Header Ads Widget

Responsive Advertisement

WAFANYAKAZI STAMICO KWA PAMOJA WAUNGA MKONO MAGEUZI YA SHIRIKA KUELEKEA KUJITEGEMEA .

 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse amewataka Watumishi kuwa wabunifu na kufanya shughuli zao kwa tija ili kukuza uchumi wa Taifa hususan katika Mwaka wa Fedha 2024/25 ili kukuza uchumi  kupitia sekta ya madini.


Dkt. Mwasse amebainisha hayo leo Julai 19, 2024 katika kikao kazi cha Watumishi wa STAMICO kilicholenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti 2023/2024 na kuweka mikakati ya mafanikio kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 jijini Dodoma


Ametumia kikao hicho kuwashukuru wanastamico kwa kuwa sehemu  ya mageuzi haya sambamba  na kuwakaribisha wafanyakazi wapya huku akiwaasa kwenda na kasi ya mageuzi ya shirika. 


Akitoa wasilisho la Fikra za Kibiashara katika kuendesha Shirika Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Dkt. Erenest Mwaswaliba  amehimiza umuhimu wa kila mfanyakazi kubadilika na kuwa na fikra ya kijasiliamali wakati  huu ambapo Shirika linaenda kujitegemea.


Amesema ili mageuzi hayo yaweze kuleta tija kwa Shirika ni lazima kubadilisha utamaduni wa utendaji kazi   ambapo kila mfanyakazi  anatakiwa kuwa sehemu  ya mnyororo wa mabadiliko na mafanikio hayo bila kuweka  vipingimamizi .


Aidha, amesema kujitegemea kwa Shirika  kunahitaji  wafanyakazi waliokuwa huru, kufanya kazi kibiashara  na kuthamini wateja na wageni wote wanaokuja katika ofisi kuhitaji huduma.


Amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kushirikiana badala ya kutegeana na kuacha idara nyingine  ikiteketea kwa kigezo cha kutohusika na jukumu hilo, kwa kuwa ushirikiano  ni silaha kuelekea  mafanikio.


"Niwakumbushe  kuwa meli inapotoboka haiwezi kuleta madhara eneo moja bali yote hivyo kila mtu anatakiwa kushiriki  kutoa maji ili meli isizame." Ameasa Dkt. Mwaswalubi


Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Kuchimba Dhahabu  STAMIGOLD Bw. Ally Ally ameshukuru kwa Uhusiano  mzuri anaoupata kutoka STAMICO hususan kupitia biashara  ya kemikali na Vilipuzi, Kiwanda  cha kusafisha  Dhahabu na uongozi bora na kuahidi kuendelea  kufanya kazi bega kwa bega 


Naye, Afisa Uhusiano  Mkuu  Bw. Gabriel  Nderumaki amewakumbusha wafanyakazi  kuzingatia itifaki na adabu kazini ili kuleta uwajibikaji wa pamoja katika kutekeleza mageuzi.


Amehasisha wafanyakazi  kujiamini na kuachana na hofu za migogoro  kutakakosaidia kufanya maamuzi yenye tija kwa shirika yanayoendana na mageuzi.


Aidha, Mkurugezi wa Mipango  Dkt. Venance Kasiki  ametoa pongezi kwa uongozi wa STAMICO,  kuandaa kikao  na kutoa mafunzo  ya kubadilisha  fikra ili kuongeza uthubutu,  utunzaji wa muda na  kujali wateja 


STAMICO imefanya kikao maalum kwa wafanyakazi  wake ili kubadilisha fikra za utendaji kazi ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji wa mageuzi  ya kihistoria yaliyofanyika na kuweka mkakati wa pamoja kuelekea nchi ya ahadi yenye maziwa na asali kuanzia Mwaka 2024/2025.

Post a Comment

0 Comments