Mbeto atoa wito akiwataka wananchi wakatae kuzugwa na Siasa za Kijinamizi

 


 Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kimewataka watanzania kutokubali kuzugwa  kwa namna yoyote na majaribu ya Siasa za  kijinimizi zisizoitakia mema nchi yetu zenye zana  ya  kupoteza ustawi wa Amani na Umoja wa Kitaifa 


Chama hicho  pia  kimesisitiza na kutaja Amani, Utulivu na Mshikamano uliopo Tanzzania  kwa miaka sitini,  umekuwa ukiwashangaza walimwengu  wengi  duniani.


Hayo yametamkwa na Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC  Zanziabr , Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo ,Khamis  Mbeto  Khamis  , aliyewahimiza Watanzania kuendelea kudumisha Amani , Umoja  na Mshikamano wa Kitaifa .


Mbeto  alisema kumekuwa na juhudi  za chini kwa chini kwa muda mrefu,  zinazofanywa na baadhi ya maadui wa Umoja Amani ,  ambao wamekuwa wakijaribu  kutaka  kuvuruga Umoja miongoni  mwa Watanzania 


Alisema kuna baadhi ya Wanasiasa na  Wanaharakati   wakiwemo baadhi ya  watu wazima hovyo   , wamekuwa wakitamani kuliparaganya  Taifa kwa kutanguliza maslahi  yao  binafsi  na kutojali  kabisa  maslahi  ya Umma.


Aliongeza kusema watu hao  wamekuwa wakifanya majaribu kadhaa ikiwemo  kukosoa   Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ,wakitumia  Ukabila, Ukanda na Udini lakini kutokana na msimamo  imara wa Watanzania , mitazamo   yote hiyo  batili imejikuta ikigonga mwamba.


"Chama  chetu kwa heshima  zote   kinawaasa na kuwataka wananchi  kutofuata mkumbo utakaopoteza Amani na Utulivu . Tunajua kuna  vitimbakwiri wachache wanaotumia mgongo wa  Demokrasia iliopo ili  kutimiza  ndoto zao haramu  " Alisema  Mbeto. 


Katibu huyo Mwenezi  aliongeza kusema   ni vema Watanzania wakakataa  kuzugwa na Wanasiasa  ambao  wamekuwa wakitoa matamshi yenye  kuitia shaka na hofu katika  jamii.


"Mataifa mengi  hususan  Barani Afrika  yameshavurugwa na kujikuta yakikumbwa na mapigano ya kijamii   yasiokwisha . Nchi kadhaa zimekuwa zikimwaga damu   wenyewe kwa wenyewe .Mataifa mengine hadi  hayajarudisha maelewano  thabit   "Alieleza


Mbeto  alisema  kutokana na utamaduni  wa watanzania kuwa waamifu kwa nchi yao  ,tunaamini  hakuna  jambo lolote  gumu  lisilozungumzika  ,hivyo    hapajawa na   haja kwa baadhi ya watu kutumia lugha za kibabe na  vitisho.


"Rais Mstaafu Jakaya Kikwete  amewahi kutukanya tusigombanie fito wakati  wote  tunajenga nyumba  moja . Maneno  haya ya dhahabu hayapaswi kupuuzwa kwani ni nadra  kuyasikia    " Alisiaitiza Mbeto 


Aidha, alisema watanzania wana wajibu wa  kuwabaini mapema Wanasiasa wa aina hiyo ambao  wamekuwa wakihaha  usiku na mchana kutaka kulizamisha Taifa letu  kwenye  bwawa la matope ya machafuko na mgawanyiko .


"Lazima tuwafichue   na kukwepa hila , ukorofi na matamshi yao  yenye ishara  mbaya  katika jamii yetu  . Maneno siku zote    hunena kuliko  vitendo. Tusimame imara  kupinga tishio lolote  la kutugawa kwa namna yoyote   " Alisema Mbeto

Post a Comment

Previous Post Next Post