NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amewataka Wakinamama kuachana na mikopo umiza (kausha damu) na badala yake watumie mikopo inayotolewa na Serikali kupitia asilimia kumi ya mapato ya ndani ya kila halmashauri.
Naibu Waziri Ummy ametoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kuzungumza na Viongozi wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Tarafa ya Mamba vunta, Gonja na Ndungu na badae kufanya mkutano wa hadhara kata ya Maore wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
Alisema kuwa, mikopo hiyo ambayo ni asilimia nne wanawake na vijana huku watu wenye ulemavu ni asilimia mbili ilikuwa imesimamishwa na serikali kwa ajili ya kuwekewa utaratibu mzuri ambapo kwa sasa itaanza kutolewa baada ya utaratibu wake kukamilika.
"Wakinamama tumekuwa tukiumizwa sana na hii mikopo umiza ambayo ni kausha damu ndoa zetu zimekuwa zikivunjika lakini tumekuwa tukikimbia familia sasa serikali imerejesha mikopo hivyo tuachane na mikopo umiza tuchukue hii ya serikali tujinufaishe" Alisema Naibu Waziri Ummy.
Aidha kiongozi huyo alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya miradi mikubwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Same na kuwataka kumuunga mkono.
Akiwa katika mkutano wa hadhara, Naibu Waziri Ummy amewahamasisha wananchi wakiwamo watu wenye ulemavu kushiriki kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kutumia haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi Bora watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Awali Diwani wa kata ya Maore, Issa Rashidi alisema kuwa, kata hiyo ilikuwa upinzani kwa miaka mitano lakini mwaka 2020 wananchi waliamua kufanya maamuzi na kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM ambapo ipo miradi mikubwa imetekelezwa.
Diwani huyo alisema kuwa, mbali na mafanikio yaliyopo katika kata hiyo lakini lipo tatizo la maji lakini wamepambana na kupata mradi wa maji wa Mbuta lakini hawaridhishwi na kasi ya ujenzi wa mradi huo na kuiomba serikali kumsukuma Mkandarasi wa mradi huo kukamilisha mapema ili wananchi waweze kuondokana na kero ya maji.
Aidha Diwani huyo alisema kuwa, mwaka 2023, Wanafunzi 500 waliohitimu darasa la saba walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ambapo kata hiyo inayo shule mbili za sekondari na kupelekea kuwa na nrundikano wa wanafunzi hivyo kata wanalo eneo ambalo wameiomba serikali kuwajengea shule nyingine ya sekondari katika eneo hilo ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani.
0 Comments