JSON Variables

Friday, May 9, 2025

Robert Prevost ni nani? Mfahamu kwa undani Papa mpya Leo XIV

 

Hata kabla jina lake halijatangazwa kutoka kwenye roshani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, umati wa watu uliokuwa chini ulikuwa ukiimba "Viva il Papa" kwa maana ya Ishi milele Papa.

Robert Prevost, mwenye umri wa miaka 69, atakuwa kiongozi wa 267 kwenye kiti cha enzi cha Mtakatifu Petro na atajulikana kama Leo XIV.

Atakuwa Mmarekani wa kwanza kushika wadhifa wa Papa, ingawa anachukuliwa kuwa Kardinali kutoka Amerika ya Kusini kwa sababu ya miaka mingi aliyotumikia kama mmisionari nchini Peru, kabla ya kuwa askofu mkuu huko.

Ana uraia wa Peru na anakumbukwa kwa upendo kama mtu aliyefanya kazi na jamii zilizotengwa na kusaidia kuungfanisha jamii katika Kanisa la eneo hilo.

Alizaliwa Chicago mwaka 1955, Prevost alihudumu kama kijana wa altare na aliwekwa wakfu kuwa padri mwaka 1982.

Katika maneno yake ya kwanza kama Papa, Leo XIV alizungumza kwa upendo kuhusu mtangulizi wake Francis.

"Bado tunasikia masikioni mwetu sauti dhaifu lakini daima yenye ujasiri ya Papa Francis ambaye alitubariki," alisema.

"Tukiungana na kushikana mikono na Mungu, tusonge mbele pamoja," aliwaambia umati wa watu waliokuwa wakishangilia.

Aliwaambia umati uliokuwa ukisikiliza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwamba alikuwa mwanachama wa Shirika la Augustino. Alikuwa na umri wa miaka 30 alipohamia Peru kama sehemu ya misheni ya Augustino.

Francis alimteua kuwa Askofu wa Chiclayo nchini Peru mwaka mmoja baada ya kuwa Papa.

Anawajua vizuri Makadinali kote ulimwenguni kwa sababu ya nafasi yake muhimu kama mkuu wa Baraza la Maaskofu.

Kwa kuwa asilimia 80 ya makadinali walioshiriki mkutano mkuu waliteuliwa na Francis, haishangazi sana kwamba mtu kama Prevost alichaguliwa.

Ataonekana kama mtu aliyeunga mkono kuendelea kwa mageuzi ya Francis katika Kanisa Katoliki.

Ingawa ni Mmarekani, na atakuwa anafahamu kikamilifu mgawanyiko ndani ya Kanisa Katoliki, historia yake ya Amerika ya Kusini pia inawakilisha mwendelezo baada ya Papa aliyetoka Argentina.

Ingawa wakati wake kama askofu mkuu nchini Peru hakuepuka kashfa za unyanyasaji wa kijinsia ambazo zimegubika Kanisa, jimbo lake lilikanusha vikali kwamba alihusika na jaribio lolote la kuficha ukweli.

Kabla ya mkutano mkuu, msemaji wa Vatican Matteo Bruni alisema kuwa wakati wa mikutano ya Baraza la Makadinali katika siku zilizotangulia mkutano mkuu walisisitiza umuhimu wa kuwa na Papa mwenye "roho ya kinabii inayoweza kuliongoza Kanisa ambalo halijifungi ndani bali linajua jinsi ya kwenda nje na kuleta mwanga kwa ulimwengu uliojaa kukata tamaa".

Kutoka BBC Swahili.

0 comments:

Post a Comment