JSON Variables

Showing posts with label Top Stories. Show all posts
Showing posts with label Top Stories. Show all posts

Thursday, May 1, 2025

KATIBU MKUU LUHEMEJA AHIMIZA UMOJA AFRIKA KUKABILI ATHARI ZA MAZINGIRA

Washiriki wakifuatilia Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) tarehe 30 Aprili 2025 katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni, Zanzibar.

Mwenyekiti wa Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) Dkt. Richard Muyungi akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mkutano huo leo tarehe 2 30 Aprili 2025 katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni, Zanzibar.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) tarehe 30 Aprili 2025 katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni, Zanzibar.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Upotevu an Uharibifu Bw. Ibrahima Diong mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) tarehe 30 Aprili 2025 katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni, Zanzibar.

.....

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kuwa na umoja wenye sauti moja yenye nguvu ili kuwa na sauti moja katika mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi. 

Ametoa wito huo wakati akifunga Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) tarehe 30 Aprili 2025 uliofanyika Zanzibar ambapo amesema Afrika iliyounganishwa yenye sauti thabiti itatoa nafasi kubwa ya kuwasilisha vipaumbele vyake kwenye mikutano ya kimataifa.

Mkutano huo uliofanyika kwa siku tatu, umewakutanisha washiriki kutoka nchi 54 barani Afrika ambao pamoja na masuala mbalimbali wamejadili ushirikiano katika uhifadhi wa mazingira.

"Afrika inahitaji kwenda mbali zaidi katika kuzungumzia mabadiliko ya hali ya hewa, na kwa hivyo, tunapaswa kwenda pamoja kukabiliana na changamoto hiyo," amesema.

Mhandisi Luhemeja alisema Afrika si bara masikini, hivyo ipo haja ya kuwa na sera na mikakati inayolinda utajiri wa Afrika kwa maendeleo endelevu ya bara hilo. 

Pia, Katibu Mkuu alisema kwa kuwa Afrika ndiyo iliyoathiriwa zaidi, hivyo kipaumbele cha bara ni kuwa na fedha za uhakika kwa kuzingatia vipaumbele na maslahi mapana ya watu wa barani humo. 

Alisisitiza mfumo wa ruzuku ni muhimu ili kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo Afrika lazima ihamasishe upatikanaji wa Dola za Marekani Trilioni 1.3 kufikia mwaka 2025.

Halikadhalika, Mhandisi Luhemeja alisema mkutano huu umesisitiza haja ya kuwa na ufafanuzi wa kupata fedha kutoka kwa Mfuko wa Hasara na Uharibifu, mchakato unaopaswa kurahisishwa kupata fedha hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN) Dkt. Richard Muyungi alisema miongoni mwa mijadala iliyojadiliwa ni utafutaji wa kiasi cha shilingi bilioni 300 kwa ajili nishati safi barani Afrika ambayo ni utekelezaji wa maelekezo hayo ya mkutano wa viongozi wakuu wa nchi uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Alisema suala la kuhakikisha upatikanaji wa fedha hizo kwa ajili ya watu milioni 300 wa Afrika kupata nishati safi lilikuwa ajenda kuu ya mkutano huo kuelekea Mkutano wa 30 Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabiachi (COP30) unaotarajiwa kufanyika Belém, Brazil.

“Kama unavyofahamu sisi Tanzania ni mwenyekiti wa AGN kwa mwaka mzima ambapo kamati hii ilielekezwa tuwe na Sekretarieti ya kudumu ambayo itakuwa na makao makuu pake Addis Ababa nchini Ethiopia na sisi tumeahidi kabla ya mwezi Juni tutaunda kamati ya kusimamia mchakato huo,” alisema Dkt. Muyungi.

Dkt. Muyungi ambaye pia ni Mshauri wa Rais kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira aliongeza kuwa imeazimiwa kuwa Afrika itaendelea kushirikisha, kufundisha na kujenga uwezo wa vijana kupitia kliniki za mabadiliko ya tabianchi kuhakikisha inarithisha ujuzi kwa vizazi kutetea maslahi ya Afrika katika majadiliano ya kimataifa.

Mkutano huo ulifunguliwa tarehe 28 Aprili 2025 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YANOGESHA MEI MOSI 2025

 

.……....

Na Sixmund Begashe - Singida

Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Leo tarehe 1 Mei 2025, wameungana na wafanyakazi wote Duniani kwenye Maadhimisho Siku ya wafanyakazi Duniani MEI MOSI ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Singida huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Mgeni rasmi.

Maadhimisho hayo yalipambwa na matembezi mbele ya jukwa kuu mapoja na burudani mbalimbali ambapo Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii walinog'esha maadhimisho hayo kwa Mavazi rasmi na mabango yaliyobeba ujumbe wa kutangaza vivutio vya Utanii na kuhamasisha Uhifadhi.

   

Tuesday, April 29, 2025

MALIASILI SC YATIKISA SINGIDA.


Na Sixmund Begashe 

Club ya Michezo ya Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama MNRT SPORTS CLUB imeibua gumzo la shangwe Mkoani Singida kwenye mashindano ya Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani MEI MOSI 2025, Mkoani Singida, kutokana ushujaa wa timu zake hususani timu ya mchezo wa kuvuta kamba wanaume iliyofanya vizuri mpaka mwisho.

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Singida na viunga vyake wamesikika wakiwapongeza wachezaji wa timu za Club hiyo yenye wachezaji wenye mbinu na ujuzi mkubwa, kwa kupambana vikali kwenye michuano hiyo hali inayoleta hamasa ya watu kupenda michezo na burudani ya aina yake.

Akizungumza na Maliasili Media, Bi. Mwantum Shabani wa Manyoni Singida amesema japo timu ya Maliasili Sports Club Wanaume Kamba imeshika nafasi ya pili lakini imeonesha upinzani mkali dhidi ya timu zingine pinzani.

" Singida kama burudani tumepata, mimi timu yangu ilikuwa Maliasili, si kwa sababu tu wanatulindia Maliasili zetu na kutuletea mapato kupitia Utalii, pia kwa namna walivyojipanga kwenye michezo hii, yaani ukishangilia hii timu haikuangushi, najivunia kuona wameibuka na Kombe hili naamini mwakani watakuwa washindi wa kwanza". Aliongeza Bi. Shabani.

Akizungumzia mashindano hayo makubwa hapa nchini, Mwenyekiti wa MNRT SPORTS CLUB Bw. Gervas Mwashimaha ameushukuru uongozi wa Wizara hiyo kwa kuiunga mkono club hiyo hali iliyowatia moyo na hari kubwa Kipindi chote cha michuano hiyo na kuahidi kuendelea kufanya vyema zaidi katika michezo mingine watakayo shiriki.

Katika mchezo wa Fainali wa Kamba wanaume, timu ya Maliasili imeshika nafasi ya pili dhidi ya timu 47 zilizoshiriki mashindano hayo huku timu ya Uchukuzi wanaume Kamba ikishika nafasi ya kwanza. 

SERIKALI IMEWEKA MSINGI IMARA KUHAKIKISHA WAANDISHI WA HABARI WANAFANYA KAZI KWA UHURU,BILA BUGHUDHA

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Gerson Msigwa.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari na kujenga mazingira salama kwa waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha uhuru wa kujieleza unaimarika nchini.


Akizungumza leo Aprili 28, 2025 jijini Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Gerson Msigwa, amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka msingi imara wa kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi kwa uhuru na bila bughudha.


"Ninawashukuru kwa mijadala yenu kuhusu Akili Mnemba; ni muhimu sana katika kazi za uandishi wa habari. Nimesikia kuhusu maazimio yenu na tutayafanyia kazi," amesema Msigwa. 

Ameeleza kuwa serikali inatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani, kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru na waandishi wanalindwa dhidi ya bughudha.

Msigwa amebainisha kuwa serikali itaendelea kulinda haki za waandishi wa habari, kuimarisha uhuru wa kujieleza, na kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha sekta ya habari nchini. 


"Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa hakuna mwandishi anayebughudhiwa na itaendelea kujenga mazingira bora zaidi ya kazi kwa waandishi wa habari," amesisitiza.

Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo, ameeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni haki ya msingi na siyo hisani, akisisitiza kuwa kila mwananchi ana jukumu la kuutetea.


Melo amesema katika dunia ya sasa yenye wingi wa taarifa, akili mnemba ni silaha muhimu katika kulinda uhuru wa habari. 


Ameongeza kuwa mageuzi ya teknolojia yamepanua uwanja wa habari kutoka kwa vyombo vya jadi hadi kwa watengeneza maudhui wa kidijitali, hivyo kila anayesambaza taarifa anapaswa kulindwa.


Hata hivyo, ametoa tahadhari kuhusu matumizi ya teknolojia mpya kama akili mnemba (AI), akieleza kuwa zinahitaji matumizi ya umakini mkubwa hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili kuepusha usambazaji wa taarifa potofu.

Katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Jamii Africa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, UNESCO na wadau wengine, viongozi wa kimataifa akiwemo Balozi wa Sweden na mwakilishi wa UNESCO wametoa wito wa kuimarisha uhuru wa habari na kuwalinda wanahabari dhidi ya vitisho vinavyochochewa na matumizi ya teknolojia mpya.

Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka 2025 yanaendelea jijini Arusha hadi Aprili 30, 2025, yakilenga kujadili mafanikio, changamoto, na njia bora za kuimarisha tasnia ya habari kwa maendeleo ya taifa.


Monday, April 28, 2025

MAPEPELE AMKABIDHI KIJITI HOSSEAH

...............

Na Sixmund Begashe

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Nteghenjwa Hosseah amekabidhiwa rasmi ofisi na aliekuwa Mkuu wa Kitengo hicho Bw. John Mapepele ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, ili kuendelea kuwatumiaka wananchi kwenye ofisi yake hiyo.

Katika zoezi hilo la kihistoria lililofanyika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Bw. Patrick Marcelline alimpongeza Bw. Mapepe kwa Utumishi wake mwema kwenye Wizara hiyo na kumtakia kila laheri katika ofisi yake mpya, huku akimkaribisha Bi.Hosseah na kumuahidi ushirikiano wakutosha kwenye utekelezaji wa majukumu yake ndani ya Wizara hiyo inayojishughulisha na Uhifadhi pamoja na Utalii nchini.

Aidha Bi.Hosseah ambaye awali alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini OR-TAMISEMI, ameushukuru uongozi wa Wizara hiyo kwa kumpokea vizuri na kuahidi Utumishi mwema katika kuiongoza vyema timu nzima ya mawasiliano ili kufikia lengo la Wizara na Taifa kwa ujumla kupitia Maliasili na Utalii, huku Bw. Mapepele akiushukuru uongozi, maafisa wa Kitengo cha Habari, Watumishi wote wa Wizara hiyo kwa ushirikiano mzuri waliompatia katika kipindi chote alichohudumu hapo.

 

Sunday, April 27, 2025

BENKI YA DUNIA YAIMWAGIA SIFA TANZANIA KWA KUSIMAMIA VIZURI UCHUMI WAKE

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kulia), akiwa na Makamu mpya wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, walipokutana na kufanya mazungumzo kwenye Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kushoto), ukiwa katika mazungumzo na Timu ya Benki ya Dunia ikiongozwa na Makamu mpya wa Rais wa Benki hiyo anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiamé Diop, kwenye Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Washington D.C, Marekani)

TANZANIA NA CHINA KUKUZA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA KIDIPLOMASIA

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akiwa ameongozana na Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na China.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akiwa katika mazungumzo mafupi na Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, baada ya kumpokea katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na China.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akipitia baadhi ya taarifa alizokabidhiwa na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. Melckzedeck Mbise, wakati alipoongoza ujumbe wa Tanzania kumpokea Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, ambaye amewasili nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na China, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wa Naibu Waziri Bw. Twaha Mwakioja.

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akisalimiana na Bw. Chu Kun, Kansela wa Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, alipowasili kwa ajili ya kumpokea Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na China.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

....................

Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania kumpokea Mhe. Tang Wenhong, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, ambaye amewasili nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe April 26 hadi 29, 2025.

Katika ziara hiyo inatarajiwa kuwa na vikao mbalimbali vya majadiliano kati ya ujumbe wa Tanzania na China, yanayolenga kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

MNDOLWA: 'MZIKI' WA RAIS SAMIA BADO UNAENDELEA UMWAGILIAJI


Mradi wa Membe Kunusuru SGR

Dodoma: Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesema kuwa kasi  ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan bado inandelea katika miradi ya umwagiliaji na kwamba kila mkoa utafikiwa. 

Mndolwa amesema miradi yote inaendelea vyema na itakamilika kwa wakati lengo likiwa kuwawezesha wakulima nchini kulima kilimo biashara chenye tija na kuachana na kilimo cha mazoea kinachotumia nguvu nyingi lakini manufaa yake ni madogo. 

Mkurugenzi Mndolwa amesema hayo katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ilipotembea Mradi wa Bwawa la Umwagiliaji Membe mkoani Dodoma. 

"Sisi Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji tuna nafuu sana. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na miradi yote inaendelea. 

"Rais Samia anatekeleza kwa vitendo ahadi zake, kila mkoa utafikiwa na miradi ya umwagiliaji na uchimbaji wa visima, yote ni kuhakilisha serikali inawawezesha wakulima kupata tija, nchi iwe na chakula cha uhakika na ziada tuuze nje, " alisisitiza. 

Mndolwa alisema mathalani kwa sasa Mkoa wa Manyara kuna miradi yenye thamani ya sh bilioni 80 inatekelezwa ukiwamo uchimbaji wa mabwawa na visima vya umwagiliaji, ufugaji wa samaki na utalii.

Akizungumzia Mradi wa Membe uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 90, Mndolwa alisema bwawa hilo lenye ujazo wa lita bilioni 12 ambalo lina uwezo wa kumwagilia hekta 2,500 likikamilika litanufaisha watu zaidi ya 1,500.

Alisema mradi huo ni kati ya miradi 22 ukikamilia utawawezesha wakulima kulima na kuvuna mwaka mzima badala ya kusubiri kuvuna kwa msimu. 

'Kubwa zaidi mradi huu ni kati ya miradi ya kimkakati wenye lengo la kudhibiti miundombinu ya Reli yetu ya Kisasa ya SGR isiharibike kwa mafuriko. 

"Sote ni mashahidi eneo la Kilosa kila mwaka tunashuhudia uharibifu mkubwa unaotoka na mafuriko. Ukipita na SGR katika eneo hilo kuna maporomoko mengi ya maji na chanzo chake ni hiki lakini ujenzi wa Bwawa hili utasaidia maji kupugua na reli yetu kuwa salama kutoka na maji hayo. "

Alisema ujenzi wa mradi huo una faida kuu tatu, moja ni killimo na ufugaji ukiwamo wa samaki, utalii na uboreshaji wa miundombinu. 

Alieleza kuwa, mradi huo utaokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumiwa na serikali kwa wanachi wa Kilosa kuokoa maisha, kununua chakula na kukarabati miundombinu mara kwa mara. 

Katibu Tawala Msaidizi Sekfa ya Uchumi, Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba alisema changamoto kubwa kwa jiji la Dodoma ni maji na kwamba ujenzi wa bwawa hilo ni fursa kubwa kwani litasababisha wakulima kulima kwa uhakika. 

"Mwaka huu Mkoa wa Dodoma tumepata mvua pungufu jambo ambalo ni hatari kwa kilimo chetu, lakini kuwepo kwa bwawa hili kutabadili kilimo chetu kiwe cha biashara na hali ya uchumi wa mwananchi mmoja itaboreka na hatimaye kuongeza pato la taifa," alifafanua Aziza.




 

JOWUTA , THRDC WALAANI WANAHABARI KUKAMATWA NA KUPIGWA

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu nchini (THRDC) wamelaani kuanza kuibuka matukio ya waandishi wa habari na watangazaji kukamatwa na baadhi kupigwa na hata kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na vyombo vya dola.

Kauli ya kulaani imetolewa leo Aprili 25 mwaka huu na Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma leo mkoani Mbeya, wakati wa mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi wa habari za uchaguzi, ulinzi na usalama kazini.

Mafunzo hayo yamehusisha waandishi kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe, ambapo Juma amesema matukio ya kukamatwa, kupigwa na kuharibiwa vitendea kazi hayakubaliki katika nchi inayojinadi kuwa inazingatia misingi ya kidemokrasia.

Juma amesema katika siku za karibuni, kumeanza kutokea matukio ya baadhi ya wanahabari kukamatwa na vyombo vya dola, kupigwa na wengine kuzuiwa kufanyakazi, jambo ambalo sio sahihi.

Mwenyekiti huyo, amesema mahusiano mazuri baina ya vyombo vya dola na wanahabari, yalikuwa yameimarishwa katika siku za nyuma lakini sasa yanaanza kuharibika jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.

“Kama mwanahabari amekiuka taratibu zozote kuna utaratibu wa kufuata kisheria, badala ya kutumika nguvu kumkamata ama kumzuia kufanyakazi yake”amesema.

Hata hivyo, Juma amewataka wanahabari nchini, kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari, hasa kipindi hiki cha harakati za uchaguzi mkuu, ikiwepo kutoandika habari za upendeleo kwa chama chochote za siasa, kuacha kuwa washabiki wa vyama na watowe fursa sawa kwa vyama vyote.

“Msimamo wa JOWUTA kama mwanahabari unataka kujihusisha na masuala ya siasa ni bora kujiweka kando mapema na tasnia ya habari hadi chaguzi zipite, badala ya kutumia chombo chako cha habari kwa maslahi binafsi ya kisiasa”amesema.

Awali,Wakili Jones Sendodo wa kutoka THRDC, amesema mtandao huo unaungana na wadau wote kulaani matukio yoyote ya kunyanyaswa, kupigwa ama kuharibiwa vitendea kazi mtetezi wa haki za binaadamu, wakiwepo wanahabari.

Wakili Sendodo amesema ni vyema vyombo vya dola kuzingatia sheria za nchi wakati wa kutekeleza wajibu wao.

“Tunapinga matukio ambayo yanaendelea kwa vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa kuwanyanyasa watetezi wa haki za binaadamu na sisi kama THRDC kwa kushirikiana na wadau wengine tutaendelea kuwatetea na kuwapa msaada wa kisheria, msaada wa ushauri wa kisaikolojia na hata makazi salama ya muda watetezi wa haki za binaadamu wakiwepo wanahabari wanapokabiliwa na majanga ama vitisho”amesema.

Wakili Sendodo pia akitoa mada katika mafunzo hayo ya uchaguzi kwa wanahabari, aliwataka kujua sheria mbalimbali ambazo zinawahusu ili kujitahidi kutozivunja, ikiwepo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Takwimu, Sheria za Uchaguzi na nyingine.

Hata hivyo, alitaka wanahabari kujali usalama wao wakiwa kazini na kuchukuwa tahadhari mbali mbali ili kuhakikisha wakati wote wanabaki salama, wakati wakitekeleza wajibu wao.

Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya aliwataka wanahabari nchini, kuendelea kujiunga na JOWUTA kwani ndio chama pekee kinachotambulika kisheria kutetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari na mazingira bora ya kazi.

"Tumekuja kuwapa elimu ya uchaguzi, lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba wafanyakazi wa vyombo vya habari mjiunge JOWUTA, ili tuwe na nguvu moja ya kupigania maslahi yetu," amesema.

JOWUTA inaendelea na kutoa mafunzo kwa wanahabari nchini kuhusiana na kuripoti vyema uchaguzi mkuu mwaka huu na kubaki salama, mafunzo hayo yamedhaminiwa na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ), Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ),THRDC, Taasisi wa Wanahabari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) na JOWUTA.

MWISHO.


Friday, April 25, 2025

SERIKALI KUENDELEA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA AFYA - DKT. BITEKO

 

.....................

Dkt. Biteko atambelea Hospitali ya Wilaya ya Meru

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Serikali imeahidi kuendelea kuboresha huduma za Afya nchini katika ngazi zote ili kuboresha huduma za Afya kwa Watanzania.

Hayo yamesemwa Aprili, 25, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa ziarani Mkoani Arusha ambapo amesema kuwa lengo la uwekezaji katika sekta ya afya ni kusigeza huduma za afya kwa wananchi."

Serikali inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea na uwekezaji mkubwa unaofanya kwa kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza baada kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Meru, iliyopo Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, Mhe. Dkt. Biteko amesema lengo la uwekezaji katika sekta ya afya ni kuboresha afya za Watanzania.

“ Kama mnavyofahamu afya ndio mtaji wa wananchi na Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga hospitali mpya na kufanyia ukarabati zilizopo,” amesema Dkt. Biteko.

Amesistiza “ Watu wote nilioongea nao hapa hospitalini wamesema hali ya utoaji huduma imeimarika na ni nzuri, nataka niwaambie Rais Samia katika uongozi wake ameapa kuboresha hali za maisha ya Watanzania. Hapo awali ilimlazimu mgonjwa kutoa makozi siku tatu mfululizo ili kumfanyia kipimo cha ugonjwa wa kifua kikuu, leo tuna mashine ya kisasa inayotumia saa mbili kupata majibu ya mgonjwa,”

Ameendelea kusema ujenzi na maboresho yaliyofanyika hospitalini hapo imetumia raslimali za ndani (force account) na kazi imefanyika kwa ubora na kuzingatia thamani ya fedha.

Ameongeza kuwa katika kuelekea miaka 61 ya Muungano uwepo wa hospitali hiyo ni kiashiria cha kuwa nchi inapiga hatua kimaendeleo. Hivyo, wananchi hawana budi kuuenzi na kuutunza Muungano.

Aidha, amewataka wagonjwa kuwa wavumilivu wanapoenda kupata matibabu huku wakizingatia kuwa wahudumu wa afya wanafanya jitihada kubwa kuwapa huduma bora.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema kuwa wananchi wa eneo hilo wanafurahia huduma nzuri zinazotolewa na sasa idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa ni 12,000 kutoka 3,000 ya awali.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Meru, Daktari Elisante Fabiani amesema kuwa uboreshaji wa majengo katika hospitali hiyo umesaidia utoaji huduma na kuongeza idadi ya vipimo vya maabara kutoka 18 hadi 32.

“ Tuna mashine ya kisasa ya kupimia vimelea vya kifua kikuu na ndani ya saa mbili pekee mgonjwa anapata majibu ya kifua kikuu na kuanza matibabu na ina uwezo wa kugundua dawa ya kutumia,” ameeleza Daktari Fabian.

Aidha, Dkt. Biteko ameendelea na ziara yake siku tano mkoani humo ambapo ametembelea Wilaya za Longido na Monduli ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.  

DKT. MWINYI: BARABARA YA KIBADA - KIMBIJI KUWA NGUZO YA MAENDELEO KIGAMBONI

Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ally Mwinyi, ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41, hatua muhimu inayolenga kukuza uchumi na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Aprili 25, 2025, katika Wilaya ya Kigamboni, Dkt. Mwinyi alisisitiza kuwa uwepo wa amani nchini ndiyo msingi wa mafanikio ya miradi ya maendeleo kama huu, na kuagiza ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango vya juu. Alibainisha kuwa barabara hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuunganisha maeneo ya pembezoni na fursa za kiuchumi.

Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuendeleza Muungano na kutatua changamoto zilizokuwa zikikumba uhusiano kati ya pande mbili za Muungano, akisisitiza kuwa umoja huo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, aliyemwakilisha Waziri wa Ujenzi, alisema mradi wa barabara hiyo ni jawabu kwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kigamboni, na sasa utafungua fursa za uwekezaji na kuinua uchumi wa eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, alimhakikishia Rais Mwinyi kuwa Mkoa upo salama na utazidi kudumisha amani licha ya changamoto za kisiasa, huku akitoa pongezi kwa Rais Samia kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama hii.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Muhammed Besta, alieleza kuwa barabara hiyo inajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 83.8 na itatekelezwa kwa awamu mbili chini ya mkandarasi kampuni ya Estim, ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 30.

Uzinduzi wa mradi huu umebeba ujumbe mzito wa kaulimbiu ya mwaka huu isemayo: “Muungano wetu, heshima na tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Muungano.