JSON Variables

Showing posts with label Top Stories. Show all posts
Showing posts with label Top Stories. Show all posts

Friday, May 9, 2025

KAPINGA AZINDUA KITUO MAMA CHA GESI ASILIA ILIYOSHINDILIWA (CNG) JIJINI DAR ES SALAAM

.............................

Ni cha Pili kwa ukubwa barani Afrika; Cha Kwanza kwa ukubwa EAC

 Kujaza Gesi Asilia kwenye magari 1200 kwa siku

 Ampongeza Dkt. Samia kutatua changamoto za wananchi kwa vitendo

Aipongeza TPDC; Ataka Vituo vya CNG kuendelea kujengwa

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amezindua Kituo Mama cha Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG) ambacho kina uwezo wa kujaza Gesi Asilia kwenye magari 1200 kwa siku huku kikifanya kazi kwa muda wa saa 24. 

Kapinga amezindua kituo hicho tarehe 9 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambapo uzinduzi huo ulienda sambamba na uzinduzi wa basi la mfano la Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ambalo litaendeshwa kwa kutumia nishati ya Gesi Asilia.

Akizungumza na halaiki iliyohudhuria hafla hiyo, Kapinga amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono, mtazamo na maelekezo yake kwa Wizara ya Nishati ambayo yanaleta matokeo chanya kielelezo mojawapo kikiwa ni uzinduzi kwa kituo hicho cha CNG.

Pia, amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa uongozi wake ambao unapelekea upatikanaji wa nishati ya uhakika ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya za wananchi.

“ Hapo nyuma kumekuwa na malalamiko ya uwepo wa foleni kubwa za ujazaji wa gesi kwenye vyombo vya moto katika vituo vya CNG ikiwemo kituo cha Ubungo Maziwa, lakini uwepo wa kituo hiki unaonyesha jinsi Serikali inavyotekeleza kwa vitendo ahadi inazotoa kwa wananchi za kupunguza kero ya upatikanaji wa CNG, nampongeza Rais Samia kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi na pia naipongeza Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa hatua hii.” Amesema Kapinga

Ameeleza kuwa, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kujaza Gesi kwenye magari nane kwa wakati mmoja, kuchochea ongezeko la vituo vingine vya CNG na kuwapatia huduma ya gesi watumiaji wengine kama viwanda, shule, hoteli n.k

Kapinga ameiagiza TPDC kuhakikisha kuwa, kituo hicho kinakuwa mfano wa kutoa huduma bora na za viwango kwa wateja huku kikizingatia masuala ya usalama na utunzaji wa mazingira.

Pia ameiagiza TPDC kuendelea kujenga vituo vya CNG katika maeneo mengine ya nchi ikiwemo Lindi na Mtwara, pia kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi ili kuendelea kuchochea uwekezaji kwenye sekta ya CNG. 

Naibu Waziri Kapinga pia ameishukuru Sekta binafsi kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya CNG.

Aidha, amewaasa Watanzania kuchangamkia fursa ya kuweka mifumo ya matumizi ya gesi kwenye magari yao kwani mifumo hiyo haiharibu magari hayo na pia watapata nafuu ya gharama za uendeshaji. 

Kuhusu kampuni ya UDART ambayo kwa mara ya kwanza imezindua basi jipya linalotumia Gesi Asilia, ikiwa ni moja ya mabasi mengi yakayotumia gesi hiyo, Kapinga amesema kuwa ushirikiano kati ya TPDC na UDART utaendelea kuchochea uwekezaji kwenye CNG na kuendelea kuboresha huduma za usafiri jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameipongeza wizara ya Nishati kwa kazi kubwa inayofanyika ili kupata matokeo makubwa kwenye sekta na kuahidi ulinzi katika miundombinu hiyo ambayo ni muhimu katika kutoa huduma kwa wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Kilumbe Ng’enda amesema Bunge limeridhishwa na hatua zinazochukuliwa kwa kasi na Serikali katika kuendeleza Sekta ya Gesi akieleza kuwa unapotumia gesi asilia kuendesha gari unapata unafuu kwa asilimia 40 ukilinganisha na mafuta. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameipongeza Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa kutekeleza mradi huo kwa mafanikio, pia ameipongeza UDART ambao watakuwa wateja wakubwa wa CNG.

Amesema mradi huo ni wa kujivunia kwani kituo hicho kilichozinduliwa ni cha Pili kwa ukubwa barani Afrika na cha kwanza kwa ukubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki

Mwenyekiti Bodi TPDC, Mhe. Balozi Ombeni Sefue amesema Bodi na Menejimenti ya Taasisi hiyo itahakikisha changamoto ya wananchi kupanga foleni ndefu kwenye vituo vya CNG inaisha na watahakikisha rasilimali ya gesi asilia inapatikana wakati wote kupitia huduma mbalimbali ikiwemo ya kupikia na kuendeshea vyombo vya moto.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Francis Mwakapalila amesema kuwa katika kuchochea matumizi ya Gesi Asilia kwenye vyombo vya moto nchini, TPDC imeamua kuweka mkazo kwa kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujazia gesi asilia kwenye vyombo vya moto ikiwemo magari na bajaji kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwa sasa tayari wameanza mchakato wa manunuzi ya vituo vitano vya CNG vinavyohamishika ambavyo vitawejwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.

Awali Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya Mafuta kutoka TPDC, Mhandisi Emmanuel Gilbert alisema kuwa kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha CNG kiasi cha futi za ujazo milioni 4.2 sawa na kilo 120 kwa siku, kina pampu nne zenye jumla ya nozeli nane na hivyo kukifanya kituo kuwa na uwezo wa kuhudumia magari nane kwa wakati mmoja ambapo kwa siku kitatoa huduma kwa magari takriban 1200.

Ameongeza kuwa, kituo kina pampu maalum tatu kwa ajili ya kujaza magari maalum ya kusafirisha CNG kwenda kwenye vituo vidogo vya kujaza gesi kwenye magari (Offline CNG Filling Stations), viwandani, taasisi na majumbani.  

WAZIRI MKUU AONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA KITAIFA YA MAZISHI YA VIONGOZI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Mei 09, 2025 ameongoza Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Mazishi ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Hayati Cleopa David Msuya kilichofanyika katika Ofisi ya ndogo za Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam.

TANZANIA YAWAKILISHWA VEMA KWENYE KAMBI YA MAFUNZO YA HUWAWEI

 

Wanafunzi wenye vipaji katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano kutoka vyuo vikuu 12 duniani, wameshiriki katika kambi ya mafunzo ya kimataifa ya Huawei Global Seeds for the Future, iliyofanyika kuanzia Aprili 9 hadi Aprili 17, 2025 katika makao makuu ya Huawei huko Shenzhen nchini China. 

Kambi hiyo ya mafunzo ilibeba maudhui yenye lengo la kuwaongezea uwezo wanafunzi hao katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la kidigiti, ubunifu na ujasiriamali. 

Kambi hiyo iliyodumu kwa muda wa wiki moja ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo ya teknolojia ya mawasiliano ya Huawei katika kuendelea kuwawezesha vijana wenye vipaji katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano. 

Nchi zilizoshiriki kambi hiyo ya mafunzo nchini China ni pamoja na Tanzania, Algeria, Cambodia, Laos, Uturuki, Ireland, Brazil, Mexico, Azerbaijan, Pakistan, Ethiopia na Afrika Kusini. 

Akizungumzia mkakati huo wa Huawei, mmoja wa wanufaika kutoka Tanzania akiiwakilisha Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Shahada ya kwanza ya Sayansi katika Uhandisi wa Kielektroniki na Mawasiliano, Natasha Nassoro amesema mada za mwaka huu hazikuacha mshiriki yeyote nyuma akiweka bayana kuwa walijifunza mambo ya ndani na nje ya tasnia ya Tehama (ICT ) chini ya mpango ulioandaliwa vyema, ukihusisha utafiti na kupendekeza teknolojia tofauti za kuchagiza juhudi za uendelevu duniani chini ya mpango wa tech4good pamoja na kujenga na kuunganishwa na mtandao wa mabingwa wengine wenye vipaji. 

Ujumbe wa wanafunzi hao kutoka vyuo 12 duniani pia ulipata fursa ya kufanya ziara katika vituo vya maendeleo ya kiteknolojia kama vile kampuni ya Alibaba, kituo cha mafunzo cha Huawei Global, Red note, duka la Huawei Flagship pamoja na ziara za kitamaduni huko Shanghai, kutembelea mgahawa maarufu duniani na ziara ya ya kutembelea Jiji la Shenzhen.

Huawei ilizindua programu ya Seeds For the Future nchini Thailand mwaka 2008, na hadi kufikia mwaka huu imefanikiwa kuwakusanya pamoja wanafunzi kutoka nchi 141 duniani huku zaidi ya wanafunzi 18,000 wakinufaika. 

Seeds for the Future ni programu kuu ya Huawei ya kurudisha kwa jamii (CSR), na imekuwa ikiendeshwa kwa kuchagua vipaji vya vijana kutoka duniani kote ili kushiriki katika mafunzo ya muda mfupi yanayolenga kuwashindanisha kwenye teknolojia, kubadilishana tamaduni na kukuza moyo wa ujasiriamali. 

Mpango huo umekuwa pia ukitoa nafasi ya upendeleo kwa wanawake kwa kiwango cha ushiriki cha angalau theluthi moja wawe wanafunzi wa kike. 

MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUFIKIA 75% MWAKA 2030 - DKT. BITEKO

* Dkt. Biteko akutana na Balozi wa Japan nchini

* Tanzania na Japan kuendelea kuimarisha ushirikiano wake

* Dkt. Biteko aishukuru Japan kufadhili m)mmradi wa umeme Singida

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha, kuimarisha, kurahisisha na kuwezesha upatikanaji wa umeme na nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu ili kupunguza athari za kiafya, mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha maisha ya wananchi.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Mei 9, 2025 ofisini kwake jijini Dar es salaam wakati alipotembelewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Youichi Mikami.

“ Serikali imedhamiria kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 21 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030 tumewashirikisha sekta binafsi ili kufikia azma hii,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Serikali imeandaa Mpango mahsusi wa Taifa wa Nishati kwa kipindi cha miaka mitano (National Energy Compact 2025 - 2030). Mpango ambao umeandaliwa kwa ushirikiano wa sekta binafsi na wameahidi kuchangia fedha mfano Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Dkt. Biteko amesema fedha hizo zitasaidia kufikia malengo ya Mpango huo wenye lengo la kuhakikisha watu milioni 300 waliopo kwenye Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara wanapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Katika mazungumzo yake na Balozi wa Japan, Mhe. Mikami Dkt. Biteko ameishukuru Serikali ya Japan kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa miradi ya umeme nchini.

“Tunawashukuru kwa ushirikiano wenu na kwa kufadhili mradi wa uunganishaji umeme kutoka Singida hadi nchini Kenya ambao tayari umekamilika. Tunapenda pia kushirikiana nanyi katika miradi ya gesi. Nchi zetu zimekuwa na ushirikiano mzuri na nia ya dhati ya kuhudumia wananchi wake” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Youichi Mikami amesema kuwa nchi yake na Tanzania zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na kuwa Japan itaendelea kuimarisha uhusiano huo.

Pia, ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali (Mission 300) uliofanyika hivi karibuni ambao ulilenga kujadili kuhusu usambazaji wa nishati ya umeme barani Afrika  

"KAMPENI YA 'SOMA NA MTI, ISHI NA MTI' YAZINDULIWA KILOMBERO: MITI LAKI MOJA KUPANDWA SHULENI"

 

........................

Katika kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wamezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya "Soma na Mti, Ishi na Mti" katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, ambapo miti 100,000 inatarajiwa kupandwa katika shule za msingi na sekondari kama sehemu ya mkakati wa kuhamasisha elimu ya mazingira miongoni mwa wanafunzi.

Uzinduzi huo umefanyika katika Shule ya Msingi Sululu na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dustan Kyobya, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuelimisha watoto kuhusu utunzaji wa mazingira tangu wakiwa wadogo.

“Mpango huu utakwenda sambamba na upandaji miti pembezoni mwa barabara kuu ya Kidatu–Mlimba. Hii si kampeni ya miti tu, ni kampeni ya maisha, kwa kuwa mazingira bora ni msingi wa maendeleo endelevu,” alisema DC Kyobya.

Aidha ameipongeza TFS kwa kutoa miche bure kwa wananchi na kuongoza juhudi za kurejesha uoto wa asili unaopotea kutokana na ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira, ambapo amesisitiza yeyote atakayehusika na uharibifu wa mazingira, ikiwemo kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi, hatavumiliwa.

Amesema Miti ni kichocheo kikubwa cha mvua, husaidia kuhifadhi unyevu ardhini, na huchangia katika kutunza vyanzo vya maji – jambo linalosaidia kilimo, uzalishaji wa umeme, na usalama wa chakula.

Kwa upande wake, Mhifadhi wa Wilaya ya Kilombero, Bi. Zalina Hassan, alisema TFS imekwisha toa miche 6,000 katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, ambayo itapandwa katika shule na maeneo ya barabara ya Kidatu–Ifakara.

“Natoa wito kwa wananchi kufika katika ofisi za TFS kuchukua miche inayotolewa bure na kushiriki katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” aliongeza Bi. Zalina.

Bi. Zalina amesema kuwa miti ina mchango mkubwa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kufyonza hewa ukaa (carbon dioxide) na kutoa oksijeni. “Tunapopanda miti tunapunguza kiwango cha gesi chafuzi hewani, tunasaidia anga letu na mustakabali wa vizazi vijavyo,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa kampeni ya "Soma na Mti Tanzania" alisema lengo ni kuwahimiza wanafunzi kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu kushiriki kikamilifu katika kupanda na kutunza miti katika maeneo yao ya jamii.

Kampeni hii inalenga kuibua kizazi chenye uelewa wa mazingira, kuhifadhi vyanzo vya maji, na kuongeza mvua kwa ajili ya shughuli za kilimo na uzalishaji wa umeme – hasa katika wilaya yenye ardhi oevu kama Kilombero.  

MAWAZIRI WA AFYA WA EAC WARIDHIA TANZANIA KUWA MWENYEJI WA VITUO VIWILI VYA UMAHIRI VYA KIKANDA

 

Mawaziri wa Afya kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana jijini Arusha katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya na kuridhia rasmi uanzishwaji wa Vituo viwili vya Umahiri vya Kikanda nchini Tanzania. 

Uamuzi huo umetokana na mapendekezo yaliyowasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuanzishwa kwa Kituo cha Umahiri cha Sayansi ya Afya ya Kinywa na meno kitakachokuwa chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Magonjwa ya Damu kitakachokuwa chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Mb.) Naibu Waziri wa Afya na Kiongozi wa ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono ajenda ya afya ya EAC kwa kuimarisha mifumo ya afya, kuwekeza katika rasilimali watu na miundombinu ya afya ili kwenda sambamba na vipaumbele vya kitaifa na kikanda. Pia alisisitiza kuanzishwa kwa vituo vya umahiri ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa huduma za afya maalum ndani ya kanda. 

Katika kukabiliana na changamoto mpya za kiafya kama ugonjwa wa Mpox, Mhe. Dkt. Mollel alitoa wito kwa nchi wanachama kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa, kuboresha maabara, na kuongeza ushirikiano katika maeneo ya mipaka.

Vilevile alitoa msisitizo wa umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii na mawasiliano sahihi katika kupambana na upotoshaji na unyanyapaa unaohusiana na magonjwa. Aidha, alisisitiza azma ya Tanzania kuendeleza elimu ya tiba kupitia miradi na program za kikanda na juhudi za kuoanisha mitaala ya tiba na udaktari katika Jumuiya. 

Thursday, May 1, 2025

BEGASHE MFANYAKAZI HODARI MALIASILI 2024/2025




 ................

Na Yusufu Kayanda

Afisa Uhusiano Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Sixmund Begashe, amesema heshima kubwa aliyoipata ya kutangazwa kuwa Mtumishi Hodari wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni heshima kwa wanahabari wote nchini, pamoja na watumishi wote wa wizara hiyo kutokana na ushirikiano mzuri waliouonesha katika kuufahamisha umma kuhusu matokeo chanya ya utekelezaji wa kazi za wizara na taasisi zake.

Bw. Begashe amesema hayo leo mkoani Singida, mara baada ya kupokea salamu nyingi za pongezi kutoka kwa viongozi wa wizara hiyo, watumishi wenzake, waandishi na wahariri wa vyombo vya habari, pamoja na watu mbalimbali, kufuatia kutangazwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Mtumishi Hodari wa mwaka 2024/2025.

"Nimeungwa mkono na wanahabari wengi nchini katika kutekeleza majukumu yangu. Wamekuwa ni sehemu ya familia yangu kikazi. Tumeshirikiana vyema na watumishi wenzangu, viongozi katika ngazi mbalimbali, pamoja na familia yangu. Hali hiyo imenipa nafasi ya kufanya vizuri katika kuhabarisha umma kuhusu matokeo chanya ya utekelezaji wa kazi za wizara yetu. Hivyo, uhodari huu ni wetu sote," alisema Bw. Begashe.

Aidha, ameongeza kuwa heshima hiyo inaendelea kumhamasisha kufanya kazi kwa bidii zaidi, huku akiendelea kushirikiana vyema na wanahabari wote chini ya miongozo bora ya msemaji wa wizara pamoja na viongozi wote kwa mujibu wa kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, pamoja na kuwapongeza watumishi wote wa wizara hiyo kwa kazi nzuri wanazozifanya, alimpongeza Bw. Begashe kwa kutangazwa Mtumishi Hodari na pia kuwatakia watumishi wote nchini Sikukuu Njema ya Mei Mosi.


</

RAIS SAMIA NA VIONGOZI MBALIMBALI WAKISHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI SINGIDA

Wafanyakazi kutoka Wizara mbalimbali, Taasisi za umma na binafsi wakipita mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Maadhimisho ya sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambazo Kitaifa zimefanyika katika uwanja wa Bombadia Mkoani Singida tarehe 01 Mei, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe,Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhi Zawadi ya Vikombe kwa Washindi wa michezo Mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa yaliyofanyika Viwanja vya Bombadia Mkoani Singida leo Mei 01,2025.