NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi ameendelea na ziara yake ambapo amefika Kata ya Mbokomu na kuongea na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi za Kata Eneo la Fukeni na kugawa miche bora ya migomba kwa wananchi.
Katika mkutano huo, Prof. Ndakidemi aliongozana na Diwani wa Kata ya Mbokomu, Rafael Materu, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhan Mahanyu, viongozi wa CCM na Serikali kutoka Kata ya Mbokomu, Mwakilishi wa TARURA Wilaya Mhandisi Mchanga na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa MUWSA, Flora Nguma.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Fukeni, Mbunge Ndakidemi aliuambia umati mkubwa uliohudhurua mkutano huo kuwa kata hiyo imepokea kiasi cha shilingi bilioni 1,256,890,864 kugharamia miradi ya maendeleo katika maeneo ya Afya, Kilimo, Maji, Barabara, Elimu na Maendeleo ya Jamii (Mikopo).
Mbunge aliishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kutenga fedha na kuwaletea wananchi wa Mbokomu Maendeleo.
Wakitoa kero zao, wananchi wengi waliopata fursa walionyesha kukerwa na ukosefu wa maji katika Kata ya Mbokomu na ubovu wa barabara.
Akijibu kero za wananchi, mwakilishi wa MUWSA , Flora Nguma alisema kwamba miundombinu ya maji iliharibiwa na mvua za vuli zilizonyesha kupita kiasi na kusababisha uharibifu mkubwa.
Alisema, MUWSA wameshanunua mabomba na utengenezaji utaanza hivi karibuni ambapo kero ya upatikanaji maji unaoikabili Kata ya Mbokomu itatatuliwa.
Mwakilishi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kutoka Wilaya ya Moshi Mhandisi Mchanga alisema kuwa wanatarajia kutatau changamoto za Miundombinu ya Barabara katika Kata ya Mbokomu kupitia bajeti ya mwaka 2024/25, na kila ikipatikana fursa watatenga fedha kuboresha miundombinu ya barabara katika kata hiyo.
Akiongea na wananchi katika mkutano huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu alimpongeza Mbunge na Diwani kwa jitihada zao kuitetea Kata ya Mbokomu na kuleta miradi ya maendeleo.
Aliwaomba wananchi waendelee kuiunga mkono Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwani kazi iliyofanyika Mbokomu ni kubwa na inaonekana.
0 Comments