Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imesema imeridhishwa na utendaji kazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kupitia mradi wa treni ya kisasa SGR ambapo umeleta matokeo chanya kwa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jason Rweikiza wakati walipotembelea ofisi za shirika hilo, amesema kwamba ushirikishwaji wa sekta binafsi ni muhimu sana kwani utaleta tija kwa TRC na kuinua uchumi wa Taifa.
Aidha, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza Mradi wa SGR kwani umeleta chachu ya kurahisisha usafiri.
"Tumeelezwa kuwa treni hii kwa safari moja inasafirisha abiria 900 kwa masaa matatu na dakika kidogo wanakuwa wamewasili Dodoma na kuendelea mashughuli zao za kijamii na kiuchumi, usafiri huu una bei nafuu" amesema Rweikiza
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema Serikali imeamua kushirikisha sekta binafsi kwenye mradi huo kutokana na Serikali kutekeleza miradi mingi ya gharama kubwa.
"Serikali ina miradi mingi inayotekeleza ya gharama kubwa, hivyo kushirikisha sekta binafsi itawezaesha kupunguza mzigo serikalini na kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati,mfano mzuri Reli ya TAZARA ambayo imeshirikisha sekta binafsi ambayo inapitisha mizigo yake kwa zaidi ya asilimia 70" amesema Kihenzile
Aidha ameongeza kuwa maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo, iliyojielekeza kuangalia masuala ya ulinzo na usalama katika reli hiyo wameyapokea nakuahidi kuyafanyia kazi ipasavyo.
Nae, Kaimu Mkurugenzi wa TRC Lameck Magandi amesema TRC ndiyo mara yake ya kwanza kuingia kwenye uendeshaji wa Reli hiyo kwa kushirikisha sekta binafsi, ili na wao washiriki katika uendeshaji wa Reli hiyo.
Hata hivyo, Magandi amesema kuwa tayari wadau mbalimbali wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye sekta ya reli, hivyo kinachosubiriwa ni ukamilishaji wa baadhi ya sheria ili mradi huo utakapokamilika sheria hizo ziwe tayari kuanza kutumia.
0 Comments