Na Happiness Shayo - Morogoro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na filamu ya "Tanzania the Royal Tour" na uwepo wa Reli ya mwendokasi SGR, idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi imeongezeka kutoka 54,021 mwaka 2019/2020 mpaka kufikia watalii 138,844 mwaka 2023/2024 huku akiwataka wawekezaji na wananchi kuongeza nyumba za wageni.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara leo Agosti 4, 2024 katika eneo la Round About ya Mikumi Mkoani Morogoro.
Ameongeza kuwa kwa sababu Serikali inaenda kujenga miundombinu kuunganisha jimbo la Mikumi na majimbo mengine na Wilaya nyingine, wakazi wa eneo hilo wategemee wageni wengi na wageni hao wanahitaji sehemu za kulala.
Katika hatua nyingine Rais Samia amesema mipango ya Serikali ni kufungamanisha reli ya TAZARA na SGR kwa lengo la kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu na kuleta maendeleo zaidi.
0 Comments