Wednesday, April 16, 2025
WAZIRI MKUU AKAGUA ATHARI ZA MVUA LINDI, ATOA MAELEKEZO KWA MAMENEJA WA TANROADS NCHINI
Tuesday, April 15, 2025
TMA YAPONGEZWA KWA UBORESHWAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA
MAKAMU WA RAIS AFUNGUA KONGAMANO LA KODI MWAK 2025
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwemo kuimarisha hali ya ulinzi, amani na usalama na kuboresha mfumo wa viwango vya kodi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kodi na Uwekezaji la Mwaka 2025 linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Ametoa rai kwa washiriki wa Kongamano hilo kujielekeza katika kuibua mawazo na mikakati mipya itakayowezesha Taifa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza utegemezi kwa wahisani.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kutumia vema fursa inayotolewa na Serikali kila mwaka kutoa maoni na kuwasilisha mapendekezo yao ya kuboresha sera za kodi na uwekezaji kwa kuchangia moja kwa moja katika jukwaa hilo au kupitia dirisha la kidigitali. Pia amewaagiza Mawaziri wa kila sekta kutoa maoni ya kuongeza mapato ya ndani katika sekta zao na kuhakikisha kuwa maoni na mapendekezo yatakayotolewa na wadau kwa njia mbalimbali yanafanyiwa kazi bila kudumaza ukuaji wa sekta husika.
Makamu wa Rais amesema zipo hatua mbalimbali zinazopaswa kutekelezwa zinazoweza kuongeza mapato ya ndani ikiwemo kuweka mkazo zaidi katika kuimarisha uwezo wa ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya ndani, kuongeza jitihada katika kuboresha mfumo wa kodi ambao utahakikisha usawa na kuondokana na misamaha ya kodi isiyo na tija pamoja na kutoa vivutio vya kutosha kwa mawakala na taasisi za kukusanya kodi na kukabiliana na vitendo vya rushwa.
Makamu
wa Rais ametaja hatua zingine za kutekelezwa ikiwemo kukuza matumizi ya TEHAMA
katika ukusanyaji wa kodi na uwekaji wa akiba, kujenga kanzidata madhubuti ya
taarifa za walipakodi na kufanya
jitihada za kuongeza idadi ya walipa kodi kama njia ya kupunguza mzigo wa kodi,
kubuni mbinu za kukabiliana na changamoto za kilojistiki na kisiasa katika
utozaji wa kodi kutoka katika sekta isiyo rasmi, kuendelea kuboresha
mazingira ya biashara ili kukuza uwekezaji pamoja na kuweka mfumo thabiti wa
usimamizi, ufuatiliaji na upimaji kwa taasisi za kodi na zile za usimamizi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ili kuongeza mapato, bado hali ya ulipaji kodi nchini inakabiliwa na changamoto mbalimbali hali inayopelekea ukuaji mdogo wa makusanyo ya ndani. Mathalan, uwiano wa mapato kwa Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kwa kasi ndogo katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili kutoka 12.0% mwaka 2001/02 hadi 14.9% mwaka 2024/25.
Makamu wa Rais amelitaka Kongamano hilo kufanya tafakuri ya kina na kuainisha maboresho yanayohitajika kisera, kisheria, kikanuni na kiutaratibu ili kuwezesha uwekezaji na biashara na hivyo kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wa kikodi na ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Saada Mkuya amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa Sekta Binafsi katika uwekezaji na hivyo imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini kupitia utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini ili sekta binafsi iweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa.
Mhe. Mkuya ameongeza kwamba kupitia mpango huo, tozo na ada ambazo ni kero takribani 380 zimefutwa na baadhi zimepunguzwa. Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha uhimilivu wa viashiria vya uchumi jumla, kuwa na sera za kodi ambazo zinatabirika na kuainisha tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za udhibiti kwa lengo la kupunguza na kuimarisha usimamizi. Vilevile amesema mpango mwingine ni n matumizi ya TEHAMA ili kuweka urahisi wa kulipa kodi pamoja na kufanya biashara kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Angelina Ngalula amesema ni vema elimu sahihi kuendelea kutolewa kwa wafanyabiashara ili waweze kurasimisha biashara zao hali itakayopelekea waweze kupata faida za mikopo na ufadhili na hivyo serikali kuongeza wigo wa ukasanyaji kodi.
Ameongeza kwamba, jitihada lazima zifanyike kupitia vitengo vya utafiti vya Wizara kuhakikisha elimu inapatikana kwa wafanyabiashara ili kuondokana na idadi ndogo ya walipa kodi ambao ni milioni mbili waliopo hivi sasa. Na kupunguza gharama ya urasimishaji wa biashara ndogo ndogo
Kongamano
hilo linashirikisha viongozi wa Serikali, wadau mbalimbali wa sekta binafsi,
wafanyabiashara na wawekezaji. Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni “ Kuongeza
ukuzaji wa rasilimali za ndani kupitia kustawisha fursa za wananchi”
WAZAZI AMBAO HAWATIMIZI WAJIBU WAO KWA WATOTO KUCHUKULIWA HATUA
Serikali mkoani Mwanza imezindua mkakati wa kuhakikisha inawaondoa watoto wanaoishi katika mazingira magumu mkoani humo.
Akizungumza katika uzinduzi wa mkakati huo mkuu wa mkoa wa Mwanza Said Mtanda amesema miongoni mwa mikakati iliyopo ni serikali za mitaa kuhakikisha zinaweka utaratibu wa kuwatambua Watoto waliotoroka katika maeneo yao ikiwa ni Pamoja na wazazi ambao hawatimizi wajibu wao kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake msimamizi wa huduma za ustawi wa jamii mkoani Mwanza Baraka Makona amesema mkakati huo utatekelezwa katika halmashauri zote 8 za mkoa huu wa Mwanza.
Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa Day care lina Roman amesema jukumu walilonalo hivi sasa nikuhakikisha wanashirikiana na serikali kutokomeza suala hilo .
UTATUZI MIGOGORO KWA NJIA MBADALA WA MAHAKAMA UNAWEZEKANA-NCC
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Dk Fauz Twaib akizungumza wakati wa mafunzo ya kuhusu utatuzi migogoro kwa njia mbadala wa mahakama yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ambayo yamefanyika kwa siku tatu jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anayehusika na sehemu ya mikataba, majadiliano na utawala, Mkadiriaji Majenzi Elias Kisamo akijibu maswali tatizi yaliyoulizwa na washiriki wa mafunzo utatuzi migogoro kwa njia mbadala wa mahakama yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ambayo yamefanyika kwa siku tatu jijini Dar es salaam.
Mhandisi wa kujitegemea, Julius Mamiro akifundisha washiriki wa mafunzo mbinu ya utatuzi migogoro kwa njia mbadala wa mahakama ambayo yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ambayo yamefanyika kwa siku tatu jijini Dar es salaam.
Baadhi ya washiriki wa wa mafunzo ya kuhusu utatuzi migogoro kwa njia mbadala wa mahakama yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ambayo yamefanyika kwa siku tatu jijini Dar es salaam.
Picha ya pamoja wakufunzi na washiriki wa wa mafunzo ya kuhusu utatuzi migogoro kwa njia mbadala wa mahakama yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) ambayo yamefanyika kwa siku tatu jijini Dar es salaam.
........................
Na Mwandishi wetu
-Yaelimisha namna ya kuitatua bila kujeruhi upande wowote
BARAZA la Taifa la Ujenzi (NCC) limesema usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, madai ya kimkataba na mingine iliyopo na inayojitokeza kwenye sekta ya Ujenzi, unawezekana bila wahusika wa migogoro hiyo kupelekana mahakamani.
Hali hiyo, kwa mujibu wa wataalamu wa masuala hayo ya usuluhishi na utatuzi wa migogoro wanaotoa mafunzo kuhusu eneo hilo, chini ya uratibu wa NCC, inasaidia si tu kuokoa muda na kuacha wahusika wakiwa na amani, bali inapunguza mirundikano ya kesi mahakamani.
Akizingumza Dar es Salaam hivi karibuni wakati mafunzo hayo yaliyoandaliwa na NCC yakiendelea, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Dk Fauz Twaib ambaye ni miongoni mwa wafundisha njia hizo, alisema: "Kinachotakiwa ni wasuluhishi kuzingatia maadili, sheria na taratibu za usuluhishi".
Alisema njia zaidi ya nne za kusuluhisha migogoro mbali na kushitakiana mahakamani, zinafundishwa na kuwawezesha waliopata mafunzo hayo kuamua kwa weledi ipi inafaa kulingana na mazingira na hali halisi ya mgogoro husika.
Kwa mujibu wa Dk Twaib, Kwa kutumia njia hizo mbadala, hakuna upande unaojeruhiwa, kwa sababu pande zote zinahusika katika hatua zote muhimu za usuluhishi, ikiwemo kuchagua nani ahusike kuwasuluhisha.
"Ikiwa hakuna mazingira yoyote ya tamaa inayoweza kusababisha upendeleo, mfano rushwa au chochote kile kitakachofanya usuluhishi uegemee upande mmoja, mlolongo wa kisuluhishi hautokei, hivyo kuokoa muda na gharama.
Kwa upande wake, Mhandisi wa kujitegemea, Julius Mamiro anayefundisha mbinu hizo, hususan majadiliano ya kisuluhishi ya madai ya kimkataba ya ujenzi alisema, maadili mazuri yanafanikisha usuluhishi.
Alisema, jambo kubwa wanalolisisitiza ni wataalamu wa masuala yote yanayoweza kuhusika kwenye migogoro, iwe ya sekta ya ujenzi au ya kibiashara nje ya sekta ya ujenzi au ya kimkataba kwenye sekta yoyote, wawe na elimu ya namna ya kuitatua migogoro yao bila kupelekana mahakamani, kisha watekeleze mbinu walizofundishwa kwa kuzingatia maadili.
Kwa maelezo yake, kujua kusuluhisha au kutatua mgogoro halafu ukauharibu utatuzi kwa kutoruhusu haki au kwa kupendelea, hata kama umefunzwa vipi, unabaki kuwa kikwazo cha usuluhishi.
"NCC inatekeleza jukumu la kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watu wengi, kwa faida ya wanaoipata, wateja wao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
Alisema, kutokana na umuhimu huo, anawashauri Watanzania kuchangamkia mafunzo hayo pindi wanaoipata fursa hiyo nyakati zote yanapotangazwa.
Katika mafunzo hayo yaliyotolewa kwa siku tatu, washiriki walifanya mazoezi ya usuluhishi kwa vitendo na kisha kutahiniwa kwa mtihani wa kuandika, lengo likiwa kupima uelewa wao kuhusu maarifa waliyapata kwenye mafunzo hayo.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anayehusika na sehemu ya mikataba, majadiliano na utawala, Mkadiriaji Majenzi Elias Kisamo, pamoja na kufundisha, alijibu maswali tatizi yaliyoulizwa na washiriki wa mafunzo hayo, hivyo kuongeza uelewa wao juu ya walichojifunza.
Kisamo alisema," Ukitaka usuluhishi uende sawa, epuka njia za mkato. Hakuna shortcuts, iwe katika majadiliano au kwenye utatuzi mwingine, epuka 'shortcuts'...














Monday, April 14, 2025
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAZIDI KUJIIMARISHA KATIKA MIPANGO NA SERA.
...................
Na Sixmund Begashe - Singida
Wataalam wa Sera na Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii wameendelea na kikao kazi Mkoani Singida kwa lengo la kupata uwelewa wa pamoja wa namna bora zaidi ya utekelezaji wa mpango wa shughuli mbalimbali za Uhifadhi na Utalii kwa mwaka 2025/2026
Akizungumza kwenye kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Bw. Abdullah Mvungi licha ya kuwapongeza wataalam hao kwa michango mizuri, amewasisitiza kuendeleza umakini katika mapitio na maboresho ya mipango hiyo ili iweze kuleta tija zaidi kipindi cha utekelezaji wake.
Bw. Mvungi ameeleza kuwa, wataalam hao kutoka Idara na Taasisi mbalimbali za Wizara hiyo wamekuwa ni chachu kubwa ya Maendeleo endelevu ya Uhifadhi na sekta ya Utalii kutokana na umahiri wao katika sera na Mipango inayotekelezeka katika Wizara hiyo yenye mchango mkubwa katika pato la taifa.




