
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais,
Mhandisi Cyprian Luhemeja akifungua kikao kazi cha kimkakati na Menejimenti na
watumishi wa Ofisi hiyo leo Jumatano (Julai 2, 2025) jijini Dodoma kilicholenga
kujadili vipaumbele vya mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi
hiyo katika mwaka 2025/2026.
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya
Makamuwa Rais, Prof. Peter Msoffe akizungumza wakati wa kikao kazi cha
kimkakati na Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo leo Jumatano (Julai 2,
2025) jijini Dodoma kilicholenga kujadili vipaumbele vya mpango kazi wa
utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo katika mwaka 2025/2026.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha
Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu akiwa katika kikao kazi cha
kimkakati na Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo leo Jumatano (Julai 2,
2025) jijini Dodoma kilicholenga kujadili vipaumbele vya mpango kazi wa
utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo katika mwaka 2025/2026.
Sehemu ya
Watendaji wa Ofiisi ya Makamu wa Rais wakifuatilia kikao kazi cha kimkakati
kilichofanyika leo Jumatano (Julai 2, 2025) jijini Dodoma kilicholenga kujadili
vipaumbele vya mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo
katika mwaka 2025/2026.
......................
Watumishi wa Ofisi ya Makamu
wa Rais wamehimizwa kuimarisha ushirikiano na mahusiano na Wizara, Taasisi na
Idara za kisekta ili kuwezesha kuimarika kwa Muungano na usimamizi endelevu wa
sekta ya hifadhi ya mazingira nchini.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano (Julai 2, 2025)
jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati
akifungua kikao kazi cha kimkakati kinacholenga kujadili vipaumbele vya mpango
kazi wa utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo katika mwaka wa fedha
2025/26.
Mhandisi Luhemeja amesema kikao hicho ni mkakati
maalum wa Ofisi hiyo katika kujiwekea malengo mahsusi ya utekelezaji wa Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2050 na hivyo kuwashirikisha watumishi wa kutambua wajibu na
majukumu waliyonayo ili kufikia malengo.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa Fedha 2025/2026
vipaumbele vya ofisi hiyo ni kuhakikisha inapatia majibu hoja mbalimbali kuhusu
masuala ya Muungano na Mazingira kupitia ushirikiano na wadau wa kimkakati
ikiwemo Wizara, Taasisi na Idara za kisekta.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha tunaimarisha uratibu
na ushirikiano na Wizara, Idara na Taasisi zote za kisekta ili kuhakikisha
tunatambulika vyema….kwa mfano masuala ya uchumi wa buluu kunahitajika
usimamizi na uratibu wetu wa karibu ili kuweza kutekeleza kwa pamoja na wizara
nyingine,” amesema Mhandisi Luhemeja.
Mhandisi Luhemaja amesema mazingira ni sekta
mtambuka inayogusa wadau wote wa kimkakati zikiwemo Wizara, Mamlaka za Serikali
za Mitaa, Mashirika na Taasisi za umma, hivyo ofisi hiyo ina wajibu wa
kusimamia uratibu wa miongozo mahsusi ya masuala ya uhifadhi wa mazingira
nchini.
Amesema kuwa ili kufikia malengo ya uratibu wa
masuala ya mazingira nchini, ofisi hiyo imechukua hatua mahsusi ikiwemo kuunda
madawati maalum ya uratibu wa masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira
katika mashirika na taasisi za umma pamoja na mamlaka za serikali za mitaa
nchini.
“Kuna zaidi ya mashirika na taasisi za umma 302
ambazo zina idara ya mazingira…tumeanza kushirikiana katika kuhimiza masuala ya
uhifadhi wa mazingira kwa kutumia fursa zilizopo…ushirikiano huu na wadau ni
muhimu katika kuchagiza agenda ya mazingira nchini” amesema Luhemeja.
Kuhusu maudhui ya mpango kazi uliondaliwa kwa
mwaka 2025/26, Mhandisi Luhemeja, amesema vipaumbele na mwelekeo wake umejikita
katika kuleta matokeo tarajiwa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo
katika kufikia malengo yaliyowekwa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira)
Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe amesema watendaji na watumishi wa
ofisi hiyo wapo tayari katika kutekeleza maelekezo yaliyotolewa kupitia kikao
hicho ili kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wenye kuleta matokeo chanya kwa
umma.
Kikao hicho cha siku 03 kitahusisha mawasilisho
ya mada mbalimbali za masuala ya Muungano na Mazingira sambamba na kujadili
Mpango wa tathimini na ufuatiliaji wa shughuli na majukumu ya ofisi hiyo kwa
mwaka wa fedha 2025/26.

0 comments:
Chapisha Maoni