Na Fadhili Abdallah, Kigoma
Vitendo vya ubakaji, mimba na adha ya kunyeshewa na mvua vilivyokuwa vikiwakabili wanafunzi wa shule ya sekondari Buyenzi wanaoishi kijiji cha Nyankoronko wilaya ya Buhigwe kumewafanya wananchi wa kijiji hicho kujenga shule yao ya sekondari ili kuwaepusha watoto wao na adha hiyo.
Hayo yamebainishwa na wananchi na viongozi wa kijiji hicho wakati wakipokea msaada wa mifuko 50 ya sementi na trip sita za mchanga kutoka kwa Mbunge wa jimbo la Buhigwe Felix Kavejuru aliyejitolea kuunga mkono ujenzi huo.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo mmoja wa wananchi wa kijiji hicho,Justin Kauzwe ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kata ya Buhigwe alisema kuwa umbali mrefu wa kilometa 13 kutoka kijijini hapo hadi shule imekuwa changamoto kubwa ya wa watoto wao kukumbwa na matukio ya ubakaji.
Akizungumzia changamoto hiyo Mwenyekiti wa kijiji cha Nyankoronko,Nehemiah Christopher alisema kuwa vitendo hivyo vya ubakaji na umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shule iliwalazimu wanafunzi hao kupanga vyumba na kuishi mbali na wazazi lakini hawakuwa na udhibiti hivyo kukumbwa na vitendo vingine vya uvunjifu wa maadili ikiwemo kupata ujauzito.
Mzazi mwingine wa wanafunzi hao, Jenisia Bahegwa alisema kuwa wakati wa mvua imekuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi hao kwenda shule na wakati mwingine mvua inapowakuta njiani hulowana na hivyo kuwa changamoto kubwa kuendelea na masomo na hivyo kuhamasishana kujenga shule yao na mpango huo umeanza kutekelezwa.
Akielezea mpango wa ujenzi wa shule hiyo Afisa Mtendaji wa kijiji cha Nyankoronko, Veronica Wilfred alisema kuwa hadi sasa tayari madarasa mawili yameshajengwa na ofisi ya walimu ambavyo vimefikia usawa wa Renta na madarasa mengine matatu yamefikia usawa wa msingi hivyo jitihada kubwa inafanywa ili shule hiyo iweze kukamilika, kusajiliwa na kuanza kutoa huduma mwakani.
Kufuatia hali hiyo Mbunge wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, Felix Kavejuru ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa shule hiyo ambapo wiki hii amewasilisha mifuko 50 ya sementi na mchanga trip sita huku akipongeza jitihada za wazazi katika kukabili changamoto iliyojitokeza.
Mbunge wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma Felix Kavejuru (katikati) akizungymza na viongozi na wananchi wa kijiji cha Nyankoronko wilaya Buhigwe mkoani Kigoma baada ya kukabidhi mifuko 50 ya sementi na trip sita za Mchanga kusaidia ujenzi wa shule ya sekondari kijijini hapo
Mbunge wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma Felix Kavejuru (katikati) akikabidhi kwa viongozi na wananchi wa kijiji cha Nyankoronko wilaya Buhigwe mkoani Kigoma mifuko 50 ya sementi na trip sita za Mchanga kuunga mkono ujenzi wa shule ya sekondari kijijini hapo
Jenisia Bahegwa mkazi wa kijiji cha Nyankoronko
Jengo la madarasa mawili na ofisi ya walimu katika shule ya Sekondari Nyankorongo ambalo linajengwa likiwa usawa wa renta.
0 Comments