JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumanne, 20 Mei 2025

Rais wa Namibia kufanya ziara yake Nchini Tanzania kwa siku mbili.


 Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah amewasili nchini Mei 20, 2025 kwa ajili ya kuanza ziara rasmi ya siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 21 Mei, 2025.


Ziara hiyo ya kwanza kwa Mhe. Nandi-Ndaitwah kufanyika hapa nchini tangu kuingia kwake madarakani mwezi Machi 2025, inafuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.


Akiwa nchini pamoja na mambo mengine, Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi ya kujadili namna ya kukuza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. 


Kadhalika Viongozi hao kwa pamoja  watazungumza na Waandishi wa Habari kuelezea makubaliano waliyofikia katika mazungumzo yao kabla ya kushiriki dhifa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa heshima ya Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah.


Akiendelea na ziara yake nchini, Mhe. Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah, Mei 21, 2025 anatarajiwa kutoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kutembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kilichopo Dar es Salaam.


Tanzania na Namibia zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa na Waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sam Nujoma kupitia mikataba mbalimbali ya uwili na masuala yote yanayohusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

WATANZANIA TUENDELEE KUMTUNZA MDUDU NYUKI


_▪️Asema lengo ni kuwa na Taifa lenye uhakika wa chakula na uchumi imara_

_▪️Azindua mpango wa kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki kwa Tanzania iliyo bora_

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kumtunza na kumuhifadhi nyuki ili kuwa na Taifa lenye uhakika wa chakula na uchumi ulio imara kwa kuwa takribani asilimia 80 ya mimea ya chakula inayozalishwa duniani huchavushwa na nyuki.

 

Pia, Waziri Mkuu amezindua mpango kabambe utakaoleta mageuzi makubwa ya sekta ya ufugaji nyuki nchini, unaojulikana kama Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki kwa Tanzania Iliyo Bora (Achia Shoka, Kamata Mzinga). 

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Mei 20, 2025) wakati akifunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani, ambayo kitaifa yamefanyika katika Kiwanja cha Chinangali jijini Dodoma. Ametoa wito kwa wadau wote wa masuala ya nyuki kushirikiana na Serikali kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.

 

“Serikali inatumia maadhimisho kuhimiza, kuelimisha na kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo, nyuki wana umuhimu mkubwa katika ustawi wa maisha ya binadamu, hususan katika uchavushaji wa mimea, uzalishaji wa chakula, uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.”

 

Waziri Mkuu amesema kupitia maadhimisho hayo, jamii hukumbushwa juu ya nafasi ya kipekee ya nyuki katika mnyororo wa maisha na umuhimu wa kuwalinda dhidi ya changamoto mbalimbali kama vile uharibifu wa mazingira, matumizi ya viuatilifu hatarishi, mabadiliko ya tabianchi na magonjwa. 

 

Amesema Tanzania inazalisha tani 34,000 za asali na tani 1,918 za nta, kiwago hicho kinaiweka nchi katika ramani ya dunia kwa kuwa ya kwanza kwa uzalishaji wa asali kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC, nchi ya pili kwa Afrika na ya 14 duniani.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema pamoja na kutambua umuhimu na mchango wa mdudu nyuki, maadhimisho hayo yanatoa nafasi kwa wananchi wa kutoka mikoa mbalimbali kujifunza na kutambua fursa zilizopo kwenye sekta hiyo ya Ufugaji Nyuki. 

 

Vilevile, Waziri huyo amesema wananchi wanapata nafasi ya kuelezwa mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwenye Sekta ya Ufugaji Nyuki katika kipindi hiki cha awamu ya sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

 

Akizungumzia kuhusu mpango uliozinduliwa na Waziri Mkuu, Balozi Dkt. Pindi amesema mpango huo unalenga kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 34,861 za sasa hadi kufikia tani 75,000 ifikapo Juni, 2035 na kuongeza mauzo ya mazao ya nyuki katika masoko ya kikanda na kimataifa. “Aidha, kupitia Mpango huo takriban ajira mpya 43,055 zinatarajiwa kuzalishwa hasa kwa vijana na wanawake.”

 

Naye, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema amefurahishwa na mabadiliko makubwa yaliyofikiwa katika tasnia ya nyuki ikiwemo ubora wa asali na vifungashio, jambo ambalo limeiwezesha asali kutoka Tanzania kufanya vizuri kwenye masoko ya kimataifa na hivyo kuchangia kwenye kukuza uchumi.

DKT. NCHEMBA AHIMIZA USHIRIKIANO WA NCHI ZA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 17 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaosimamia masuala ya fedha na uchumi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (17th SCFEA), uliofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo Jijini Arusha, leo tarehe 20 Mei, 2025, ambapo amehimiza nchi wanachama kuimarisha zaidi utengamano wa kikanda ili kuharakisha maendeleo ya nchi hizo.


Mkutano huo, pamoja na masuala mengine, umejadili taarifa ya mashauriano ya kibajeti kuhusu viwango vya pamoja vya Ushuru wa Forodha vya Afrika Mashariki kwa mwaka 2025/26; kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 16 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaosimamia masuala ya Fedha na Uchumi (16th SCFEA); na kupokea na kujadili Taarifa ya Mkutano wa Kamati ya Kikanda ya Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Aidha, agenda nyingine ilikuwa kupokea na kujadili taarifa ya mkutano wa pamoja wa Kamati ya Kisekta ya Masuala ya Bajeti na Kamati Ndogo ya masuala ya Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; kupokea na kujadili taarifa ya Warsha ya 11 ya kikanda ya Masuala ya Usimamizi wa Fedha na Bajeti na kupokea na kujadili taarifa ya Mkutano wa 28 wa Kamati ya Masuala ya Fedha (MAC).


Vile vile, mkutano umepokea wasilisho la nchi wanachama kuhusu mwenendo wa viashiria vya uchumi jumla, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa vigezo vya uchumi jumla vya mtangamano wa kikanda na vipaumbele vya bajeti kwa mwaka 2025/26 kutoka kwa nchi wanachama; kujadili dhima za bajeti za nchi wanachama kwa mwaka 2025/26; pamoja na kubuni kauli mbiu moja ya bajeti ya EAC.

 

KHAMIS MBETO KHAMIS: MLINZI WA FIKRA, NGOME YA UENEZI NA KIELELEZO CHA UZALENDO NDANI YA CCM ZANZIBAR.


Kama ilivyo kawaida ya historia, kila zama huja na mashujaa wake. Wako waliobeba silaha, lakini pia wako waliobeba fikra. Katika sura ya siasa ya Zanzibar ya sasa – sura ya utulivu, maendeleo na maono mapana ya kitaifa – anasimama imara Khamis Mbeto Khamis, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, akiwa mstari wa mbele kuihubiri kweli ya Chama na kutetea itikadi kwa akili, ujasiri na ustahimilivu wa ajabu.*



*Ndani ya utawala wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mbeto si tu kiongozi – ni alama ya uhai mpya wa CCM visiwani. Ni taa katika giza la upotoshaji, ni daraja kati ya sera na uelewa wa wananchi, na ni chemchemi ya hoja zenye mantiki katika zama za makelele ya kisiasa.*



*1. Sauti Yenye Maono: Mbeto Kama Mtunzi wa Tumaini.*


*Kila neno la Mbeto huja kama risala ya matumaini. Akizungumza, si kwa sauti tu bali kwa uzito wa fikra, huteka hisia za wasikilizaji na kuacha mbegu za tafakuri. Katika majukwaa ya chama na mitandao ya kisasa, Mbeto huibua siasa ya uzalendo, si ya vurugu. Huinua hoja, si jazba. Kwa hakika, amekuwa kioo cha usemi unaojenga – si unaobomoa.*



*2. Uenezi Kama Kazi Takatifu: Si Taaluma Tu, Bali Ibada.*


*Mbeto amelipa jukumu la uenezi sura ya heshima. Ameufanya kuwa mwito wa kujenga taifa kupitia fikra, si kazi ya kuchafua au kushambulia. Katika kipindi chake, uenezi umekuwa somo linalofundisha, linahamasisha, na kulinda misingi ya Chama Cha Mapinduzi kwa njia ya kujenga umoja, si migawanyiko.*



*3. Itikadi Kama Jiwe la Msingi: Mbeto, Mlinzi wa Msingi wa Mapinduzi.*


*Katika historia ya Zanzibar, mapambano ya kisiasa yamekuwa si tu ya madaraka, bali ya fikra. Mbeto, akiwa mlezi wa itikadi, amekuwa nguzo ya kuendeleza falsafa ya Mapinduzi ya 1964 – akiwaelekeza vijana kujivunia urithi wa taifa lao, kuwaepusha na siasa za tamaa, na kuwahamasisha kuiona CCM kama mwamvuli wa matumaini ya vizazi vijavyo.*



*4. Lugha ya Kisasa, Mizizi ya Asili.*


*Kwenye ulimwengu wa kidijitali, siasa hutawaliwa na taarifa fupi fupi na mijadala ya papo kwa papo. Mbeto amedhihirisha uwezo wa kipekee wa kuoanisha urithi wa kisiasa wa CCM na matumizi ya lugha nyepesi, ya kisasa, lakini yenye mizizi ya maadili na heshima. Katika mitandao ya kijamii, sauti yake ni ya ushawishi, si ya uchochezi. Ni sauti ya hekima, si ya hasira.*



*5. Mbeto Ndani ya Uongozi wa Dkt. Mwinyi: Nguzo ya Uelewano kati ya Chama na Serikali.*


*Katika uongozi wa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kama Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto amekuwa kiungo muhimu kati ya dhana ya utawala bora na dhima ya chama kuongoza kwa mfano. Amekuwa msemaji wa mafanikio ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar – lakini pia msikilizaji wa maoni ya wananchi. Anasafiri na dhamira ya chama, lakini pia huzungumza kwa sauti ya wananchi waliowapa dhamana hiyo.*




 *Mbeto si tu Mtu – ni Harakati, ni Njozi ya CCM Mpya.*


*Khamis Mbeto Khamis ni miongoni mwa wachache wanaobeba bendera ya CCM si kwa sababu ya wadhifa, bali kwa sababu ya imani ya dhati kwamba Chama hiki ndicho kinachobeba matumaini ya walio wengi. Ameandika ukurasa mpya katika kitabu cha uenezi – ukurasa wa amani, hoja, ukweli na maadili.*



*Katika uso wa siasa ya Zanzibar leo, jina lake linang'aa kama taa ya baharini – ikiongoza meli ya matumaini kuelekea bandari ya ustawi wa kitaifa.*


Zanzibar Imara (ZA I)

RC CHALAMILA AZINDUA MAGARI MAPYA MAWILI (2) -DSM


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila amezindua na kukabidhi magari mapya mawili kwa ajili ya katibu Tawala wa Mkoa huo na Mkuu wa wilaya ya Ilala ambapo amewataka kutumia magari hayo katika kutoa huduma kwa wananchi ili kutatua changamoto zao huku akisisitiza suala la kuhamasisha wananchi kuendelea kuhuisha taarifa zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu 2025


Akizungumza leo Mei 20,2025 Jijini Dar es salaam RC Chalamila amesema magari hayo yametolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ikiwa ni mkakati wa kuendana na Dira ya maendeleo ya Taifa hivyo amewataka viongozi wote waliokabidhiwa magari kufanya kazi ya kuwatumikia watanzania kwa uadilifu ili kubadili hali zao za maisha na kutatua changamoto zao


Aidha RC Chalamila pamoja na kumshukiru Rais Dkt Samia kwa kuendelea kuwezesha upatikanaji wa magari Mkoani humo pia amemshukuru kwa kuidhinisha fedha kiasi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika mwaka huu wa fedha kutokana na uhitaji Mkubwa wa ofisi hiyo ambayo kwa sasa iko pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Ilala


Vilevile RC Chalamila ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha viongozi na wananchi wa Mkoa huo kutambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo ni muhimu kuendelea kuhuisha taarifa zao ili kuweza kushiriki uchaguzi mkuu wa mwezi oktoba mwaka huu ambapo amewataka viongozi kuendelea kuhamasisha wananchi kuhuisha taarifa zao kwa siku zilozobakia


Kwa upande wa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bwana Laurance Malangwa amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa magari hayo yatakwenda kutumika kwa kuzingatia taratibu za kisheria za serikali ili yaweze kudumu na kuhudumu kwa muda mrefu huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe Edward Mpogolo akiahidi kuwahudumia kwa karibu   wananchi ili kutatua kero zao na kuwakumbusha suala la kuhuisha taarifa zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

NCAA YANADI VIVUTIO VYA UTALII MAADHIMISHO YA SIKU YA NYUKI DUNIANI YALIYOFANYIKA DODOMA



Na Philomena Mbirika, Dodoma 

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetumia fursa ya maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yanayofanyika jijini Dodoma kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii  vinavyopatikana katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. 

Maadhimisho hayo yaliyoanza Mei 17 na kuhitimishwa leo Mei 20, 2025 katika Viwanja vya Chinangali Park Dodoma Mgeni rasmi akiwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, yamewakutanisha wadau wa sekta ya nyuki kutoka Mikoa mbalimbali nchini kujadili maswala yanayohusu sekta ya ufugaji nyuki katika uhifadhi na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.


Katika maadhimisho hayo NCAA imepata fursa ya kutangaza vivutio vyake vya utalii vikiwemo Bonde la kreta ya Ngorongoro lenye muonekano wa pekee, wanyama mbalimbali ikowemo wa wanyama wakubwa watano “The big Five “,  Laitoli zinakopatikana Nyayo za binadamu wa kale aliyeishi miaka milioni 3.7 iliyopita, Olduvai George eneo lenye gunduzi za kihistoria ya akiolojia, Kreta ya Empakai iliyopambwa na ndege aina ya Flamingo, Tambarare za Ndutu, Kreta ya Olmoti, Jabali la Nasera (Nasera Rock”, Pango la Olkarien, Mchanga unaohama na vivutio vingine.

Akizungumza ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye maadhimisho hayo Afisa wa Uhifadhi- Utalii Joseph Mzaga amesema kwamba maadhimisho haya yamewakutanisha na taasisi mbalimbali pamoja na watu binafsi ambao wameza kuwaeleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na NCAA kwenye Utalii, Uhifadhi na maendeleo ya jamii. 

“Maadhimisho haya yametupa fursa ya pekee ya kutangaza vivutio vilivyopo ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa watu  mbalimbali zikiwemo taasisi, watu binafsi na makundi ya wanafunzi walioweza kukutembelea mahali hapa ambapo wameonesha shauku kubwa ya kwenda kutembelea vivutio hivi” Alisema Joseph 


Katika kuelekea Mkutano wa 50 wa Kimataifa wa Shirikisho la Umoja wa Vyama vya Wafugaji nyuki Duniani (Apimondia 2027) unaotarajiwa kufanyika Tanzania, NCAA imejipanga kuonesha utajiri wa rasilimali za asili, utalii wa kipekee na jitihada za uhifadhi  kupitia sekta ya nyuki na utalii.

KAMATI MPYA YA UKAGUZI WIZARA YA NISHATI YAFANYA ZIARA KATIKA MIRADI YA UMEME MKOANI PWANI.


📌 Yapongeza Serikali utekelezaji miradi ya umeme


Kamati mpya ya  Ukaguzi ya Wizara ya Nishati imefanya ziara  katika miradi ya umeme mkoani Pwani ili kujionea utekelezaji wa miradi hiyo hali itakayopelekea  Kamati husika  kumshauri vyema Katibu Mkuu Wizara ya Nishati  juu ya usimamizi wa rasilimali za Wizara ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi.

Ziara hiyo imefanyika katika Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Chalinze mkoani Pwani tarehe 19 na 20 Mei 2025

 Baada ya kujionea utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imekamilika,  Mwenyekiti wa  Kamati,  Mhandisi Kenneth Nindie ameipongeza Serikali kwa kazi Kubwa inayofanya kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

 Amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza fedha nyingi katika miradi ya umeme, hivyo Wizara ya Nishati wajibu wake ni kufanya usimamizi mzuri  wa miradi ili thamani ya fedha ionekane.

 Kamati hiyo pia  imewataka wakandarasi wanaopewa kazi ya kutekeleza  miradi kuwa wazalendo kwa kuzingatia viwango na ubora ili miradi inayofanyika  idumu kwa  muda mrefu na kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.

"Tunaipongeza Serikali kwa kweli inafanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi mikubwa katika nchi yetu kwa manufaa mapana ya wananchi, kikubwa tunawasihi wakandarasi kuwa  wazalendo katika kutekeleza majukumu yao, mikataba iliyowekwa izingatiwe kwa kutekeleza kazi kwa viwango na Ubora ili miradi hii iwe na tija kwa Taifa." Amesema Nindie

BODI YA ETDCO YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA UMEME TABORA – KATAVI

Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (ETDCO) wakipokea taarifa ya maendeleo ya mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, unaotekelezwa na ETDCO na ambao umefikia asilimia 96, wakati wa ziara ya kukagua mradi huo iliyofanyika Juni 19, 2025 Mkoani Tabora.

Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (ETDCO) wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kampuni hiyo katika eneo la mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo iliyofanyika Juni 19, 2025, mkoani Tabora.


Bodi ya Wakurugenzi Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Kusafirisha na Kusambaza Umeme (ETDCO) imeridhishwa na usimamizi bora wa utekelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi.

Akizungumza Mkoani Tabora wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bw. Raymond Mbilinyi, amesema kuwa maendeleo ya mradi yameridhisha, huku akieleza kuwa mpaka kufikia mwisho wa mwezi Juni mwaka huu, umeme kutoka kwenye gridi ya taifa utakuwa umefika Wilayani Mpanda, Mkoa wa Katavi.

“Tumeridhishwa na maendeleo ya mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi, ambapo kwa sasa umefikia asilimia 96” amesema Bw. Mbilinyi.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, CPA. Sadock Mugendi, ameieleza bodi hiyo kuwa ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri na sasa upo hatua za mwisho za ukaguzi wa laini.

Ameongeza kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2025, mradi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na kufikisha umeme Mkoani Katavi.

Naye Mkurugenzi wa TANESCO Kanda ya Magharibi, Mhandisi Richard Swai, amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Tabora na Katavi.

Mhandisi Swai amewataka wananchi wa mikoa hiyo kujiandaa kupokea umeme wa gridi ya taifa, ambao utachochea shughuli za kiuchumi na maendeleo kupitia sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, usindikaji na uongezaji thamani wa mazao.

Listen Mkisi Radio