Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea kusimamia mkakati wake
maalum wa kuzuia vitendo vyote vya kihalifu katika jiji la Dar es Salaam. Tarehe 28 Juni
2024 lilimkamata na kumuhoji kwa kina Mussa Khamis Bakari @buda (30) wakala wa
Forodha, Mkazi wa Temeke kwa tuhuma za mauaji ya Abdallah Twahir Selemani
ambaye alikuwa rafiki yake na baada ya kumuua alifanikiwa kuiiba pesa za marehemu
Tsh Milioni 61 kutoka kwenye akaunti ya huyo rafiki yake.
Taarifa fupi za tukio ni kuwa tarehe 1 Mei, 2024 majira ya saa 10:20 asubuhi huko
maeneo Mbutu Kichangani, Kigamboni pembezoni mwa barabara itokayo Cheka
kuelekea beach ya Kichangani uliokotwa mwili wa mtu mmoja mwanaume akiwa
ameshafariki na baadae mwili huo ulitambuliwa kuwa ni Abdallah Twahir Selemani
mkazi wa Chanika.
Awali tarehe 4 Mei 2024 Jeshi la Polisi lilipokea taarifa ya kupotea kwa Abulllah Twahir
Selemani kutoka kwa mama yake kuwa alipotea katika mazingira ya kutatanisha. Uchunguzi wa Jeshi la Polisi baadae uligundua kuwa tarehe 30 Aprili 2024 mtuhumiwa
Mussa Khamis Bakari @buda alikuwa na marehemu wakitumia gari namba T.928 DFY
Suzuki Kei wakitokea Magomeni kuelekea Temeke, Kijichi mpaka eneo ulipokutwa mwili
wa marehemu. Uchunguzi wa vitu mbalimbali umebainisha mtuhumiwa alimuua na
baadae kwenda kutupa mwili huo pembezoni mwa barabara ulipookotwa.
Baada ya kumuua, mtuhumiwa alichukua kadi ya benki ya marehemu na kwa nyakati
tofauti tofauti alianza kutoa pesa kiasi cha shilingi Milioni 61 kutoka kwenye akaunti ya
marehemu. Chanzo cha mauaji ni tamaa ya kutaka kuiba pesa kutoka kwa rafiki yake
ambaye sasa ni marehemu. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.
Katika tukio lingine Jeshi la Polisi limefuatilia matukio ya unyan’ganyi na wizi wa pikipiki
katika Jiji la Dar es Salaam na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 23 na pikipiki 39
zilizoibwa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia mbinu ya kujifanya abiria na wakifika njiani
hujitokeza watu wengine ambao humtishia dereva kwa mapanga kumjeruhi na kumuibia
pikipiki hiyo, wakatii mwingine pikipiki zinazokuwa zimeegeshwa nje hutumia mbinu ya
kuunganisha waya, kuwasha na kuiba pikipiki hizo.
Ufuatiliaji wa Jeshil la Polisi umebaini watuhumiwa hao baada ya kuziiba pikipiki
wamekuwa wakiziuza kwa gharama nafuu mikoa mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Dodoma
na Singida.
Ufutiliaji huo umefakiwa kukamata risiti za kugushi 18 za kusafirishia pikipiki za wizi, kadi
11 za usajili wa pikipiki za kugushi, kadi (03) za usajili wa magari za kugushi, vyeti
mbalimbali vya kuzaliwa na kimoja cha ndoa vya kugushi, plate number (03) za pikipiki,
kitabu kimoja cha bima ya magari, nyaraka mbalimbali za TRA, barua mbalimbali zenye
nembo za jeshi la Polisi Tanzania, mihuri mbalimbali ya manispaa ya Kinondoni,Temeke,
IIala, Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, RITA, Mamlaka ya Bandari na mhuri mmoja wa
moto ulioandikwa "United Republic of Tanzania" wenye nembo ya bibi na bwana, leaf 56 za
kutengenezea kadi za vyombo vya moto, leaf 86 za kutengenezea vyeti vya vizazi na vifo
vyenye nembo ya msajili wa vizazi na vifo.
Wakati huo huo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linakanusha taarifa ya
sauti inayosambaaa kwenye mitandao ya kijamii ikielezea kuwepo kwa tukio la
mwanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kutekwa nyara maeneo ya kituo cha
kontena kilichopo ndani ya chuo hicho na watu wasiojulikana wakitumia usafiri wa bajaji
kisha kupelekwa Kimara na baadae kutelekezwa eneo la Masaki.
Jeshi la Polisi limefanya ufuatiliaji wa taarifa hiyo na kubaini kuwa ujumbe huo wa sauti ni
wa muda mrefu zaidi ya miaka mitano nyuma na uliwahi kusambazwa kama ulivyo na
ufuatiliaji wake ulifanyika ikabainika kuwa hazikuwa habari za kweli .
Polisi wamebaini pia tukio lililoelezwa kuwa kuna mtu aliuawa Sinza kisha kuondolewa ziwa
upande wa kushoto na sehemu za siri, hazikuwa habari za kweli na hakuna tukio la namna
hiyo kama linavyoelezwa.
Kuzusha taarifa za uongo zenye lengo la kujenga taharuki au hofu ni
makosa.Tunatahadharisha juu ya tabia hizo na Jeshi halitasita kuwatafuta na kuwahoji
wanaohusika kwa hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam pia katika kusimamia mifumo ya
kisheria ya haki jinai limeendelea kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa matukio
mbalimbali ya kihalifu na hatimaye kupatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu. Jeshi la
Polisi limekuwa likichukizwa sana na vitendo vya ubakaji na ulawiti na katika hatua hiyo
mwaka 2023 Juni, mshtakiwa Hussein Shomvi (50) fundi ujenzi, mkazi wa Chanika
Zogoali alikamatwa na baadae kufikishwa Mahakama ya Kinyerezi na baada ya
mashauri yake kusikilizwa tarehe 10 Juni 2024 alipatikana na hatia ya kosa kulawiti
watoto wawili wa kiume wa shule ya msingi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Washtakiwa wengine Shamim Hamadi @dj mush (30) Mkazi wa Kimara Mwisho, na
Waziri Ramadhani (26) Mkazi wa Mbezi Luis na Seif Salum (19) mkazi wa Manzese wote
kwa pamoja mwaka 2022 walifikishwa Mahakama ya Kinondoni mbele ya Hakimu Mkazi
Nabwike Mbaba na baada ya mashauri yao kusikilizwa terehe 10 Juni 2024 walipatikana
na hatia ya Unyangayi wa kutumia silaha na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. Jeshi
la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali, zitatunzwa na
wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Imetolewa na;
Muliro J. MULIRO - SACP
Kamanda Kanda Maalum ya Polisi
Dar es Salaam
0 Comments