JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Top Stories. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Top Stories. Onyesha machapisho yote

Jumatano, 4 Juni 2025

VITONGOJI 284 ARUMERU MASHARIKI VYAFIKIWA NA UMEME


...........

๐Ÿ“Œ  Ni kati ya Vitongoji 330 vya Jimbo la Arumeru Mashariki.

๐Ÿ“ŒKapinga asema upelekaji umeme unafanyika kwa  awamu kulingana na upatikanaji wa fedha

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imevifikishia huduma ya umeme Vitongoji 284 katika Jimbo la Arumeru Mashariki kati ya Vitongoji 330.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Juni 03, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Dkt. John Danielson Pallangyo aliyeuliza ni  lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA katika Vitongoji 37 ambavyo vipo gizani katika Jimbo la Arumeru Mashariki.

"Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitongoji 17 vipo katika hatua ya utekelezaji kupitia Mradi wa Ujazilizi (Densification IIB) na mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji Awamu ya Pili  A (HEP IIA), aidha, katika Vitongoji 29 zabuni imetangazwa ili kupata Wakandarasi wa kutekeleza miradi kupitia mradi wa kupeleka umeme Vitongojini Awamu ya Pili B (HEP IIB). 

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo, kutawezesha vitongoji vyote vya Jimbo la Arumeru Mashariki kufikiwa na umeme.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Dkt.John Danielson Pallangyo aliyeuliza kuhusu  Kata za Arumeru Mashariki zinazo pata maji kutoka msitu wa mlima Arumeru na kuwa na  flouride ambapo Kampuni ya Kweka imejitolea kuweka mtambo wa kusafisha lakini kinachohitajika ni umeme,   Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali imetenga fedha katika mwaka ujao wa fedha kukipelekea umeme wa uhakika Kitongoji cha Seneto Kata ya Legeruki kwa ajili ya kutibu flouride katika maji.

Akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Mhe. Profesa Patrick Alois Ndakidemi aliyeuliza Serikali itakiunganishia lini umeme Kitongoji cha Orera kilichopo Kijiji cha Mweka, Mhe. Kapinga amesema katika Jimbo la Moshi Vijijini yupo Mkandarasi anayetekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji 15 vya kila Mbunge na kuongeza kuwa kitongoji hicho kipo katika orodha hiyo ya Mkandarasi.

Akijibu swali la Mbunge wa Kondoa Mjini, Mhe. Ally Makoa aliyeuliza Serikali itapeleka lini umeme kwenye mitaa ya Mongoroma, Chandimo na Hachi,  Mhe. Kapinga amesema Serikali imeipelekea umeme mitaa ya Kondoa Mjini ambapo imebaki mitaa hiyo mitatu na kuongeza kuwa itatengwa fedha katika bajeti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuifikishia mitaa hiyo umeme.

Mhe. Kapinga ameongeza kuwa upelekaji wa umeme unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na bajeti ambayo imetengwa.

Akijibu swali la Mbunge wa Mwibara, Mhe. Charles Kajage aliyeuliza kuhusu lini Serikali itavipelekea umeme Vitongoji vya Jimbo la Mwibara ambavyo havina umeme, Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Mwibara lina miradi ya Vitongoji ambayo inaendelea kutekelezwa. 

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mhe. Rita Kabati aliyeuliza kauli ya Serikali kuhusu uwepo wa nguzo Kata ya Ilula Wilaya ya Kilolo toka mwezi wa 11 mwaka jana na hadi leo umeme haujawaka, Mhe. Kapinga amesema hadi kufikia mwezi wa saba eneo hilo litakuwa limefikiwa na huduma ya umeme.

Jumatatu, 2 Juni 2025

WAZIRI AWESO ATAKA WANANCHI WALINDE VYANZO VYA MAJI


......................

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewataka wananchi kulinda mazingira ya vyanzo vya maji kwa kuacha kukata miti ovyo na kufanya shughuli za kibinadamu ili kuepuka ukame. 

Ametoa wito huo mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 2, 2025 yanayoendelea kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma. 

Mhe. Aweso amesema kuwa uwepo kwa rasilimali za maji toshevleu ni usalama wa taifa kwakuwa uwepo wa maji ni uhakika wa chakula, nishati ya umeme pamoja na mipango ya kimaendeleo ambapo yote hayo yanategemea na mazingira endelevu.

Pia, Waziri Aweso alisema ni wakati sasa Watanzania watambue kuwa athari za mazingira ziwe funzo, akitolea mfano Mto Ruvu mkoani Pwani ulivyokauka kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yalisababishwa na binadamu wenyewe. 

“Athari za mazingira ziko wazi kwa mfano ukienda Pangani athari zikio wazi, leo tunaona bahari imekula mji na hivyo kina cha maji kinaongezeka kina kwahiyo changamoto hizi za kimazingira tunazoziona sasa ziwe funzo kwetu,” alisema. 

Pamoja na changamoto hizo, alishukuru na kuipoingeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa mikakati thabiti na hatua madhubuti inazochukua katika kuyasimamia na kuyatunza mazingira.

Amesema hayo yote yanafanyika kutokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa kusimamia agenda ya mazingira.

“Nashukuru kwa kupata nafasi ya kutembelea mabanda haya, hakika Ofisi ya Makamu wa Rais mmejipanga na sisi kama Wizara ya Maji tutaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuyalinda na kuyatunza mazingira ili kuhakikisha Tanzania inakuwa bora na salama, kama mtakumbuka tumefanya mabadiliko ya Sera ili yaendane na mazingira,” alisema Mhe. Aweso.

 

Maonesho hayo ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 5, 2025 ambayo ndio kilele.

 

TAWA MGUU SAWA KUDHIBITI WANYAMAPORI WAKALI IKUNGI

.................

Ester Maile Dodoma

Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori(TAWA) imeanza kutekeleza mikakati ya kudhibiti makundi ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akijibu swali la  Miraji Jumanne Mtaturu ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuondoa Tembo Singida Mashariki ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya Wananchi.

Aidha  Kitandula alisema Katika kudhibiti tembo wanaovamia na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki, Serikali kupitia TAWA imeendelea  kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka vikosi viwili vyenye Askari 24 wakiwemo Wahifadhi 13 na Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) 11 na kutoa magari matatu (3).

Vilevile, TAWA imeimarisha matumizi ya ndege nyuki kwa kuwafukuza tembo kutoka kwenye maeneo ya wananchi na kuwarejesha hifadhini. Mathalan, kati ya mwezi Novemba 2024 na Mei 2025 kikosi maalum cha Askari Wahifadhi 18 na VGS 6 kikitumia ndege nyuki 2 na mabomu baridi kiliweka kambi katika Jimbo la Singida Mashariki, Wilayani Ikungi na kufanikiwa kudhibiti makundi 23 ya tembo kwa kuwarudisha ndani ya hifadhi. 

Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo. Mathalan, kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Mei 2025 elimu hiyo imetolewa kwa wananchi 517 na Askari 110 wa Jeshi la Akiba katika Kata za Mkiwa, Igombwe, Iglansonia, Mang’onyi, Issuna, Ntuntu na Ikungi.

‘Serikali itaendelea kutumia teknolojia ikiwemo ndege nyuki na kufunga visukuma mawimb (GPS Satellite Collars) ili kufuatilia mienendo ya tembo na kuwadhibiti’ alisisitiza  Kitandula.

Jumapili, 1 Juni 2025

PROFESA MDEBE: MATUMIZI YA NISHATI JADIDIFU YAMESAIDIA KUPUNGUZA VIFO VYA WATOTO NJITI


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Shule ya Madini na Jiosayansi , Profesa Evelyne Mbede (wa pili kushoto) na  wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA), Prosper Magali wakiwa na Katibu Mtendaji wa TAREA, Mhandisi Mathew Matimbwi akifuatilia. akitembelea madanda anuai ya wadau wa nishati jadidifu kwenye hafla ya ufungaji wa Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu yaliofanyika jijini Dar es Salaam. 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Shule ya Madini na Jiosayansi , Profesa Evelyne Mbede (wa pili kushoto) na  wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA), Prosper Magali wakiwa na Katibu Mtendaji wa TAREA, Mhandisi Mathew Matimbwi akifuatilia. akitembelea madanda anuai ya wadau wa nishati jadidifu kwenye hafla ya ufungaji wa Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu yaliofanyika jijini Dar es Salaam. 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Shule ya Madini na Jiosayansi , Profesa Evelyne Mbede (wa pili kushoto) akitembelea madanda anuai ya wadau wa nishati jadidifu kwenye hafla ya ufungaji wa Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu yaliofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mtendaji wa TAREA, Mhandisi Mathew Matimbwi akifuatilia.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Shule ya Madini na Jiosayansi , Profesa Evelyne Mbede akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunga rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu yaliofanyika jijini Dar es Salaam.

Katibu Mtendaji wa TAREA, Mhandisi Mathew Matimbwi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hafla ya kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu yaliofanyika jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Shule ya Madini na Jiosayansi , Profesa Evelyne Mbede amesema matumizi ya Nishati Jadidifu yamesaidia kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya miezi yao kutimia (njiti).

 Profesa Mbede ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu aliyasema hayo Mei 29, 2025 wakati akifunga maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

“Zamani wajawazito walikuwa wakijifungua kwa shida vijijini kutokana na kukosa umeme hadi kusababisha watoto waliozaliwa chini ya muda wao (njiti) kupoteza maisha lakini leo hii kwa kutumia nishati jadidifu imesaidia kuokoa maisha ya watoto hao,” alisema Mbede.

Alisema nishati jadidifu hivi sasa inatumika katika vituo vya afya na zahanati mbalimbali nchini na si kwa Tanzania tu bali dunia nzima kusaidia nishati ya umeme kwenye vituo hivyo muhimu kwa jamii.

Profesa Mdebe alisema kumalizika kwa maadhimisho hayo ndio mwanzo wa maandalizi ya maadhimisho ya msimu mwingine wa 2026 mwakani.

Alisema maadhimisho hayo yamekuwa yakipanua wigo wa ubunifu, kwani vijana wengi wamekuwa wakiibuka na bunifu mbalimbali na kuongeza matumizi ya nishati jadidifu na kusaidia maeneo yenye uhitaji, ambako hakuna umeme wa TANESCO na REA na kutatua changamoto za wananchi.

Profesa huyo alisema Tanzania kushiriki katika maadhimisho hayo ni kuendana na hali ya mazingira dunia ili kufikia malengo ya 2030 ya kukabiliana na tabianchi.

 “Maonesho haya yanatija sana, kama nchi tumetoka mbali zamani tulikuwa tukitegemea umeme wa Tanesco pekee lakini hivi sasa tunazalisha umeme kwa kutumia vifaa mbalimbali na hii ni hatua kubwa,” alisema Mbede.

Maadhimisho hayo yaliandaliwa na Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Ijumaa, 30 Mei 2025

WAKULIMA WA PARACHICHI WAPONGEZA RUZUKU YA MBOLEA

................

Wakulima wa parachichi mkoani Njombe wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia mbolea ya ruzuku ambayo imewasaidia kuongeza tija na uzalishaji katika zao hilo.

Wakizungumza na wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) walipotembelea Chama cha Msingi cha Ng’anda AMCOS na kampuni ya mkulima wa parachichi ya Avo Nemes Green Limited, tarehe 28 Mei, 2025, wakulima hao walisema ruzuku hiyo imepunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha kuajiri nguvu kazi zaidi kwenye mashamba yao.

Mkulima mkubwa wa parachichi, Bw. Stephen Mlimbila, alieleza kuwa kupitia ruzuku hiyo, amepunguza gharama na fedha alizokuwa akizitumia kununua mbolea sasa zimeelekezwa kwenye ulipaji wa vibarua wanaohudumia shamba lake lenye ukubwa wa ekari 210 na kuwa chanzo cha ajira kwa wananchi wengi wasiokuwa na kazi.

Akijibu ombi la wakulima wa chama cha Ushirika Ng’anda cha kusajiliwa kuwa wakala wa mbolea za ruzuku, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA,  John Cheyo, amemwelekeza Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Joshua Ng’ondya, kuhakikisha Chama hicho  kinasajiliwa na kusaidia kusambaza pembejeo hiyo kwa wanachama wake na kutatua changamoto ya ucheleweshaji pindi inapohitajika.

Cheyo alisisitiza kuwa serikali inatamani kuona wakulima wanaongeza tija na uzalishaji, akiwahimiza kulima kwa bidii ili kuzalisha mara mbili zaidi ya msimu uliopita ili kukuza uchumi wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya GBRI Business Solutions Company Limited,  inayojihusisha na ununuzi na uongezaji thamani wa zao la parachichi  Hadija Jabir, amewasihi wakulima kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea kwenye zao la parachichi  ili wazalishe kwa wingi na ubora unaohitajika kwenye soko la nje.


 

Alhamisi, 29 Mei 2025

WATUHUMIWA 12 WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke,  Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya utendaji wa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2025.

Wanahabari na maafisa TAKUKURU walioshiriki kwenye mkutano wa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke,  Holle Makungu akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa taarifa ya utendaji wa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2025.

..........

NA MUSSA KHALID

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Temeke imewafikisha mahakamani  watuhumiwa kumi na wawili kwa mashtaka ya uhujumu uchumi,Ubadhirifu na Utakatishaji fedha kiasi cha zaidi ya milioni 165.14

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa TAKUKURU (M)Temeke,Holle Makungu  wakati akizungumza na wananahabari akitoa taarifa ya kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu ambapo amesema mashtaka hayo yamefunguliwa katika mahakama ya Wilaya Kigamboni.

Mkuu huyo wa TAKUKURU Temeke amewataja baadhi ya washtakiwa hao kuwa ni pamoja na Annie Nyabugumba Maugo ambaye ni Afisa Hesabu(Ofisi ya Rais TAMISEMI)Tumsifu Christopher Kachira,(afisa mwandamizi OR-TAMISEMI) na Aidani Zabron Mponzi (Ofisa hesabu OR-TAMISEMI).

Wengine ni Jonathan Stanley Manguli (aliyekuwa Afisa hesabu OR TAMISEMI),Godrey James Martiny(aliyekuwa mkuu wa kitengo cha Fedha na Uhasibu),Juvenalis Mauna(Mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na Usafi wa Mazingira),Josephat Mtembei(Mhandisi),Bibiana Mdete (Mtunza Bohari)na  Henry Herman(Afisa Ugavi).

Mbali na Watendaji hao wapo pia wakandarasi walioshatakiwa katika kesi hiyo ni Hamis Kashinje Manfred,Paulo Sam Mwakyusa na Godwin Adamson Cheyo ambao kampuni zao zinatumika kutakatisha fedha hizo.

 Aidha,Makungu,amesema kwa mujibu wa hati ya mashtaka,makosa wanayoshtakiwa nayo ni kusababisha hasara kinyume cha kifungu cha 10(1) cha jedwali la kwanza na kifungu cha 57 na 60(2) cha sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 mapitio ya 2022,kosa la utakatishaji fedha k/f cha 12(1)(a) na 13(1) (a) cha Sheria ya utakatishaji fedha sura 423 ya mapitio 2022,ubadhirifu kinyume na k/f cha 28(2) cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa sura ya 329.

 Aidha Makungu,amesema washtakiwa hao wamepelekwa mahabusu kwa kuwa makosa yao hayana dhamana hadi kesi yao itakapokuja tena mahakamani hapo tarehe 12/6/2025 kwa ajili ya kutajawa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watuhumiwa wanakabiliwa na kosa la kusababisha hasara, kinyume na kifungu cha 10(1) cha Jedwali la Kwanza pamoja na vifungu vya 57 na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (Marejeo ya 2022).

Kosa la utakatishaji fedha, kinyume na vifungu vya 12(1)(a) na 13(1)(a) vya Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sura ya 423 (Marejeo ya 2022) pamoja na kosa la ubadhirifu, kinyume na kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329

Katika hatua nyingine,TAKUKURU mkoa wa Temeke imefuatili miradi 13 yenye thamani ya TZS zaidi Bilioni 11,ambapo kati ya miradi 13 miradi mitano (5) ilitolewa ushauri wa kurekebisha mapungufu yaliyobainika.

Hata hivyo Taasisi hiyo imetaja mikakati yake kwa kipindi cha April mpaka Juni mwaka huu kuwa ni kuimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau mbalimbali katika kukabili tatizo la rushwa hasa katika uchaguzi wa viongozi wa kisiasa unaotarajiwa kufanyika kwa mwaka.

pIA TAKUKURU inaendelea kuelimisha jamii kwa njia mbalimbali, zikiwemo kuimarisha klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi, sekondari, na vyuo, kufanya mikutano ya hadhara na semina, kushiriki maonesho mbalimbali pamoja na kurusha vipindi vya televisheni na redio

KAPINGA ATAJA VIGEZO VYA ZIADA UPELEKAJI UMEME VITONGOJINI


........................

  Lengo ni kuhakikisha kila Jimbo linakuwa na vitongoji vingi vilivyofikiwa na umeme

 Vinahusisha mahitaji ya kiuchumi na Kijamii, ukubwa wa Jimbo na Kitongoji

  Mkurugenzi Mkuu REA atakiwa kumsimamia kwa karibu Mkandarasi wa miradi ya Vitongoji Ziwa Tanganyika

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya umeme katika Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada ikiwemo ukubwa wa vitongoji, ukubwa wa Jimbo pamoja na mahitaji ya kiuchumi na kijamii.

Lengo la kuweka vigezo hivyo ni kuhakikisha kuwa kila jimbo linakuwa na vitongoji vingi vilivyofikiwa na nishati ya umeme.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 29, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Simanjiro, Mhe. Christopher Olesendeka aliyeuliza kwamba  Serikali imejipangaje kutekeleza miradi ya Vitongoji kulingana na jiografia ya Wilaya ya Simanjiro ambapo umbali kutoka Kitongoji kimoja hadi kingine ni zaidi ya kilometa kumi.
 
"Mheshimiwa Naibu Spika, tunatekeleza miradi hii ya Vitongoji kwa kuzingatia vigezo vya ziada, tumeangalia ukubwa wa jimbo husika, ukubwa wa Vitongoji na mahitaji ya kiuchumi na kijamii katika jimbo husika. Niwahakikishie Wabunge mtaona utofauti katika miradi hii tunayoitekeleza hivi sasa."  Amesema  Kapinga

Akijibu swali la Mbunge wa Nyasa Mhe. Stella Manyanya aliyeuliza kuhusu kitongoji cha  Songea Pori kilichopo katika Kijiji cha Lunyele  na Kitongoji cha Nindi kilichopo Kijiji cha Konganywita kufikishiwa nishati ya umeme, Mhe. Kapinga amesema Vitongoji hivyo vimefanyiwa upembuzi yakinifu na kubainika vinahitaji njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kati kwa umbali wa kilometa tatu.

Amesema  Serikali inatarajia kuvipelekea umeme vitongoji hivyo kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vitongojini Awamu ya Pili B  (HEP IIB) ambao utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2025/2026. 

Kuhusiana na kasi ndogo ya Mkandarasi anayetekeleza miradi ya umeme katika Jimbo la Nyasa Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali imeshakutana na Mkandarasa na kumuagiza kuweka Wakandarasi wadogo (sub contractors) katika miradi yake anayotekeleza.

Akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Mhe. Aida Khenani aliyetaka  kauli ya Serikali kuhusu kusuasua kwa Mkandarasi ambaye amepewa kazi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika, Mhe. Kapinga amesema katika utekelezaji wa miradi ya Vitongoji Serikali imehakikisha inawapata wakandarasi wenye weledi.

Kuhusu Wakandarasi ambao wanasuasua,  Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza mradi huo wa umeme kwenye Vitongoji vilivyozunguka ziwa Tanganyika.

Aidha, amemuagiza kuchukua hatua za ziada kwa Mkandarasi huyo kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa haraka na kwa weledi
 

Jumanne, 27 Mei 2025

MILIONI 815.453 KUMALIZA KERO YA MAJI VIJIJI VINNE WILAYANI MTWARA

Picha no 382 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akiangalia kisima cha maji katika kilichofanyiwa ukarabati mkubwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa Wananchi wa Vijiji vya Ndumbwe,Dihimba,Mpondomo na Kinyamu Wilayani Mtwara,kushoto Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike na kulia Mkuu wa Wilaya hiyo Abdala Mwaipaya.

Picha no 387 Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara Hamis Mashindike kushoto,akitoa maelezo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi kuhusu ukarabati wa Mradi wa Maji  Dihimba unaohudumia zaidi ya Wakazi 7,489 wa vijiji vinne Wilayani Mtwara. Na Mwandishi Maalum, Mtwara SERIKALI kupitia Wizara ya Maji,imetoa Sh.815,453,185 ili kukarabati mradi wa Maji Dihimba utakaohudumia wakazi zaidi  7,489 wa Vijiji vya Dihimba,Mpondomo,Kinyamu na Ndumbwe vilivyopo Halmashauri ya Wilaya Mtwara Mkoani Mtwara. Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike  alisema,kati ya fedha  hizo Sh.694,271,895 zimetumika kulipa Mkandarasi na Sh.121,181,200 zimetumika kwa ajili ya kununua bomba na Ruwasa Makao Makuu kwa kumtumia Mkandarasi M/S Zonghi Plumbing&General Supplies  Company Ltd. amesema,mradi huo ulianza kufanyiwa ukarabati Mwezi Januari 2024 na ulitakiwa kukamilika Mwezi Septemba, lakini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa malipo ya hati ya madai na mvua nyingi umeshindwa kukamilika kwa muda,hivyo uliongezwa muda  na utakamilika Mwezi Juni Mwaka huu. Mashindike amesema,mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi M/S Seba Construction umefikia asilimia  75 na Mkandarasi amelipwa  malipo ya awali kiasi cha Sh.100,766,635.90 na  ulianzishwa ili kusogeza huduma ya majisafi na salama kwa Wananchi wa Vijiji hivyo na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji katika  Wilaya Mtwara. Alisema,ukarabati  huo umehusisha ujenzi wa tenki moja la lita 100,000 katika kijiji cha Mpondomo,ukarabati wa matenki mawili ya lita 200,000 katika Kijiji cha Ndumbwe na ujenzi wa vituo 17 vya kuchotea maji. Alitaja kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa nyumba ya muhudumu,ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO),ununuzi na ulazaji wa bomba za maji umbali wa kilometa 9.74 zilizonunuliwa na Mkandarasi na ulazaji  wa bomba umbali wa kilometa 14.781 zilizoletwa na Ruwasa Makao Makuu. Kwa mujibu wa Mashindike,faida zilizopatikana kutokana na mradi huo ni pamoja na kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa Wananchi kutoka asilimia 37.04 ya awali hadi asilimia 93.47 mwaka 2025  ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 56.43. “Faida nyingine zilizopatikana ni kutatua changamoto ya maji iliyokuwepo katika vijiji vya Dihimba na Mpondo,Kinyamu na Ndumbwe,kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya mlipuko katika jamii yanayotokana na matumizi ya maji yasio safi na salama,kuchochea maendeo na umetoa ajira za muda mfupi na mrefu kwa baadhi ya Wananchi”alisema. Alieleza kuwa,mradi umezingatia sera ya maji ya kumtua mama ndoo kichwani  kwa kuzingatia umbali usiozidi mita 400 kutoka kituo kimoja cha kuchotea maji kwenda kingine na hadi sasa jumla ya kaya 48,taasisi 2 za umma zimeunganishiwa maji na vituo 12 vipya vya kuchotea maji vimejengwa. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Patrick Sawala alisema,mradi wa maji Dihimba ulizinduliwa mwaka 1989, lakini tangu wakati huo haujafanyiwa ukarabati  wowote hivyo ulishindwa kutoa maji ya kutoshelezaji mahitaji ya Wananchi wa vijiji husika. Alisema,kutokana na changamoto hiyo Serikali imeamua kutoa fedha  ili kukarabati mradi huo ambao sasa umewezesha wananchi kupata huduma ya majisafi na salama na kupunguza muda kwa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao. Alisema,katika Mkoa wa Mtwara kuna miradi mikubwa na midogo ya maji inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo mradi wa Maji wa Miji 28 wa Mto Ruvuma unaotarajiwa kupeleka maji katika Mji wa Mangaka,Masasi na Nachingwea Mkoa jirani wa Lindi. Alisema,miradi hiyo ikikamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 71 maeneo ya Vijijini hadi asilimia 85 ifikapo mwaka 2030 ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi ili kuwaondolea Wananchi changamoto ya majisafi na salama. Mkazi wa Kijiji cha Dihimba Mwanahawa Rashid alisema,kabla ya ukarabati huo walitembea kilometa 2 hadi 3 kila siku  kwenda vijiji vya jirani kutafuta maji kwa kuwa katika kijiji chao kulikuwa na bomba moja tu lililojengwa kupitia mradi wa Jaica ambalo halikutosheleza kutoa maji ya uhakika. “Tunaishukuru sana Serikali yetu ya awamu ya sita iliyofanikisha kukarabati   mradi wa maji katika Kijiji chetu cha Dihimba,nawapongeza watendaji wa Ruwasa kusimamia vizuri mradi ambao umetusaidia sana kupata maji ya uhakika”alisema.

MABADILIKO YA MITAALA NGUZO MUHIMU YA KUIMARISHA ELIMU NCHINI - PROF MKENDA


...........................

 Na Ester Maile: Dodoma 

Serikali  kupitia  wizara ya Elimu,sayansi na Teknolojia inaendelea  Kuboresha   mfumo wa elimu kupitia maboresho makubwa ya mitaala katika ngazi zote za elimu nchini.

Maboresho hayo, yanalenga kuongeza ujuzi, maarifa na stadi za wanafunzi, ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuhakikisha elimu inakuwa chachu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Hayo yamebainishwa  leo 27 may 2025 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia  Prof Adolf Mkenda wakati akizungumza     na waandishi  wa habari  akieleza mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita Waziri Mkenda amesema kuwa Serikali imeanzisha mikondo miwili ya elimu ya Sekondari, Mkondo wa Jumla na Mkondo wa Amali, pamoja na kuweka mfumo wa elimu kuwa nyumbufu, ili kuhakikisha wanapokea ujuzi na maarifa yanayozingatia mahitaji halisi ya taifa na soko la ajira.

Tumeweka somo la lazima la elimu ya Biashara na Historia ya Tanzania, huku tukiboresha mifumo ya ufundishaji lugha ili kuongeza ufanisi wa ujifunzaji,” amesema Waziri Mkenda.

Aidha, amebainisha kuwa mitaala 389 katika elimu ya ufundi na mitaala 563 katika elimu ya juu imeboreshwa ili kuendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na kuzingatia stadi za karne ya ishirini na mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Waziri Mkenda pia ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya mapitio ya Sheria ya Elimu (Sura 353) ili kuendana na mabadiliko haya ya sera na mitaala.

 “Tunaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kuhakikisha Sheria yetu inakidhi mahitaji ya sasa,” amesema.

Aidha, Serikali imehuisha miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Taifa wa Tuzo na Sifa Linganifu za Kitaaluma (TQF), Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule, Mwongozo wa Utambuzi wa Vipawa na Vipaji, pamoja na Mwongozo wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini.

Pia, Waziri Mkenda ametangaza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika elimu, ikijumuisha miongozo ya matumizi ya teknolojia katika shule, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, pamoja na matumizi ya Akili Bandia (Artificial Intelligence) kwa mwaka 2025.

Amesema Serikali imeandaa Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Ujifunzaji unaolenga kurahisisha upimaji wa wanafunzi katika shule za msingi na kuimarisha huduma kwa walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Katika sekta ya elimu ya juu, Waziri Mkenda amesema Serikali imeanza ujenzi wa majengo ya madarasa, maabara na mabweni katika kampasi kuu na za pembezoni katika mikoa 16 ambayo haikuwa na taasisi za elimu ya juu. 

Mradi huo wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wenye thamani ya shilingi bilioni 972, utaongeza uwezo wa taasisi hizi katika kudahili wanafunzi zaidi na kupunguza uhaba wa wahadhiri kwa asilimia 20.

“Tunahakikisha kwamba elimu yetu inazalisha wataalamu wenye ujuzi na stadi zinazohitajiwa katika soko la ajira ili kuchangia maendeleo ya Taifa letu,” alisisitiza Waziri Mkenda.

Waziri amewataka wananchi na wadau wa elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mfumo wa elimu nchini.

WAZIRI MASAUNI ATOA ONYO UZALISHAJI NA MATUMIZI BIDHAA ZA PLASTIKI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni,akizungumza na waandishi wa habari  leo Mei 27, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitakuwa jijini Dodoma.

......

Serikali imetoa onyo kali kwa watu na kampuni zinazoendelea kuzalisha bidhaa za mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na kuingiza katika matumizi kwa njia za panya.

Imesema itaendelea kufanya doria za kushtukiza katika viwanda, viwanda bubu na masoko ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika wote wanaojihusisha na biashara hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema hayo leo Mei 27, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitakuwa jijini Dodoma na mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hatua hiyo inakuja kutokana na kujitokeza kwa changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya tubings kutumika kama vibebeo na vifungashio ambavyo havina sifa na kutokukidhi matakwa yaliyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kufuatia hatua, Mhandisi Masauni amelielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mamlaka nyingine za umma kuendelea kufuatilia na kuwabaini wahusika wote wanaokiuka sheria na kuzalisha bidhaa za plastiki zilizopigwa marufuku kuzalishwa na kutumika nchini. 

“Niwakumbushe Watanzania wenzangu kuzingatia maelekezo ya Serikali kuachana na mifuko ya plastiki na kutumia mifuko mbadala ambayo kwa sasa inapatikana nchini kote kwa gharama nafuu” amesisitiza Mhandisi Masauni.

Aidha, alisema kuwa pamoja na changamoto hiyo, kwa kiasi kikubwa Tanzania imepiga hatua katika kudhibiti taka za plastiki baada ya kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kuanzia Juni, 2019, hatua iliyosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kuhusu kutambua mifuko na vifungashio vya plastiki vilivyoruhusiwa, Mhe. Masauni alisema kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma sambamba na ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa mifuko mbadala ambazo ni rafiki kwa mazingira.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Waziri Masauni alisema yatachagizwa na maonesho ya Wadau ya Bidhaa, Huduma na Ubunifu kuhusu Hifadhi ya Mazingira yakayoanza Juni mosi hadi 5, 2025 jijini Dodoma.

Pia, alisema Kutakuwa na Kongamano la Vijana litakalowatanisha vijana mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa vyuo, wajasiriamali na mabalozi wa mazingira litakalofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 3 Juni, 2025.

Kwa mujibu wa Mhandisi Masauni, Kaulimbiu ya madhimisho ya mwaka huu ni ‘Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki’ inayolenga kuikumbusha jamii kuwa mazingira na rasilimali zake ni msingi wa uhai na maisha pamoja na ukuaji wa Uchumi, hivyo utunzaji na uhifadhi wa mazingira na rasilimali zake ni jambo muhimu.

DKT DIALLO : WAKULIMA PIMENI AFYA YA UDONGO KUEPUKA HASARA

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo akizungumza na wakulima wa Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa Miwa (AMCOS) cha Mkula, Halmashauri ya Ifakara mkoani Morogoro wakati wa ziara iliyolenga kujifunza, kupokea na kutatua changamoto za wakulima hao wa miwa tarehe 26 Mei, 2025.
Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo wa pili kutoka kushoto, Dkt. Peter Shimo (kulia) mjumbe wa bodi, Hadija Jabir (kushoto) mjumbe wa bodi na Kaimu Mkurugenzi wa TFRA, Robert Mtendamema (wa kwanza kulia) wakisikiliza maswali ya wakulima Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa Miwa (AMCOS) cha Mkula, tarehe 26 Mei, 2025 Ifakara mkoani Morogoro
Wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa Miwa (AMCOS) cha Mkula, Halmashauri ya Wilaya ya Ifakara, mkoani Morogoro, wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo, wakati wa ziara ya kikazi ya Bodi na Menejimenti ya TFRA iliyolenga kujifunza kusikiliza na kutatua changamoto za wakulima hususan katika suala la matumizi sahihi ya mbolea
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Robert Mtendamema akizungumza mara baada ya kuwasili katika kiwanda cha sukari cha Kilombero mkoani Morogoro tarehe 26 Mei, 2025

.................

Na Mwandushi Wetu, Ifakara

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo, ametoa wito kwa wakulima wadogo wa miwa kupima afya ya udongo wa mashamba yao kabla ya kutumia mbolea, ili kuhakikisha wanatumia mbolea sahihi na kuongeza tija ya uzalishaji.

Dkt. Diallo amesema, "Ili kupata matokeo bora, ni muhimu kila mkulima kupima afya ya udongo wa shamba lake binafsi badala ya kuchukua sampuli za jumla ili kumsaidia mkulima kufanya maamuzi sahihi na kuepusha hasara."

Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 26 Mei, 2025, katika mkutano na wakulima wa Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa Miwa (AMCOS) cha Mkula, Halmashauri ya Wilaya ya Ifakara, mkoani Morogoro, wakati wa ziara ya kikazi ya Bodi na Menejimenti ya TFRA.

Dkt. Diallo amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza, kupokea changamoto za wakulima na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuwahimiza kupima afya ya udongo ili kuongeza mavuno na kupunguza gharama zisizo za lazima.

Kwa upande wake, Meneja wa AMCOS hiyo, Clemency Mjami, ameishukuru serikali kwa kutoa ruzuku ya mbolea, akieleza jinsi ilivyosaidia kupunguza gharama kwa wakulima.    

"Kupitia ruzuku hii, bei ya mbolea imepungua kutoka shilingi 120,000 hadi 68,000 kwa mfuko.

 Wakulima wa AMCOS yetu wamepata jumla ya mifuko 11,740 ya mbolea sawa na tani 587, yenye thamani ya ruzuku ya shilingi 182,707,521 kwa kipindi cha miaka mitatu tangu 2022/2023," amesema Mjami.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wakulima wameelekeza shukrani zao kwa serikali na kueleza kuwa Ruzuku hiyo imewasaidia sana na kuiomba serikali iendelee kutoa ruzuku hii kwani bila hiyo, wengi wao hawawezi kumudu gharama za pembejeo.

Mkulima mwingine kutoka Kijiji cha Msofini, Kata ya Mkula, Amanda Punguti, amesema ruzuku imewasaidia wakulima wenye hali duni kupata pembejeo na kuongeza uzalishaji.

 "Ruzuku ya mbolea imekuwa mkombozi kwa wakulima wadogo. Tunaiomba serikali iendelee kutupa moyo huu wa kusaidia wakulima."




 

Ijumaa, 23 Mei 2025

TANZANIA YAZIDI KUJIIMARISHA UHIFADHI WA URITHI WA UTAMADUNI NA HISTORIA



..........,,......

Na Sixmund Begashe,Dodoma

Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha juhudi za kuhifadhi urithi wa historia na utamaduni kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambacho kina mpango wa kuanzisha makumbusho ya kudumu.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi mahususi za kuthamini, kuendeleza na kuhifadhi mila, desturi na historia ya taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa maonesho ya utamaduni wa makabila mbalimbali ya Tanzania, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale, Dkt. Christowaja Ntandu, amesema kuwa kuanzishwa kwa makumbusho ya kudumu UDOM kutachangia katika kukuza tafiti za kitaalamu, kutoa mafunzo ya stadi za ujasiriamali, pamoja na kuwapa vijana fursa za kujiajiri na kujiendeleza kitaaluma.

"Tutaangalia namna bora ya kusaidia juhudi za kuanzishwa kwa makumbusho ya kudumu, kushirikiana katika tafiti, kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kusaidia vijana wanaotaka kuanzisha miradi ya kiutamaduni na utalii kama njia mpya ya kukuza utalii wa kiutamaduni," amesema Dkt. Ntandu.

Aidha, Dkt. Ntandu ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta ya urithi wa historia na utamaduni, hasa kwa kuwawezesha vijana kupata elimu itakayowawezesha kutambua fursa zilizopo ndani ya sekta hiyo.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, amesema kuwa chuo hicho tayari kina mikusanyo na vielelezo vya kitamaduni, hasa kutoka jamii ya Wagogo, kama hatua ya awali kuelekea kuanzishwa kwa makumbusho rasmi chuoni hapo.

“Niwahakikishie kuwa chuo chetu kitaendelea kuwekeza katika kukuza vipaji, stadi za uongozi, maadili ya Kitanzania na ujenzi wa taifa kupitia elimu jumuishi yenye mwelekeo wa maendeleo. Tutahakikisha kila mwanafunzi anayehitimu hapa anatoka akiwa na maarifa, ujuzi na moyo wa kujitegemea,” amesema Prof. Lokina.

Maonesho hayo yaliyopewa kaulimbiu "Utamaduni Wetu ni Moyo wa Taifa Tuuenzi" yalipambwa na maonyesho ya utamaduni wa Kabila la Wahaya, ngoma na mavazi ya asili ya makabila ya Kigogo, Kisukuma, Kimasai, Kihehe, Kihaya na kutoka Zanzibar.

 

Jumanne, 20 Mei 2025

KAMATI MPYA YA UKAGUZI WIZARA YA NISHATI YAFANYA ZIARA KATIKA MIRADI YA UMEME MKOANI PWANI.


๐Ÿ“Œ Yapongeza Serikali utekelezaji miradi ya umeme


Kamati mpya ya  Ukaguzi ya Wizara ya Nishati imefanya ziara  katika miradi ya umeme mkoani Pwani ili kujionea utekelezaji wa miradi hiyo hali itakayopelekea  Kamati husika  kumshauri vyema Katibu Mkuu Wizara ya Nishati  juu ya usimamizi wa rasilimali za Wizara ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi.

Ziara hiyo imefanyika katika Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Chalinze mkoani Pwani tarehe 19 na 20 Mei 2025

 Baada ya kujionea utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imekamilika,  Mwenyekiti wa  Kamati,  Mhandisi Kenneth Nindie ameipongeza Serikali kwa kazi Kubwa inayofanya kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

 Amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi katika miradi ya umeme, hivyo Wizara ya Nishati wajibu wake ni kufanya usimamizi mzuri  wa miradi ili thamani ya fedha ionekane.

 Kamati hiyo pia  imewataka wakandarasi wanaopewa kazi ya kutekeleza  miradi kuwa wazalendo kwa kuzingatia viwango na ubora ili miradi inayofanyika  idumu kwa  muda mrefu na kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.

"Tunaipongeza Serikali kwa kweli inafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi mikubwa katika nchi yetu kwa manufaa mapana ya wananchi, kikubwa tunawasihi wakandarasi kuwa  wazalendo katika kutekeleza majukumu yao, mikataba iliyowekwa izingatiwe kwa kutekeleza kazi kwa viwango na Ubora ili miradi hii iwe na tija kwa Taifa." Amesema Nindie

Listen Mkisi Radio