NA WILLIUM PAUL, SAME.
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika mwaka wa fedha 2023/24 imetoa zaidi ya shilingi milioni 247 kwa ajili ya kulipa fidia baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro walioathirika na uvamizi wa Wanyama wakali na waharibifu wakiwemo tembo.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kupokea vifaa vya kudhibiti wanyama hao pindi wanapovamia kwenye makazi ya wananchi vilivyotolewa na mashirika mawili yasiyo ya kiserikali ya OIKOS na WWF, (Shirika la uhifadhi wa mazingira na Wanyama pori) Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amesema fedha hizo ni sehemu ya madai ya wakazi hao ya muda mrefu baada ya kupisha Serikali kufanya tathmini ya uharibifu uliofanywa na wanyama hao.
“Kweli kumekuwa na migogoro baina ya baadhi ya wakazi wa Same na hawa Wanyama pori ambao wamekuwa wakitoka kwenye hifadhi na kuja kwenye makazi ya wananchi na kusababisha athari mbalimbali, hivyo tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutenga kiasi hicho cha fedha na kuweza kuwafuta machozi wakazi wa Same ambao wameathirika na hao wanyama waharibifu” alisema Kasilda.
Kwa upande wao wawakilishi wa mashirika hayo wamesema vifaa hivyo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita ya kukabiliana na adha wanayoipata wananchi ya kuvamiwa na wanyama pori katika maeneo yenye hifadhi ikiwemo Same ambayo imezungukwa na hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka kwa mamlaka husika na uhifadhi wa wanyama pori Wilayani Same zinasema kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita takribani watu kumi wamepoteza maisha kwa kushambuliwa na wanyama hao ikiwemo Tembo.
0 Comments