Wiki ya Utalii Osaka Expo 2025 iliyoanza rasmi tarehe 25 Aprili, 2025 inatarajiwa kumalizika tarehe 6 mwezi May, 2025 ambapo mojawapo ya tukio kubwa linaloloendelea kufanyika katika wiki hii ni pamoja na Tanzania kuonesha vivutio vya Utalii vilivyopo nchini ikiwakilishwa na Bodi ya Utalii Tanzania pamoja na taasisi zilizopo chini ya wizara ya Maliasili na Utalii.
Hifadhi ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, Visiwa vya Zanzibar, Serengeti pamoja na vivutio vingine vya malikale na urithi wa utamaduni vimeweza kuwa na mvuto mkubwa kwa wageni mbalimbali wanaofika katika Banda la Tanzania nchini Japan na kujionea namna nchi hiyo ilivyoweza kuwa na rasilimali nyingi na za kuvutia.
Balozi wa Tanzania nchini Japan Mheshimiwa Baraka Luvanda aliongoza timu ya Tanzania katika ufunguzi wa maonesho hayo katika banda la Tanzania na kupongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii katika kuhakikisha kuwa wageni wengi wanafikiwa kwa kupata taarifa ya vivutio vilivyopo na namna ya kuweza kuvitembelea vivutio hivyo.
“Hongereni sana TTB na TanTrade kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuitangaza nchi yetu katika maonesho kama haya, hii inasaidia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwavutia wageni wengi kuja kuona vivutio tulivyonavyo na hapa kwa kweli tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii wetu”,alisema Balozi Luvanda.
Mkurugenzi wa Masoko kutoka Bodi ya Utalii Tanzania Ernest Mwamwaja alieleza kwamba sekta ya utalii imekuwa ikifanya vizuri kadri miaka inavyosonga mbele hasa kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa za kutangaza vivutio vyote vilivyopo kwa nguvu kubwa ambapo kwa sasa imekuwa ikiingiza asilimia katika ya 17 mpaka 20 ya pato la taifa.
“Sekta hii inakua na ndiyo maana mpaka sasa tumevuka lengo la watalii milioni tano kama ilivyoelekezwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi, tutaendelea kuutangaza utalii katika kila matukio kwani hii ndiyo njia sahihi ya kupeleka taarifa kwa wadau na watumiaji wa sekta hii.”alisema Mwamwaja.
Meneja wa banda la Tanzania nchini Japan bwana Deo Shayo alisema kuwa Tantrade imekuwa ikiwaunganisha wadau wa sekta mbalimbali katika maonesho makubwa kama EXPO 2025 ili kutoa fursa kwa kila sekta kuweza kujitangaza katika masoko ya kimataifa na kusaidia pia kuvutia wawezekezaji kutoka mataifa mengine.
Kwa upande wake Afisa Makoso Mkuu kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana Michael Makombe alisema EXPO 2025 inaonesha kuwa na faida kubwa kwa Tanzania na Ngorongoro kwa ujumla kutokana na wageni wengi kuonesha kuvutiwa na utalii wa wanyama na hivyo maonesho hayo yatasaidia kuongezeka kwa idadi ya wageni msimu ujao wa utalii.
Maonesho ya EXPO 2025 yanaendelea nchini Japan ambapo kwa wiki mbili hizi wadau wa sekta ya utalii wamekuwa katika pilika pilika kubwa ya kutangaza vivutio na kujiandaa kwa mikutano ya wadau wa sekta hiyo ili kuweza kubadilishana mawazo na kuainisha maeneo ambayo wanaweza kutembelea.