Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Pugu Kazimzumbwi, wilayani humo, mkoani Pwani.
NA ABRAHAM NTAMBARA, KISARAWE
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti amesema kuwa wanatarajiwa kuwa na Tamasha Kubwa la Kimataifa linalojulikana kama "BATA MSITUNI" litakalofanyika Pugu Kazimzumbwi wilayani humo, mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 29, 2024 Pugu Kazimzumbwi, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani DC Magoti, amebainisha kuwa Tamasha hilo litaanza Septemba 3 hadi 9 mwaka huu ambapo nchi zaidi ya tatu (3) zitashiriki.
"Pugu Kazimzumbwi ni moja ya eneo la msitu mkubwa wenye hekari zaidi ya 8000, na eneo hili ni mahususi kwa ajili ya utalii na watu wengi hawakujua Pugu ikoje. Na sisi watu wa Pwani tuna eneo ambalo watu wanaweza kuja kupata faraja, kuja kupata mapumziko, kupata upepo wa asili, hivyo ni vizuri ku-share nao sasa kwamba tunatangaza tamasha linaitwa "BATA MSITUNI", hili ni tukio la Kimataifa ambalo halijawahi kufanyika nchini," amesema DC Magoti na kuongeza,
"Tunaenda kutengeneza Tamasha kubwa sana na ndiyo maana leo mnaona tuna mwakilishi mmoja wa watu maarufu kutoka UGanda yupo hapa, tutakuwa na nchi zaidi ya tatu hapa, tutaanza 'event' yetu tarehe 3 mwezi wa tisa mpaka tarehe 9 mwezi wa tisa, 2024, tutakuwa na siku saba nzima za kula bata, kwa sababu tunafanya kazi sana, hivyo tunahitaji kukutana, tunahitaji kubadilishana mawazo, uzoefu, kujifunza, lakini kuunganisha watu,".
DC Magoti ameeleza kuwa pamoja na hayo tamasha hilo litatumika kuonesha utamaduni wa Wazaramo katika Wilaya ya Kisarawe na kwamba kutakuwa na shughuli nyingi kwenye tamasha hilo.
Akieleza kwanini wamaliita Tamasha hilo "BATA MSTITUNI", DC Magoti amesema Bata Msituni ni sehemu yenye uoto wa asili ambayo wamebarikiwa kama inavyofahamika kuwa Tanzania ni nchi yenye misitu mikubwa.
Hivyo Kisarawe imebarikiwa kuwa na eneo la Pugu Kazimzumbwi lenye zaidi ya Hekta 8300 ambalo limebarikiwa kuwa na vivutio na kwamba wapo kwenye ujenzi wa hosteli za kisasa ndani ya eneo hilo.
"Tunaamini Mwenyezi Mungu akitujaliwa tarehe 25 mwezi wa Nane zitakuwa zimekamilika, kuna sehemu za VIP ambazo tunazijenga katika hali ya uasili, tofauti watu walizoea kulala kwenye mahoteli makubwa yenye viyoyozi, huku unalala kwenye Lodge nzuri, lakini unapata upepo mzuri kabisa. Kwahiyo tukaona watu waje wajifunze matumizi ya utalii," amebainisha DC Magoti.
Kwamba kutokana na jinsi Rais Dkt. Samia Sukuhu Hassan alivyotangaza utalii kupitia The Royal Tour, wameamua kuunga mkono hatua hiyo kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuenedeleza na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa tamasha hilo litaambatana na kukimbia riadha ya msituni jambo ambalo halijawahi kutokea, kutakuwa na mashindano ya baiskeli ambayo yataanza Septemba 3, 2024, mashindano ya pikipiki.
0 Comments