Mkuu wa wilaya ya Ubungo,Hassan Bomboko ameipongeza kampuni ya Magic Builders International Kwa kuwapa thamani Mafundi wa ujenzi hapa nchini Kwa kuwaunganisha pamoja kupitia sekta ya Michezo.
DC Bomboko aliyasema hayo Jijini Dar Es Salaam jana Julai 13,2024 katika mchezo wa fainali wa michuano ya White Scheme Mafundi Cup Mkoa wa Dar Es Salaam uliozikutanisha timu za mafundi za Vitukim FC na Dolphin FC katika uwanja wa Kinesi uliopo Sinza ambapo timu ya Dolphin FC ilitawazwa Mabingwa wa michuano hiyo Kwa mwaka 2024 baada ya kuicharaza timu ya Vitukum Mabao 2 kwa nunge.
Mkuu huyo wa wilaya alisema mafundi wamekuwa wakichukuliwa kama kada iliyokosa thamani lakini kupitia michuano ya Mafundi Cup,iliyodhaminiwa na kampuni ya Magic Builders wameiheshimisha sekta hiyo na kuiongezea thamani Jambo ambalo ni jema kwa Jamii.
"Kwanza niipongeze kampuni hii kwa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya Michezo kupitia mpira wa miguu,Kwa kuwaleta mafundi pamoja na kuwaandalia mashindano yao na kuwa Tanzania inakuwa nchi ya Kwanza kuendesha michuano ya mpira wa miguu kwa mafundi ujenzi kupitia kampuni yenu"alisema Bomboko.
Aidha DC Bomboko pia aliushukuru uongozi wa chama Cha mpira wa miguu wilaya ya Ubungo kwa kutoa ushirikiano wakati wote wa mashindano ya White Scheme Mafundi Cup 2024 mpaka Kufikia tamati hapo jana.
"Uwekezaji huu wa mpira wa miguu kupitia kada ya mafundi imeonyesha jitihada za kampuni ya Magic Builders International katika kukuza sekta ya Michezo kwa vijana ambao hawakupata fursa za kucheza kwenye timu Kubwa hivyo niwasihi wananchi muwaunge mkono kampuni hii Kwa kununua bidhaa zao "aliongeza DC Bomboko.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Magic Builders International,David Barongo alisema waliamua kuandaa michuano hiyo kama sehemu ya kurudisha kwa Jamii baada ya kupokelewa vyema Kwa bidhaa za kampuni hiyo na watanzania.
Alisema pia waliamua kuandaa mashindano yatakayowakutanisha mafundi wa ujenzi kwani mafundi hao wamekuwa hawapewi thamani inayostahili katika Jamii,hivyo wakaamua kuwaunganisha Kwa pamoja ikiwemo kuwapatia mafunzo na kuwaleta Kwa pamoja katika Michezo kwa kuandaa michuano ya White Scheme Mafundi Cup.
Barongo aliongeza kuwa wataendelea kuipa thamani kada ya mafundi hapa nchini kwani ni moja ya kada muhimu kwa Taifa.
White Scheme Mafundi Cup 2024 ilizikutanisha katika fainali timu Mbili zote kutoka Wilayani Kigamboni Jijini Dar Es Salaam ambapo Mabingwa wa Michuano hiyo Dolphin FC iliibuka mshindi na kupata zawadi ya Kombe pamoja na Shilingi za kitanzania milioni 5 huku mshindi wa pili ambayo ni Klabu ya Vitukim FC ikijishindia Kombe na zawadi ya Shilingi milioni 3 huku mshambuliaji wa timu hiyo Paul Mofid akinyakua Kiatu baada ya kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo kwa kupachika kambani magoli 6.
0 Comments