JSON Variables

Friday, May 9, 2025

THE ROYAL TOUR YAZIDI KUIFUNGUA SEKTA YA UTALII. 

...........

Na Mwandishi wetu 

Filamu ya The Royal Tour imezidi kuleta matokeo chanya katika sekta ya Utalii kutokana na mwamko mkubwa kwa wawekezaji hususan wa Hotel za kitalii kuendelea kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye Hifadhi za Taifa ili kwendana na kasi kubwa ya watalii wanaoingia nchini.

Akizungumza baada ya kutembelea Hoteli ya Serengeti Explore by Elewana na Hoteli ya Serengeti Lake Magadi, Mkoani Mara, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema ujenzi wa Hoteli hizo ni mwitikio wa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuinua sekta ya Utalii hasa kupitia Filamu ya “Tanzania-The Royal Tour,” ambayo imechagiza zaidi kuleta wageni wengi na kufungua fursa zaidi kwa wawekezaji kuwekeza katika malazi.

“Tunamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia kwa kujitoa kwake kutangaza Utalii wa Tanzania ambapo leo matunda yake yanaonekana, wawekezaji wanaendelea kujitokeza kuwekeza kwa kujenga hoteli za kisasa na za kimataifa ambazo zitavutia wageni wengi zaidi kwenye Hifadhi zetu,” alisema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi pia ameendelea kutoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa adhimu kuwekeza kwa kujenga hoteli katika hifadhi za kusini ikiwa ni mkakati wa Serikali katika kuifungua zaidi Kusini pamoja na kutangaza vivutio vipya vya utalii.

Aidha Dkt. Abbasi asema, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika kwa wadau wote wenye nia ya kuwekeza kwenye maeneo ya vivutio, kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. 

Hoteli ya Serengeti Explore ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 na Lake Magadi ambayo ujenzi wake unaendelea kwa jumla zina vyumba 150, hivyo zinaongeza zaidi wigo wa Hoteli za Kitalii katika kuwahudumia wageni wengi zaidi wanaoingia nchini.

0 comments:

Post a Comment