Mwezi Machi Ambani aliandaa karamu ya siku tatu ya kabla ya harusi ya mwanawe. Sherehe hiyo ilifanyika katika mji wa nyumbani wa familia hiyo wa Jamnagar katika jimbo la magharibi la Gujarat, ambalo pia ni eneo la kiwanda cha kusafisha mafuta cha Ambani – kiwanda kikubwa zaidi duniani.
Wageni wapatao 1,200 walihudhuria, akiwemo Mark Zuckerberg wa Meta na Bill Gates wa Microsoft.
Sherehe ilianza kwa chakula cha jioni katika jumba la kifakhari lililojengwa kwa ajili ya hafla hiyo. Muundo wa jumba hilo unafanana na Palm House, lililoko Brooklyn Botanic Garden, Marekani.
Sherehe hiyo ilifuatiwa na onyesho la Rihanna na video za mtandaoni zilionyesha familia ya Ambani ikijumuika na mwimbaji huyo jukwaani.
Wapishi mashuhuri walipika vyakula 2,000, vyenye asili ya nchi tofauti, wageni waliwekwa katika mahema ya kifahari, wakiwa na wapambaji na wanamitindo wakiwahudumia.
Pia kulikuwa na mwongozo wa kurasa 10 juu ya kanuni za mavazi kwa ajili ya matukio hayo, ambayo yalijumuisha mavazi kwa ajili ya kutembelea hifadhi ya wanyama inayomilikiwa na familia hiyo, ikifuatiwa na sherehe katika ukumbi mkubwa ambao ni sehemu ya makazi yao ya kifahari.
Bibi harusi mtarajiwa alivalia mavazi yaliyotengenezwa kwa hariri, vito na mavazi mengine ya gharama.
Bwana harusi alivalia mavazi ya Dolce & Gabbana na saa ya mkononi ya Richard Mille, yenye thamani ya takribani dola za kimarekani milioni 1.5m. Video ya mtandaoni ya Zuckerberg na mkewe Priscilla Chan wakitazama saa hiyo ilisambaa nchini India.
Magazeti na tovuti zilinasa utajiri na matukio haya ya kuvutia, yaliyohudhuriwa na watu wakubwa kutoka kote ulimwenguni.
0 Comments