Umoja wa Mataifa umepinga amri iliyotolewa na Israel Gaza kuwataka wakaazi wa eneo hilo kuondoka huku Jeshi la taifa hilo likiripotiwa kusababisha mauaji ya wapalestina 18 katika siku ya pili ya mashambulizi yao Gaza.
Israel imetanua onyo lake kwa maeneo mengine mengi ya Ukanda wa Gaza, ikitaka wakazi wa maeneo hayo kuondoka mara moja ili iendelee na operesheni yake ya kuwaangamiza wanamgambo wa Hamas.
Tangu tarehe 27 Juni, Israel imetoa amri tatu za Wapalestina kuondoka katika mji wa Gaza na katika eneo la kusini la mji huo. Tayari shirika la Umoja wa Mataifa limekadiria kuwa maelfu ya Wapalestina wameshautoroka mji.
Wakaazi waliobakia huko wameripoti kusikia milio ya makombora na ufyatulianaji risasi pamoja na kuona ndege za helikopta angani usiku kucha katika maeneo ya Kusini Magharibi mwa Gaza.
Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, imeshitushwa na amri ya Israel kutaka Wapalestina waondoke makwao ikisema tayari watu hao wamepoteza makaazi yao mara kadhaa kuelekea katika maeneo ambayo pia jeshi la Israel linaendelea kushambulia na raia pia kuendelea kuuwawa na kujeruhiwa.
Huduma za Dharura kwenye eneo hilo zimesema wanaamini kuwa watu kadhaa waliuawa katika maeneo ya mashariki mwa Gaza lakini hawakuweza kuwafikia watu hao kutokana na mashambulizi yanayoendelea huko Tel Al-Hawa, Sabra, Daraj, Rimal, na vitongoji vya Tuffah.
0 Comments