Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya, Bi. Christine Grau, kujadili njia za kuboresha sekta ya afya nchini, huku wakisisitiza umuhimu wa teknolojia katika kuimarisha huduma na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili mchango mkubwa wa maabara tembezi (mobile laboratories) katika kugundua na kudhibiti magonjwa ya mlipuko, hasa katika maeneo ya mipakani na nchi jirani kama Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, na nyinginezo. Maabara hizi zitarahisisha uchunguzi wa haraka, hivyo kusaidia kuchukua hatua za mapema kuzuia kusambaa kwa magonjwa hatari.
Aidha, wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa kupitia mashirika kama Red Cross na CDC, ambayo hutoa msaada wa kiufundi katika kuimarisha mifumo ya afya. Viongozi hao wamekubaliana kwamba uwekezaji zaidi katika teknolojia na miundombinu ya afya ni muhimu ili kufanikisha lengo la Huduma ya Afya kwa Wote (UHC).
Dkt. Mollel ameishukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada wao endelevu, akibainisha kuwa ushirikiano huu utasaidia Tanzania kukabiliana na changamoto za kiafya kwa ufanisi zaidi.
Bi. Grau ameahidi kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama, hasa katika maeneo yenye changamoto kubwa za kiafya.
0 Comments