JSON Variables

Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Ijumaa, 20 Juni 2025

RAIS SAMIA AZUNGUMZA NA WALINZI WA JADI 'SUNGUSUNGU' CCM KIRUMBA JIJINI MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na walinzi wa jadi (Sungusungu) kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Tabora katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza tarehe 20 Juni, 2025

................ 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyataka makundi mbalimbali ya kijamii kushiriki kikamilifu katika kulinda amani na utulivu wa nchi kwa kuwa usalama ni msingi wa maendeleo na mshikamano wa kitaifa. Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo katika mkutano wa hadhara na makundi mbalimbali ya kijamii uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, Jijini Mwanza. Katika mkutano huo uliowakutanisha walinzi wa jadi (sungusungu), maafisa usafirishaji (bodaboda) na viongozi wa dini kama wadau wa amani, Rais Dkt. Samia amesema katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, jamii inapaswa kuongeza umakini na ushirikiano na vyombo vya dola katika kuimarisha usalama wa maeneo yao. Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amewapongeza walinzi wa jadi (sungusungu) kwa mchango wao wa muda mrefu katika kulinda amani katika jamii na kulitaka kundi hilo kuongeza ushirikiano na kuzingatia miongozo inayotolewa na viongozi wa mikoa na wilaya kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya maendeleo, mali na watu. Aidha, Rais Dkt. Samia ametambua mchango wa kundi la maafisa usafirishaji (bodaboda) katika kuwezesha uchumi na kuongeza fursa za ajira, huku akitoa rai kwao kuzingatia sheria za usalama barabarani na kudumisha nidhamu. Rais Dkt. Samia pia amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa elimu na msaada kwa makundi maalum ya bodaboda, sungusungu na mama lishe ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya Halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mapema leo, Rais Dkt. Samia alizindua Mradi wa Chanzo cha Maji cha Butimba uliogharimu Shilingi Bilioni 71 unaotarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 450,000 wa Jiji la Mwanza na viunga vyake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya kimkakati. Katika uzinduzi huo, Rais Dkt. Samia alisisitiza umuhimu wa wananchi kulinda vyanzo vya maji ili huduma mbalimbali za kijamii zinazotegemea vyanzo hivyo ziwe endelevu. Shaaban Kissu Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu. 

Makundi mbalimbali ya walinzi wa jadi (Sungusungu) pamoja na bodaboda kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, Shinyanga na Tabora yakipita mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza tarehe 20 Juni, 2025.

 Matukio mbalimbali katika mkutano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja makundi mbalimbali ya walinzi wa jadi (Sungusungu) katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza tarehe 20 Juni, 2025.

0 comments:

Chapisha Maoni

Listen Mkisi Radio