VIDEO KESI ZA WAFUNGWA NA MAABUSU👇👇👇
Atoa maelekezo kufuatia matamko ya CHADEMA.
Asema hakuna ‘VIP treatment’ kwa wanaotaka kuwaona Wafungwa na Mahabusu.
Aagiza Jeshi la Polisi kudhibiti maandamano na matishio ya kiusalama.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema kuwa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania litaendelea kuwawezesha Wafungwa na Mahabusu kusikiliza mashauri yao wakiwa magerezani kupitia Mahakama Mtandao, hasa kunapokuwepo na viashiria vya matishio ya kiusalama, ili kudumisha amani na kulinda usalama wa raia na mali zao.
Ameeleza kuwa mojawapo ya sababu ya kuendelea kutumia Mahakama Mtandao ni masuala ya kiusalama, ambapo hivi karibuni baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wametoa matamko yanayoashiria uvunjifu wa amani na usalama, hali iliyosababisha baadhi ya Wafungwa na Mahabusu kusikiliza mashauri yao kwa njia ya mtandao.
Bashungwa ameyasema hayo leo, tarehe 30 Aprili 2025 jijini Dodoma, alipoambata na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), kukagua Makasha ya kisasa ya Mahakama Mtandao yanayowezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya kiteknolojia katima Gereza la Isanga -Dodoma
“Jeshi la Polisi linapokuwa na taarifa za kiinterejensia za wazi na zisizo wazi, kwa mfano maandamano ya CHADEMA na Watanzania ni mashahidi, Viongozi wa CHADEMA walisema waziwazi kwamba waandamana wakakinukishe. Jeshi linapokuwa na taarifa za kiusalama likashirikiana na Mahakama kutoa haki ile ile lakini kwa kutumia teknologia ya Mahakama Mtandao ili kuzuia fujo mtaani, naomba Watanzania watuelewe” amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa Vyombo vya Usalama vitaendelea kuhakikisha kuna utulivu kwa kudhibiti maandamano, matishio ya kiusalama, na vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi.
“Niendelee kuliagiza Jeshi la Polisi kusimamia sheria na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na amani, hata yule ambaye hataki amani, sisi tutamlazimisha kuhakikisha nchi yetu inakuwa amani na salama” amesisitiza Bashungwa
Pia, Bashungwa ameliagiza Jeshi la Magereza kusimamia kwa ukamilifu sheria na taratibu kwa wale wanaotaka kuwaona Wafungwa na Mahabusu, akieleza kuwa taratibu hizo lazima ziheshimiwe bila upendeleo.
““Niliona moja ya viongozi akisema anataka ‘Special treatment’ anapoenda kumuona Maabusu, hiyo nayo sio sawa. Zipo taratibu zinazosimamiwa ndugu, jamaa na rafiki anapotaka kwenda kumuona Maabusu au Mfungwa, kwahiyo mkitaka tuwe na ‘VIP treatment’ na yenyewe sio sawa” amesema Bashungwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Vita Kawawa, amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuendelea kuwawezesha Wafungwa na Mahabusu kupata haki zao kwa kusikiliza mashauri kupitia Mahakama Mtandao, hatua inayotekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.