JSON Variables

Friday, May 9, 2025

WATUMISHI SEKTA YA AFYA ZINGATIENI MAADILI YA KAZI ZENU – DKT. MAGEMBE


Na. WAF, Arusha

 

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amewataka watumishi wa sekta ya afya nchini kuzingatia maadili ya kazi zao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

 

Dkt. Magembe ameyasema hayo Mei 8, 2025 jijini Arusha, wakati akizungumza na watumishi katika ziara yake ya kikazi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru.

 

Amesema kuwa kila mtumishi wa afya anatakiwa kufanya kazi kwa weledi  na  kuwa na mawasiliano mazuri baina yao na wagonjwa, ndugu wa wagonjwa pamoja na kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa wote wanaokwenda kupata huduma katika hospitali hiyo na kuongeza kuwa hatua za kisheria zichukuliwe kwa mtumishi atakayekwenda kinyume na kanuni na sheria za kiutumishi kwa kuwafikisha

kwenye mabaaraza ya kitaaluma.

 

“Ndio maana kuna Mabaraza ya Kitaaluma ambayo kazi yao kubwa ni kulinda taaluma na kuhakikisha maadili yanazingatiwa kinyume cha hapo ni kumchukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria mtumishi anayekiuka maadili ya taaluma yake, ikumbukwe pia kila mtumishi wa afya alikula kiapo kuwa atawahudumia wananchi kwa nguvu zote na sio vinginevyo, hivyo tuyazingatie hayo na kufanya kazi kadri inavyopaswa na isitokee mwananchi amepoteza maisha kwa uzembe,” amesema Dkt. Magembe.

 

Aidha, Dkt. Magembe ameeleza kuwa Mkoa wa Arusha umejipambanua katika eneo la utalii na agenda ya Royal Tour imeubeba sana  mkoa huo hivyo ni vyema kuwahakikishia wananchi na watalii kiujumla wana uhakika wa matibabu pale wanapopata changamoto ya kiafya.

 

“Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Arusha - Mount Meru imekuwa kimbilio kwa watalii wengi wanaokuja kwenye vivutio vilivyopo nchini pale wanapopata changamoto ya kiafya na hospitali ya Mount Meru imekuwa ikifanya vizuri na niwaombe muendelee hivyo ili muwe mfano wa kuigwa,”amesisitiza Dkt. Magembe.

Dkt. Magembe amewashukuru watumishi wote kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwahudumia wananchi na kusisitiza kuzingatia miiko, na maadili ya taaluma zao ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

0 comments:

Post a Comment