JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Jumatano, 21 Mei 2025

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU TAHADHARI YA MAGONJWA YA MFUMO WA NJIA YA HEWA NA MAGONJWA YANAYOENEZWA NA MBU

 


TAREHE 20 MEI, 2025 

Wizara ya Afya imeendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa za kila siku kuhusu magonjwa ya mlipuko pamoja na tetesi za uwepo wa magonjwa hayo nchini. Katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Aprili 2025, tumeshuhudia ongezeko la tetesi zinazohusiana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa katika jamii hapa nchini, hasa katika mkoa wa Dar es Salaam.


 Kwa kutumia mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa, ambayo imekuwepo tangu mwaka 2008, tumekuwa tukifuatilia mwenendo wa magonjwa haya ili kubaini aina za vimelea vinavyosababisha maambukizi, ongezeko la visa, pamoja na uwezekano wa kujitokeza kwa kirusi kipya chenye uwezo wa kusambaa kwa haraka. Vipimo vya maabara vimebaini kuongezeka na kupungua kwa virusi vya influenza hali ambayo imekuwa ikionekana pia katika miaka iliyopita na ndiyo maana hujulikana kama ‘Seasonal influenza”. Aidha vipimo hivyo vimeonesha kuwa hakuna kirusi kipya kinachoweza kusambaa kwa haraka na kusababisha mlipuko wa aina ya Pandemiki.


 Ugonjwa wa UVIKO-19, ambao ulitangazwa kwa mara ya kwanza hapa nchini mwezi Machi 2020, umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama yalivyo magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa. Tangu Februari hadi Aprili 2025, ufuatiliaji wa virusi hivi umeonesha ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka asilimia 1.4 (wagonjwa 2 kati ya watu 139 waliopimwa) mwezi Februari hadi asilimia 16.3 (wagonjwa 31 kati ya 190 waliopimwa) mwezi Machi, na kisha asilimia 16.8 (wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa) mwezi Aprili 2025. Hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huu imekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa ugonjwa huu mwaka 2020. Kwa kipindi hiki ongezeko hili linaonekana zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam. 


Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa nchini na kutoa taarifa. Kupitia vituo vyake vya kutolea huduma, Wizara imeelekeza wataalam kuhakikisha wanaendelea kufanya utambuzi wamagonjwa haya kwa kutumia vipimo vya maabara na kutoa matibabu stahiki kwa wagonjwa wote wanaobainika kuwa na maambukizi.


Aidha, natoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za afya ili kujikinga na kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa ikiwa ni pamoja na:

 • Kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, pamoja na kuvaa barakoa pale inapohitajika; 

• Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara;

 • Kudumisha usafi wa mwili binafsi na wa mazingira yanayotuzunguka.

 Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, hususan katika mikoa ya pwani mwa Tanzania, kumekuwa na ongezeko la hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na mbu, kama vile Homa ya Dengue, Malaria, na magonjwa mengine ya aina hiyo. Ili kujikinga na madhara yatokanayo na magonjwa haya, nawasihi wananchi wote kuchukua tahadhari kwa kuzingatia yafuatayo:

 1. Kuangamiza mazalia ya mbu – kuondoa maji yaliyotuama karibu na makazi, ikiwemo madimbwi, ndoo, chupa, matairi ya zamani, na vifaa vingine vinavyoweza kuhifadhi maji;

 2. Kutumia vyandarua vyenye dawa;

 3. Kupulizia viuatilifu (sprays) ndani ya nyumba mara kwa mara ili kuua mbu waliopo ndani;

 4. Kuvaa nguo ndefu zinazofunika mwili hasa wakati wa jioni na alfajiri;

 5. Kufunga madirisha na milango au kutumia wavu ili kuzuia mbu kuingia ndani ya nyumba.

 Magonjwa haya yanayosababishwa na virusi yana dalili zinazoshabihiana hivyo ni vigumu kuyabaini bila kupata vipimo vya maabara. Hivyo, nawasihi kuwahi katika vituo vya kutolea huduma mara mnapopata dalili zozote za homa, maumivu ya kichwa, macho, misuli, viungo, au vipele mwilini au dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile kikohozi, mafua, kuwashwa koo au kupumua kwa shida ili kupata vipimo na matibabu stahiki. 

Serikali kupitia Wizara ya Afya ina uwezo, utaalamu, na mifumo madhubuti ya kufuatilia, kutambua, na kudhibiti magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa pamoja na magonjwa mengine ya mlipuko. Tutaendelea kutoa taarifa sahihi kwa wakati kwa lengo la kuwalinda na kuhakikisha usalama wa afya za Watanzania wote.

 Mwisho, nawasihi tuendelee kushirikiana kwa karibu, tufuate maelekezo ya wataalam wa afya, na tuendelee kuilinda jamii yetu dhidi ya magonjwa yanayoambukiza.

Imetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace E. Magembe

0 comments:

Chapisha Maoni

Listen Mkisi Radio