Na Lucy Lyatuu
NAIBU Waziri Mkuu, na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, amezindua Sera mpya ya taifa ya biashara na kubainisha mambo matano ambayo ni pamoja na sera hiyo kuimarisha uwezeshaji na kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara.
Aidha ametaka itumike kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na kuongeza ushindani wa mauzo ya bidhaa za Tanzania na nchi za nje.
Dkt. Biteko amesema hayo Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Sera hiyo, hafla ambayo ilihudhuriwa na mabalozi wa nchi mbalimbali, mawaziri, naibu mawaziri na makatibu wakuu pamoja na wadau mbalimbali wa biashara.
Amesema kuna umuhimu wa kutumia Sera hiyo kuondoa vikwazo vya biashara na kuweka mfumo wa sheria unaolenga kuimarisha na kukuza biashara na kuwataka maofisa wa serikali kuachana na tabia ya kukwamisha mambo.
“Tuunge mkono ndoto za kiongozi wetu Rais Samia na asiwepo wa kukwamisha utekelezaji wa sera hivyo na pindi ikitokea hatosita kuchukua hatua,” amesema Dkt Biteko na kuongeza kuwa Waziri wa Wizara husika ajue kuwa atapatà mapingamizi mengi kwa baadhi ya watu lakini atamsaidia.
Amesema hakuna faida ya kuwa na Sera nzuri lakini wakawepo maofisa ambao kazi yao ni kukwamisha wafanyabaishara na aliwataka kutumia sera kuwa kiunganishi baina ya wafanyabiashara na serikali.
Amesema Sera ni nyaraka na isiposimamiwa itabakia kuwa kitabu Cha hadithi kwa hiyo ni muhimu kubadilisha mtazamo na fikra Ili kuwa wazuri kwenye kuandika na kuyafanyia kazi pia.
Amewataka wafanyabiashara wote nchini kufahamu kuwa serikali ni yao na kwamba inapenda kuona wananufaika na biashara wanazofanya huku akiwaonya wenye tabia ya kukwepa kodi.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Selemani Jafo amesema sera hiyo imewezekana kutokana na msaada wa wadau mbalimbali zikiwemo balozi za nchi mbalimbali na kampuni ya Trade Mark Afrika.
“Wadau wengi sana wamehusishwa lengo likiwa ni kuhakikisha tunapata Sera inayoakisi hali halisi ya sasa, nawapongeza wataalamu wa wizara yangu wamefanyakazi usiku na mchana na kupitia sera hii tunatarajia kuongeza sana mauzo ya nje ikiwemo masoko ya Afrika,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta binafsi (TPSF) ,Rafael Maganga amesema wamekuwa wakipigia kelele muda mrefu, kwa hatua hiyo Sekta binafsi imefurahishwa
Itasimamia masuala ya Biashara Kwa urahisi zaidi.
0 Comments