JSON Variables

Tuesday, May 6, 2025

TANZANIA YAENDELEA KUSHIRIKIANA NA NCHI WASHIRIKA KUKABILIANA NA UJANGILI


Na, Mwandishi Wetu – Arusha 


Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama wa Mkataba wa Lusaka katika kukabiliana na biashara haramu ya Wanyamapori na mazao ya misitu inayovuka mipaka ya Nchi ili kuboresha uhifadhi, kuendeleza utalii na kukuza uchumi. 


Akifungua Mkutano wa 14 wa Kamati ya Wataalam wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka ulioanza leo Mei 06, 2025 Jijini Arusha, Mkurugenzi wa Wanyamapori  Dkt. Alexander Lobora amesema Mkataba huo umekuwa na manufaa makubwa kwa Nchi Wanachama kwa kuunganisha nguvu za pamoja kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka. 

“Tumekuwa tukishirikiana na nchi nyingine kwa kupeana taarifa za kiintelijesia  za wahalifu pale ambapo wanatenda kosa na kukimbilia nchi nyingine, au kuwa na washirika wa uhalifu katika mataifa mengine na kuchukua hatua za kuwakamata na kuwarudisha katika nchi walikotenda uhalifu ili sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.” Amesema Dkt. Lobora


Aidha Dkt. Lobora amesisitiza juu ya wananchi wanaojishughulisha na ujangili kuacha mara moja na  kujielekeza katika kazi halali za kujipatia kipato kwa kuwa utekezaji wa mkataba huo hautaruhusu wahalifu kujificha popote.


Awali, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambae pia ni  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya Prof. Erustus Kanga ametoa rai kwa nchi za Afrika kushirikiana katika juhudi za kupambana na biashara haramu  za mazao wanyamapori na misitu ikiwemo uwindaji haramu wa wa wanyamapori adimu wakiwemo faru kwa ajili ya vipusa na ndovu kwa ajili ya meno yao. 

“Kupitia mkataba huu tungependa kuona Bara letu la Afrika hakuna mtu yeyote anayejihusisha na uwindaji haramu, wa Faru au Ndovu, atoe pembe Kenya ama atoe Tanzania na avuke mipaka ama, atoke Tanzania aende Zambia ama atoke Kenya aende kuziuza Kongo, hilo ndiyo jawabu letu kubwa kabisa.  Tunataka kuona rasilimali zetu zinalindwa kwa kukomesha biashara haramu za mazao ya wanyamapori na misitu ili tuweze kunufaika na rasilimali zetu za asili.” Amesema Prof. Kanga

Mkataba wa Lusaka ulianzishwa mwaka 1994 Jijini Lusaka Zambia na Tanzania ni miongoni mwa mataifa sita yaliyoanzisha Mkataba na kuridhia utekelezaji wake mwaka 1996. Katika Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba, Tanzania itakadhiwa kiti cha urais wa Baraza kwa kipindi cha miaka miwili kutoka Kenya

0 comments:

Post a Comment