JSON Variables

Tuesday, May 13, 2025

HALMASHAURI ZATAKIWA KUSIMAMIA ZOEZI LA USAFI WA BARABARA

 

Iringa


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi-Tamisemi anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinasimamia kikamilifu zoezi la usafi wa barabara, akisisitiza kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.


Mhandisi Mativila amesema hayo mkoani  Iringa wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Wenda–Mgama Km.19 inayojengwa na TARURA kupitia mradi wa RISE kwa gharama ya shilingi bilioni 29.7 ambayo imefikia asilimia 99 ya utekelezaji.

Mhandisi Mativila amesema usimamizi mzuri wa barabara unahitajika ili kuhakikisha barabara hizo zinadumu na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.


"Ni wajibu wa kila halmashauri kuhakikisha kuwa barabara hizi zinatunzwa, hasa kwa kuhakikisha zinaendelea kuwa safi na salama kwa matumizi. Hili ni jukumu la pamoja,” amesema Mativila.


Ameongeza kuwa uwepo wa barabara bora unachochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuwawezesha wananchi kusafirisha bidhaa na huduma kwa urahisi, hali inayosaidia kuongeza mapato ya halmashauri kupitia ushuru na tozo mbalimbali.

Aidha, Mhandisi Mativila ametoa onyo kwa wakandarasi wazembe wanaoshindwa kutekeleza miradi kwa viwango vilivyokusudiwa au kuchelewesha kazi, akisema serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.


“Serikali inataka kuona thamani ya fedha inaonekana katika kila mradi na hatutavumilia uzembe unaokwamisha juhudi hizi za maendeleo,” amesisitiza.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Wenda–Mgama ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha miundombinu ya vijijini kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi.

0 comments:

Post a Comment