WATANZANIA
wamehimizwa kulipa uzito na msisitizo suala la uhifadhi na usimamizi wa
mazingira nchini kwani ni agenda muhimu ya kimaendeleo kwa binadamu.
Hayo
yamesemwa leo Jumapili (Julai 6, 2025) Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu
Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati akizindua Siku ya
Mazingira iliyoadhimishwa katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es
Salaam (DITF).
Luhemeja
amesema Dunia inakabiliwa
na changamoto za kimazingira zikiwemo ukataji miti, upotevu wa viumbehai, kupanda
kwa joto, hivyo jitihada za pamoja baina ya Serikali, Asasi zisizo za Serikali,
sekta binafsi na wananchi zinahitajika katika kukabiliana na hali hiyo.
”Natoa rai kwa Watanzania kudumisha
utamaduni wa kutunza mazingira kwa kuepuka kutupa taka na kukata miti hovyo. Aidha,
tuendeleze utamaduni wa kupanda miti na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa
kutumia nishati safi ya kupikia” amesema Mhandisi Luhemeja.
Ameongeza kuwa Tanzania imebarikiwa
urithi mkubwa wa rasilimali asilia na vivutio vya kipekee vinavyotambulika
kitaifa na kimataifa ikiwemo misitu, ukanda wa bahari, uchumi wa bahari, eneo la misitu ya mikoko, hivyo endapo mazingira yataendelea kuharibiwa rasilimali
hizo hazitakuwa salama.
Mhandisi Luhemeja awataka wananchi na
wadau kupunguza matumizi ya plastiki kwa
kutumia falsafa ya ”Punguza, Tumia Tena na Rejeleza” ambapo kwa mujibu wa
tafiti zimebainisha kuwa taka za plastiki huchukua miaka 400
mpaka 1,000 kuoza ardhini na hivyo kuleta athari hasi kwa afya ya binadamu, mazingira
na uchumi.
Ameeleza kuwa katika kukabiliana na
changamoto za mazingira, Serikali kwa
kushirikiana na wadau imefanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa na kutekeleza Sera
ya Taifa ya Mazingira, Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya
Tabianchi, Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Mpango wa
Taifa wa Kudhibiti Maafa.
Ameeleza kuwa zaidi ya asilimia 90
ya kaya nchini bado zinaendelea kutegemea kuni na mkaa kama chanzo kikuu cha
nishati ya kupikia, hivyo Serikali imezindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) unaolenga
kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia
ifikapo 2034.
“Mkakati
huu unaonesha dhamira ya kweli ya kumkomboa Mtanzania dhidi ya athari za
nishati chafu, hasa wanawake ambao ndio wahanga wakubwa. Hili si suala la
majiko au mafuta tu, bali linagusa afya, heshima, fursa na haki ya kuishi
katika mazingira bora” amesema Mhandisi Luhemeja.
Awali
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania
(TANTRADE), Bi. Lulu Mkudde amesema tukio la uzinduzi wa Siku ya Mazingira ni la
kwanza kufanyika tangu shughuli na huduma za maenesho hayo kuanza nchini.
Amesema
kuwa TANTRADE itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Makamu
wa Rais katika masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini hususani kuhamasisha
jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na upandaji miti.
“Tunatambua
suala la uhifadhi wa mazingira kwa sasa limekuwa ni fursa ikiwemo biashara ya
kaboni ambayo imeendelea kunufaisha jamii ya Watanzania. Tutaendelea kuunga
mkono juhudi hizi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii yetu” amesema Mkudde.
MWISHO
0 comments:
Chapisha Maoni