JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Top Stories. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Top Stories. Onyesha machapisho yote

Jumatatu, 14 Aprili 2025

TPDC, ZPDC ZAENDELEA KUSHIRIKIANA UENDELEZAJI SEKTA YA GESI NCHINI

.................

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) mwezi Februari, 2022 liliingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Petroli Zanzibar (ZPDC) ambapo kupitia ushirikiano huo masuala mbalimbali yamekuwa yakifanyika kuiendeleza Sekta  ikiwemo kubadilishana ujuzi na utaalam.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 14, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Kwahani, Mhe. Khamis Yussuf Mussa Mkenge aliyeuliza ni lini Serikali  itainufaisha Zanzibar katika matumizi ya Nishati ya Gesi ili iweze kutumika katika magari.

"Mheshimiwa Spika katika ushirikiano huu suala la kupeleka gesi Zanzibar ni mojawapo ya agenda kuu. Pande zote mbili bado zinaangalia namna bora ya kufikisha gesi asilia Zanzibar ili iweze kupatikana kwa bei nafuu kwa watumiaji.". Amesema Mhe. Kapinga 

Jumamosi, 12 Aprili 2025

BALOZI NCHIMBI ASAINI KANUNI ZA MAADILI YA UCHAGUZI MKUU 2025

******

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameshiriki katika utiaji saini wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025. Shughuli hiyo imefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ikitanguliwa na mjadala wa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa vyote vyenye usajili wa kudumu, waliohudhuria na kuridhia kanuni hizo, leo Jumamosi, tarehe 12 Aprili 2025.







 

Ijumaa, 11 Aprili 2025

KAPINGA ASEMA KIPAUMBELE CHA SERIKALI NI KUFIKISHA UMEME KWENYE TAASISI ZOTE


.............................

📌 Taasisi 1,272 zaunganishwa na umeme  Lindi

📌  Maeneo ya pembezoni mwa miji kuendelea kuguswa na miradi ya umeme

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha Taasisi zote zinazotoa huduma za kijamii, kiuchumi na kidini zinafikiwa na nishati ya umeme wakati wa utekelezaji wa miradi ya umeme Vijijini.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 11, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Maimuna Pathan aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha kupeleka umeme kwenye Shule na Taasisi zote zikiwepo za dini katika Mkoa wa Lindi.

"Hadi kufikia mwezi Machi 2025, jumla ya Taasisi  1,272 zimeunganishiwa umeme katika Mkoa wa Lindi zikijumuisha: Zahanati 259; Vituo vya Afya 42; Hospitali 9; Shule za Msingi 554; Shule za Sekondari 151; na Taasisi za Dini 257 (Misikiti 142 na Makanisa 115). ". Amesema Mhe. Kapinga

Ameeleza kuwa, kupitia miradi inayoendelea kutekelezwa na kusimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Taasisi 27 zinatarajiwa kupatiwa umeme mkoani humo.. 

Akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga aliyeuliza kuhusu Makanisa na Misikiti Mbogwe kutokuwa na umeme na mpango gani Serikali inao kuzipelekea Taasisi hizo umeme, Mhe. Kapinga amesema Taasisi hizo zitafikiwa na huduma ya umeme kupitia miradi ya Vitongoji inayoendelea katika Jimbo la Mbogwe, 

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Dkt. Christina Mzava kwa niaba ya Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo aliyetaka kujua ni ipi kauli ya Serikali juu ya Kata ambazo hazijaunganishiwa umeme Kahama na Shinyanga, Mhe. Kapinga amesema Serikali ina mikakati ya kuweka miradi ya umeme pembezoni mwa miji ili wananchi waunganishiwe umeme kwa bei rahisi.

Awali, akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo juu ya lini vijiji 42 vilivyobaki vya Wilaya ya Kishapu vitapatiwa umeme, Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Kishapu lina jumla ya vijiji 117 ambapo hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2025 vijiji vyote 117 sawa na asilimia 100 vilikuwa vimekwisha unganishwa na huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Serikali.

Akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara aliyetaka kufahamu wananchi wa Nywamwaga, Sirari na Nyamongo ni lini wataanza kuunganisha umeme kwa bei ya shilingi elfu 27, Mhe. Kapinga amesema maeneo ya Vijijini yanaunganishwa na umeme kwa shilingi elfu 27 na kwa yale ya pembezoni ipo miradi mingine ya pembezoni mwa mji.

 

Alhamisi, 10 Aprili 2025

NCC YAFUNZA MBINU KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI


  

..........................

Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa sekta ya ujenzi nchini kwa kutoa mafunzo yatakayowawezesha kutekeleza miradi kwa ufanisi, kupunguza gharama zisizotarajiwa, na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa.

Kupitia mafunzo hayo, NCC imelenga kuwajengea uwezo waajiri, wakandarasi na washauri elekezi kusimamia mabadiliko ya kazi, madai na migogoro kwa njia inayozuia upotevu wa muda, fedha, na rasilimali nyingine hali inayopunguza gharama kwenye miradi ya ujenzi.

Kwa mujibu wa wataalamu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), miradi ya ujenzi huathiriwa na mabadiliko ya kazi, ucheleweshaji wa kushughulikia madai, na migogoro, ambavyo kwa pamoja husababisha ongezeko la gharama, muda wa mradi na hata kushusha viwango vya ubora.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Mhandisi Tumaini Lemunge kutoka NCC amesema, lengo lao ni kuona miradi ya ujenzi inatekelezwa kwa gharama zilizopangwa na kwa ubora unaokubalika.

“Kupitia mafunzo haya, washiriki wamepata mbinu za kupunguza mabadiliko yasiyo ya lazima, kushughulikia madai mapema, na kutatua migogoro kwa mujibu wa mikataba” amesema Mhandisi Tumaini

Aidha Wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi waliopata nafasi ya kushiriki wameeleza namna mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhandisi Lyda Osena kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema “Mafunzo haya yameniongezea uwezo wa kutambua, kuepusha na kusimamia migogoro na madai kwa njia ya kisheria, vilevile yatanisaidia kutekeleza miradi kwa ufanisi zaidi, ndani ya muda, bajeti na ubora uliokusudiwa.”

Mkadiriaji Majenzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi amesema kuwa amepata  uelewa mpya kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mikataba ya ujenzi hivyo anafahamu kuwa mabadiliko hayawezi kuepukwa lakini yanahitaji usimamizi makini ili kuepusha gharama zisizokuwa za lazima.

Kwa upande wake, Mwanasheria Elizabeth Kimako kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) amesema, Mwanasheria anaposhiriki katika mchakato wa ujenzi anatakiwa kuelewa kwa kina masuala ya kimkataba.

Amesema kuwa mafunzo hayo yamempa uelewa wa kusaidia taasisi yake kuendesha miradi mbalimbali kwa kwa ufanisi mzuri.

Jumatano, 9 Aprili 2025

FISI WAHARIBIFU WAZIDI KUDHIBITIWA, SIMIYU NA KONGWA.


..….....

Na Sixmund Begashe - Dodoma

Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuongeza jitihada zaidi za kukabiliana na Wanyamapori wakali na waharibifu hususani Fisi katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na usalama.

Akizungumzia jitihada hizo Jijini Dodoma, Mkurugenzi Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACC) Fidelis Kapalata, amesema Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi tangu imeunda kikosi kazi maalum cha kupambana na Wanyamapori wanaoleta usumbufu kwenye makazi ya watu, imesaidia kutatua changamoto hiyo hususani Mkoani Simiyu.

SACC. Kapalata amesema kuwa, katika kikosi kazi hicho chenye Askari wa Uhifadhi 27 kwa kushirikiana na serikali za Halmashauri za Wilaya katika Mkoa huo pamoja na wananchi, wameweza kudhibiti Fisi zaidi ya 25 ambao walikuwa kero kubwa kwa wananchi.

"Napenda kutoa shukrani na pongezi kwa askari wetu waliopo uwandani, wananchi na Serikali za Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu, kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika kuwakabili Wanyamapori hao waharibifu, niendele kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana askari wetu katika zoezi hili, ili tuweze kufikia malengo yanayokusudiwa". Amesema SACC. Kapalata

Aidha, SACC. Kapalata amesema kuwa hivi karibu kumeripotiwa uwepo na Fisi waharibifu katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, ambapo tayari Wizara imeshachukuwa hatua ya kupeleka kikosi kazi cha askari wake ambao wamesha weka kambi na kazi ya kuwasaka Fisi hao imeshaanza.

"Kuhusu taarifa ya uwepo wa Fisi hatarishi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Wilayani Kongwa, tumesha peleka askari wetu na tayari wameshaanza kazi ya kuwasaka Fisi hao ni imani yetu tutaitokomeza changamoto hiyo kwa mafanikio makubwa kama ilivyokuwa katika Mkoa wa Simiyu". Aliongeza SACC. Kapalata.

Ikumbukwe kuwa, uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii umeendelea kuunga mkono jitihata za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama bila kubughudhiwa na Wanyamapori wakali na waharibifu, kwa kuchukuwa hatua mbalimbali hususan za matumizi ya teknolojia ya kisasa, kuunda kikosi kazi maalum kutoka kwa askari wa Taasisi zote zinazounda Jeshi la Uhifadhi, kuongeza vitendwa kazi, kuelimisha umma, kushiriana na wananchi pamoja na uongozi wa maeneo husika.

Jumanne, 8 Aprili 2025

MIRADI YA UTALII KULETA MAGEUZI



***********

Na Mwandishi wetu - Singida

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuimarisha Sekta ya Utalii, kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuchechemua ongezeko la watalii na kukuza pato la Taifa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Utalii (TDL).

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao kazi cha viongozi wa Taasisi za Wizara hiyo zinazotekeleza miradi kupitia mfuko huo, Mkoani Singida, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Abdullah Mvungi amesema kikao hicho kimelenga kupata uelewa wa pamoja wa uboreshaji wa mipango na mikakati ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati inayolenga kutoa matokeo chanya kwa jamii.

Bw. Mvungi amesema kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa vitendo kukuza utalii kupitia Mfuko huo hivyo ni vyema kwa Viongozi wa Taasisi zinazotekeleza miradi kupitia Mfuko huo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi itakayotekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.

Aidha, Bw. Mvungi ameongeza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo umelenga kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wale wa nje, kuongeza mapato ya fedha za ndani na za kigeni, kuongeza ajira pamoja na kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia Sekta ya Utalii.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. John Mapepele ameeleza kuwa Wizara itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya mafanikio yanayopatikana katika miradi.

ULEGA: UJENZI WA DHARURA WA MADARAJA HAUTAATHIRI MIPANGO YA KUDUMU


........................

Serikali imefafanua kwamba kazi ya ujenzi wa madaraja matano kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam - Lindi zilikuwa zinaendelea na haitaathiriwa na juhudi za sasa za kukarabati maeneo yaliyoharibiwa na mafuriko ya mvua katika siku za karibuni. 

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, katika eneo la Somanga na Matandu mkoani Lindi ambapo anasimamia ukarabati wa dharura wa barabara iliyoharibiwa na mvua. 

Ulega alitumia fursa hiyo kutangaza pia kwamba serikali tayari imetenga fedha kwa ajili qpya ujenzi wa madaraja ya kudumu na ni kazi endelevu hadi itakapokamilika.

“Tutambue kuwa ujenzi wa madaraja sio suala la wakati mmoja ni la hatua kwa hatua. Niwatoe hofu Watanzania kwamba toka ilipotokea dharura mwaka jana ya kukatika maeneo hayo Serikali imechukua hatua madhubuti na kila mahali yupo Mkandarasi anafanya wajibu wake”, amesisitiza Ulega.

Aidha, Ulega amewahakikishia Watanzania kuwa huduma za usafiri na usafirishaji kwa mikoa ya kusini zimerejea  tangu alfajiri na zinaendelea kuimarika ambapo magari madogo, mabasi ya abiria na magari makubwa ya mizigo  yanaendelea kupita katika eneo la Somanga na Matandu ili wananchi waweze kuendelea na safari.

Hatahivyo, Ulega ametoa wito kwa wananchi waliosimama  kituo cha Mabasi yaendayo Mikoa ya Kusini cha Mbagala kutokana na hofu ya kushindwa kuvuka katika eneo la Somanga - Mtama kuendelea na safari kwani eneo hilo sasa ni salama  na linapitika.

Ulega amewashukuru wananchi wote waliokumbwa na changamoto hiyo kwa uvumilivu na subira pamoja na kuwapongeza Wakandarasi  na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kushiriki zoezi hilo usiku na mchana ili kuhakikisha mawasiliano yanarajea.


KAPINGA ASEMA KAZI YA KUPELEKA UMEME KWENYE MIGODI MIDOGO INAENDELEA


..........................

📌 Wachimbaji wa chumvi pia wafikiwa

📌 Wananchi Kibiti wampongeza Rais Samia kwa mradi wa umeme wa zaidi ya shilingi Bilioni 3.8.

📌 Kituo cha umeme Uhuru wilayani Urambo chakamilika

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi midogo yakiwemo maeneo yanayozalisha chumvi wilayani Bagamoyo.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 08, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Bagamoyo, Mhe. Muharami Shabani Mkenge aliyeuliza ni lini Serikali itapeleka umeme katika eneo la Kitame Kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo ili kuwasaidia wazalishaji wa chumvi.

"Hadi kufikia mwezi Machi 2025, jumla ya maeneo 14 ya migodi midogo imepelekewa umeme ambapo kati ya hayo, maeneo 3 ni ya wachimbaji wa chumvi wanaopatikana katika eneo la Kitame Kata ya Makurunge ambapo jumla ya wachimbaji 34 wanaopatikana katika maeneo hayo wamefikiwa na huduma ya umeme". Amesema Mhe. Kapinga

Ameeleza kuwa, kazi ya kupeleka umeme kwa wachimbaji wa chumvi waliosalia itaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.

Ameongeza kuwa,  upo mradi mwingine ambao unapeleka umeme kwenye pampu za maji takribani 411 na kwenye maeneo ya kilimo na maeneo ya migodi 605.

Akijibu swali Mbunge wa Kibiti, Mhe. Twaha Mpembenwe aliyeuliza kuhusu mkakati wa Serikali kupeleka umeme kwenye Kitongoji cha Kitame ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa nishati hiyo, Mhe. Kapinga amesema katika eneo hilo Serikali inatekeleza miradi ya umeme ya Vitongoji.

Katika hatua nyingine Mhe. Mpembenwe kwa niaba ya wananchi wa Kibiti amemuomba Mhe. Judith Kapinga kufikisha pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi ya umeme ya zaidi ya shilingi Bilioni 3.8 katika  Jimbo la Kibiti.

Mhe. Kapinga  kwa upande wake, amesema Serikali inapokea pongezi za wananchi hao wa Kibiti kwa Mhe. Rais kutokana na kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya nishati ambayo inasimamiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko.

Akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Mhe. Margreth Sitta aliyeuliza ni lini Serikali itakizindua kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Uhuru kilichopo Urambo Tabora baada ya kukamilika, Mhe. Kapinga amesema kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Uhuru kimekamilika Machi 26, 2025 na wananchi wa Urambo, Kaliua na maeneo jirani wananufaika kupitia kituo hicho cha umeme.

Akijibu swali la Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakar Asenga aliyetaka kufahamu ni lini mkakati wa kuvipelekea umeme Vitongoji 15 kwa kila Mbunge utaanza jimbo la Kilombero, Mhe. Kapinga amesema tayari Serikali imeshampata Mkandarasi wa kupeleka umeme katika Jimbo hilo na ameshaanza kazi katika baadhi ya maeneo na Serikali itaendelea kumsimamia ili aongeze kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

RAIS MWINYI AWAKARIBISHA WAFANYABIASHARA WA UINGEREZA KUWEKEZA ZANZIBAR

........................

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha Wawekezaji kutoka Uingereza kuwekeza  Zanzibar katika fursa mbalimbali ikiwemo sekta ya Uchumi wa buluu, utalii,  usafiri wa baharini,  uvuvi , nishati na miundombinu ya kidijitali.


Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipojumuika kwenye chakula cha jioni na Wakurugenzi wa Taasisi mbalimbali za biashara na uchumi za Uingereza kilichoandaliwa na Taasisi ya Eastern Africa Association ya Uingereza katika Jiji la London, tarehe 7 Aprili 2025.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema katika kipindi cha Miaka 4 Uchumi wa Zanzibar unaendelea kukua zaidi  ya asilimia 7 kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta mbalimbali.

Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa  wawekezaji hao  kuwekeza katika zao la Mwani, ameeleza kuwa Zanzibar ndio  mzalishaji namba moja wa zao hilo Afrika ambalo soko lake linaendelea kukua zaidi.


 

MAWASILIANO SOMANGA- MTAMA YAANZA KUREJEA ABIRIA WASHUKURU


......................

Mawasiliano ya Barabara Somanga - Mtama yameanza kurejea kwa hatua katika barabara iendayo mikoa ya Kusini tangu leo alfajiri  baada ya wataalamu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana kurekebisha eneo la Somanga na Matandu lililoharibiwa na mvua na kufanya njia isipitike.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ambaye ameweka kambi katika eneo hilo tangu jana, amewaambia waandishi wa habari kwamba magari madogo 230, mabasi 10 na baadhi ya malori 30 yaliyobeba bidhaa mbalimbali ikiwemo mawe makubwa yamefanikiwa kuruhusiwa kupita katika eneo la Somanga Mtama na Matandu kuanzia leo kati ya saa 11:30 alfajiri hadi saa 12:00 asubuhi.

Ulega ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa ya awali akiwa mkoani Lindi wakati akiendelea kusimamia zoezi la urejeshaji wa maeneo yaliyokatika katika barabara kuu ya Dar es Salaam - Lindi linaofanywa na Timu ya  Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kushirikiana na Mkandarasi.

Baadhi ya abiria waliolazimika kusubiri usafiri usiku kucha wamezungumza na waandishi wa habari na kutoa shukrani kwa wataalamu waliofanikisha kazi hiyo kwa kufanya kazi usiku kucha.

“Tunaishukuru sana serikali hasa wataalamu wake na mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ambaye tumeshinda naye hapa kutwa nzima mpaka jioni na akatuahidi leo tutaondoka na neno lake limetimia,” alisema Shaaban Matwanga mkazi wa Lindi ambaye ameondoka kwenda Dar es Salaam leo.

Katika maelezo yake, Ulega alisema matengenezo zaidi katika maeneo ya Somanga Mtama na Matandu yanaendelea kuimarishwa kwa kuendelea kuwekwa mawe makubwa ili kuruhusu na magari mengine yaliyobakia kupita.

Ulega amewahakikishia Watanzania kuwa serikali ipo kazini usiku na mchana katika kuhakikisha miundombinu ya barabara hiyo inaimarishwa ili isiwe kikwazo kwa wasafiri.

MSD YAPELEKA MASHINE AKILI MNEMBA JKCI

.......................

Bohari ya Dawa (MSD), imenunua na kupeleka mashine za kisasa zenye Tekinolojia ya akili mnemba kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ili  kuiwezesha taasisi hiyo kutoa huduma za kisasa.

Mashine hizo ambazo baadhi tayari zimefungwa zinatarajia  kuanza kutoa huduma muda wowote kuanzia sasa.

Akizungumza baada ya kupokea mashine hizo   Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge ameipongeza MSD kwa juhudi zake za kuhakikisha huduma za moyo zinakuwa za kisasa kwenye hospitali hiyo. “

Dkt. Kisenge ameishukuru  MSD kwa kuleta mashine hizi ambazo zitasaidia kutoa huduma za moyo kwa ufanisi kwani mashine hizi zinauwezo wa kupiga picha sahihi kwa ajili ya matibabu lakini pia mashine hizi zinauwezo wa kutafsiri taarifa mbalimbali zenyewe kwa kutumia  tekinolojia za kisasa.

Kwa upande mwingine Dkt. Kisenge, ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa juhudi zake za kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa vya kisasa vya afya kwa haraka, jambo linaloimarisha huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo. "Tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na MSD katika kuhakikisha dawa na vifaa vya kisasa vinapatikana kwa haraka na kwa ufanisi," alisema Dkt. Kisenge. 

Amesema kuwa kwa sasa, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inahudumia zaidi ya wagonjwa elfu moja, na zaidi ya asilimia 95 ya wagonjwa hao  wanapata vipimo na matibabu kwa kutumia vifaa vya kisasa ambavyo MSD imevinunua na kuvisambaza. Vifaa hivi vikiwemo mashine za kisasa za ECG (Electrocardiogram),  na vifaa vya upasuaji wa moyo vinavyowezesha kutoa matibabu bora na ya haraka.

Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Bi. Betia Kaema amesema JKCI ni moja ya hospitali maalumu hivyo wanahakikisha huduma wanazowapa zinakuwa na ubora  wa hali ya juu na kwa haraka kuanzia pale wanapopokea maombi yao, kuwa na vikao endelevu na vya mara kwa mara ili  kuhakikisha huduma zinakuwepo muda wote na changamoto zote zinatatuliwa kwa wakati.

Vifaa hivyo ambavyo vimekabidhiwa vinagharimu jumla ya shilingi milioni 800

KIKWETE AWASILISHA UJUMBE MAALUM WA RAIS SAMIA KWA RAIS WA UGANDA


...............

Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amewasilisha Ujumbe Maalum wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Rais wa Jamhuri ya  Uganda, Mhe. Yoweri Museveni na kufanya naye mazungumzo kwenye Viwanja vya Ikulu ya Uganda. 

Akiwasilisha ujumbe huo, Mhe. Kikwete ameelezea  uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Uganda, na dhamira ya Mhe. Rais Samia ya kuimarisha zaidi ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.  

Kwa upande wake, Rais Museveni amepongeza uongozi thabiti wa Mhe. Rais Samia, si tu ndani ya Tanzania bali pia katika Bara la Afrika kwa ujumla. 

Ameeleza furaha yake kwa kumkaribisha Rais Mstaafu wa Tanzania katika Ikulu ya Uganda na kusisitiza kuwa Tanzania ni mfano bora wa uongozi wenye utulivu na demokrasia imara barani Afrika.

Jumatatu, 7 Aprili 2025

Watu 249 wachunguzwa na kutibiwa moyo Zanzibar


................

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

07/04/2025 Watu 249 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku nne katika uwanja wa Amaani uliopo Zanzibar.

Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aika Nnkya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi hiyo ya upimaji na matibabu ya moyo.

 

Dkt. Aika alisema kati ya watu 249 waliowafanyia uchunguzi watu 199 walikutwa na matatizo ya moyo hii ni sawa na asilimia 80 ya watu wote waliowaona ambapo watu 77 sawa na asilimia 31 hawakuwa wanajijua kuwa na matatizo ya moyo.

 

“Wagonjwa 22 ambao tumewakuta na matatizo ya moyo ya kuziba kwa mishipa ya damu, mfumo wa umeme wa moyo na valvu tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu ili tuwafanyie uchunguzi zaidi”.

“Ninatoa wito kwa wananchi zinapotokea nafasi za upimaji kama hizo wajitokeze  kwa wingi kupima afya zao kwa mfano katika kambi hii watu waliokutwa na matatizo  wametibiwa na kupewa dawa za kutumia mwezi mmoja bila malipo yoyote yale” alisema Dkt. Aika.

Kwa upande wake mratibu  wa kambi hiyo ya matibabu daktari bingwa wa moyo kutoka  hospitali ya Rufaa Lumumba Khamis Mustafa alishukuru kuwepo kwa kambi hiyo na kusema kuwa imesogeza kwa karibu huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.

“Ninazishukuru sana Idara za Habari maelezo kwa kuja na wazo hili katika mkutano wao kuwepo na huduma ya upimaji na matibabu kwa wananchi kwani wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) , Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wametoa huduma za matibabu ya magonjwa  mbalimbali”.

“Ninaomba kambi hii ya matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali ambayo inahusisha hospitali hizi kubwa tatu iwe endelevu kwani inawasaidia wananchi kupata huduma za matibabu ya kibingwa kwa wakati na bila gharama yoyote ile tofauti na ambavyo wangezifuata Dar es Salaam”, alisema Dkt. Ndiz.

Nao wananchi waliopata matibabu katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma walizozipata na kusema kuwa zimwewasaidia kufahamu hali za afya ya miili yao na wengine kupata matibabu kutokana na matatizo waliyokuwa nayo.

“Ninaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutuletea wataalamu hawa mimi nilikuwa nikilala moyo wangu unakwenda kasi sana baada ya kufanyiwa uchunguzi nimeambiwa moyo wangu unashida kidogo nimepewa dawa za kwenda kutumia”, alishukuru Halima Shaaban mkazi wa Mwera.

“Baada ya kusikia kuna huduma za matibabu nilikuja hapa kutibiwa kwani mimi ninatatizo la mgongo na presha , nimefanyiwa vipimo na kupewa dawa za kwenda kutumia ninashukuru sana na ninawaomba wananchi wenzangu wachangamkie fursa hii ya matibabu pindi inapotokea”, alisema Juma Abdala mkazi wa Makunduchi.

Huduma hiyo ya matibabu ilitolewa kwa wananchi za Zanzibar na washiriki wa kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kilichoandaliwa na Idara za Habari – Maelezo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mwisho


 

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI KUMBUKIZI YA MIAKA 53 YA KIFO CHA HAYATI KARUME


..................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameungana na Viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi katika Dua na  Kumbukizi ya Miaka 53 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hayati Sheikh Abeid Amani Karume iliyofanyika Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui Zanzibar leo tarehe 07 Aprili 2025.

Kumbukizi hiyo imeongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Zungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid, Marais Wastaafu wa Zanzibar Mhe. Ali Mohamed Shein na Mhe. Amani Abeid Karume, Mjane wa Hayati Abeid Karume Mama Fatma Karume pamoja na familia ya hayati Karume.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM - Bara Mhe. Stephen Wasira, Viongozi, Wanachama na Wazee wa Chama cha Mapinduzi Viongozi wa Mahakama, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Dini mbalimbali.

Listen Mkisi Radio