Friday, April 11, 2025
SERIKALI INAENDELEA NA UKARABATI WA MIUNDOMBINU YA UMEME – KAPINGA
Thursday, April 10, 2025
NCC YAFUNZA MBINU KUPUNGUZA GHARAMA ZA UJENZI
..........................
Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa sekta ya ujenzi nchini kwa kutoa mafunzo yatakayowawezesha kutekeleza miradi kwa ufanisi, kupunguza gharama zisizotarajiwa, na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa.
Kupitia mafunzo hayo, NCC imelenga kuwajengea uwezo waajiri, wakandarasi na washauri elekezi kusimamia mabadiliko ya kazi, madai na migogoro kwa njia inayozuia upotevu wa muda, fedha, na rasilimali nyingine hali inayopunguza gharama kwenye miradi ya ujenzi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), miradi ya ujenzi huathiriwa na mabadiliko ya kazi, ucheleweshaji wa kushughulikia madai, na migogoro, ambavyo kwa pamoja husababisha ongezeko la gharama, muda wa mradi na hata kushusha viwango vya ubora.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Mhandisi Tumaini Lemunge kutoka NCC amesema, lengo lao ni kuona miradi ya ujenzi inatekelezwa kwa gharama zilizopangwa na kwa ubora unaokubalika.
“Kupitia mafunzo haya, washiriki wamepata mbinu za kupunguza mabadiliko yasiyo ya lazima, kushughulikia madai mapema, na kutatua migogoro kwa mujibu wa mikataba” amesema Mhandisi Tumaini
Aidha Wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi waliopata nafasi ya kushiriki wameeleza namna mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhandisi Lyda Osena kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema “Mafunzo haya yameniongezea uwezo wa kutambua, kuepusha na kusimamia migogoro na madai kwa njia ya kisheria, vilevile yatanisaidia kutekeleza miradi kwa ufanisi zaidi, ndani ya muda, bajeti na ubora uliokusudiwa.”
Mkadiriaji Majenzi kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi amesema kuwa amepata uelewa mpya kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mikataba ya ujenzi hivyo anafahamu kuwa mabadiliko hayawezi kuepukwa lakini yanahitaji usimamizi makini ili kuepusha gharama zisizokuwa za lazima.
Kwa upande wake, Mwanasheria Elizabeth Kimako kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) amesema, Mwanasheria anaposhiriki katika mchakato wa ujenzi anatakiwa kuelewa kwa kina masuala ya kimkataba.
Amesema kuwa mafunzo hayo yamempa uelewa wa kusaidia taasisi yake kuendesha miradi mbalimbali kwa kwa ufanisi mzuri.


Wednesday, April 9, 2025
MNRT SPORTS CLUB YATINGA KAMBINI KWA KISHINDO.

..,............
Na Sixmund Begashe - Dodoma
Club ya michezo ya Wizara ya Maliasili na Utalii ijulikanayo kama "MNRT SPORTS CLUB" imeanza kwa kishindo mazoezi ya kujifua tayari kwa kukabiliana na timu yeyote itakayo kutana nayo kwenye michezo ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Dunia (MEI MOSI) inayotarajiwa kurindima Mkoani Singida hivi karibu.
Akizungumzia uwepo wa Kambi hiyo Jijini Dodoma, Mwenyekiti Msaidizi wa Club hiyo yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa Bi ,Sharifa Dunia Salum amesema mwaka huu wamejipanga vyema katika kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono katika kila mchezo.
"Wachezaji wetu wote wako imara na wanahari kubwa ya kuhakikisha Wizara yetu ya Maliasili na Utalii inaibuka kidedea katika michezo yote, hatutakuwa na huruma na timu yeyote itakayokuja mbeleyetu tutaiadhibu vikali" Alisema Bi. Salum
Aidha Bi. Salum ameushukuru Uongozi wa Wizara chini ya Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, kwa kuiwezesha Club hiyo kuingia kambini na kwenda kushiriki mashinda hayo muhimu kwa ustawi wa Wafanyakazi na Taifa kwa ujumla.
"Tunaushukuru sana uongozi wa Wizara yetu, umetupa heshma kubwa na sisi tunaahudi tutailinda heshma hii kwa kutoka na ushindi wa kishindo katika michezo yote na kurejea na Makombe" Alisisitiza Bi. Salum
Club hiyo maarufu ya michezo, imekuwa ikifanya vyema kila mwaka katika michezo yake mbalimbali dhidi ya wapizao wao ambao ni timu za Wizara mbalimbali hapa nchini, na sasa inakwenda tena kuzitunishia misuli timu hizo kwenye michezo ya Mei Mosi 2025.
FISI WAHARIBIFU WAZIDI KUDHIBITIWA, SIMIYU NA KONGWA.
Na Sixmund Begashe - Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuongeza jitihada zaidi za kukabiliana na Wanyamapori wakali na waharibifu hususani Fisi katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na usalama.
Akizungumzia jitihada hizo Jijini Dodoma, Mkurugenzi Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACC) Fidelis Kapalata, amesema Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi tangu imeunda kikosi kazi maalum cha kupambana na Wanyamapori wanaoleta usumbufu kwenye makazi ya watu, imesaidia kutatua changamoto hiyo hususani Mkoani Simiyu.
SACC. Kapalata amesema kuwa, katika kikosi kazi hicho chenye Askari wa Uhifadhi 27 kwa kushirikiana na serikali za Halmashauri za Wilaya katika Mkoa huo pamoja na wananchi, wameweza kudhibiti Fisi zaidi ya 25 ambao walikuwa kero kubwa kwa wananchi.
"Napenda kutoa shukrani na pongezi kwa askari wetu waliopo uwandani, wananchi na Serikali za Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu, kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika kuwakabili Wanyamapori hao waharibifu, niendele kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana askari wetu katika zoezi hili, ili tuweze kufikia malengo yanayokusudiwa". Amesema SACC. Kapalata
Aidha, SACC. Kapalata amesema kuwa hivi karibu kumeripotiwa uwepo na Fisi waharibifu katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, ambapo tayari Wizara imeshachukuwa hatua ya kupeleka kikosi kazi cha askari wake ambao wamesha weka kambi na kazi ya kuwasaka Fisi hao imeshaanza.
"Kuhusu taarifa ya uwepo wa Fisi hatarishi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Wilayani Kongwa, tumesha peleka askari wetu na tayari wameshaanza kazi ya kuwasaka Fisi hao ni imani yetu tutaitokomeza changamoto hiyo kwa mafanikio makubwa kama ilivyokuwa katika Mkoa wa Simiyu". Aliongeza SACC. Kapalata.
Ikumbukwe kuwa, uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii umeendelea kuunga mkono jitihata za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama bila kubughudhiwa na Wanyamapori wakali na waharibifu, kwa kuchukuwa hatua mbalimbali hususan za matumizi ya teknolojia ya kisasa, kuunda kikosi kazi maalum kutoka kwa askari wa Taasisi zote zinazounda Jeshi la Uhifadhi, kuongeza vitendwa kazi, kuelimisha umma, kushiriana na wananchi pamoja na uongozi wa maeneo husika.

TANZANIA, UINGEREZA ZAJADILI MPANGO WA KUONGEZA THAMANI MADINI MUHIMU, MKAKATI
*Dodoma*
Serikali ya Tanzania na Uingereza Aprili 8, 2025 zilikutana na kujadili kwa pamoja Taarifa ya Uchambuzi wa Kina iliyoonesha fursa za kuongeza thamani madini za muda Mfupi na wa Kati wa Madini Muhimu na Mkakati ya Tanzania ambayo iliwasilishwa na Ujumbe kutoka Mpango wa Manufacturing Afrika unaofadhiliwa na Uingereza.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, ujumbe huo ukiongozwa na Mkuu wa Sehemu ya Diplomasia na Uchumi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini, Bi Tamsin Clayton, ulibainisha fursa zipatazo 13 za kuongeza thamani madini ya aina zipatazo 11 za madini muhimu na mkakati yanayopatikana nchini.
Uchambuzi huo unalingana na moja ya mikakati inayoandaliwa na Wizara ya Madini ambayo inatoa fursa kwa Tanzania kuzalisha mapato ya hadi Dola za Marekani bilioni 11 kwa mwaka huku ukitarajia pia kuzalisha ajira hususan kwa vijana na wanawake.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde aliushukuru ujumbe huo kwa mchango wao muhimu na kusisitiza kwamba taarifa hiyo iliyowasilishwa inakwenda sambamba na mkakati wa Serikali ambao Wizara imeundaa kwa ajili ya kuwezesha manufaa ya haraka ya uongezaji thamani madini nchini.
Alisistiza kuhusu umuhimu wa kufanya utafiti wa kina wa madini ili kubaini kiwango cha madini muhimu na mkakati kilichopo nchini na kuongeza kwamba, shughuli za uongezaji thamani madini hayo kwa kiwango kikubwa kitategemea hali ya upatikanaji wa rasilimali hiyo.
Waziri pia alisisitiza haja ya kuwa na ushirikiano wa kitaifa, akitolea wito wa utekelezaji wa mpango wa Serikali kwa pamoja ili kufanikisha kuzitumia fursa hizo, akirejelea ahadi ya Wizara yake kuongeza ushirikiano na taasisi na mashirika muhimu ya Serikali.
Mwisho, Waziri Mavunde alitoa shukrani kwa timu yake ya kiufundi ya Wizara kwa kwa karibu na kikamilifu katika utafiti huo na kubainisha dhamira yake ya kuendeleza ajenda ya kuongeza thamani ya madini nchini Tanzania.
*#InvestInTanzaniaMiningSector*
*#MadininiMaishanaUtajiri*
RAIS MWINYI:UCHUMI WA ZANZIBAR UMEKUA KWA ASILIMIA ZAIDI YA 7
JELA MIAKA 60 KWA KUBAKA, KUMPA MIMBA MWANAFUNZI
Mwanza.Mkazi wa kijiji cha Kinamweli, wilaya ya Kwimba mkoa wa Mwanza, Iddy Renatus Makungu (30), amehukumiwa na mahakama ya wilaya hiyo kwenda jela miaka 60 kwa kosa la kubaka na kumsababishia ujauzito mwanafunzi (14).
Hukumu hiyo imesomwa leo tarehe 08.04.2025 na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Ndeko Dastan Ndeko ambapo amesema mshatakiwa huyo alitenda kosa kwa nyakati tofauti kati ya mwezi wa nne mwaka 2024 na mwezi wa tano mwaka 2024 huko katika kijiji cha Kinamweli wilaya ya Kwimba.
Kwa mujibu wa Hakimu Ndeko, mshtakiwa alitenda kosa hilo katika kesi ya jinai namba 31962 ya mwaka 2024 kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mbele ya Hakimu Ndeko, Mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Kiparo amesema kuwa Mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza Mahakamani hapo tarehe 11.11.2024 na kusomewa mashtaka ya kubaka na kumpa mimba binti huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, shule ya msingi Kinamweli, ambapo mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo yote mawili.
Upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano akiwemo mhanga na Mahakama kujiridhisha kwamba upande wa mashtaka umethibitisha makosa hayo pasi na kuacha Shaka dhidi ya mtuhumiwa.
Mshtakiwa katika utetezi wake alidai kwamba amesingiziwa makosa hayo kwani awali alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng'ombe kwa mjomba wa mhanga huyo.
" Mheshimiwa Hakimu., nimesingiziwa kesi baada ya kudai pesa zangu za mshahara nilizochunga ng'ombe" alijitetea Makungu
Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali utetezi huo kwa kukosa mashiko na kumhukumu mshtakiwa kwenda jela miaka 30 kwa kila kosa na kuelekeza kwamba adhabu hizo zitaenda kwa pamoja na hivyo mtuhumiwa atatumikia miaka 30.
*Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza*
Tuesday, April 8, 2025
JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA KIZIWI