JSON Variables

Friday, April 25, 2025

DKT. MWINYI: BARABARA YA KIBADA - KIMBIJI KUWA NGUZO YA MAENDELEO KIGAMBONI

Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ally Mwinyi, ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kibada – Mwasonga – Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41, hatua muhimu inayolenga kukuza uchumi na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Aprili 25, 2025, katika Wilaya ya Kigamboni, Dkt. Mwinyi alisisitiza kuwa uwepo wa amani nchini ndiyo msingi wa mafanikio ya miradi ya maendeleo kama huu, na kuagiza ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango vya juu. Alibainisha kuwa barabara hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuunganisha maeneo ya pembezoni na fursa za kiuchumi.

Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuendeleza Muungano na kutatua changamoto zilizokuwa zikikumba uhusiano kati ya pande mbili za Muungano, akisisitiza kuwa umoja huo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, aliyemwakilisha Waziri wa Ujenzi, alisema mradi wa barabara hiyo ni jawabu kwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Kigamboni, na sasa utafungua fursa za uwekezaji na kuinua uchumi wa eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, alimhakikishia Rais Mwinyi kuwa Mkoa upo salama na utazidi kudumisha amani licha ya changamoto za kisiasa, huku akitoa pongezi kwa Rais Samia kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama hii.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Muhammed Besta, alieleza kuwa barabara hiyo inajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 83.8 na itatekelezwa kwa awamu mbili chini ya mkandarasi kampuni ya Estim, ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 30.

Uzinduzi wa mradi huu umebeba ujumbe mzito wa kaulimbiu ya mwaka huu isemayo: “Muungano wetu, heshima na tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Muungano. 

WAZIRI MASAUNI AWASILI BAJETI YA MWAKA 2025/26

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiwasilisha hotuba ya mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 bungeni jijini Dodoma leo tarehe 25 Aprili 2025.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiteta jambo na Naibu Waziri wake Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa Kikao cha 12 cha Mkutano wa Nane wa Bunge ambapo amewasilisha hotuba ya mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 bungeni jijini Dodoma leo tarehe 25 Aprili 2025.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akiwa na viongozi waandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakifuatilia Kikao cha 12 cha Mkutano wa Nane wa Bunge kuhusu uwasilishaji wa bajeti ya Ofisi hiyo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 25 Aprili 2025.

........

Waziri wa Nchi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amelieleza Bunge kuwa katika mwaka 2024/2025 Serikali imeanzisha Mfumo wa Kielektroniki wa kuratibu masuala ya Muungano na Yasiyo ya Muungano (UNUMMiS).

Akiwasilisha hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025 na makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2025/2026, Waziri. Masauni amesema mfumo huo umelenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na utendaji kazi

Waziri Masuani amesema mfumo huo kwa sasa upo katika hatua za majaribio ili kuona kama unakidhi matakwa ya watumiaji na pindi utakapokamilika utasaidia wananchi kufahamu kwa kina masuala muhimu yanayohusu Muungano.

Aidha Mhe. Masauni amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu masuala ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuhakikisha Wizara/Idara na Taasisi zinafanya vikao vya ushirikiano.

Ameongeza kuwa hadi kufikia mwezi Machi 2025 jumla ya vikao vinane vya ushirikiano vilifanyika vilivyolenga katika kubadilishana uzoefu, Sera, Sheria na utaalamu katika utekelezaji wa mambo yasiyo ya Muungano.

Mhandisi Masauni amesema katika kuimarisha sekta ya hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini, Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni imesajili jumla ya Miradi 73 ya Biashara ya Kaboni ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ameongeza kuwa Biashara ya kaboni imeanza kuleta manufaa kiasi katika baadhi ya maeneo nchini ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 45 zimelipwa na kunufaisha wananchi katika Halmashauri 10 nchini kama gawio la mauzo ya viwango vya kaboni.

“Ofisi iliratibu vikao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kikao cha kuwajengea uwezo Makatibu Wakuu 21 kuhusu biashara ya kaboni, Wawakilishi wa Makampuni 27 yanayojihusisha na biashara ya Kaboni, Vikao vya kimkakati vya kuimarisha usimamizi wa biashara ya Kaboni baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara za kisekta” amesema Waziri Masauni.

Kuhusu uchumi wa Buluu, Waziri Masauni amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu utekelezaji wa sera ya taifa ya uchumi wa buluu ikiwemo kuandaa Mpango wa Matumizi wa Maeneo ya Maji pamoja na kuwezesha uwepo wa utafiti na ujuzi katika matumizi ya rasilimali za Uchumi wa Buluu nchini.

Kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Sura 191, Mhandisi Masuani amesema hadi kufikia machi 2025, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilipokea na kushughulikia malalamiko 247 yaliyohusu kelele, utupaji taka ovyo, utiririshaji ovyo wa majitaka, ujenzi holela, uchimbaji usio rasmi wa mchanga na uchafuzi wa hewa.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 81,864,190,000 kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2025/2026.

NAIBU WAZIRI MKUU DKT. BITEKO AKEMEA MIGOGORO ARUSHA 

....................

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka viongozi kote nchini kuweka maslahi ya wananchi mbele na kuacha migogoro inayotokana na ubinafsi wao.

"Hawa Watanzania hawataki migogoro yetu sisi viongozi na wakati mwingine migogoro tuliyonayo ni migogoro ya maslahi binafsi. Tumeacha kuwahudumia wananchi tunashughulikiana, tunataka huyu akwame, huyu afanikiwe kwa sababu tuna cartel (makundi)," amesema Dkt. Biteko 

Akizungumza Aprili 24, 2025 Mundarara, Wilayani Longido, Dkt. Biteko amesema kuwa amani ndiyo msingi wa utoaji huduma bora "Tunataka watu waungane, wafanye kazi ya pamoja. Hakuna kitu kinachotia aibu kama unakuta kiongozi umepewa nafasi mahali fulani ama wewe una cheo mahali fulani badala ya kuzungumza shida za watu unawazungumza watu, Huyu kwako mbaya, yule mbaya, huyu mbaya, Wewe ukiulizwa uzuri wako huna cha kuonesha." 

Amesisitiza kuwa viongozi waliopata nafasi wanapaswa kumtumia mwananchi kama mteja wao wa kwanza, wa pili, na wa tatu "Viongozi tuliopata nafasi mteja wetu wa kwanza awe mwananchi, mteja wetu wa pili awe mwananchi, mteja wetu wa tatu awe mwananchi. Hawa wananchi ndiyo wanatupa uhalali wa sisi kuitwa viongozi, tukumbuke ni kwa kodi zao tupo hapa, Tusihubiri chuki. ”amesisitiza Dkt. Biteko.  

TANZANIA HAIWEZI KUWEPO BILA YA MUUNGANO, TUULINDE KWA WIVU- DKT. TULIA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa ni wajibu wa kila mtanzania kuhakikisha anailinda kwa wivu wote tunu ya Muungano iliyoanzishwa na waasisi wa taifa hilo.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 25 Aprili 2025 wakati akizungumza na wananchi wa wa Mkoa wa Pwani wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika stendi ya Kibaha ikiwa ni sehemu ya shughuli za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika katika mkoa huo.

Kiupekee, Dkt. Tulia amemshukuru na kumpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anasimamia maendeleo katika nyanda zote za bara na visiwani.

“Tanzania haiwezi kuwepo bila Muungano, Muungano huu umejengwa katika misingi imara umedumu na utaendelea kudumu. Kila mmoja wetu anapaswa kutafakari matendo na maneno yake yawe chachu ya kudumisha Muungano wetu, niwahakikishie kwamba Bunge litaendelea kuwa daraja katika pande zote mbili ili kuhakikisha Muungano unazidi kuwa madhubuti, unadumu na kuwa imara zaidi” Amesisitiza Dkt. Tulia 

HIZI HAPA HABARI KUBWA ZILIZO PEWA NAFASI KWENYE KURASA ZA MBELE YA MAGAZETI LEO TAREHE 25.04.2025

 Good morning, Habari gani popote ulipo mdau wetu kupitia Mkisi Digital, Natumia fursa hii kuku karibisha kupitia vichwa vya habari magazetini leo ijumaa tarehe 25.04.2025

Unamaoni gani kwenye habari ambayo imekubamba kupitia vichwa hivi/ habari hizi zilizo pewa nafasi kubwa sana kwenye kurasa za mbele ya magazeti.
























Thursday, April 24, 2025

DCEA YAKAMATA KG.4,568 YA DAWA ZA KULEVYA,YAZUIA TANI 14 ZA KEMIKALI BASHIRIFU KUINGIA NCHINI

Kamishna Jenerali wa Mamlaka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo wakati akitoa taarifa kuhusu operesheni ya Mwezi machi hadi April mwaka huu ambayo wameifanya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola katika mikoa ya Dar es salaam,Shinyanga,Tabora,Songwe,Mbeya na Arusha.
Mkurugenzi Msaidizi Malalamiko kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ) Thobias Ndaro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

......................

 NA MUSSA KHALID

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata Kilogram 4,568 za dawa mbalimbali za kulevya na kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi pamoja na kushikilia magari,pikipiki tano na bajaji moja vilivyohusika kwenye uhalifu huo.

Pia imefanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu zilizokuwa ziingizwe nchini kinyume na sheria pamoja na pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo Aretas Lyimo wakati akitoa taarifa kuhusu operesheni ya Mwezi machi hadi April mwaka huu ambayo wameifanya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola katika mikoa ya Dar es salaam,Shinyanga,Tabora,Songwe,Mbeya na Arusha.

Kamishna Lyimo amesema kuwa katika operesheni zilizofanyika mkoani Mbeya,raia wa Uganda Herbert Kawalya mwenye hati ya kusafiria Na.B00132399  na mmiliki wa Kampuni ya Hoxx Wells Lux Tour Limo alikamatwa akiwa na pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa dawa aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu ya tetrahydrocannabinol (THC).

“Aidha katika tukio lingine Mkoani Mbeya zilikamatwa kilogram 1658 za bangi aina ya skanka na kilogram 128.7 za bangi zilizokuwa zinaingizwa nchini kutoka Malawi’amesema Kamishna Lyimo

Ameendelea kusema kuwa katika operesheni waliyoifanya jijini Dar es salaam,zilifanikisha ukamataji wa kilogram 220.67 za bangi aina ya skanka katika kata yaChanika zikiwa zimefichwa chooni huku kilogram 11 zikikamatwa eneo la ukaguzi wa mizigo kwenye bandari ya kuelekea Zanzibar

“Katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Arusha,Tanga na Manyara zilikamatwa Kilogram 733.74 za dawa za kulenya aina ya Methamphetamine,kilogram 91.61 za heroin,kilogram 692.84 za mirungi iliyokuwa inaingizwa kutokea nchini Kenya na Kilogram 115.05 za bangi pamoja na kuteketeza ekari mbili za mashamba ya bangi’amesema Kamishna Lyimo

Vilevile Kamisha Lyimo amesema katika operesheni zilizofanyika Wilaya ya Uyui na Nzega mkoani Tabora,Kilogram 845 za bangi zilikamatwa na ekari za mashamba ya bangi ziliteketezwa.

Katika hatua nyingie Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa watendaji wa serikali za mitaa kudhibiti uhalifu huo katika maeneo yao na watachukuliwa hatua endapo watashindwa kukomesha na wakibainika kuhusika katika uhalifu huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Malalamiko kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ) Thobias Ndaro amesema watahakikisha wanafuatilia kwa umakini watumishi wa umma ambao wanachangia au kuenea kwa changamoto ya dawa za kulenya nchini.

Ametumia fursa hiyo kutoa wito wa watumishi wa umma kuwa waadilifu kwa kutochangia madawa ya kulevya kushamiri katika maeneo yao.

Hata hivyo wazazi na walezi mnahimizwa kuwa makini na kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wenu ikiwa ni pamoja na kuwaasa wajiepushe na mazingira na sababu zozote zinazoweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.