JSON Variables

Friday, May 9, 2025

Katika historia 2003 Ndipo Kundi hili la Wakilisha Lilipatikana.

 

WAKILISHA.

Mwaka 2002, kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola ilianzisha mradi wa kuibua vipaji vya muziki kupitia wasanii wanaochipukia nchini.


Kampuni hiyo ikaandaa Project ya vijana kushindana kuimba. Project hiyo ikapewa jina la “Coca-Cola Pop Idol”. Vijana mbalimbali wakajitokeza kushiriki.


Hatimaye Project ikapata mshindi. Msanii Banana Zorro akatangazwa kuwa kinara. Hata hivyo Banana alikuwa tayari ni 'Star' kutoka kundi la "B Love M" ikilinganishwa na washiriki wengine ambao hawakuwa wakijulikana.


Ushindi wa Banana ulitokana na kuimba kwa umahiri kibao "My Love" cha kundi la Westlife. Banana akakwea pipa kuzuru nchini Afrika Kusini katika ziara fupi ya kujifunza zaidi muziki.


Kanuni za shindano hilo zilieleza mapema kuwa mshindi wa kwanza atapata fursa ya kwenda nchini Afrika Kusini ili kunolewa kipaji chake. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa.


Ushindi wa Banana ukahamasisha vijana wengi mno kujitosa kushiriki msimu wa pili wa Project hiyo, ambao sasa ukapewa jina jipya la "Coca-Cola Pop Star", badala ya Coca-Cola Pop Idol, lililokuwa la mwanzo.


Mwanamuziki wa kundi la Kwaito la ‘'TKZee'’ kutoka Afrika Kusini, Zwai Bala, akafika nchini kwa mwaliko wa Coca-Cola kama Chief Judge, ili kusaidia Project hiyo kupata vipaji halisi katika msimu huo wa pili.


Hapa ndipo Coca-Cola Pop Star (2003) ikapata washindi watatu, ambao kanuni mpya za mashindano hayo zikahitaji waunde kundi moja litakalosafirishwa nchini Afrika Kusini ili kunolewa zaidi.


Washindi hao ni Langa Kileo, Sarah Kaisi na Witness Mwaijaga. Kundi lao likaitwa “Wakilisha” wakimaanisha wao ndiyo wawakilishi wa Kimataifa kutokea Tanzania katika project hiyo ambayo ilikuwa pia kwa nchi za Kenya na Uganda.


Ndani ya Wakilisha, Langa na Sarah walikuwa wachanga zaidi tofauti na Witness (Bad Gar) aliyekwishakuwa na msanii Florence Kasela (Dataz) kwenye kundi moja la Hip Hop liitwalo "The Dream Team".


"Wakilisha" wakawa moto haswa. Vibao vyao vya "Hoi" na "Kiswanglish" vikalipandisha chati kundi hilo ukanda wote wa Afrika Mashariki. Kila mtu akavutiwa na vijana hao kutoka Coca-Cola Pop Star.


Lakini kama ambavyo wahenga walisema kuwa 'Ivumayo Haidumu', ndivyo ilivyokuwa kwa "Wakilisha". Mafanikio ya kundi hili yakapelekea kupata msukosuko iliyoonesha dalili ya kundi hilo kufa siku si nyingi. 


Haiwi Ikawa, Msanii Sarah Kaisi (Shaa) akatangaza kujitoa kwenye kundi lao la Wakilisha na kufanya kundi hilo sasa kubakia na wasanii wawili tu, Langa Kileo na Witness Mwaijaga.


Kuondoka kwa Sarah (Shaa) Wakilisha, kukapelekea wasanii Langa na Witness kuondoa jina la "Sha" (Shaa) mbele ya jina la "Wakili-Sha", na sasa kundi lao kujulikana kama "Wakili" badala ya "Wakilisha".


Kuona hiyo haitoshi, "Wakili" wakatoa kibao kipya kiitwacho ‘No Chorus' wakilenga kumpiga dongo Sarah ambaye alikuwa mahiri zaidi kwa kuimba viitikio (Choruses) katika nyimbo za kundi hilo.


Kibao cha "No Chorus" kikaonekana kumshambulia Sarah kimtindo. Langa na Witness wakaimba kwenye wimbo huo kuwa wanasonga bila viitikio, na hakuna tatizo kwa wao kubaki wawili.


Biashara ya "Wakilisha" mpaka "Wakili" ikatamatika rasmi mwaka 2005. Langa na Witness wakaamua kuvunja kundi lao la kihistoria lililotokana na mradi wa kuibua vipaji wa Coca-Cola Pop Star.


Langa akapita kushoto, Witness akapita kulia. Kila mtu akageuka kujiangaikia yeye mwenyewe kama Solo Artist. Kifo rasmi cha "Wakilisha" kikawasikitisha wengi.


Enzi zikafika mwisho. 

Miaka miwili ikatosha kulilaza kwa amani kundi la "Wakilisha". Pumzika Langa Kileo. Kila la kheri kwenu Sarah na Witness. Ahsanteni kwa mchango wenu kwenye tasnia ya muziki.

#Balozi [0713 555 773]

0 comments:

Post a Comment