ya abiria maarufu kama treni ya Mwakyembe inayofanya safari zake kati ya Kariakoo na Pugu jijini Dar es Salaam, kupata ajali baada ya mabehewa yake matatu kuacha njia.


Ajali hiyo imetokea leo Mei 13, 2025, majira ya saa 11:00 jioni eneo la Kamata ikielekea Machinga Complex uelekeo wa Pugu.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, amekiri kupokea majeruhi 10 waliotokana na ajali hiyo kati yao nane ni wanawake na wawili ni wanaume.

SERIKALI INAITHAMINI SEKTA BINAFSI - WAZIRI MKUU

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya kazi kwa karibu sana na sekta binafsi ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

 

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Mei 12, 2025) wakati akishiriki mjadala uliojumuisha mawaziri wakuu wanne kutoka Tanzania, Ivory Coast, Guinea na Cameroun katika moja ya vikao vya jukwaa la siku mbili la Maafisa Watendaji Wakuu barani Afrika ambao unaendelea hoteli ya Sofitel jijini Abidjan, Ivory Coast.

 

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jukwaa hilo alitumia fursa hiyo kuelezea namna ambavyo Serikali ya Tanzania imekuwa ikiishirikisha sekta binafsi kwa kufungua milango ya fursa mbalimbali ili iweze kutumika na kuleta manufaa katika nchi.

 

“Serikali ya Tanzania inafanya kazi kwa karibu na Tanzania Private Sector Foundation, vyama vya wafanyakazi, vya waajiri na wenye viwanda na pia inawapa fursa ya kujenga mshikamano kwa kufanya kazi na Serikali. Pia imefungua milango kwa wawekezaji kutoka ndani ya nchi, nje ya bara la Afrika na duniani kwa ujumla ili kukuza uchumi wa ndani.”

 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza faida za African Continental Free Trade Area (AfCFTA) na jinsi ambavyo Tanzania imetumia fursa hiyo kuimarisha miundombinu ya reli na bandari kutokana na nafasi yake kijiografia. “Tumeimarisha bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara na pia tuna mpango wa kuanza ujenzi wa bandari ya Bagamoyo,” alisema.

 

Amesema Tanzania inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ili kuziunganisha nchi za Congo, Rwanda na Burundi, pia kuna reli ya TAZARA inayokwenda Zambia. Tumeimarisha usafiri wa anga na barabara ili kuwawezesha wanaokuja kuwekeza Tanzania wapate urahisi wa huduma muhimu.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Cosato Chumi alisema kwenye jukwaa hilo limetoa fursa ya kuithibitishia dunia azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza diplomasia ya uchumi na kuifungua Tanzania kiuchumi.

 

“Washiriki wengi hapa wanaelezea mafanikio ya mkutano mkubwa uliofanyika Januari, 2025 wa Energy Summit, na mikutano mingine mikubwa ambayo nchi yetu imeiandaa. Pia tumepata taarifa kuwa Burkina Faso wanataka kuja nchini kujifunza kuhusu uendeshaji wa hospitali ya Jakaya Kikwete ili nao waweze kujenga hospitali kama hiyo.”

 

Naye Balozi wa Tanzania nchini Nigeria ambaye ni mwakilishi wa Tanzania nchini Ivory Coast, elestine Kakele amesema ushiriki wa Tanzania kwenye jukwaa hilo unasaidia kutangaza fursa ambazo Tanzania inazo na hasa kwenye zao la mkonge. “Hii ni nafasi muafaka kwa sekta binafsi kuchukua nafasi yake kama injini ya kusukuma maendeleo.”

 

Naye Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu alisema uwepo wa Tanzania kwenye jukwaa hilo umetoa nafasi ya kukutana na wadau mbalimbali wa maendeleo barani Afrika na hivyo kutoa fursa kwa nchi kujitangaza ili kuvutia uwekezaji ambao utawezesha kuiinua nchi kiuchumi.

 

“Tunaamini kwenye vikao hivi wameendelea kuijua Tanzania na fursa zake zilizoko kwenye uwanda wetu wa logistics, katika madini, kilimo na hata katika sekta ya fedha.”