
Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bw. Erick Mvati, akikabidhiwa vipeperushi na
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha
Bw. Santley Kibakaya, vyenye mada mbalimbali ikiwemo akiba, mikopo na uwekezaji
ambazo zitafundishwa kwa wananchi wa Halmashauri hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bw. Erick Mvati, akiwasikiliza Timu ya wataalamu
kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambao walifika ofisini kwake
kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo
mbalimbali ya Halmashauri hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bw. Erick Mvati, akizungumza alipokutana na Timu
ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake ambao walifika ofisini
kwake kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo
mbalimbali ya Halmashauri hiyo.
Afisa Masoko
Mwandamizi, Kampuni ya Uwekezaji ya UTT – AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akiwafungulia
akaunti ya uwekezaji watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza baada ya
mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Baadhi ya watumishi wa
Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wakifuatilia mada mbalimbali ikiwemo akiba,
mikopo, uwekezaji, bima, kujiandaa kustaafu wakati wa mafunzo ya elimu ya
fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Afisa Usimamizi wa
Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth
Mnzava, akiteta jambo na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza,
baada ya kumalizika kwa mafunzo ya elimu ya fedha kwa watumishi hao
yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Afisa Sheria
Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Bw. Ramadhani Myonga, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa watumishi wa
Halmashauri ya Jiji la Mwanza, yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
(Picha na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini WF, Mwanza)
.........................
Na. Josephine Majura,
WF, Mwanza
Watumishi wa Umma na
Sekta Binafsi wameshauriwa kujifunza kuhusu uwekezaji mapema ili kuhakikisha
kuwa baada ya kustaafu wanaendelea kuishi maisha mazuri, kama walivyokuwa
kazini.
Ushauri huo umetolewa
na Afisa Masoko Mwandamizi, Kampuni ya Uwekezaji ya UTT – AMIS, Bw. Rahim
Mwanga, wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa kwa watumishi wa
Halmashauri hiyo na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Aliongeza kuwa
kustaafu hakupaswi kuwa chanzo cha matatizo ya kifedha, kwa mfanyakazi yoyote
aliyekuwa analipwa mshahara bali iwe fursa ya kufurahia matunda ya kazi ya muda
mrefu.
“Tukijijengea
utamaduni wa kuwekeza mapema kutatusaidia sisi wafanyakazi kuepuka changamoto
za kifedha baada ya kustaafu na kuwa na maisha ya uhakika”, alisema Bw. Mwanga.
Aidha aliwasisitiza
wafanyakazi wote nchini kuhakikisha michango yao inalipwa kwa wakati na waajiri
wao lakini pia watumie Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotoa faida kubwa.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bw. Erick Mvati, aliipongeza
Wizara ya Fedha kwa kufika katika Mkoa wa Mwanza kutoa elimu ya fedha ambayo ni
muhimu kwa wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Aliongeza kuwa elimu
hiyo ikifika kwa wananchi wote katika makundi mbalimbali itasaida kupunguza
matatizo katika jamii kwa kuwa wananchi wataelewa haki zao lakini pia watajua
sheria mbalimbali zitakazowaongoza na kujiepusha na migogoro ya mikopo.
Naye Afisa Usimamizi
wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Santley
Kibakaya, alisema kuwa Wizara inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya fedha kwa
wananchi ili wafahamu fursa mbalimbali zinazopatikana katika Sekta ya Fedha.
Aliongeza kuwa Sekta
ya Fedha imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, kupitia elimu hiyo
inayoendelea kutolewa, wataalamu hao wanapata fursa ya kusikiliza changamoto,
ushauri na maoni yanayotolewa na wananchi kwa ajili ya kufanyiwa utatuzi zile
ambazo zinatakiwa kufanyiwa utatuzi, ushauri na maoni kwa ajili ya kuboresha
zoezi hilo kwa mikoa ambayo haijafikiwa.