Bila shaka Rais wa Kenya William Ruto anajihisi kukwama - baada ya kupata pigo jingine kwa mipango yake ya kuongeza ushuru kwa serikali yake yenye ukosefu wa fedha na inayolemewa na madeni.
Baada ya maandamano ya hivi majuzi ya kupinga ushuru - ambayo yalishuhudia bunge likichomwa moto - alikubali shinikizo la umma na kuondoa mswada wake wa fedha wa kipindi kipya cha fedha .

Lakini wiki iliyopita mahakama ya rufaa ilivunja mipango yake ya kodi ya mwaka jana .
Majaji watatu kwa kauli moja waliamua kwamba sheria ya 2023 iliyopandisha ushuru kwenye mishahara, mafuta na miamala ya pesa kwa njia ya simu "ilikuwa na dosari kubwa" na "kinyume cha katiba" kwa kuwa haikufuata taratibu zilizowekwa.
Hatua zote mbili zinaleta changamoto kwa uwezo wa serikali kukusanya fedha za ziada kufadhili bajeti ya taifa na kulipa deni lake la umma la $78bn (£61.4bn).
Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya bajeti, Ndindi Nyoro, aliiambia BBC kuwa uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama unaweza kusababisha upungufu mkubwa katika bajeti ya mwaka huu na kuifanya serikali isiweze kuendesha shughuli zake.
"Ukiangalia hatua zote mbili za kifedha ambazo sasa zimezuiwa , kwa jumla, tunazungumzia zaidi ya shilingi trilioni nusu [$3.8bn] kama mapato yaliyopotea," Bw Nyoro alisema.
Serikali inawasilisha mswada wa sheria ya fedha bungeni kabla ya mwanzo wa kila mwaka wa fedha mwezi Julai, ikiwasilisha kodi mpya au kubadilisha zilizopo, ili kupata pesa zaidi.
Wakati huo huo serikali pia inawasilisha kile kinachojulikana kama mswada wa matumizi - hii inaonyesha jinsi mapato yatakavyogawanywa na kutumika katika idara zote za serikali.
Mkwamo katika fedha za serikali umedhihirika wakati mswada wa matumizi ya mwaka huu ulipotiwa saini kuwa sheria huku wakati huo huo mswada unaolingana wa fedha wa kufadhili mpango wa matumizi ukiondolewa.
Huku mipango ya serikali ya kodi kwa miaka miwili mfululizo ikivurugika, wachambuzi wanasema huenda matumizi yakalazimika kuwiana na sheria ya fedha kuanzia 2022.
Mwanauchumi Odhiambo Ramogi anasema uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama pia unaleta shaka kwa walipa kodi, ingawa mahakama iliamua kwamba ushuru ambao tayari umekusanywa hauwezi kurejeshwa.
Serikali imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Mahakama ya Juu, mahakama kuu nchini humo - na kuomba uamuzi wa mahakama ya mwanzo usitishwe hadi rufaa yake isikizwe.
Ilisema kuwa haikuwezekana kusanidi upya mifumo mara moja kwa sheria ya 2022, na hali hiyo inaweza kusababisha kukwama kwa baadhi ya huduma za serikali.
Mahakama ya Juu ilikataa lakini ikakubali kuwa ni suala la dharura na kwamba kesi hiyo itasikilizwa mwezi huu - ingawa kwa kawaida mwezi Agosti huwa ni kipindi cha mapumziko kwa mahakama.
0 Comments