JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Ijumaa, 27 Juni 2025

DKT BITEKO MGENI RASMI NISHATI BONANZA 2025


.........................

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe Dkt Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bonanza la Wizara ya Nishati na Taasisi zake litakalofanyika jumamosi Juni 28, 2025 jijini Dodoma.

Akizungumzia maandalizi ya Bonanza hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Bi. Neema Mbuja amesema kuwa, Nishati Bonanza litafanyika kwenye Viwanja vya Jamhuri mjini Dodoma na kushirikisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na wadau kutoka Wizara nyingine.

‘’ Nipende kuchukua fursa hii kuzikaribisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kushiriki kikamilifu bonanza ambalo linaleta fursa ya kufahamiana na kubadilishana mawazo baada ya muda wa kazi pamoja na kufanya mazoezi ili kujenga afya." Amesema Mbuja

Ameongeza kuwa, kwa mwaka huu Nishati Bonanza linaongozwa na kauli mbiu ya "Michezo kwa Afya bora, Shiriki uchaguzi 2025 ikiwa na lengo pia la kuhamasisha wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 .

Amesema maandalizi yote yameshakamilika na timu zitakazoshiriki michezo mbalimbali zimeshawasili Dodoma kushiriki bonanza hilo litakaloshirikisha watu takribani 1000.

Ametaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni ni pamoja na Mpira wa miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu, Mpira wa Kikapu, Kuvuta Kamba, pamoja na michezo ya jadi kama vile bao na drafti, pia kufukuza kuku.

Taasisi zitakazoshiriki Bonanza hilo la Nishati ni pamoja na TANESCO, REA, TPDC, PURA, EWURA, TGDC, ETDCO, TCPM, TANOIL, GASCO, PBPA.

Hili ni Bonanza la pili kufanyika tangu kuasisiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt Doto Biteko mwaka jana.









SERIKALI YASISITIZA UFUATILIAJI NA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa SELF, Bi. Sentiel Yona, wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Washiriki wa mafunzo yaliyotolewa na Wizara ya Fedha kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, wakibadilishana uzoefu baada ya kumalizika kwa mafunzo kwa waratibu hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Mmoja wa watoa mada kuhusu huduma za uwekezaji, Afisa Mauzo, Watumishi Housing Investment, Bw. Jafari Chaukunde, wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya maandalizi ya mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, baada ya kumalizika kwa halfa ya kufunga, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma. Kulia ni Afisa Msimamizi Fedha Mkuu, Idara ya Uendelezaji Fedha Wizara ya Fedha Bw. Magesa Mafuru na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, baada ya kumalizika kwa halfa ya kufunga, katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma. Kulia ni Afisa Msimamizi Fedha Mkuu, Idara ya Uendelezaji Fedha Wizara ya Fedha Bw. Magesa Mafuru na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dodoma)

.............................

Na. Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma

Katika kuhakikisha usimamizi madhubuti wa Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha, Serikali imewaagiza waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha kote nchini kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera na Sheria za Huduma Ndogo za Fedha katika maeneo wanayoyasimamia ili kuwabaini na kuwachukulia hatua watoa huduma wanaotoa huduma kinyume na utaratibu uliowekwa.

Agizo hilo limetolewa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Dionesia Mjema, wakati akifunga mafunzo ya kitaalamu kwa watoa huduma ndogo za fedha kutoka katika ngazi za mikoa, wilaya na halmashauri, yaliyolenga kuwaongezea ujuzi wa kiutendaji katika kutambua changamoto, kushughulikia ukiukwaji wa sheria na kuwajengea uwezo wa kusimamia kwa ufanisi huduma hizo.

“Ni muhimu kila mmoja wetu awe mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha inatekelezwa ipasavyo, na wale wanaokiuka Sheria hiyo wanachukuliwa hatua stahiki,” alisema Bi. Mjema.

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa Sheria si chaguo bali ni wajibu wa kila mtoa huduma na msimamizi wa sekta hii, kwa kuwa utekelezaji huo ndio msingi wa kuhakikisha uwajibikaji, uadilifu, na uendelevu wa huduma ndogo za fedha katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Aidha, aliwasisitiza kujenga mazoea ya kuandaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa Sheria hizo kila baada ya miezi mitatu, kwa mujibu wa miongozo, kwa kuwa taarifa hizo ni nyenzo muhimu katika kutathmini maendeleo, changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa sheria katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Bi. Mjema, aliwasihi waratibu hao kushirikiana kwa karibu na maafisa ushirika, wahamasishaji, wasajili, pamoja na maafisa maendeleo ya jamii, ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Sera na Sheria za Huduma Ndogo za Fedha unafanyika kwa ufanisi.

“Ushirikiano huo unatarajiwa kujenga mfumo madhubuti na endelevu wa huduma ndogo za fedha, unaolenga kuwafikia wananchi wa kipato cha chini kwa kutumia mbinu bora, salama na zenye ufanisi, ili kuchochea ustawi wa kiuchumi na kuchangia maendeleo jumuishi ya taifa zima”alisema Bi. Mjema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha mkoani Mbeya, Bi. Sebastiana Mwapinga, ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa kichocheo muhimu cha mabadiliko chanya, na kwamba wataendelea kuboresha utendaji wao hususan katika maeneo yaliyokuwa na changamoto hapo awali, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kifedha zitakazowawezesha kuinua hali zao za kiuchumi.

Naye, mmoja wa wahamasishaji, Bi. Teodomila Mwenda, amesema kuwa hatua ya Serikali kuwapatia mafunzo na kuwajengea uwezo wa kitaalamu siyo tu imedhihirisha dhamira yake ya dhati ya kuimarisha sekta hiyo, bali pia imeongeza ari na motisha kwao kuendelea kutoa elimu kwa ufanisi zaidi.

Katika mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, taasisi mbalimbali zilipata fursa ya kutoa elimu kuhusu huduma za uwekezaji wanazotoa ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji UTT- AMIS, Mfuko wa SELF pamoja Watumishi Housing Investment ambazo ni muhimu kwa wananchi kuzifahamu na kuzitumia ipasavyo ili kuongeza kipato chao na kuboresha maisha yao ya kiuchumi.

Jumla ya waratibu 130 wa huduma ndogo za fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu katika maeneo mbalimbali, yaliyolenga kuwaimarisha katika kusimamia na kufuatilia kwa ufanisi utoaji wa huduma ndogo za fedha katika ngazi za watoa huduma.

MWISHO

Alhamisi, 26 Juni 2025

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA MIFUMO RASMI YA KIFEDHA KUKUZA UCHUMI WA MWANANCHI

Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema, akimkaribisha Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, ili aweze kufungua mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Janeth Hiza, akizungumza wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, iliyofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, wakifuatilia mawasilisho mbalimbali wakati wa mafunzo kwa Waratibu hao yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, yaliyofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja (katikati) akisikiliza baadhi ya michango iliyokua inatolewa na washiriki wa mafunzo yaliyohusisha Wizara ya Fedha na Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri Bi. Evelyine Mangweha, akiuliza swali wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Dionisia Mjema na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.
Mchumi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Felista Malibate, akitoa mada kuhusu Kanuni za Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mwaka 2019 wakati wa mafunzo kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.
Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha wa Manispaa ya Ubungo, Bi.Evelyine Mangweha,  akichangia mada wakati wa mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha yaliyofanyika jijini Dodoma.
Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, baada ya kumalizika kwa halfa ya ufunguzi, iliyofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Kamishna Msaidizi, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionesia Mjema na kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii (TAMISEMI) Bi. Everine Kapologwe.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dodoma)

.......................
Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma

Serikali imewataka Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha nchini kuongeza kasi, ubunifu na weledi katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mifumo rasmi ya kifedha inayotambulika na kusimamiwa na Serikali ili kuhakikisha wanapata maarifa yatakayowawezesha kujikwamua kiuchumi kwa njia salama na endelevu.

Agizo hilo limetolewa na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, wakati akufungua mafunzo maalum kwa Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri, yaliyolenga kuwawezesha waratibu hao kutoa elimu sahihi kwa jamii wanazozihudumia.

Dkt. Mwamwaja alisisitiza umuhimu wa kutumia mafunzo hayo kama jukwaa la kubadilishana mawazo, uzoefu na mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazowakabili waratibu hao katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Maarifa haya msiyabakize kwenye makabrasha, pelekeni kwa wananchi waelimisheni waelewe faida ya kutumia mifumo rasmi ya kifedha kama benki, SACCOS, VICOBA vilivyosajiliwa na taasisi zingine zilizo chini ya uangalizi wa Serikali kwa kuwa ndiyo njia salama ya kuwasaidia kuinuka kiuchumi,” alisema Dkt. Mwamwaja.

Aliongeza kuwa mafanikio ya sekta hiyo hayatategemea tu uwepo wa Sera, Sheria na Kanuni nzuri, bali yanategemea zaidi utekelezaji wenye tija, weledi, uwajibikaji na ufuatiliaji makini unaoanzia kwa Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha ambao ndio kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kufikisha elimu na huduma bora za kifedha.

Aidha, aliwapongeza Waratibu wote kwa kujitokeza kwa wingi na kwa wakati katika mafunzo hayo, na kuwataka kuyachukulia kama fursa ya kuimarisha uwezo wao wa kuwaelimisha wananchi kwa njia shirikishi, rafiki na yenye matokeo chanya.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Mohamed Nyange, alisema kuwa mafunzo hayo yamewapa maarifa ya kina na mbinu sahihi zitakazowawezesha kuwafikia wananchi kwa ufanisi, kutoa elimu inayoeleweka, na kusaidia jamii kuelewa umuhimu wa kutumia huduma rasmi za kifedha kwa maendeleo yao ya kiuchumi.

“Ili tuweze kutoa elimu sahihi kwa wananchi tunaowahudumia lazima nasi tuwe na uelewa wa kutosha kwanza, niwapongeze Wizara ya Fedha kwa kutujengea uwezo huu, tutaenda kutumia maarifa haya kwa kuhakikisha wananchi wetu wanajua, wanaelewa na wanatumia huduma za kifedha rasmi kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi,” alisema Bw. Nyange.

Mafunzo haya yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), lengo ni kuhakikisha nchi inakuwa na mtandao mpana wa waratibu waliobobea katika kutoa elimu ya kifedha kwa jamii.

Serikali imeendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo watendaji wake ili kuhakikisha elimu ya fedha inamfikia kila Mtanzania, kupitia elimu hiyo, wananchi wataweza kufanya maamuzi sahihi ya kifedha ikiwemo kutumia mifumo rasmi inayotambuliwa na Serikali kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Jumla ya mikoa 13 imeshiriki katika mafunzo hayo, ambayo ni: Mbeya, Pwani, Njombe, Shinyanga, Dar es Salaam, Tanga, Singida, Morogoro, Dodoma, Simiyu, Iringa, Arusha na Kilimanjaro.

BUNGE LARIDHIA MAREKEBISHO YA MPAKA WA HIFADHI YA TAIFA NYERERE

...............

Na Anangisye Mwateba, Dodoma

Bunge limeridhia ombi la Serikali la kumega sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa lengo la kutatua migogoro ya mipaka na kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea katika mazingira rafiki kwa jamii na uhifadhi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, akiwasilisha azimio hilo bungeni, amesema kuwa Serikali imeamua kumega eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,617 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kulirejesha katika Pori la Akiba Selous.

Amesema hatua hiyo imepunguza ukubwa wa hifadhi hiyo kutoka kilomita za mraba 30,893 hadi kufikia kilomita za mraba 29,276.

Akifafanua zaidi, Mhe. Chana amesema hatua hiyo inalenga kuondoa migogoro ya muda mrefu ya mipaka baina ya hifadhi hiyo, vijiji vinavyoizunguka, Pori la Akiba Selous na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Mbarang’andu, Juhiwangumwa, Iluma, Jukumu, Magingo na Nalika.

“Kwa kufanya hivyo, tunaimarisha usalama wa maeneo yaliyohifadhiwa, tunajenga mahusiano bora kati ya wananchi na hifadhi, na kuondoa migogoro iliyodumu kwa muda mrefu,” amesema Mhe. Chana.

Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa marekebisho hayo ya mpaka yanalenga kulinda mfumo ikolojia muhimu unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba Selous, sambamba na kuhakikisha mtiririko endelevu wa maji katika Mto Rufiji, ambao ni chanzo kikuu cha uzalishaji umeme kupitia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).

Mhe. Chana amebainisha kuwa hatua hiyo itaongeza tija kwa Taifa kwa kuimarisha shughuli za utalii, uwindaji wa kitalii katika Pori la Akiba Selous na maeneo yanayozunguka, na hivyo kuchangia mapato ya ndani kupitia sekta ya utalii.

“Kwa sasa, tunaelekea katika uboreshaji wa uhifadhi wa maliasili kwa ujumla wake – wanyamapori, mimea, mazalia ya viumbe wa majini na pia kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya wakulima, wafugaji na wavuvi,” ameongeza.

 

Jumatano, 25 Juni 2025

KAMATI YA USHAURI MRADI WA EMA YAKUTANA DODOMA


................

Kamati ya Ushauri ya Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) imekutana kwa ajili ya kujadili na kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 jijini Dodoma leo Juni 25, 2027. 

Kikao hicho kimeongozwa na Bw. Wanjara Jandwa kutoka Kitengo cha Huduma za Sheria cha Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambaye aliwapongeza kwa kazi nzuri ya kutoa maoni yenye kujenga. 

Bajeti hiyo iliyowasilishwa na Mratibu wa Mradi Bw. Richard Masesa imejadiliwa na wajumbe walioshiriki kikao hicho kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC, Wizara za kisekta na halmashauri. 

Mradi wa EMA unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, unafadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA), unakusudia kushughulikia changamoto kuu za mazingira na kuondoa vizuizi vya kisekta vilivyopo katika Wizara na mamlaka maalumu za kisheria na kuongeza wigo wa utendaji.

Kwa mantiki hiyo, mradi huo ni nyenzo mojawapo ya kuboresha uratibu wa usimamizi wa mazingira nchini unaokusudia kushughulikia changamoto kuu za mazingira.

WADAU WAMCHANGIA UMMY MWALIMU MILIONI 1.3 ZA FOMU YA UBUNGE

......................

NA: MWANDISHI WETU, TANGA 

Wadau mbalimbali wamemchangia Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, fedha kiasi cha Shilingi 1,300,000, ili zimuwezeshe kuchukua fomu ya Ubunge ili agombee tena nafasi hiyo kwa kipindi kingine katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu 

Fedha hizo ni matokeo ya michango ya hiari kutoka kwa wadau kama vile Taasisi ya Mguu Kwa Mguu, Friends of Odo Ummy, Sema na Tanga na watu wengine nje na taasisi hizo.

Alikabidhi fedha hizo, Abdallah Mukulu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva wa Magari ya IT Tanga, amesema kutokana na kazi nzuri alizozifanya za maendeleo katika Jimbo la Tanga Mjini, wameona wamshike mkono kwa kiasi hicho licha ya kwamba Mbunge huyo anao uwezo wa kujilipia yeye mwenyewe gharama za fomu.

"Mheshimiwa Mbunge wetu Ummy Mwalimu, napenda kukukabidhi Shilingi 1,300,000 kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo Tanga ambao wamejichangisha wao wenyewe ili zisaidie kulipia fomu ya Ubunge. Kwa kweli tunaridhishwa na utendajikazi wako na namna unavyotatua kero za wananchi. Katika kipindi cha uongozi wako, Jimbo la Tanga Mjini limepata miradi mingi ya maendeleo, kwa kweli umefanya makubwa, tunatamani urudi tena madarakani uendelee kuwatumikia wananchi wako," amesema Mukulu.

Vilevile, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sema na Tanga, Said Massa, amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 Tanga Mjini imetekelezwa ipasavyo, hivyo anaunga mkono zoezi la kumchangia fomu ya Ubunge Ummy Mwalimu ili aendeleze kazi nzuri.

"Kwa kweli Jimbo la Tanga Mjini limenufaika sana na uongozi wako ulioacha alama katika maisha ya wananchi kwani umetekeleza miradi mingi ya maendeleo kama vile maji, afya, elimu, Bandari ya Tanga, umeme, barabara na miradi mingine mingi," amesema Massa.

Elias Mpayi ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Mguu Kwa Mguu amesema Ummy Mwalimu amewezesha Tanga Mjini kupata maendeleo makubwa katika kipindi kifupi cha uongozi wake, hivyo anastahili kuongoza kwa mara nyingine.

Baada ya makabidhiano hayo, Ummy Mwalimu, amewashukuru wadau hao waliojitoa kwa hali na mali kumchangia fomu ya Ubunge kwani bado ana dhamira ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa Tanga Mjini.

"Moyo wangu umelemewa na shukrani nyingi, nimefurahi kwa kuwa mmetambua kazi kubwa zilizofanyika Tanga Mjini. Nimshukuru pia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea nguvu katika utekelezaji wa miradi, kwa kweli kazi zimefanyika na wananchi mnajionea kwa macho yenu," amesema Ummy Mwalimu.

Jumanne, 24 Juni 2025

SEKTA YA NISHATI YACHANGIA ASILIMIA 14.4 YA PATO LA TAIFA

....,...

Kapinga ampongeza Rais, Dkt. Samia kwa uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Nishati

 Aeleza mafanikio yaliyofikiwa katika Umeme, Gesi Asilia na Mafuta

 Asisitiza kuwa Nishati ni moyo wa uchumi

Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Sekta ya Nishati ni moja kati ya Sekta tatu nchini ambazo zimechangia ukuaji wa pato la Taifa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 hadi 2025.

Kapinga ameyasema hayo wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji Bungeni Jijini Dodoma.

"Mheshimiwa Mwenyekiti ukiangalia kwa tathmini kati ya mwaka 2024 hadi 2025 Sekta ya Nishati imefanya vizuri katika kuchangia pato la Taifa, Sekta hii imetoka asilimia 5.8 mwaka 2015 na sasa hivi tunazungumzia asilimia 14.4”. Amesema Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa, Sekta ya Nishati imeweza kufanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika miradi ambapo amepongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo mkubwa.

"Katika Gesi na Mafuta yamepatikana mafanikio makubwa sana ikiwemo uendelezaji wa miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa gesi asilia, katika kitalu cha Mnazibay na Songosongo Serikali imeweza kuzalisha futi za ujazo bilioni 25.51 kwa kipindi cha miaka minne kwa kila kimoja.

Ameongeza kuwa, Serikali imesaini mkataba katika kitalu cha Ruvuma Ntorya na sasa hivi kipo katika hatua za awali katika kuzalisha na kuendeleza gesi asilia.

Amesema katika kipindi cha miaka minne Sekta ya Nishati imepata mafanikio makubwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ambapo Serikali imeweza kuongeza hisa katika kitalu cha MnaziBay kutoka asilimia 20 hadi kufikia asilimia 40.

Ameeleza kuwa, Sekta ya gesi asilia ni muhimu kutokana na kuchagiza matumizi ya sekta nyingine ikiwemo matumizi ya gesi iliyoshindiliwa katika magari na kuunganisha mtandao wa gesi majumbani, miradi ambayo inafanyika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Lindi.

Akielezea kuhusu mafuta amesema Serikali imekuwa na mafanikio katika kusimamia na kudhibiti bei kikomo za bidhaa za mafuta na kuongeza kuwa bei ya ndani ya bidhaa za mafuta imeendelea kuwa himilivu kutokana na Serikali kuweka ruzuku kwenye bidhaa hiyo.

Kuhusu mfumo wa pamoja wa kuagiza mafuta amesema kuwa umeendelea kuimarika.

Kuhusu Sekta ya umeme, Kapinga amesema kuwa Sekta hiyo ni moyo wa uchumi katika Taifa na kutanabaisha kuwa, mwaka 2021 uwezo wa kuzalisha umeme ulikuwa takribani megawati 1,600 na hivi sasa ni takribani megawati 4,000.

Ameeleza kuwa, kuongezeka kwa megawati hizo kunatokana na uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika miradi ya kuzalisha umeme ukiwemo mradi wa kimkakati wa Julius Nyerere.

Kwa upande wa miradi ya usafirishaji umeme, Kapinga amesema njia za kusafirisha umeme zilikuwa kilometa takribani 6,000 mwaka 2021 na sasa hivi zipo kilometa takribani 8,000 na njia za usambazaji zimetoka kilometa 144,000 hadi kilometa 200,000.

Akielezea miradi ya umeme Vijijini, Kapinga amesema kwa kipindi cha miaka minne Serikali imekamilisha upelekaji wa umeme katika Vijiji vyote na hivi sasa Serikali imejikita kupeleka umeme katika Vitongoji.</

Jumatatu, 23 Juni 2025

UJENZI KITUO CHA KUPOZA UMEME NKANGAMO-MOMBA KUKAMILIKA MEI 2026


...............

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Nkangamo- Momba unatarajiwa kukamilika Mei mwakani.

Kapinga ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Momba, Condester Sichalwe (CCM) ambaye aliuliza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha kusambaza umeme Nkangamo – Momba.

 Kapinga amesema ujenzi wa kituo hicho cha Nkangamo - Momba ulianza mwezi Mei, 2024 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 30.

Jumapili, 22 Juni 2025

WADAU WAALIKWA KUTOA MAONI YA KODI KUPITIA MFUMO WA KIELEKTRONIKI

Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi, Idara wa Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. Daved Massawe akitoa elimu kwa Bi. Zainabu Kyama kuhusu huduma zinazotolewa katika Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma. 
Afisa Kumbukumbu, Kitengo cha Pension, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bi. Stella Mtally akitoa elimu kuhusu Pensheni inayolipwa na Hazina kwa Wastaafu kwa Mkazi wa Dodoma Bw. Andrew Madeha, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, katika Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma. 
Afisa TEHAMA, Idara ya Mifumo ya Kifedha, Wizara ya Fedha, Bi. Zaina Mwanga akitoa elimu kwa Bi. Sophia Matara kuhusu maelekezo ya matumizi ya Aplikesheni ya Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Grace Samwel, akitoa elimu ya fedha kuhusu uwekaji akiba, uwekezaji na matumizi kwa wakazi wa Dodoma waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma. 
Afisa Msimamizi wa Fedha, Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. James Kamomonge, akitoa elimu kuhusu maandalizi ya bajeti ya Serikali na Usimamizi wake kwa Bw. Emmanuel John, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha,Dodoma)

...........................

Na. Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma

Wizara ya Fedha imetoa wito kwa wananchi kujenga mazoea ya kushiriki mchakato wa kutoa maoni ya maboresho ya mfumo wa kodi kupitia mfumo wa kieletroniki wa kuwasilisha maoni (Maoni Portal) ili Serikali iweze kuyafanyia kazi kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.

Wito huo umetolewa na Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. David Massawe, wakati akitoa elimu ya masuala ya kodi kwa watu waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

“Mwezi Desemba kila mwaka, Serikali kupitia Wizara ya Fedha hutoa fursa kwa wananchi kupitia dirisha la mfumo wa kieletroniki wa maoni portal ambapo wananchi hualikwa kuwasilisha maoni ya kuboresha mfumo wa kodi ili kuhakikisha kuwa sera za kodi nchini zinazingatia kanuni za usawa, ufanisi, kuakisi matakwa ya wananchi na zenye kuendana na mazingira halisi ya kiuchumi nchini” alisema Bw. Massawe.

Aliongeza kuwa makundi mbalimbali yakiwemo taasisi binafsi na taasisi za umma, wakiwemo wafanyabiashara, wakulima, vijana, wanawake na wastaafu wanashiriki kutoa maoni ili Serikali iweze kuandaa sera za kodi rafiki kwa makundi yote.

Wiki ya Maadhimisho ya Utumishi wa Umma imeanza Juni 16 na inatarajiwa kuhitimishwa Juni 23 mwaka huu ikiwa na kauli mbiu ya “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidigiti ili kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchangia Uwajibikaji”.


 

Jumamosi, 21 Juni 2025

MADEREVA WAJA NA "TUNAKWENDA NA SAMIA 2025"

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Patrobas Katambi akizungumza katika kongamano la Kitaifa la madereva wa malori na mabasi na masafa marefu na kati ambalo limefanyika Leo Tar 21/6/2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam  Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Patrobas Katambi akikabidhiwa Tuzo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoka Kwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Madereva wa masafa marefu na ya kati Tanzania Hassan Dede katika kongamano la Kitaifa la madereva wa malori na mabasi na masafa marefu na kati ambalo limefanyika Leo Tar 21/6/2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mkoani Dar es salaam Albert Msando akizungumza katika kongamano la Kitaifa la madereva wa malori na mabasi na masafa marefu na kati ambalo limefanyika Leo Tar 21/6/2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam  Mwenyekiti wa Taasisi ya Madereva wa masafa marefu na ya kati Tanzania Hassan Dede akizungumza katika kongamano la Kitaifa la madereva wa malori na mabasi na masafa marefu na kati ambalo limefanyika Leo Tar 21/6/2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam  Mrakibu wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania -Mussa Manyama akizungumza katika kongamano la Kitaifa la madereva wa malori na mabasi na masafa marefu na kati ambalo limefanyika Leo Tar 21/6/2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam  Mr Chuki Shaban,Mwenyekiti wa wamiliki wa Malori (TAMSTOA) akizungumza katika kongamano la Kitaifa la madereva wa malori na mabasi na masafa marefu na kati ambalo limefanyika Leo Tar 21/6/2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.(PICHA ZOTE NA MUSSA KHALID)

Baadhi ya Madereva walioshiriki katika kongamano la Kitaifa la madereva wa malori na mabasi na masafa marefu na kati ambalo limefanyika Leo Tar 21/6/2025 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam 

.....................

NA MUSSA KHALID 
Serikali imeendelea kuwasisitiza madereva wa masafa marefu nchini  kudumisha amani ulinzi na usalama wa vyombo, ikiwemo kutiii Sheria na taratibu za kimamlaka na usimamizi ili kuonyesha uzalendo kwa Taifa.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Patrobas Katambi ametoa wito huo leo wakati akizungumza katika kongamano la Kitaifa la madereva wa malori na mabasi na masafa marefu na kati ambalo limefanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam yenye kauli mbiu isemayo "madereva tunakwenda na Samia 2025".

Aidha Naibu Waziri Katambi amewapongeza madereva hao kwa kuandaa kongamano hilo lenye dhamira ya kuipongeza serikali katika kazi kubwa iliyofanywa nchini.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Katambi amesema kuwa serikali inaendelea kusisitiza utoaji wa mikataba kwa madereva ili kuonyesha makubaliano kati ya mmiliki wa chombo na madereva.

"Ni muhimu sana kutoa mikataba kwa sababu inaonyesha haki ya wajibu kwa Mmiliki wa chombo na Dereva lakini usalama wa chombo ni kupitia mkataba"amesema Naibu Waziri Katambi

Awali akizungumza Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Albert Msando amesema kuwa watahakikisha wanaendeleza ushirikiano na madereva wote wanaofanya shughuli zao kwani Ubungo imekuwa ni lango la kwenda katika maeneo mbalimbali nchini 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Madereva wa masafa marefu na ya kati Tanzania Hassan Dede ametumia fursa hiyo kusema madereva wanakiu kubwa kuona mambo yanabadilika.

Naye Mrakibu wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania -Mussa Manyama amesema wao kama wasimamizi wa sheria wanawakumbusha madereva kuendelea kutii Sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali.
Amewataka kuondoka na kuendesha magari Kwa mwendo wa masi kwani imekuwa ni chanzo kikubwa cha ajali barabarani
Mr. Chuki Shaban ni Mwenyekiti wa wamiliki wa Malori (TAMSTOA) amesema ni vyema wamiliki wote wa Malori kuingia kwenye Vyama ili kuweza kutambulika Kwa haraka.

NAIBU WAZIRI -UTUMISHI ATEMBELEA BANDA LA NCC

Naibu Waziri Deus Sangu wa UTUMISHI akionesha kitu katika moja ya machapisho ya NCC ambapo alishauri ifanyike kazi ya ziada kuhakikisha taarifa za NCC zinaifikia jamii yote ya Watanzania na si wakandarasi pekee au wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi tu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe. Deus Sangu, akisikiliza maelezo ya NCC baada ya kutia sahihi kwenye kitabu cha wageni cha taasisi hiyo.

...............

Naibu Waziri-UTUMISHI atembelea banda la NCC

• Aipongeza kwa mchango wake katika kukuza sekta ya ujenzi

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu, ametembelea banda la Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na kuelezwa masuala mbalimbali yanayohusu Baraza hilo.

Mhe. Sangu ameelezwa majukumu yanayotekelezwa na NCC, huduma zinazotolewa na Baraza hilo, pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana kwa kutolewa huduma hizo, ambapo alipongeza jitihada zinazofanywa na kusema kuwa ofisi yake itatoa ushirikiano, pindi itakapohitajika kutoa msaada wa kiutumishi.

Akizungumza baada ya kusikia maelezo hayo, Mhe. Naibu Waziri alisema, NCC ina umuhimu mkubwa kwa taifa, kutokana na majukumu inayoyatekeleza, ikiwemo kuratibu usuluhishi wa migogoro inayohusu sekta ya ujenzi, pamoja na kutoa elimu ya mbinu mbadala za kutatua migogoro kwa wadau wa sekta hiyo na nyingine.

“Awali palikuwa na migogoro mingi katika sekta ya ujenzi nchini, lakini sasa inazidi kupungua...

 Tunaamini NCC ina mchango mkubwa katika kuipunguza kwa namna yoyote ile inayofanya ikiwemo kutoa mafunzo ya usuluhishi tofauti na mahakama. Tunatambua hili na tunapongeza jitihada hizi,”Naibu Waziri Sangu amesema. 

Ameongeza kuwa, uwepo wa NCC umeleta uwiano wa mambo mengi katika sekta ya ujenzi nchini.

Aidha, kuhusu ushiriki wa NCC kwenye Wiki ya Utumishi wa Umma Naibu Waziri Sangu ameitaka taasisi hiyo izidishe ushiriki wake kwenye matukio mengi zaidi, kama ilivyo shikiri kwenye Wiki ya Utumishi wa umma. Amesema lengo ni kuhakikisha Watanzania wanaifahamu vizuri zaidi taasisi hiyo, hivyo kuitumia.

Amesema, majukumu ya NCC ni makubwa na ya msingi yanayopaswa kutangazwa zaidi, ili yajulikane kwa jamii yote na wala si kwa makandarasi au wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi pekee.

“Tumefurahia maandalizi ya banda lenu na ushiriki wenu katika wiki hii muhimu. NCC imeonesha utayari wa kuhudumia wananchi hivyo, Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaahidi kuwaunga mkono,” 

Banda la NCC limetembelewa na viongozi mbalimbali kwa siku tofauti, akiwemo Naibu Waziri huyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (UTUMISHI) Bw.Juma Mkomi, pamoja na Mkurugenzi wa ofisi hiyo, Bw. Benard Makhanda, Mkurugenzi Msaidizi wa UTUMISHI, Bw. Jafari Maganga na wengine wenye nyadhifa tofauti, walioambatana nao.

Listen Mkisi Radio