JSON Variables

Tuesday, May 13, 2025

Mwili wa Charles Hilary, umewasili leo Visiwani Zanzibar


 Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Zanzibar na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Charles Hilary, umewasili leo Visiwani Zanzibar na kupokelewa katika Bandari ya Malindi na umati wa watu wakiwemo ndugu, jamaa, marafiki na viongozi wa Serikali, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mheshimiwa Idrisa Kitwana Mustafa.


Baada ya mapokezi hayo ya heshima, mwili wa marehemu ulipelekwa nyumbani kwao eneo la Makadara, ambako ulifanyiwa ibada ya sala fupi na maombi ya kumuombea marehemu apumzike kwa amani.


Itakumbukwa kuwa marehemu Charles Hilary alifariki dunia alfajiri ya tarehe 11 Mei 2025 katika Hospitali ya Lugalo, jijini Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa muda mfupi. 


Marehemu atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha mawasiliano ya Serikali na kuwa daraja kati ya Serikali na wananchi kupitia nafasi yake ya Uongozi Ikulu.


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia viongozi wake wakuu, imetoa pole kwa familia, marafiki na wote walioguswa na msiba huu mkubwa, na imesisitiza kuwa Taifa limepoteza mmoja wa watumishi wake mahiri, mwadilifu na mzalendo.

0 comments:

Post a Comment