JSON Variables

Thursday, March 13, 2025

KAMATI YA BUNGE PIC: JENGO JIPYA WMA LITAONGEZA MORALI KUWAHUDUMIA WANANCHI

 

🟠 *Mwenyekiti Vuma ampongeza Rais, Serikali, Wizara na WMA* 


🟠 *Katibu Mkuu asema maono ya Rais Samia utoaji huduma bora kwa wananchi yatafikiwa* 


 *Dodoma*


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Augustine Vuma amesema kukamilika kwa Jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo (WMA), kutaongeza morali ya watumishi katika utendaji kazi hivyo kuboresha zaidi huduma zake kwa wananchi.


Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari, Machi 13, 2025 baada ya Kamati hiyo kuzuru na kujionea Jengo hilo jipya la kisasa lililojengwa na kampuni ya wakandarasi wazawa ijulikanayo kama Ms. Mohammedi Builders Ltd kwa gharama ya shilingi za kitanzania bilioni 6.1


“Ujio wa Mradi huu unaamsha ari ya kufanya kazi kwa watumishi na ubunifu zaidi, jambo ambalo tunaamini litaongeza tija kwa maana ya makusanyo ya Wakala, lakini pia miradi itaenda kuwasaidia Watanzania kulindwa vizuri dhidi ya watu wasio waaminifu ambao huwapunja wananchi kwenye vipimo mbalimbali,” amesema Mhe. Vuma.


Aidha, Mhe. Vuma ametoa pongezi kwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za ujenzi wa jengo hilo.


Vilevile ametoa pongezi kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Menejimenti yote ya Wizara pamoja na Uongozi wa WMA kwa usimamizi mzuri uliowezesha kufanikisha ujenzi husika.


Katika hatua nyingine, Mhe. Vuma amempongeza Mkandarasi wa jengo hilo na kutoa rai kwa Serikali pamoja na wadau wengine kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mbalimbali ili fedha wanazolipwa ziendelee kubaki nchini na kuchangia katika kukuza uchumi.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Samia kuwezesha ujenzi huo, pia amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutawezesha kutimiza maono yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi.


Dkt. Hashil ameiahidi Kamati ya Bunge kutimiza maelekezo waliyoyatoa, hususan yanayohusu Wizara na WMA kuutumia muda wa mwaka mmoja wa matazamio ya jengo kwa kuhakikisha dosari ndogo ndogo zitakazojitokeza zinarekebishwa.


Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari kuhusu kuanza kutumika kwa jengo, Katibu Mkuu amebainisha kuwa tayari makabidhiano yalikwishafanyika na kwamba utaratibu wa kuhamisha watumishi umekwishaanza.


Ujenzi wa Jengo hilo ulianza kutekelezwa Julai 2022 ambapo imeelezwa kuwa kukamilika kwake kutaokoa matumizi ya kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kinalipwa kama kodi ya pango kutokana na Wakala kutumia majengo ya kukodi kwa ajili ya Ofisi yake kuu kwa muda mrefu.


Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi Kuu ya Wakala wa Vipimo umesimamiwa na Mshauri Elekezi Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

WAZIRI WA BIASHARA NA MAENDELEO YA VIWANDA ZANZIBAR AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI WA SADC



Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika jijini Harare, Zimbabwe kuanzia tarehe 12 hadi 14 Machi, 2025. 

 

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao mbalimali ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu, pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali ikiwemo kutathmini utekelezaji wa Maamuzi  ya Baraza na yale ya  Wakuu wa Nchi na Serikali pia utajadili Mpango wa Bajeti ya Jumuiya ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 hususan katika kutekeleza maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa kwenye  Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (RISDP) wa mwaka 2020-2030.


Agenda za Tanzania za kipaumbele katika Mkutano huo ni pamoja na kuhimiza kufanyika kwa tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika Lugha ya Kiswahili baada ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC.

 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Mhe. Prof. Dkt. Amon Murwira amesema umefika wakati sasa kwa Nchi Wanachama wa SADC kuwekeza katika rasilimali ilizojaliwa ikiwemo watu na maliasili ili kuiwezesha Jumuiya kufikia malengo iliyojiwekea kupitia program mbalimbali za maendeleo zikiwemo zile za viwanda na miundombinu ya kuinganisha kanda na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje.

 

Amesema Baraza hilo limepewa jukumu la kusimamia ufanisi katika kanda kwa kuhakikisha kwamba sera zinaendana na dira ya SADC ya kuweka mbele maslahi ya watu wake kwa kuhakikisha maisha na vipato vyao vinabadilika, hivyo  Mkutano huo  uwe jukwaa ambalo litajadili na kuja na mapendekezo ya namna ya kujipanga kama kanda na kumiliki agenda yake ya maendeleo ikiwemo kuja na mikakati ya kutumia rasilimali lukuki zilizopo ikiwemo watu ili kupiga hatua za maendeleo zilizokusudiwa. 


“Upatikanaji wa rasilimali fedha na nyingine zinazohitajika ni muhimu katika mustakabali wa Kanda yetu. Tunatakiwa kuunganisha nguvu zetu ili kutekeleza agenda zetu za maendeleo ikiwemo kukuza viwanda. Hii ni pamoja na kuongeza thamani kwa rasilimali nyingi tulizojaliwa na hapa nasisitiza kuwa, SADC tunayoitaka itajengwa na watu wake wenyewe” alisisitiza Mhe. Prof. Murwira.


Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi amesema bado suala la amani na usalama katika kanda linapewa kipaumbele ambapo jitihada za Nchi Wanachama zinaendelea katika kutafuta suluhu ya kudumu hususan katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).


Akizungumzia umuhimu wa nishati katika maendeleo ya Kanda, Bw. Magosi amesema jitihada zaidi zinahitajika ili kuwezesha takriban raia milioni 172 sawa na asilimia 29 wa SADC ambao wanaishi bila nishati ya umeme kufikiwa na huduma hiyo na kuutaja Mkutano kuhusu Nishati uliofanyika Tanzania mwezi Februari, 2025 chini ya uenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kama moja ya hatua za mfano zinazopaswa kuchukuliwa katika kukabiliana na changamoto hiyo.


Mbali na Waziri Shaaban, ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,  Balozi Said Shaibu Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Suleiman Hassan Serera, Mratibu wa Kitaifa wa masuala ya SADC ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.


Baraza la Mawaziri ni chombo muhimu katika SADC ambacho  kinahusika na kusimamia uendeshaji wa SADC ili kuhakikisha sera na maamuzi mbalimbali yanayofikiwa kwenye vikao yanafanyiwa kazi ipasavyo. Baraza hili linaundwa na Mawaziri kutoka  Nchi Wanachama 16 za SADC, hususan kutoka katika Wizara zinazoshughulikia masuala ya Mambo ya Nje, Mipango na Fedha au Biashara, na hukutana mara mbili kwa mwaka.

TANZANIA HAINA UGONJWA WA MARBURG, TUMEUDHIBITI



Na WAF - Biharamulo, Kagera


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Tanzania imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa mlipuko wa Marburg na ameutangazia Umma wa Watanzania kuwa ugonjwa huo umeisha kutokana na kutokuwepo kwa mgonjwa mwengine yeyote tangu mgonjwa wa mwisho alipopatikana tarehe 28 Januari, 2025 na hadi kufikia tarehe 11 Machi, 2025 siku 42 zimepita. 


Waziri Mhagama amethibitisha hayo leo Machi 13, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wilayani Biharamulo, Kagera kwamba siku 42 zimepita tangu mgonjwa wa mwisho alipofariki  mgonjwa wa mwisho afariki na kisayansi Tanzania inakidhi vigezo vya kutangaza kuwa mlipuko huo umeisha.


"Tarehe 20 Januari, 2025, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliutangazia umma na jamii ya Kimataifa juu ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg uliotokea katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, naomba nichukue fursa hii leo tarehe 13 Machi, 2025 kuutangazia umma na jamii ya Kimataifa kuwa, sasa Tanzania haina mlipuko wa ugonjwa wa Marburg," amesema Waziri Mhagama.


"Ugonjwa wa “Marburg” ni miongoni mwa magonjwa hatari yanayotokana na virusi ambavyo husababisha kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili na husambaa kwa haraka kwa kupitia kugusa majimaji ya mwili wa mtu au mnyama aliyeathirika na ugonjwa huo ambao husababisha madhara mbalimbali ikiwemo ulemavu na vifo," amesema Waziri Mhagama


Aidha, Waziri Mhagama ameendelea kuwakumbusha Watanzania juu ya kuchukua tahadhari kwakuwa nchi zinazotuzunguka zinaendelea kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Mpox na Ebola, hivyo nchi yetu pia ipo kwenye hatari kutokana na mwingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi, pamoja na uwepo wa mipaka ya moja kwa moja baina ya nchi hizi. 


"Hivyo naomba niwasihi wananchi wote kuendelea kushirikiana na wataalam wa afya na mamlaka husika ili kuendelea kutekeleza afua za kujikinga na magonjwa haya, na sisi kama Serikali tumedhamiria kuhakikisha tunaimarisha zaidi huduma za tiba kwa wagonjwa wakati wa dharura na mlipuko," amesema Waziri Mhagama.


Pia, Waziri Mhagama amesema dhamira ya Serikali ya kujenga hospitali maalum kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa ya mlipuko katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera iko palepale pamoja na kuongeza maabara jongezi yenye uwezo wa kupima magonjwa ambukizi ya mlipuko ili  kujihakikishia kinga na udhibiti zaidi wa magonjwa hayo. 


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajat Fatma Mwassa ametoa shukran kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akielekeza na kutoa ushauri wa jinsi ya kudhibiti ugonjwa wa Marbug pamoja na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama aliyekuwa msimamizi wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais na hatimaye kuumaliza ugonjwa huu.


"Lakini pia Mhe. Waziri tunakushukuru kwa kuweka kipaumbele cha kujenga hospitali ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko hapa Biharamulo, kuwa na wodi ya kwanza ya kuwatenga wagonjwa wa mlipuko ambayo itaanza kujengwa hapa pamoja na kutupatia vifaa vya mobile lab kwa ajili ya kupima magonjwa mbalimbali ya vihatarishi na sisi kama mkoa tutaendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa magonjwa haya hujirudia," amesema Hajat Mwassa.


Naye, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema kuwa Serikali imeimarisha miundombinu mbalimbali ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo uimarishaji wa maabara zenye uwezo wa kupima magonjwa ya mlipuko hasa za Taifa, utolewaji wa elimu ya afya kwa umma hasa katika mikoa inayopakana na nchi jirani pamoja na upatikanaji wa huduma za maji safi na salama. 


"Mhe. Waziri, katika jitihada hizi tumeshirikiana na wenzetu wa Wizara za kisekta pamoja na wadau wakiwemo wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Wizara ya Habari pamoja na wadau wa maendeleo wakiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Charles Sagoe-Moses.

RIBA YA HUDUMA NDOGO YA FEDHA NI ASILIMIA 3.5 KWA MWEZI


 

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara wametakiwa kujua kiwango cha juu cha riba kinachopaswa kutolewa kisheria na vikundi na watoa huduma ndogo za fedha ili kutoingia kwenye mikopo yenye riba kubwa itakayosababisha washindwe kurejesha mikopo.

 

Hayo yameelezwa na Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Khalfan Kimaro, alipokuwa akitoa elimu ya Fedha kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.

 

Bw. Kimaro alisema kuwa  kuna kiwango cha juu cha riba ambacho Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka kwa watoa huduma ndogo za fedha ambacho hutolewa kabla ya mtoa huduma kupewa leseni na ndicho kinachostahili kutozwa mtu anapochukua mkopo.

 

“Ukiachana na mabenki, kiwango cha juu cha riba kinachopaswa kutozwa na watoa huduma ndogo za fedha na vikundi ni asilimia 3.5 kwa mwezi na kwa mwaka ni asilimia 42, kinyume na hapo ni kukiuka miongozo na taratibu za huduma hiyo”, alisema Bw. Kimaro.

 

Alisema kabla ya kuchukua mkopo ni vema kujilidhisha na kiwango cha riba na pia ukopaji uelekezwe kwenye kuzalisha kitu ambacho kitaweza kurejesha mkopo kwa muda uliowekwa na iwapo mkopo umechukuliwa kwa shughuli za kijamii ni vema kukawa na chanzo kingine cha mapato ambacho kitaweza kurejesha mkopo huo bila kuathiri familia.

 

Aidha alisema kuwa kabla ya kukopa ni vema kusoma mkataba vizuri na iwapo haujaeleweka mkopaji anatakiwa kupata ushauri kwanza ili kuepuka kuingia kwenye hasara.

 

Vilevile aliwataka watumishi kufuatilia michango inayotakiwa kuwasilishwa na Mwajili kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kwa kuwa iwapo kutakuwa na miezi ambayo mchango haujawasilishwa itasababisha usumbufu wakati wa kudai mafao mtumishi anapostaafu.

 

Kwa upande wa uwekezaji, Afisa Masoko Mwandamizi wa Kampuni ya Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, alisema kuwa uwekezaji unafanyika ili kutunza thamani ya fedha kwa kuwa fedha ina tabia ya kupungua thamani kadri miaka inavyosogea.

 

Bw. Mwanga aliwataka watumishi kuwekeza kwenye Hati Fungani za Serikali na Hisa ili kuwa sehemu ya umiliki wa Kampuni ambapo inasaidia kupata faida kupitia gawio na  kuuza Hisa wakati inapopanda thamani.

 

Alisema kuwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam kuna Kampuni 28 ambazo mtumishi anaweza kuwekeza ikiwa ni pamoja na kampuni za ndani na nje ya nchi ambapo uwekezaji kwenye Hisa unatakiwa kuwa wa muda mrefu kwa kuwa Hisa zina tabia ya kupanda na kushuka.

 

Kwa upande wa watumishi wa Wilaya hiyo, waliipongeza Serikali kwa mpango huo wa kutoa elimu ambapo wameeleza kuwa elimu hiyo ingewahi ingewanusuru watumishi wengi hususani wa umma kuingia kwenye migogoro na umasikini kutokana na kukosa elimu sahihi kuhusu mikopo na uwekezaji na pia kujiwekea mazingira mazuri kabla ya kustaafu.

IRAN NA TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO

 


Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El maamry Mwamba amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Nikhal, katika ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, ambapo pa moja na mambo mengine wamezungumza na kukubaliana masuala mbalimbali ya Ushirikiano hususan katika masuala ya uchumi, biashara na uwekezaji.

Utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo

 

Kutoka TMA mamlaka ya hali ya hewa imetoa mwenendo wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo.

ELIMU YA FEDHA KUYAFIKIA MAKUNDI YOTE


Serikali inatambua umuhimu wa kuhakikisha kwamba makundi yote maalumu, yakiwemo watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi), wanawake, vijana, na wazee, wanapata elimu ya fedha nchini ili waweze kujikwamua kiuchumi. 


Hayo yameelezwa na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya , wakati wa mafunzo kwa watu wenye ulemavu wa kusikia yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.


“Elimu hii inalenga kuyawezesha makundi haya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kuwajenga uwezo wa kusimamia rasilimali zao, na kuboresha maisha yao kwa ujumla”, alisema Bw. Kibakaya.


Alisema kuwa katika utoaji wa elimu ya fedha katika makundi mbalimbali nchini, washiriki wamepewa elimu katika maeneo ya usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji  akiba, mikopo, uwekezaji, bima, bima ya amana, kodi na kujipanga kwa maisha ya uzeeni.


Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Athuman Khalid (mlemavu wakusikia) alieleza furaha yake kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo ya elimu ya fedha.


“Kwa muda mrefu tulihisi kutengwa katika masuala ya fedha, lakini leo tumefikiwa na kupewa elimu kuhusu kupanga matumizi, kujiwekea akiba, kufanya uwekezaji na kutumia Taasisi rasmi kuchukua mikopo”, alisema Bw. Khalid.


Naye Mkalimani, Bi. Dainess Wilson, aliiomba Serikali kuendelea kutoa mafunzo endelevu kwa Wakalimani nchini ili kuboresha ujuzi na weledi wao katika kazi na kutoa huduma za utaalamu wa hali ya juu na kuongeza tija katika utendaji wao.


Wizara ya Fedha kwa kutambua umuhimu wa mchango wa Taasisi za Fedha Timu ya Wataalamu kutoka wizarani ambayo ipo mkoani Mara kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali imeambatana na Wataalamu kutoka  Taasisi nyingine za Serikali, ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na  NSSF, pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki ya Biashara Tanzania (TCB), CRDB, NMB, NBC.

DKT. NCHEMBA ASHIRIKI MKUTANO WA 50 WA BODI YA WADHAMINI YA BENKI YA EADB

 


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Mawaziri wenzake wa Fedha, Mhe. Matia Kasaija (Uganda), Mhe. Ng’ongo John Mbadi (Kenya) na Mhe. Yusuf Murangwa (Rwanda) wameshiriki Mkutano wa 50 wa Bodi ya Wadhamini (Governing Council) ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), unaofanyika leo tarehe 13 Machi 2025, katika Hoteli ya Serena, Kampala-Uganda.


Tanzania ikiwa moja wa nchi Wanahisa wa Benki hiyo na inanufaika kwa ufadhili wa miradi ya kimkakati na ya kijamii ikiwemo Mradi wa Reli ya Kisasa SGR pamoja na Benki hiyo kuiwezesha Sekta Binafsi ya Tanzania kupata mikopo yenye riba nafuu.


Mkutano huo umewashirikisha Wadhamini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Benard Mono.