JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Ijumaa, 20 Juni 2025

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI MKUTANO WA AFRIKA NA ITALIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Ubia wa Maendeleo baina ya Afrika na Italia kupitia mpango wa Mattei (Mattei Plan) na Mpango wa Ulaya (Global Gateway) utasaidia katika kuendeleza miundombinu, rasilimali watu, kilimo na maendeleo ya kidijitali barani Afrika.

Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kushiriki Mkutano wa Ubia wa Maendeleo kati ya Bara la Afrika na Serikali ya Italia (Mattei Plan) pamoja na Mpango wa Ulaya (Global Gateway) unaofanyika katika Viwanja vya Villa Doria Pamphilj Jijini Roma nchini Italia akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema mkutano huo umejadili zaidi vipaumbele vya nchi za Afrika na kudhamiria kutekeleza miradi kwa vitendo.  Ameongeza kwamba majadiliano katika uongezaji thamani ya mazao hususani zao la kahawa yamelenga kuhakikisha Afrika inapata manufaa zaidi kutokana na kilimo hicho pamoja na kuongeza ajira kupitia zao hilo. 

Makamu wa Rais amesema Tanzania ikiwa ni nchi ya nne barani Afrika kwa uuzaji wa kahawa nje ya bara hilo itanufaika zaidi na mpango wa uongezaji thamani wa zao hilo.

Pia amesema mkutano huo umejadili uwekezaji unaohitajika katika rasilimali watu ili kutengeneza mazingira mazuri zaidi kwa wananchi wa Afrika na kuwaepusha kukimbia nchi zao kuelekea mataifa ya Ulaya. 

Makamu wa Rais amesema Mpango wa Mattei unabadili utoaji wa misaada ya maendeleo na kuleta mfumo mpya wa uwekezaji wa pamoja katika sekta za kimkakati ambao utatengeneza ajira na kuchochea mageuzi kwa maendeleo endelevu.

Katika Mkutano huo masuala yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na uongezaji thamani katika zao la kahawa, nishati endelevu, uboreshaji miundombinu ikiwemo ushoroba wa Lobito pamoja na maendeleo ya kidijitali kama vile matumizi ya akili mnemba katika kukuza uchumi. Tanzania ni moja kati ya Mataifa 14 barani Afrika ambayo yanapewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan).

Miradi ya kipaumbele katika Mpango huo ni pamoja na nishati, elimu na kilimo ambapo euro bilioni 5.5 zimetengwa kwaajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya miradi hiyo. 

Mpango wa Umoja wa Ulaya (EU Global Gateway) ni wa kuboresha miundombinu katika sekta za kidijitali, nishati, usafirishaji, afya, elimu, na utafiti. Mpango huu unalenga uwekezaji wa Euro bilioni 300 ifikapo mwaka 2027, ambapo Euro bilioni 150 zimeelekezwa barani Afrika. 

Umoja wa Ulaya wamedhamiria upanuzi wa mradi wa mawasiliano wa kidijiti (blue raman – submarine cable) unaopita chini ya bahari ambao unaunganisha Ulaya na India ili ufike nchini Tanzania na hivyo kuiunga Afrika Mashariki katika mradi huo. 

Mkutano huo umeshirikisha Viongozi mbalimbali wa Afrika, Umoja wa Ulaya pamoja na Taasisi za Fedha za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Taasisi za fedha za kimataifa, Umoja wa Ulaya pamoja na Serikali ya Italia zimeahidi kutoa fedha kwaajili ya kugharamia miradi mbalimbali itakayotekelezwa katika Mpango huo.

0 comments:

Chapisha Maoni

Listen Mkisi Radio