Mjumbe wa bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ( TFRA), Dkt. Peter Shimo akiwa katika picha na watumishi wa TFRA mara baada kutembelea Banda la Mamlaka katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea jijini Dar es Salaam tarehe 5 Julai 2025.
Mjumbe wa Bodi ya TFRA, Dkt. Peter Shimo akipokea maelezo kutoka kwa mtafiti wa Kilimo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Mgaya Maumba alipotembelea banda hilo wakati wa maonesho ya 49 ya biashara ya Kimataifa (SABASABA) tarehe 5 Julai, 2025
.....................
Mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Peter Shimo, ameridhishwa na namna Mamlaka hiyo inavyotoa elimu kwa umma kuhusu mnyororo wa thamani wa mbolea kupitia Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika banda la TFRA tarehe 5 Julai 2025, Dkt. Shimo amepongeza ubunifu na ushirikiano mzuri kati ya TFRA na taasisi mbalimbali chini ya Wizara ya Kilimo katika kuwawezesha wakulima kuongeza tija kupitia huduma za ugani na upatikanaji wa mbolea kwa wakati.
"Ushirikiano huu ni muhimu sana katika kusambaza elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kanuni bora za kilimo kwa wakulima wetu," amesema Dkt. Shimo.
Ametoa wito kwa TFRA kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea hasa kipindi hiki tunapoelekea msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2025/2026, ili kuongeza uzalishaji kwa wakulima.
Aidha, ameitaka Mamlaka kuongeza juhudi za kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuimarisha uzalishaji wa mbolea nchini na kuhakikisha upatikanaji wake kwa wakati.
Awali, Meneja wa Uhusiano, Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TFRA, Bi. Matilda Kasanga, alisema wananchi wengi wamejitokeza kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa Mamlaka tangu kuanza kwa maonesho hayo.
"Wakulima kutoka ndani na nje ya nchi wanapata taarifa sahihi kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta ya mbolea na wanajiandikisha kwenye mfumo wa pembejeo za ruzuku ili kunufaika na huduma zitakazotolewa na serikali kupitia mfumo huo," ameeleza Bi. Kasanga.
Katika ziara hiyo, Dkt. Shimo pia ametembelea mabanda ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), na Agrami Afrika, na kujionea shughuli zinazotekelezwa na taasisi hizo katika kuendeleza kilimo nchini.
Akiwa kwenye mabanda hayo, Dkt.Shimo alisisiitiza suala la kukuza na kuendeleza ushirikiano na mahusiano mazuri baina ya taasisi za kilimo ili kumsaidia mkulima kuzalisha kwa tija na hivyo kuongeza kipato chake na taifa kwa ujumla.
0 comments:
Chapisha Maoni