JSON Variables

Sunday, March 30, 2025

WAUMINI  WA  DINI  YA  KIISLAAM   MKOANI TANGA  WATAKIWA KUYAISHI  YALE  WALIYOJIFUNZA  KATIKA MWEZI MTUKUFU  WA RAMADHANI

...................

TANGA - Wumini wa dini ya Kiislam  na  Watanzania  kwa ujumla  wametakiwa kuyaishi yale waliyojifunza ndani ya Mwezi mtukufu wa Ramadhan ikiwa ni pamoja kujenga tabia ya kuwa na hofu ya Mungu.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti  wa Chama cha Mapinduzi  (CCM) Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa,  Rajabu   Abdulrahman wakati akitoa salamu zake kuelekea  Sikuku  ya Iddi  el Fitri ambayo inatarajiwa kuswaliwa  Machi 31 mwaka  huu sawa na Mwezi Mosi Shaawal mwaka 1446.

Aidha Rajab  Abdulrahmana amewapongeza wafanyabiashara wa Mkoa  wa Tanga kwa kuuheshimisha mwezi wa Ramadhan kwa kutopandisha bei za bidhaa zao  tofauti na miaka mingine .

"Niwapongeze sana wafanyabiashara wa Mkoa wa tanga bei za bidhaa ukiangalia kwa upatikanaji wake kabla ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na ndani ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani  bei ni zile zile kwa hiyo tunawashukuru na tunawapongeza na tunapokwenda kuimaliza ibada hii ya mwezi mtukufu wa Ramadhani nipende kuwaasa sana wana Tanga wenzangu tuendelee kuishi kwa namna ambavyo Mwenyezi mungu (S.W) ametuamrisha, tuache yale yote Mwenyezi Mungu ametukataza na hiyo maana halisi ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani" amesema Rajabu  Abdulrahman.

Katika hatua nyingini mwenyekiti huyo wa CCM  Mkoa amewataka wakazi wa Mkoa Tanga kuendelea kudumisha amani, upendo,Umoja na Mshikamano  huku akionya wale wale wote wenye nia  ovu ya  kupanga ama kujaribu kuleta vurugu ndani mkoa wa Tanga.

"Tusikubali waje watu waturubuni kwa maneno ya kisiasa, waje watu waturubuni kwa nama wanavyojua wao wenyewe kwa waliowatuma kuvunja amani ndani ya mkoa wetu wa Tanga,Tumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais amejipambanua wazi katika suala zima la amani wenye kuichezea amani hana msalie Mtume kwa sabababu tunajua madhara yake " amesema  Mwenyekiti wa ccm Mkoa wa Tanga  Rajab Abdul Rahman.

Mbali na hayo Rajab Abdulrahman amewataka wakazi wa Mkoa  wa Tanga  kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa na afya njema ili aweze kuwatumikia Watanzania.

</

Friday, March 28, 2025

TAASISI ZA FEDHA ZATAKIWA KUTOA ELIMU KWA WAKOPAJI KABLA YA KUWAPA MIKOPO


Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.

Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha wakiangalia filamu yenye mada mbalilimbali ikiwemo mikopo, akiba na uwekezaji zilizofundishwa wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Buchosa, Mwanza)

...............

Na. Josephine Majura, WF, Buchosa, Mwanza

Serikali imezitaka Taasisi za Fedha nchini kutoa elimu kwa wakopaji ili wawe na uelewa mpana kuhusu masharti ya mikopo, viwango vya riba, gharama za ziada, na athari za kutorejesha mkopo kwa wakati kabla ya kusaini mikataba husika.
 
Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake kwa wananchi wa Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
 
Alifafanua kuwa Taasisi za Fedha zinapaswa kutoa taarifa sahihi na mafunzo kwa wateja wao kabla ya kusaini mikataba ya mikopo ili kuhakikisha wanachukua uamuzi wa kukopa wakiwa na taarifa sahihi. 
 
“Serikali inaendelea kuweka sera na miongozo inayolinda wakopaji dhidi ya unyonyaji wa kifedha na kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa maendeleo ya kiuchumi”, alisema Bw.  Myonga.
 
Aliongeza kuwa kukiwa na uwazi  katika utoaji mikopo na elimu ikatolewa vizuri kwa wakopaji kutapunguza unyonyaji wa kifedha na kutawasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kwenye mikopo wanayoomba.
 
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Halmashauri ya Buchosa, Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Bi. Grace Machunda, aliwahamasisha wanavikundi mbalimbali nchini kusajili vikundi vyao ili kupata mikopo ya Serikali na kusaidiwa kisheria kutakapotokea changamoto kwenye vikundi.
 
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha, mkazi wa Buchosa, Bw. Musa Kilaba, aliwashauri washiriki wenzake wa mafunzo hayo kwenda kufanyia kazi  walichofundishwa.
 
Bw. Kilaba aliishauri Serikali kuongeza semina za mafunzo ya elimu hiyo katika ngazi zote nchini na kuongeza idadi wa watoa elimu ili waweze kuwafikia wananchi wengi kwa mara moja.
 
Naye Bi. Laurencia Msabi, mkazi wa Buchosa, aliahidi kuwa Balozi wa elimu ya fedha katika vikundi ambavyo ni mwanachama  na jamii inayomzunguka.

SERIKALI: TUNATAMBUA MCHANGO WA WATOA HUDUMA ZA FEDHA


Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, Mhe. Christopher Ngubiagai, akizungumza alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambao walifika ofisini kwake kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe , mkoani Mwanza, Bw. Goodlucky Mtigandi, akikabidhiwa vipeperushi na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, vyenye mada mbalimbali ikiwemo akiba, mikopo na uwekezaji ambazo zitafundishwa kwa wananchi wa Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, Mhe. Christopher Ngubiagai, akizungumza alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambao walifika ofisini kwake kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Bw. Goodlucky Mtigandi, akizungumza alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambao walifika ofisini kwake kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, akigawa vipeperushi vyenye mada mbalimbali ikiwemo akiba, uwekezaji, mikopo kwa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake, wilayani Ukerewe, Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, Mhe. Christopher Ngubiagai, akiwasikiliza Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambao walifika ofisini kwake kujitambulisha ili kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Nansio, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Afisa Masoko Mwandamizi, Kampuni ya Uwekezaji ya UTT – AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Nansio, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha mkazi wa Nansio, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, Bw. Octavius Kasyololo, akiuliza swali kuhusu kiwango cha riba wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Afisa Biashara, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha, Bw. Mango Chacha, akitoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wakazi wa Nansio, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza walioshiriki mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha na Taasisi zake.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Ukerewe, Mwanza)

..............


Na. Josephine Majura, WF, Ukerewe, Mwanza

Serikali imesema inatambua mchango mkubwa wa watoa huduma za kifedha nchini katika kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanapata fursa ya kufanya miamala ya kifedha kwa urahisi, hasa katika maeneo ambayo benki hazijafika.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mkoa wa Mwanza, Mhe. Christopher Ngubiagai, alipokutana na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambayo ipo mkoani Mwanza kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali.

Aliongeza kuwa watoa huduma za fedha wamekua na mchango katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kuwa kupitia watoa huduma hao wananchi wameweza kupata mikopo, kujiwekea akiba na kufanya malipo kwa njia za kidijitali.

“Serikali itaendelea kushirikiana na watoa huduma za fedha nchini ili kuhakikisha kuwa huduma hizi zinaimarishwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan waliopo vijijini na maeneo ya mbali.” Alisema Mhe. Ngubiagai.

Alifafanua kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na watoa huduma za fedha nchini, aliwataka kufuata sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha usalama wa mifumo ya kifedha, ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha na kukuza uaminifu katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Bw. Goodlucky Mtigandi, alisema mafunzo ya elimu ya fedha yamefika wakati muafaka kipindi ambacho wanashughulikia migogoro mbalimbali ya mikopo umiza.

“Tuamini mafunzo haya yatawasaidia wananchi kutambua umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha kwa maisha ya leo na kesho”, alisema Bw. Mtigandi.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, alizisisitiza Taasisi za Fedha zinazotoa mikopo kwa wananchi kuhakikisha wanarudisha dhamana kwa wakopaji mara tu wanapomaliza marejesho ya mikopo.

Akizungumza baada ya kupatiwa mafunzo ya fedha mmoja wa washiriki, ambaye ni Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Wilaya ya Ukerewe, Bw. Baraka Jeremiah, aliiomba Serikali kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa mkopaji na mkopeshaji ili pande zote mbili zijue haki, wajibu na sheria zinazotakiwa kufuatwa.

Wednesday, March 26, 2025

RAIS SAMlA AFANYA MAZUNGUMZO NA MJUMBE MAALUM WA RAIS TSHISEKEDI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mhe. Félix Antoine Tshisekedi ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo Mhe. Thérèse Kayikwamba Wagner, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 26 Machi, 2025. 

RAIS SAMIA AFTURISHA WATOTO KIKOMBO DODOMA

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza wakati wa  iftar iliyofanyika kwenye  Makao ya Taifa  ya Watoto Kikombo jijini Dodoma Machi 25, 2025 katika iftar iliyoandaliwa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naibu Waziri Mwanaidi alimwakilisha Rais Samia katika shughuli hiyo.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akipokea msaada wa vifaa mbalimbali kwaajili ya watoto wanaolelewa kwenye Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo wakati wa  iftar iliyofanyika kwenye  Makao hayo jijini Dodoma Machi 25, 2025 katika iftar iliyoandaliwa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naibu Waziri Mwanaidi alimwakilisha Rais Samia katika shughuli hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu  akishiriki   iftar iliyofanyika kwenye  Makao ya Taifa  ya Watoto Kikombo jijini Dodoma Machi 25, 2025 katika iftar iliyoandaliwa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis  i alimwakilisha Rais Samia katika shughuli hiyo.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
Na WMJJWM- Dodoma 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewafuturisha Watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Dodoma katika Kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Akizungumza wakati wa Iftari hiyo iliyofanyka Machi 25,2025 kwa niaba yake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alitoa shukurani kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yenye lengo la kuondoa kabisa changamoto zinazowakabili watoto walio katika mazingira hatarishi. 
“Kipekee kabisa, ninamshukuru tena Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kufuturisha watoto wanaoishi katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo pamoja na maeneo mengine ya nchi hususani Watoto wa Mkoa wa Arusha na Dar Es Salaam”. ameeleza Naibu Waziri Mwanaidi.
Aidha aliongeza kuwa Wizara inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na wadau kwa lengo la kuhakikisha watoto walio katika mazingira hatarishi wanapatiwa huduma ya malezi ya muda mfupi katika Makao ya Watoto.
“Serikali na Wadau tutaendelea kushirikiana kutoa huduma kulingana na sheria, kanuni na miongozo tuliyojiwekea, nitumie fursa hii kuwaomba wamiliki wa makao ya kulelea watoto kuhakikisha mnatoa huduma kwa mtoto kwa kuzingatia maslahi mapana ya mtoto”. amesema Naibu Waziri Mwanaidi.
Mhe. Mwanaidi alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi, walezi na watendaji wa Wizara kwa kuendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika makao yote hapa nchini. 
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt.John Jingu amewasihi watoto waishio katika makao hayo kuishi kwa upendo na amani huku wakiweka bidii katika masomo yao na stadi za kazi kwa ujumla ili waweze kufikia malengo yao ya baadae.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Abbot fund Edna Hauli ameipongeza Serikali kwa juhudi zake katika kuhakiksha watoto wanakuwa salama na kuahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao muhimu na kuweza kufikia utimilifu wao kama binadamu.
Sanjari na hilo katika tukio hilo pia kuliambatana na tukio la kukabidhi mashine ya kufulia 4, printer na photocopy mashine 1, vitabu 1670 friji 2 nguo na mahitaji mengine ambavyo vilitolewa na Shirika la Abbot Fund vikiwa na thamani ya shiling Milioni 88 ili viweze kurahisisha majukumu ya utendaji kazi ndani ya Makao hayo.

DCEA YAMNASA KINARA WA MIRUNGI, YATEKETEZA EKARI 285.5 SAME

Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo akiwa katika operesheni ya uteketezaji wa mashamba ya mirungi iliyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 25 Machi wilayani Same, Kilimanjaro.

............................

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 19 hadi 25 Machi 2025. 

Katika operesheni hiyo, ekari 285.5 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa na watuhumiwa saba (7) wamekamatwa, akiwemo kinara wa biashara haramu ya mirungi nchini aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, Interindwa Zinywangwa Kirumbi, maarufu kwa jina la mama Dangote.

Akizungumza baada ya operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo, amesema kuwa, mama Dangote ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini. Kwa zaidi ya miaka 30, amekuwa akiendesha mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hizo za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya kujua kuwa ni kinyume cha sheria.

Aidha, kamishna Lyimo ameongeza kuwa, mwaka juzi Mamlaka ilifanya operesheni wilayani humo na kutoa elimu kwa wananchi ili waachane na kilimo cha mirungi na badala yake wajikite katika kilimo cha mazao mbadala pamoja na ufugaji.

“Mwaka juzi tuliteketeza jumla ya ekari 535 za mashamba ya mirungi. Kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya, tulitoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya, ikiwemo mirungi. Lengo lilikuwa kuwawezesha wakazi wa eneo hili kujikita katika kilimo cha mazao mbadala na ufugaji kama njia ya kujiongezea kipato” alisema Kamishna Jenerali Lyimo.

Pia, Kamishna Lyimo alieleza kuwa, pamoja na jitihada hizo, uongozi wa wilaya ya Same na Wizara ya Kilimo na mifugo waliwapelekea wananchi wa maeneo hayo miradi ya ufugaji wa nguruwe na kugawa miche ya kahawa, iliki na mazao mengine.
Kutokana na juhudi hizo, wananchi wengi wameachana na kilimo na mirungi na kuanza kulima mazao mbadala, japo wapo wananchi wachache waliokaidi na kuendelea na kilimo na biashara ya mirungi.

Kamishna Lyimo amesisitiza kwamba Mamlaka itaendelea kufanya operesheni kuhakikisha wananchi wote wanaojihusisha na biashara ya mirungi wanakamatwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunatokomeza biashara na matumizi ya mirungi hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa, eneo hili la Same ni kitovu cha uzalishaji mirungi nchini hali inayohatarisha ustawi wa taifa letu ndio maana tunafanya operesheni hizi endelevu nchi nzima kuhakikisha tunadhibiti uzalishaji,usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya za mashambani na viwandani ili zisiendelee kuathiri wananchi”, amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.

Kwa upande wake Agness Mshana mtendani wa kata ya Ekondi amekiri kutambua uwepo wa watu wanaojihusisha na kilimo cha mirungi na wao kama serikali wameendelea kutoa elimu juu ya madhara ya mirungi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata mazao mbadala ili kuepukana na kilimo hicho.

“Tumejitahidi kuwaletea mradi wa nguruwe pamoja na miche ya miparachichi na kuwapa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa maana mirungi inamadhara mengi yakiwemo kuchanganyikiwa, kupoteza nguvu za kiume, kushindwa kuhudumia familia vizuri, kupata kansa na kadhalika”, alieleza Agness

Naye Bi. Hawa, mwananchi wa kata ya Tae wilaya ya Same amesema kuwa, hajui sababu ya watu kuendelea kujihusisha na kilimo cha mirungi kwani, kuna mazao mengi yanayostawi kama vile vitunguu, karoti na iliki pamoja na miradi ya nguruwe iliyoletwa na serikali. Aidha, ameiomba serikali kuimarisha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayozalishwa kupelekwa sokoni, hali itakayosaidia wananchi kuwa na uhakika wa masoko ya mazao yao na hivyo kuachana na biashara ya mirungi.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya inatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wazalishaji, wasambazaji, na watumiaji wa dawa za kulevya. Ushirikiano huu utasaidia kutokomeza kabisa biashara hii haramu na kulinda ustawi wa jamii. Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika ili kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa salama na lenye maendeleo endelevu.
Uteketezaji wa mirungi kwenye baadhi ya mashamba wakati wa operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wilayani Same.
Muonekano wa baadhi ya maeneo yanayozalisha mirungi katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro


TANZANIA, UHOLANZI WAZINDUA MRADI WA MTAALA WA KUKU UTAKAOTUMIKA VYUONI

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Utabibu wa Wanyama Tanzania (TVLA), Dkt Stella Bitanyi akizungumza na watafiti, watunga sera, wageni, wakulima na wadau wa ufugaji wa kuku wakati wa uzinduzi wa mradi wa tathmini ya mtaala wa ufugaji wa kuku Dar es Salaam jana.
Mshauri wa Masuala ya Ushirikiano wa Kiuchumi kutoka Ubalozi wa Uholanzi, John Mike Jagger, akizungumza na wageni wakati wa uzinduzi wa mradi wa kutathmini mtaala wa mafunzo ya ufugaji kuku hapa nchini  
Mgeni rasmi, Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala wa Maabara ya Utabibu wa Wanyama Tanzania (TVLA), Dkt Stella Bitanyi, na Mshauri wa Masuala ya Ushirikiano wa Kiuchumi katika Ubalozi wa Uholanzi, John Mike Jagger, wakifungua pazia kuonyesha uzinduzi rasmi wa mradi huo wa kutathmini mtaala wa ufugaji wa kuku hapa nchini uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Wa pili kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala wa Mafunzo ya Vyuo vya Mifugo nchini (LITA).
Mshauri wa Kilimo kutoka Ubalozi wa Uholanzi nchini, Theo Mutabingwa, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa kutathmini mtaala wa ufugaji wa kuku kwa ajili ya vyuo vya ufundi na wafugaji nchini

..........................

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ubalozi wa Uholanzi Tanzania na wadau wa ufugaji wa kuku kwa pamoja wamezindua mradi wa kutathmini mtaala wa mafunzo ya ufugaji wa kuku kwa vyuo vya mifugo, unaolenga kuongeza ufanisi na uzalishaji wa kuku nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Utabibu wa Wanyama Tanzania (TVLA), Dkt Stella Bitanyi, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, alisema mradi huo unalenga kuweka misingi katika kuboresha mtaala wa ufundishaji wa ufugaji wa kuku.

Aliongeza kwamba mradi huo unakuja na majawabu ya namna bora ya kufundisha Watanzania wakulima, hasa wanawake na vijana jinsi ya ufugaji bora wa kuku wa kibiashara na kwa vitendo zaidi.

 Alisema nchini Tanzania, asilimia 96 ya wakulima wa mifugo wanafuga kuku wa kienyeji, mara nyingi katika makundi madogo ya kuku kwa wastani wa hadi kuku 20, lakini hutoa chini ya asilimia 20 ya mahitaji ya nyama ya kuku na mayai nchini.

“Kasi ya ukuaji wa sekta hii ni ndogo, ikiwa ni wastani wa asilimia 2.6 kwa mwaka, uzalishaji wa mayai ni chini ya mayai bilioni 2.5 kwa mwaka, na kiwango cha matumizi ni sawa na yai moja kwa kila mtu kwa wiki,” alisema.

Alieleza kwamba kuku mmoja kwa kila mtu kwa mwaka, matumizi yanapendelea kwa wakazi wa maeneo ya mijini na wenye kipato cha kati hadi cha juu, lakini mahitaji ni makubwa nchi nzima.

Alisisitiza kwamba ufugaji wa kuku ni mojawapo ya njia bora za kupunguza umaskini hasa kwa wanawake na ajira kwa vijana katika ufugaji wa kuku.

Dkt Bitanyi aliongeza kwamba mradi wa kupitia mtaala wa tathmini ya ufugaji wa kuku ni muhimu kwa sababu unachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha lishe na usalama wa chakula ili kuhakikisha ukuaji endelevu wa sekta hiyo.

“Sekta ya ufugaji wa kuku nchini Tanzania inakua kwa kasi kutokana na mahitaji ya protini yanayoongezeka kulingana na idadi ya watu inayokua kwa haraka, lakini sekta hii bado inafanya kazi kwa njia ya kiasili zaidi katika muundo usio rasmi,” alieleza.

Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi Dar es Salaam, Mshauri wa Masuala ya Uchumi, John Mike Jagger alisema wao kama Ubalozi na makampuni ya Uholanzi wanafurahi kuzindua mradi huu unaolenga kuharakisha maendeleo ya ufugaji wa kuku.

“Sekta ya ufugaji wa kuku nchini Tanzania ina uwezo mkubwa na inakua kwa kasi, ikiongozwa na mahitaji ya protini kwa sababu ya idadi ya watu inayokua kwa haraka,” alisema.

Aliongeza kwamba ingawa sehemu kubwa ya sekta hii bado inafanya kazi kwa njia isiyo rasmi, wakulima wengi wa kuku wanahama kutoka kwa kilimo cha kujikimu kwenda kwenye uzalishaji wa kibiashara.

Jagger alifafanua zaidi kwamba mradi wa tathmini ya mtaala wa ufugaji wa kuku utaleta fursa zinazovutia zitakazowezesha wakulima kupata maarifa sahihi, mafunzo, na maendeleo ya ujuzi katika sekta ya ufugaji wa kuku na kuongeza ajira nchini.

“Kuwekeza katika elimu na maendeleo ya ujuzi ni muhimu kwa kuboresha ufanisi, na uzalishaji endelevu katika sekta hii,” alisema.

Johan Hissink, kutoka Mradi wa Kituo cha Mafunzo cha Aeres, Uholanzi, alisema kwa kushirikiana na Wakala wa Mafunzo wa Vyuo vya Mifugo nchini (LITA) wataainisha changamoto, matatizo, na vikwazo vya sekta ya ufugaji wa kuku nchini Tanzania na kushirikiana kupitia mtaala ili kuyashughulikia kwa ufanisi.

“Tupo hapa kusaidia kukuza mtaala wa ufugaji wa kuku utakaosaidia sekta hii kushughulikia changamoto zake kuanzia kwenye vituo vya mafunzo ya ufundi hadi ngazi ya mashambani hasa kwa wakulima vijana na wanawake vijijini,” alieleza.

Afisa Mtendaji Mkuu wa LITA, Dkt Pius Mwambene alisema mradi wa kupitia mtaala wa tathmini ya ufugaji wa kuku utawafundisha wakulima na wadau wengine wa ufugaji wa kuku ujuzi zaidi na mbinu za kiufundi.

“Tuna mtaala katika sekta ya ufugaji wa kuku na kilimo lakini huu utaangazia zaidi maendeleo ya ujuzi kwa kuwafanya wakulima kuwa na ujuzi katika ufugaji wa kuku,” alisisitiza.

Dkt Mwambene aliongeza kwamba mradi huo unalenga kubadilisha mafunzo yawe ya vitendo zaidi na ubunifu katika ufugaji wa kuku kwa ajili ya maendeleo endelevu ya sekta hiyo kama msingi wa ustawi wa jamii nchini.

Angelina Nyansambo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) alisema kwamba kama taasisi ya kifedha wanachukulia sekta ya ufugaji wa kuku kama sekta muhimu ya ujumuishaji wa kifedha itakayochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Tuesday, March 25, 2025

YANGA WANAHANGAIKA NA TFF ,SIMBA YAJA NA MPANGO KABAMBE DHIDI YA AL MASRY

 Wakati mjadala mzito wa kuahirishwa ukiendelea kuunguruma miongoni mwa mashabiki wa soka nchini ,hali ni tofauti kwa uongozi wa klabu ya Simba. Uongozi wa klabu hiyo umejikita kuimarisha ushirikiano na mashabiki wake kuelekea mchezo wa robo fainali ya kombe la shirikisho dhidi ya Al Masry yanchini misrimchezo wa raundi ya kwanza utakaopigwa April 2.

Simba wamekaa kimya katika sakata hilo na kuwaacha wapinzani wao wa jadi Yanga waendelee kupambana na Bodi ya Ligi na TFF wakati wao wakiendelea na mazoezi makali kwa ajili ya mchezo huo muhimu unaoweza kwenda kubadili historia ya klabu hiyo. 


Simba yaja na mbinu za kivita kuelekea mchezo wa April 2

Uongozi wa Simba unaamini utulivu ndiyo msingi wa mafanikio ya klabu yao, Klabu hiyo ni mnufaaika mkubwa wa mashabiki wake hasa linapokuja suala la mechi za kimataifa.Si Al Ahly,Zamalek,Kaiser Chief wala Asec Mimosa anayependa kuja dimba la Benjamini mkapa kwa sababu mashabiki wa Simba wamekuwa wakileta msisimko wa kipekee kwa wachezaji wao na kuwapoteza wapinzani wao.

Kuelekea michezo ya tarehe 02 na 09 April Simba imeanza kampeni zake za kuwaweka pamoja mashabiki na hilo limefanyika kwa kuanza na kampeni ya WESE LA UBAYA UBWELA inayowataka mashabiki wa Simba kujaza mafuta katika vituo vya Lake Energies na kufanya hivyo kutainufaisha klabu kwa mapato yatakayokusanywa.


naye msemaji wa klabu hiyo Bw.Ahmed Ally amenukuliwa akisema “Hii ni bidhaa mpya ambayo Simba na Lake Energy tumeingiza sokoni. Bidhaa hii inaweza kutumiwa na Wanasimba na watu wengine. Lakini pia ni mpango maalumu wa kujitengenezea mapato. Kwa kufahamu kwamba uhitaji wa mafuta ni mkubwa nchini, Simba Sports Club tukaiona fursa kushirikiana na Lake Energy ili kuwahudumia Wanasimba lakini pia kuwawezesha kuchangia klabu yao lakini pia kwa Lake Energy kurudisha kwa Jamii.”

“Kwenye vituo vyote vya Lake Energies kutakuwa na namba maalumu au sehemu ya ku’scan’ na ukishaweka mafuta utawambia unalipa kwa njia ya mtandao iwe kwa benki au mitandao ya simu. Huduma hii inafanya kazi kwa njia ya mtandao tu na kila lita unayoweka kuna asilimia inakuja Simba.”
“Jukumu la kuipatia mapato Simba ni jukumu la kila Mwanasimba hivyo kuanzia sasa kwa kila Mwanasimba, kituo chake cha kuweka mafuta ni Lake Energies. Na ukilipa tumia njia ya mtandao, ukilipa kwa cash hiyo siyo yetu lakini ukilipa kwa mtandao tunapata chetu, tunakwenda kuwalipa kina Chasambi, kina Mpanzu wanakwenda kutufanyia ubaya.”