JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Top Stories. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Top Stories. Onyesha machapisho yote

Jumatano, 2 Julai 2025

ASANTENI WANA RUANGWA -MAJALIWA

..............

WAZIRI MKUU, na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Kassim Majaliwa leo Julai 2, 2025 ametangaza rasmi kutokugombea tena ubunge wa jimbo la Ruangwa baada ya kulitumikia jimbo hilo kwa miaka 15.

Akizungumza na wajumbe wa kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya ya Ruangwa Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumuunga mkono wakati wote ambao amekuwa mbunge wa jimbo hilo.

"Imefika wakati kwa mshikamano tulioujenga  sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa Wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili Kauli mbiu yetu ya Ruangwa kwa maendeleo inawezekana iweze kusonga mbele zaidi."

Aidha, ametoa wito wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya kuwapa ushirikiano wagombea wote wenye nia ya kugombea ubunge wa jimbo hilo.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi Wana-Ruangwa kuendelea kushikamana na itakapofika siku ya uchaguzi waweze kuchagua wagombea wote watakaowakilisha chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi huo. 

"viongozi wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dkt. Nchimbi watakapokuja tujitokeze kwa wingi kwenye mikutano tusikilize sera, lakini siku ya kupiga kura tuwapigie kura nyingi za kutosha."

Aidha, amemshukuru Rais Dkt. Samia  Viongozi wakuu wa chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kumuamini na kumpa fursa ya kuwatumikia wana Ruangwa.

Mheshimwa Majaliwa alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa mwaka 2010 na amehudumu kwa kipindi cha miaka 15.

Jumatatu, 30 Juni 2025

MAKAMU WA RAIS AKISHIRIKI UFUNGUZI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA UFADHILI WA MAENDELEO NCHINI HISPANIA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na  na Viongozi mbalimbali kabla ya kuanza kwa  Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Fibes Jijini Sevilla nchini Hispania. Tarehe 30 Juni 2025.

MKINGA ACHUKUA FOMU KUOMBA UBUNGE LUDEWA

Mtia nia James Innocent Mkinga (kulia), Mtaalamu mbobezi katika Fani ya Teknojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) akichukua fomu yake kuomba kuteuliwa kugombea jimbo hilo.

 

James Innocent Mkinga, Mtaalamu mbobezi katika Fani ya Teknojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

JOTO la Siasa katika Jimbo la Uchaguzi la Ludewa limezidi kupanda kufuatia kuendelea kujitokeza kwa watia nia mbalimbali wanaoashiria kuwepo kwa mchuano mkali jimboni humo. 

Jumapili Juni 29 2025, Mtia nia James Innocent Mkinga, Mtaalamu mbobezi katika Fani ya Teknojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Kada CCM na mwana harakati wa Maendeleo ya Vijana amejitokeza kwa mara ya pili kuchukua Fomu ili kushiriki katika mchakato wa kupata nafasi ya kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa Mbunge wa Jimbo hilo.

BIASHARA YA KABONI NYENZO MUHIMU KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mha. Hamad Yussuf Masauni akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Juni 30, 2025 mara baada ya kupokea Taarifa ya Tathmini ya Mwenendo wa Biashara ya Kaboni kutoka kwa Kamati ya Biashara ya kaboni.

.......................

Mwandishi Wetu Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mha. Hamad Yussuf Masauni amesema Biashara ya Kaboni ni miongoni mwa nyenzo muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo nchi, taasisi, kampuni na wananchi wanaweza kushiriki katika jitihada za Kitaifa na Kimataifa za kupunguza gesijoto duniani. 

Waziri Masauni amesema hayo jijini Dar es Salaam Juni 30, 2025 mara baada ya kupokea Taarifa ya Tathmini ya Mwenendo wa Biashara ya Kaboni kutoka kwa Kamati ambapo amesema Tanzania imeimarisha usimamizi wake kwa kuanzisha Kanuni za mwaka 2022 na marekebisho yake ya mwaka 2023, pamoja na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC).

Amesema NCMC ina jukumu la kusajili miradi, kuwezesha ufuatiliaji, uthibitishaji wa gesijoto, utoaji wa elimu na uhamasishaji wa wadau. Tangu kuanza kutumika kwa kanuni, jumla ya miradi 73 ambayo miradi 69 ipo katika hatua mbalimbali za usajili na miradi 4 ipo katika hatua ya utekelezaji.

Ameongeza kwa upande wa Zanzibar imeanza kupokea maombi ya miradi ya kaboni kufuatia kupitishwa kwa Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2025. Kufikia Mei 2025, kampuni nne (4) zilionesha nia ya kutekeleza miradi hiyo, ambapo mbili (2) kati yao zimewasilisha maandiko dhana.

“Kamati hii ilipewa jukumu la kufanya tathmini na kutoa mapendekezo ya kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa biashara ya Kaboni nchini, lengo kuu ni kufanya tathmini ya hali ya sasa ya biashara ya kaboni nchini Tanzania na kutoa mapendekezo kwa serikali kuhusu njia bora za kuimarisha mifumo na mwenendo wa biashara ya kaboni Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema katika kuimarisha uelewa na ushirikishwaji wa wadau katika Biashara ya Kaboni, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa elimu kwa Umma ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu biiashara hiyo.

Amesema Kamati imependekezwa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Biashara ya Kaboni, kuandaa miongozo ya mafunzo kwa wadau wa ngazi zote, pamoja na kuanzishwa majukwaa ya wadau la majadiliano katika ngazi mbalimbali.

Utekelezaji wa Biashara ya Kaboni nchini utaimarika kwa kufanya mapitio ya kanuni na miongozo ya biashara ya Kaboni, kuboresha rejesta ya Taifa ya Kaboni, kuweka mkakati mahususi wa utoaji wa elimu kwa umma, kuboresha mifumo ya usimamizi na utunzaji wa takwimu na kuhamasisha ushirikishwaji wa wadau ikiwemo sekta binafsi.

Ameongeza kwa upande wa Miradi ya kimkakati kunufaika na Biashara ya Kaboni, Tathmini inaonesha kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na Biashara ya Kaboni kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta mbalimbali, ikiwemo reli ya kisasa ya umeme (SGR), Mabasi yaendayo haraka (Dar es Salaam Rapid Transit - DART), uzalishaji wa umeme, gesi asilia, misitu, kilimo, majengo, elimu, madini, udhibiti wa taka na uchumi wa buluu.  

Jumapili, 29 Juni 2025

ETDCO YANG'ARA TUZO SEKTA YA UJENZI

Mwakilishi wa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya ETDCO, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa kampuni hiyo, Mhandisi Dismas (wa pili kutoka kushoto), akipokea Tuzo ya Heshima ya Sekta ya Ujenzi kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Gaudence Mmassy. Tuzo hizo zimeandaliwa na Construction Times Gala and Award 2025 kwa lengo la kutambua mchango wa kamapuni mbalimbali zilizofanyika 28 Juni 2025, jijini Dar es Salaam. Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Gaudence Mmassy akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa makampuni mbalimbali baada ya kutoa tuzo. 

 ..............

 Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imefanikiwa kupata Tuzo ya heshima ya Mkandarasi Bora wa Ujenzi na Miundombinu ya Umeme pamoja na uendeshaji wa kampuni kutoka Construction Times Gala and Award 2025 zilizofanyika 28 Juni 2025, jijini Dar es Salaam. 

 Katika tuzo hizo, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, CPA Sadock Mugendi, pia ametunukiwa Tuzo ya Uongozi Bora katika Uendeshaji wa Kampuni, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kusimamia kwa mafanikio miradi.

 Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo hizo, iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa Jarida la Ujenzi, Afisa Uwekezaji Mwandamizi wa TIC, Bw. Gaudence Nicholaus Mmassy, amepongeza washindi wote kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini. 

 Akizungumza wakati kupokea tuzo hizo Kwa niaba ya Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Kampuni ya ETDCO, Mhandisi Dismas Masawe, amesema kuwa tuzo hizo ni uthibitisho wa kutambuliwa kwa mchango mkubwa wa kampuni katika ujenzi wa miundombinu ya umeme nchini kwa kuonesha dira ya maendeleo wanayoifuata katika utekelezaji wa majukumu yao. 

 “Siri ya mafanikio haya ni usimamizi thabiti kutoka kwa menejimenti ya Kampuni, pamoja na kujitolea kwa dhati kwa wafanyakazi wetu, na utekelezaji wa miradi kwa weledi wa hali ya juu.” amesema Mhandisi Masawe. 

 Katika tuzo hizo za heshima zilizotolewa na Construction Times, jumla ya makampuni nane yalitunukiwa tuzo hizo za heshima, huku ETDCO ikijivunia kuondoka na tuzo mbili kubwa kutokana na utendaji wake bora, hasa katika usimamizi wa miradi na uendeshaji wa kampuni.


TUWE NA MAONO YA KUIONA KESHO YETU – DKT. BITEKO


................


📌Ni katika Bonanza la Wizara ya Nishati na Taasisi zake

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuwa na maono ya kuweza kuona mbali hali itakayowasaidia  katika utendaji wa kazi na kupata suluhisho ya changamoto zinazoweza kutokea kabla ya changamoto hizo kutokea.

Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Julai 28,2025 katika viwanja vya Jamhuri  Jijini Dodoma, wakati akizungumza na watumishi wa wizara na Taasisi zake wakati wa kufunga Bonanza la michezo mbalimbali lililohusisha Wizara ya Nishati na Taasisi zake.








 

Ijumaa, 27 Juni 2025

DKT BITEKO MGENI RASMI NISHATI BONANZA 2025


.........................

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe Dkt Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bonanza la Wizara ya Nishati na Taasisi zake litakalofanyika jumamosi Juni 28, 2025 jijini Dodoma.

Akizungumzia maandalizi ya Bonanza hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Bi. Neema Mbuja amesema kuwa, Nishati Bonanza litafanyika kwenye Viwanja vya Jamhuri mjini Dodoma na kushirikisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na wadau kutoka Wizara nyingine.

‘’ Nipende kuchukua fursa hii kuzikaribisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kushiriki kikamilifu bonanza ambalo linaleta fursa ya kufahamiana na kubadilishana mawazo baada ya muda wa kazi pamoja na kufanya mazoezi ili kujenga afya." Amesema Mbuja

Ameongeza kuwa, kwa mwaka huu Nishati Bonanza linaongozwa na kauli mbiu ya "Michezo kwa Afya bora, Shiriki uchaguzi 2025 ikiwa na lengo pia la kuhamasisha wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 .

Amesema maandalizi yote yameshakamilika na timu zitakazoshiriki michezo mbalimbali zimeshawasili Dodoma kushiriki bonanza hilo litakaloshirikisha watu takribani 1000.

Ametaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni ni pamoja na Mpira wa miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu, Mpira wa Kikapu, Kuvuta Kamba, pamoja na michezo ya jadi kama vile bao na drafti, pia kufukuza kuku.

Taasisi zitakazoshiriki Bonanza hilo la Nishati ni pamoja na TANESCO, REA, TPDC, PURA, EWURA, TGDC, ETDCO, TCPM, TANOIL, GASCO, PBPA.

Hili ni Bonanza la pili kufanyika tangu kuasisiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Doto Biteko mwaka jana.









SERIKALI YASISITIZA UFUATILIAJI NA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa SELF, Bi. Sentiel Yona, wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Washiriki wa mafunzo yaliyotolewa na Wizara ya Fedha kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, wakibadilishana uzoefu baada ya kumalizika kwa mafunzo kwa waratibu hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Mmoja wa watoa mada kuhusu huduma za uwekezaji, Afisa Mauzo, Watumishi Housing Investment, Bw. Jafari Chaukunde, wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya maandalizi ya mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, baada ya kumalizika kwa halfa ya kufunga, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma. Kulia ni Afisa Msimamizi Fedha Mkuu, Idara ya Uendelezaji Fedha Wizara ya Fedha Bw. Magesa Mafuru na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, baada ya kumalizika kwa halfa ya kufunga, katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma. Kulia ni Afisa Msimamizi Fedha Mkuu, Idara ya Uendelezaji Fedha Wizara ya Fedha Bw. Magesa Mafuru na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dodoma)

.............................

Na. Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma

Katika kuhakikisha usimamizi madhubuti wa Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha, Serikali imewaagiza waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha kote nchini kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera na Sheria za Huduma Ndogo za Fedha katika maeneo wanayoyasimamia ili kuwabaini na kuwachukulia hatua watoa huduma wanaotoa huduma kinyume na utaratibu uliowekwa.

Agizo hilo limetolewa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Dionesia Mjema, wakati akifunga mafunzo ya kitaalamu kwa watoa huduma ndogo za fedha kutoka katika ngazi za mikoa, wilaya na halmashauri, yaliyolenga kuwaongezea ujuzi wa kiutendaji katika kutambua changamoto, kushughulikia ukiukwaji wa sheria na kuwajengea uwezo wa kusimamia kwa ufanisi huduma hizo.

“Ni muhimu kila mmoja wetu awe mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha inatekelezwa ipasavyo, na wale wanaokiuka Sheria hiyo wanachukuliwa hatua stahiki,” alisema Bi. Mjema.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa Sheria si chaguo bali ni wajibu wa kila mtoa huduma na msimamizi wa sekta hii, kwa kuwa utekelezaji huo ndio msingi wa kuhakikisha uwajibikaji, uadilifu, na uendelevu wa huduma ndogo za fedha katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Aidha, aliwasisitiza kujenga mazoea ya kuandaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa Sheria hizo kila baada ya miezi mitatu, kwa mujibu wa miongozo, kwa kuwa taarifa hizo ni nyenzo muhimu katika kutathmini maendeleo, changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa sheria katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Bi. Mjema, aliwasihi waratibu hao kushirikiana kwa karibu na maafisa ushirika, wahamasishaji, wasajili, pamoja na maafisa maendeleo ya jamii, ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Sera na Sheria za Huduma Ndogo za Fedha unafanyika kwa ufanisi.

“Ushirikiano huo unatarajiwa kujenga mfumo madhubuti na endelevu wa huduma ndogo za fedha, unaolenga kuwafikia wananchi wa kipato cha chini kwa kutumia mbinu bora, salama na zenye ufanisi, ili kuchochea ustawi wa kiuchumi na kuchangia maendeleo jumuishi ya taifa zima”alisema Bi. Mjema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha mkoani Mbeya, Bi. Sebastiana Mwapinga, ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa kichocheo muhimu cha mabadiliko chanya, na kwamba wataendelea kuboresha utendaji wao hususan katika maeneo yaliyokuwa na changamoto hapo awali, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kifedha zitakazowawezesha kuinua hali zao za kiuchumi.

Naye, mmoja wa wahamasishaji, Bi. Teodomila Mwenda, amesema kuwa hatua ya Serikali kuwapatia mafunzo na kuwajengea uwezo wa kitaalamu siyo tu imedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kuimarisha sekta hiyo, bali pia imeongeza ari na motisha kwao kuendelea kutoa elimu kwa ufanisi zaidi.

Katika mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, taasisi mbalimbali zilipata fursa ya kutoa elimu kuhusu huduma za uwekezaji wanazotoa ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji UTT- AMIS, Mfuko wa SELF pamoja Watumishi Housing Investment ambazo ni muhimu kwa wananchi kuzifahamu na kuzitumia ipasavyo ili kuongeza kipato chao na kuboresha maisha yao ya kiuchumi.

Jumla ya waratibu 130 wa huduma ndogo za fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu katika maeneo mbalimbali, yaliyolenga kuwaimarisha katika kusimamia na kufuatilia kwa ufanisi utoaji wa huduma ndogo za fedha katika ngazi za watoa huduma.

MWISHO

Alhamisi, 26 Juni 2025

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA MIFUMO RASMI YA KIFEDHA KUKUZA UCHUMI WA MWANANCHI

Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, akimkaribisha Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, ili aweze kufungua mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Janeth Hiza, akizungumza wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, wakifuatilia mawasilisho mbalimbali wakati wa mafunzo kwa Waratibu hao yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, yaliyofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja (katikati) akisikiliza baadhi ya michango iliyokua inatolewa na washiriki wa mafunzo yaliyohusisha Wizara ya Fedha na Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri Bi. Evelyine Mangweha, akiuliza swali wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Dionisia Mjema na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.
Mchumi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Felista Malibate, akitoa mada kuhusu Kanuni za Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mwaka 2019 wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.
Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha wa Manispaa ya Ubungo, Bi.Evelyine Mangweha,  akichangia mada wakati wa mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha yaliyofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, baada ya kumalizika kwa halfa ya ufunguzi, iliyofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dodoma)

.......................
Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma

Serikali imewataka Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha nchini kuongeza kasi, ubunifu na weledi katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mifumo rasmi ya kifedha inayotambulika na kusimamiwa na Serikali ili kuhakikisha wanapata maarifa yatakayowawezesha kujikwamua kiuchumi kwa njia salama na endelevu.

Agizo hilo limetolewa na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, wakati akufungua mafunzo maalum kwa Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyolenga kuwawezesha waratibu hao kutoa elimu sahihi kwa jamii wanazozihudumia.

Dkt. Mwamwaja alisisitiza umuhimu wa kutumia mafunzo hayo kama jukwaa la kubadilishana mawazo, uzoefu na mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazowakabili waratibu hao katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Maarifa haya msiyabakize kwenye makabrasha, pelekeni kwa wananchi waelimisheni waelewe faida ya kutumia mifumo rasmi ya kifedha kama benki, SACCOS, VICOBA vilivyosajiliwa na taasisi zingine zilizo chini ya uangalizi wa Serikali kwa kuwa ndiyo njia salama ya kuwasaidia kuinuka kiuchumi,” alisema Dkt. Mwamwaja.

Aliongeza kuwa mafanikio ya sekta hiyo hayatategemea tu uwepo wa Sera, Sheria na Kanuni nzuri, bali yanategemea zaidi utekelezaji wenye tija, weledi, uwajibikaji na ufuatiliaji makini unaoanzia kwa Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha ambao ndio kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kufikisha elimu na huduma bora za kifedha.

Aidha, aliwapongeza Waratibu wote kwa kujitokeza kwa wingi na kwa wakati katika mafunzo hayo, na kuwataka kuyachukulia kama fursa ya kuimarisha uwezo wao wa kuwaelimisha wananchi kwa njia shirikishi, rafiki na yenye matokeo chanya.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Mohamed Nyange, alisema kuwa mafunzo hayo yamewapa maarifa ya kina na mbinu sahihi zitakazowawezesha kuwafikia wananchi kwa ufanisi, kutoa elimu inayoeleweka, na kusaidia jamii kuelewa umuhimu wa kutumia huduma rasmi za kifedha kwa maendeleo yao ya kiuchumi.

“Ili tuweze kutoa elimu sahihi kwa wananchi tunaowahudumia lazima nasi tuwe na uelewa wa kutosha kwanza, niwapongeze Wizara ya Fedha kwa kutujengea uwezo huu, tutaenda kutumia maarifa haya kwa kuhakikisha wananchi wetu wanajua, wanaelewa na wanatumia huduma za kifedha rasmi kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi,” alisema Bw. Nyange.

Mafunzo haya yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), lengo ni kuhakikisha nchi inakuwa na mtandao mpana wa waratibu waliobobea katika kutoa elimu ya kifedha kwa jamii.

Serikali imeendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo watendaji wake ili kuhakikisha elimu ya fedha inamfikia kila Mtanzania, kupitia elimu hiyo, wananchi wataweza kufanya maamuzi sahihi ya kifedha ikiwemo kutumia mifumo rasmi inayotambuliwa na Serikali kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Jumla ya mikoa 13 imeshiriki katika mafunzo hayo, ambayo ni: Mbeya, Pwani, Njombe, Shinyanga, Dar es Salaam, Tanga, Singida, Morogoro, Dodoma, Simiyu, Iringa, Arusha na Kilimanjaro.

BUNGE LARIDHIA MAREKEBISHO YA MPAKA WA HIFADHI YA TAIFA NYERERE

...............

Na Anangisye Mwateba, Dodoma

Bunge limeridhia ombi la Serikali la kumega sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa lengo la kutatua migogoro ya mipaka na kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea katika mazingira rafiki kwa jamii na uhifadhi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, akiwasilisha azimio hilo bungeni, amesema kuwa Serikali imeamua kumega eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,617 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kulirejesha katika Pori la Akiba Selous.

Amesema hatua hiyo imepunguza ukubwa wa hifadhi hiyo kutoka kilomita za mraba 30,893 hadi kufikia kilomita za mraba 29,276.

Akifafanua zaidi, Mhe. Chana amesema hatua hiyo inalenga kuondoa migogoro ya muda mrefu ya mipaka baina ya hifadhi hiyo, vijiji vinavyoizunguka, Pori la Akiba Selous na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Mbarang’andu, Juhiwangumwa, Iluma, Jukumu, Magingo na Nalika.

“Kwa kufanya hivyo, tunaimarisha usalama wa maeneo yaliyohifadhiwa, tunajenga mahusiano bora kati ya wananchi na hifadhi, na kuondoa migogoro iliyodumu kwa muda mrefu,” amesema Mhe. Chana.

Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa marekebisho hayo ya mpaka yanalenga kulinda mfumo ikolojia muhimu unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba Selous, sambamba na kuhakikisha mtiririko endelevu wa maji katika Mto Rufiji, ambao ni chanzo kikuu cha uzalishaji umeme kupitia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).

Mhe. Chana amebainisha kuwa hatua hiyo itaongeza tija kwa Taifa kwa kuimarisha shughuli za utalii, uwindaji wa kitalii katika Pori la Akiba Selous na maeneo yanayozunguka, na hivyo kuchangia mapato ya ndani kupitia sekta ya utalii.

“Kwa sasa, tunaelekea katika uboreshaji wa uhifadhi wa maliasili kwa ujumla wake – wanyamapori, mimea, mazalia ya viumbe wa majini na pia kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya wakulima, wafugaji na wavuvi,” ameongeza.

 

Jumatano, 25 Juni 2025

KAMATI YA USHAURI MRADI WA EMA YAKUTANA DODOMA


................

Kamati ya Ushauri ya Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) imekutana kwa ajili ya kujadili na kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 jijini Dodoma leo Juni 25, 2027. 

Kikao hicho kimeongozwa na Bw. Wanjara Jandwa kutoka Kitengo cha Huduma za Sheria cha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambaye aliwapongeza kwa kazi nzuri ya kutoa maoni yenye kujenga. 

Bajeti hiyo iliyowasilishwa na Mratibu wa Mradi Bw. Richard Masesa imejadiliwa na wajumbe walioshiriki kikao hicho kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC, Wizara za kisekta na halmashauri. 

Mradi wa EMA unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, unafadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA), unakusudia kushughulikia changamoto kuu za mazingira na kuondoa vizuizi vya kisekta vilivyopo katika Wizara na mamlaka maalumu za kisheria na kuongeza wigo wa utendaji.

Kwa mantiki hiyo, mradi huo ni nyenzo mojawapo ya kuboresha uratibu wa usimamizi wa mazingira nchini unaokusudia kushughulikia changamoto kuu za mazingira.

WADAU WAMCHANGIA UMMY MWALIMU MILIONI 1.3 ZA FOMU YA UBUNGE

......................

NA: MWANDISHI WETU, TANGA 

Wadau mbalimbali wamemchangia Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, fedha kiasi cha Shilingi 1,300,000, ili zimuwezeshe kuchukua fomu ya Ubunge ili agombee tena nafasi hiyo kwa kipindi kingine katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu 

Fedha hizo ni matokeo ya michango ya hiari kutoka kwa wadau kama vile Taasisi ya Mguu Kwa Mguu, Friends of Odo Ummy, Sema na Tanga na watu wengine nje na taasisi hizo.

Alikabidhi fedha hizo, Abdallah Mukulu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva wa Magari ya IT Tanga, amesema kutokana na kazi nzuri alizozifanya za maendeleo katika Jimbo la Tanga Mjini, wameona wamshike mkono kwa kiasi hicho licha ya kwamba Mbunge huyo anao uwezo wa kujilipia yeye mwenyewe gharama za fomu.

"Mheshimiwa Mbunge wetu Ummy Mwalimu, napenda kukukabidhi Shilingi 1,300,000 kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo Tanga ambao wamejichangisha wao wenyewe ili zisaidie kulipia fomu ya Ubunge. Kwa kweli tunaridhishwa na utendajikazi wako na namna unavyotatua kero za wananchi. Katika kipindi cha uongozi wako, Jimbo la Tanga Mjini limepata miradi mingi ya maendeleo, kwa kweli umefanya makubwa, tunatamani urudi tena madarakani uendelee kuwatumikia wananchi wako," amesema Mukulu.

Vilevile, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sema na Tanga, Said Massa, amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 Tanga Mjini imetekelezwa ipasavyo, hivyo anaunga mkono zoezi la kumchangia fomu ya Ubunge Ummy Mwalimu ili aendeleze kazi nzuri.

"Kwa kweli Jimbo la Tanga Mjini limenufaika sana na uongozi wako ulioacha alama katika maisha ya wananchi kwani umetekeleza miradi mingi ya maendeleo kama vile maji, afya, elimu, Bandari ya Tanga, umeme, barabara na miradi mingine mingi," amesema Massa.

Elias Mpayi ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mguu Kwa Mguu amesema Ummy Mwalimu amewezesha Tanga Mjini kupata maendeleo makubwa katika kipindi kifupi cha uongozi wake, hivyo anastahili kuongoza kwa mara nyingine.

Baada ya makabidhiano hayo, Ummy Mwalimu, amewashukuru wadau hao waliojitoa kwa hali na mali kumchangia fomu ya Ubunge kwani bado ana dhamira ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa Tanga Mjini.

"Moyo wangu umelemewa na shukrani nyingi, nimefurahi kwa kuwa mmetambua kazi kubwa zilizofanyika Tanga Mjini. Nimshukuru pia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea nguvu katika utekelezaji wa miradi, kwa kweli kazi zimefanyika na wananchi mnajionea kwa macho yenu," amesema Ummy Mwalimu.

Listen Mkisi Radio