![]() |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Gerson Msigwa. |
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari na kujenga mazingira salama kwa waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha uhuru wa kujieleza unaimarika nchini.
Akizungumza leo Aprili 28, 2025 jijini Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari–MAELEZO, Gerson Msigwa, amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka msingi imara wa kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi kwa uhuru na bila bughudha.
"Ninawashukuru kwa mijadala yenu kuhusu Akili Mnemba; ni muhimu sana katika kazi za uandishi wa habari. Nimesikia kuhusu maazimio yenu na tutayafanyia kazi," amesema Msigwa.
Ameeleza kuwa serikali inatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani, kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa uhuru na waandishi wanalindwa dhidi ya bughudha.
Msigwa amebainisha kuwa serikali itaendelea kulinda haki za waandishi wa habari, kuimarisha uhuru wa kujieleza, na kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha sekta ya habari nchini.
"Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa hakuna mwandishi anayebughudhiwa na itaendelea kujenga mazingira bora zaidi ya kazi kwa waandishi wa habari," amesisitiza.
![]() |
Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo |
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo, ameeleza kuwa uhuru wa vyombo vya habari ni haki ya msingi na siyo hisani, akisisitiza kuwa kila mwananchi ana jukumu la kuutetea.
Melo amesema katika dunia ya sasa yenye wingi wa taarifa, akili mnemba ni silaha muhimu katika kulinda uhuru wa habari.
Ameongeza kuwa mageuzi ya teknolojia yamepanua uwanja wa habari kutoka kwa vyombo vya jadi hadi kwa watengeneza maudhui wa kidijitali, hivyo kila anayesambaza taarifa anapaswa kulindwa.
Hata hivyo, ametoa tahadhari kuhusu matumizi ya teknolojia mpya kama akili mnemba (AI), akieleza kuwa zinahitaji matumizi ya umakini mkubwa hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili kuepusha usambazaji wa taarifa potofu.
Katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Jamii Africa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, UNESCO na wadau wengine, viongozi wa kimataifa akiwemo Balozi wa Sweden na mwakilishi wa UNESCO wametoa wito wa kuimarisha uhuru wa habari na kuwalinda wanahabari dhidi ya vitisho vinavyochochewa na matumizi ya teknolojia mpya.
Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka 2025 yanaendelea jijini Arusha hadi Aprili 30, 2025, yakilenga kujadili mafanikio, changamoto, na njia bora za kuimarisha tasnia ya habari kwa maendeleo ya taifa.