JSON Variables

Thursday, April 17, 2025

RAIS MWINYI:TUTANGAZE FURSA ZA UWEKEZAJI NA KUZINGATIA DIPLOMASIA YA UCHUMI.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika Nchi mbalimbali kuzingatia Diplomasia ya Uchumi na Kuzitangaza fursa za Uwekezaji ziliopo.


Rais Dkt, Mwinyi ameyasema hayo   alipozungumza  na Mabalozi wa  Tanzania wa Nchi za Rwanda,Zimbabwe ,Sweden na Msumbiji Waliofika Ikulu kumuaga  kabla ya kwenda katika Vituo vyao vya Kazi Baada ya kuteuliwa hivi karibuni.


Amewahimiza Mabalozi  hao kufanya Juhudi Maalum za kuitangaza Sera ya Uchumi wa Buluu na Utalii katika Mataifa hayo Ili kuvutia Wawekezaji Zaidi kuwekeza  Nchini.


Amesema Zanzibar bado inahitaji Wawekezaji wengi Hususan katika Sekta hizo Kuu za kipaumbele kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi ikiwemo Uvuvi,Utalii na Mafuta na Gesi.


Halikadhalika Rais Dkt, Mwinyi ameeleza kuwa  Suala la Mahusiano ya Kimataifa hivi sasa limeelekezwa zaidi katika Uchumi hivyo wanapaswa kuzingatia zaidi Kuimarisha Uhusiano wa Kiuchumi.


Ameyataja Maeneo ambayo Yana fursa za kutosha kuwa ni Uwekezaji katika Sekta ya Bandari ikiwemo Bandari za Makontena ,Usafirishaji wa Mzigo, na Mafuta na Gesi.


Akizungumzia Sekta ya Biashara  amewaagiza Mabalozi hao kuzitafutia Masoko Bidhaa za Tanzania ikiwemo Bidhaa za Viungo zinazozalishwa kwa Wingi hapa Zanzibar pamoja na Utalii wa huduma na  Vivutio vya Utalii ili kuwavutia Watalii wa Mataifa hayo kutembelea Zanzibar.


Nao Mabalozi hao  wameahidi kuyatumia Maelekezo ya Rais Dkt, Mwinyi kuwa ni nyenzo na dira ya kufanya Kazi zao kwa Ufanisi pamoja na kuyazingatia Maeneo Muhimu ya Kiuchumi  kwa kuwashawishi Wawekezaji  kuwekeza.


Mabalozi walioaga ni Balozi Dkt, Habibu Kambanga- Rwanda, Balozi CP Suzane Kaganda- Zimbabwe, Balozi Mobhare Matinyi - Sweden na Balozi CP Hamad Hamad - Msumbiji.

NJE SPORTS YAICHAPA WIZARA YA UJENZI 1-0 KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI SINGIDA



Timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Nje Sports) imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya Wizara ya Ujenzi katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Mwenge, mkoani Singida.


Mchezo huo, ambao ulikuwa na ushindani mkubwa na nidhamu ya hali ya juu kutoka kwa timu zote mbili, ulikuwa sehemu ya maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yanayotarajiwa kufanyika Mei Mosi, 2025.


Bao pekee la Nje Sports lilifungwa katika kipindi cha pili na mshambuliaji Juma Jongo, aliyepokea pasi safi kutoka kwa kiungo Mukrim, baada ya shambulizi la pamoja lililotokana na umiliki mzuri wa mpira katikati ya uwanja.


Licha ya juhudi za Wizara ya Ujenzi kusawazisha bao hilo, safu ya ulinzi ya Nje Sports ilionyesha uimara mkubwa, huku kipa wao Adam Mlele akiokoa michomo kadhaa ya hatari na kudhihirisha uwezo mkubwa langoni.


Timu hizo zipo mkoani Singida kushiriki michezo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka huu.

TFS Yapewa Pongezi kwa Kusaidia Upandaji Miti Sekondari ya Nyambili–Nyambunda


Na Mwandishi Wetu, Kibiti

17 Aprili 2025


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bungu, Mhe. Ramadhan Mpendu, ameongoza zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Nyambili–Nyambunda jana, ikiwa ni sehemu ya kampeni endelevu ya kutunza mazingira.


Katika zoezi hilo, jumla ya miti 150 ya matunda na kivuli imepandwa shuleni hapo, ambapo Mhe. Mpendu aliipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa uzalishaji na usambazaji wa miche bure kwa wananchi na taasisi mbalimbali.


“Tutunze miti, itatufaa kwa vizazi vijavyo. TFS wamefanya kazi kubwa – miche hii ni dira ya mustakabali wa mazingira bora,” alisema Mhe. Mpendu mara baada ya zoezi hilo kukamilika.


Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Mhe. Omari Msumi, Mkuu wa shule ya Sekondari Nyambili–Nyambunda, walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo ambao walishiriki kikamilifu katika upandaji miti.


Mhe. Mpendu pia aliwatia moyo walimu na wanafunzi kwa kujitoa kwao katika kutunza mazingira, akisema shule hiyo inatoa mfano bora wa kuigwa katika kulinda rasilimali za asili.

Wednesday, April 16, 2025

FEDHA ZISIZOTUMIKA HADI MWISHO WA MWAKA KURUDI MFUKO MKUU WA SERIKALI

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma, lililoulizwa na Mbunge wa Tandahimba Mhe. Katani Ahmad Katani, aliyetaka kujua lini Serikali itarejesha fedha za miradi zilizochukuliwa na Hazina.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha)

...................

Na. Josephine Majura, WF, Dodoma

Serikali imesema kuwa fedha ambazo hazijatumika hadi mwisho wa mwaka hurudi Mfuko Mkuu wa Serikali ikiwa ni utaratibu wa kusimamia uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya fedha zilizotengwa katika bajeti.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tandahimba Mhe. Katani Ahmad Katani, aliyetaka kujua lini Serikali itarejesha fedha za miradi zilizochukuliwa na Hazina.

Mhe. Dkt. Nchemba, alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha Sheria ya Bajeti SURA 439, fedha ambazo hazijatumika hadi mwisho wa mwaka zinakoma matumizi yake na kurudishwa Mfuko Mkuu wa Serikali. 

Aliongeza kuwa iwapo kuna miradi au shughuli ambazo hazijakamilika, Fungu husika linatakiwa kutenga bajeti na kuwasilisha maombi kwa kuambatisha hati za madai au nyaraka za utekelezaji wa miradi hiyo.

Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa miradi yote inatekelezwa ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

WAZIRI MKUU AKAGUA ATHARI ZA MVUA LINDI, ATOA MAELEKEZO KWA MAMENEJA WA TANROADS NCHINI


.....................

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wote nchini kuhakikisha wanakagua vipenyo vya makalvati na madaraja yote katika maeneo yao kabla na baada ya msimu wa mvua ili  kujiridhisha  kama vinapitisha maji kwa urahisi bila kuathiri barabara.

Majaliwa ametoa maelekezo hayo  leo Aprili 16, 2025 mara baada ya kuwasili mkoani Lindi na kukagua miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoathiriwa  na mvua ambapo ameridhishwa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Timu ya Watalaam kutoka Wizara ya Ujenzi na TANROADS ya kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanarejea katika hali yake ya kawaida.

“Kila Meneja wa TANROADS ni wajibu wake ahakikishe makalvati na madaraja yote  yanakaguliwa ili vipenyo vilivyowekwa vipitishe maji  kwa urahisi, Hivyo fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya ukaguzi wa madaraja na makalvati zitumike kwa kazi hiyo”, amesisitiza Majaliwa.

Aidha, Majaliwa ameelekeza Meneja wa TANROADS mkoa wa Lindi pamoja na timu yake kuweka kambi katika maeneo yaliyopata athari za mvua kwenye barabara hiyo ili kuhakikisha barabara zinakuwa salama na kutoa msaada endapo changamoto yoyote itakapojitokeza kwa uharaka.

Waziri Mkuu Majaliwa amefafanua kuwa barabara ya Dar es Salaam - Lindi imeharibika katika maeneo  mbalimbali yenye madaraja na makalvati kutokana na wingi wa maji unaosababishwa na mvua zinazonyesha mkoani Morogoro yakipitia Mbuga ya Seluous kuelekea baharini.

Halikadhalika, Waziri Mkuu ametoa salamu za pole kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wote wa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma waliopata kadhia ya kukwama katika barabara hiyo na kueleza kuwa Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji  hazikwami katika barabara zote nchini.

Vilevile, Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wakandarasi pamoja na kutoa taarifa za maeneo yanayopata changamoto kwa vyombo husika ili yaweze kutatuliwa kwa uharaka kwa kuwa  Serikali ipo kazini usiku na mchana katika kuhakikisha hakuna kinachokwama.

Majaliwa ameeleza kuwa Mpango wa Serikali ni kuhakikisha hatua kwa hatua inaijenga upya barabara hiyo kwa kiwango cha lami kuanzia Dar es Salaam hadi Mnazi Mmoja mkoani Lindi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameeleza kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 130 kimeidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa madaraja mbalimbali katika Mkoa wa Lindi.

Ulega amefafanua kuwa ujenzi wa daraja la Somanga Mtama  (M 60) linatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya M/S Hunan Construction Enginering kwa gharama ya shilingi Bilioni 12 ambapo tayari Mkandarasi huyo ameshalipwa Shilingi Bilioni 4.1 sawa na asilimia 36.


Tuesday, April 15, 2025

TMA YAPONGEZWA KWA UBORESHWAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA

Dkt. Rozalia Rwegasira,  Kaimu Katibu Tawala Mkoa, sehemu ya uchumi na uzalishaji wa mkoa wa Morogoro akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Jamii Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na matukio ya Hali Mbaya ya Hewa, kwaajili ya Kupunguza Hasara na Uharibifu ,iliyofanyika mkoani Morogoro katika ukumbi wa NSSF, tarehe 15/4/2025.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Jamii Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na matukio ya Hali Mbaya ya Hewa, kwaajili ya Kupunguza Hasara na Uharibifu ,iliyofanyika mkoani Morogoro katika ukumbi wa NSSF, tarehe 15/4/2025.
.......................

Na Mwandishi wetu Morogoro, 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imepongezwa kwa uboreshwaji wa utabiri wa hali ya hewa na taarifa za tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini. 

Hayo yamesemwa na Mhe. Dkt. Rozalia Rwegasira,  Kaimu Katibu Tawala Mkoa, sehemu ya uchumi na uzalishaji wa mkoa wa Morogoro wakati wa ufunguzi wa Semina ya Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Jamii Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na matukio ya Hali Mbaya ya Hewa, kwaajili ya Kupunguza Hasara na Uharibifu ,iliyofanyika mkoani Morogoro katika ukumbi wa NSSF, tarehe 15/4/2025.

“Utabiri wa hali ya hewa umeendelea kuboreshwa na tahadhari za mvua kubwa na matukio ya hali mbaya ya hewa zinatolewa kwa wakati na hivyo kuchangia kuokoa maisha ya watu na mali zao. Tunaishukuru na kuipongeza serikali kwa kupitia TMA kwa kazi hii njema”. Alisema Dkt. Rozalia.

Aidha, Dkt. Rozalia alitoa ahadi ya kushirikiana na TMA katika kufanikisha utekelezwaji wa mradi huu kwani utakuwa na faida kubwa na chanya kwa wananchi wa Tanzania.

“Katika kufanikisha utekelezaji wa Mradi huu, kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tuanaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika na taarifa  zitakazozalishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia Mradi huu, ili wadau na wananchi kwa ujumla kuweza kuchukua tahadhari kwa lengo la kupunguza athari zitokanazo na matukio ya hali mbaya ya hewa”.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a aliishukuru Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa nchini.

“Nitumie fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza na kuisaidia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini kwa kuweka sera, mikakati na mazingira wezeshi yanachochea ubunifu na umahiri".

Dkt. Chang’a alisisitiza kwamba uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu ya hali ya hewa nchini ndio chanzo kikuu cha uboreshwaji wa taarifa za hali ya hewa nchini na kuwasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia  na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari zinazotolewa na TMA, na pia kuzingatia sheria  ya Mamlaka ya Hali ya Hewa namba 2 ya mwaka 2019 na kanuni zake.

Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoa shukrani za dhati kwa Tume ya sayansi na teknolojia (COSTECH) kwa kufadhili mradi huu muhimu ambao utaongeza ufanisi katika mchakato wa kukabiliana na mabadiliako ya hali ya hewa  na tabianchi nchini.


MAKAMU WA RAIS AFUNGUA KONGAMANO LA KODI MWAK 2025


......................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwemo kuimarisha hali ya ulinzi, amani na usalama na kuboresha mfumo wa viwango vya kodi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kodi na Uwekezaji la Mwaka 2025 linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Ametoa rai kwa washiriki wa Kongamano hilo kujielekeza katika kuibua mawazo na mikakati mipya itakayowezesha Taifa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza utegemezi kwa wahisani.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kutumia vema fursa inayotolewa na Serikali kila mwaka kutoa maoni na kuwasilisha mapendekezo yao ya kuboresha sera za kodi na uwekezaji kwa kuchangia moja kwa moja katika jukwaa hilo au kupitia dirisha la kidigitali. Pia amewaagiza Mawaziri wa kila sekta kutoa maoni ya kuongeza mapato ya ndani katika sekta zao na kuhakikisha kuwa maoni na mapendekezo yatakayotolewa na wadau kwa njia mbalimbali yanafanyiwa kazi bila kudumaza ukuaji wa sekta husika.

Makamu wa Rais amesema zipo hatua mbalimbali zinazopaswa kutekelezwa zinazoweza kuongeza mapato ya ndani ikiwemo kuweka mkazo zaidi katika kuimarisha uwezo wa ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya ndani, kuongeza jitihada katika kuboresha mfumo wa kodi ambao utahakikisha usawa na kuondokana na misamaha ya kodi isiyo na tija pamoja na kutoa vivutio vya kutosha kwa mawakala na taasisi za kukusanya kodi na kukabiliana na vitendo vya rushwa.

Makamu wa Rais ametaja hatua zingine za kutekelezwa ikiwemo kukuza matumizi ya TEHAMA katika ukusanyaji wa kodi na uwekaji wa akiba, kujenga kanzidata madhubuti ya taarifa za walipakodi  na kufanya jitihada za kuongeza idadi ya walipa kodi kama njia ya kupunguza mzigo wa kodi, kubuni mbinu za kukabiliana na changamoto za kilojistiki na kisiasa katika utozaji wa kodi kutoka katika sekta isiyo rasmi, kuendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kukuza uwekezaji pamoja na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi, ufuatiliaji na upimaji kwa taasisi za kodi na zile za usimamizi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ili kuongeza mapato, bado hali ya ulipaji kodi nchini inakabiliwa na changamoto mbalimbali hali inayopelekea ukuaji mdogo wa makusanyo ya ndani. Mathalan, uwiano wa mapato kwa Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kwa kasi ndogo katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili kutoka 12.0% mwaka 2001/02 hadi 14.9% mwaka 2024/25.

Makamu wa Rais amelitaka Kongamano hilo kufanya tafakuri ya kina na kuainisha maboresho yanayohitajika kisera, kisheria, kikanuni na kiutaratibu ili kuwezesha uwekezaji na biashara na hivyo kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wa kikodi na ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Saada Mkuya amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa Sekta Binafsi katika uwekezaji na hivyo imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini kupitia utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini ili sekta binafsi iweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa.

Mhe. Mkuya ameongeza kwamba kupitia mpango huo, tozo na ada ambazo ni kero takribani 380 zimefutwa na baadhi zimepunguzwa. Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha uhimilivu wa viashiria vya uchumi jumla, kuwa na sera za kodi ambazo zinatabirika na kuainisha tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za udhibiti kwa lengo la kupunguza na kuimarisha usimamizi. Vilevile amesema mpango mwingine ni n matumizi ya TEHAMA ili kuweka urahisi wa kulipa kodi pamoja na kufanya biashara kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Angelina Ngalula amesema ni vema elimu sahihi kuendelea kutolewa kwa wafanyabiashara ili waweze kurasimisha biashara zao hali itakayopelekea waweze kupata faida za mikopo na ufadhili na hivyo serikali kuongeza wigo wa ukasanyaji kodi.

Ameongeza kwamba, jitihada lazima zifanyike kupitia vitengo vya utafiti vya Wizara kuhakikisha elimu inapatikana kwa wafanyabiashara ili kuondokana na idadi ndogo ya walipa kodi ambao ni milioni mbili waliopo hivi sasa. Na kupunguza gharama ya urasimishaji wa biashara ndogo ndogo

Kongamano hilo linashirikisha viongozi wa Serikali, wadau mbalimbali wa sekta binafsi, wafanyabiashara na wawekezaji. Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni “ Kuongeza ukuzaji wa rasilimali za ndani kupitia kustawisha fursa za wananchi” 

WAZAZI AMBAO HAWATIMIZI WAJIBU WAO KWA WATOTO KUCHUKULIWA HATUA

 


Serikali mkoani Mwanza imezindua mkakati wa kuhakikisha inawaondoa watoto wanaoishi katika mazingira magumu mkoani humo.


Akizungumza katika uzinduzi wa mkakati huo mkuu wa mkoa wa Mwanza Said Mtanda amesema miongoni mwa mikakati iliyopo ni serikali za mitaa kuhakikisha zinaweka utaratibu wa kuwatambua Watoto waliotoroka katika maeneo yao ikiwa ni Pamoja  na wazazi ambao hawatimizi wajibu wao kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kwa upande wake msimamizi wa huduma za ustawi wa  jamii mkoani Mwanza  Baraka Makona amesema mkakati huo utatekelezwa katika halmashauri zote 8 za mkoa huu wa Mwanza.


Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa Day care lina Roman  amesema jukumu walilonalo hivi sasa nikuhakikisha wanashirikiana na serikali kutokomeza suala hilo .