Thursday, March 13, 2025
MAJALIWA AZINDUA KITUO CHA MABASI NZEGA MJINI.
MARIAM MWINYI AKUTANA NA UJUMBE WA SHIRIKA LA ACTION AID
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema hakuna maendeleo endelevu na ya haraka endapo Wanawake hawatashirikishwa na kuwezeshwa Ipasavyo Kiuchumi .
Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation amesema hayo alipozungumza na timu ya Watendaji wa Shirika la Action Aid Tanzania Waliofika Ofisini kwake Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa bado kuna Kazi kubwa ya kufanya inayohitaji Ushirikiano wa Taasisi hizo mbili Ili kuwainua Wanawake Kiuchumi Hususani Wakulima wa zao
la Mwani.
Ameainisha eneo jengine la Ushirikiano kuwa ni Mapambano dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji wa Jinsia wanavyofanyiwa Wanawake na Watoto alilosema linahitaji kuwa na Mkakati Maalum wa kuwajengea Uwezo wa kupaza sauti zao na kutambua haki zao za Msingi.
Mama Mariam Mwinyi amefahamisha kuwa tatizo la muhali ni kubwa linaloikabili Zanzibar Katika Juhudi za kukabiliana na Vitendo vya Udhalilishaji.
" Ninatamani kuona Watoto wote wanafundishwa kujua haki zao ili kuwalinda na Udhalilishaji" alisisitiza Mama Mariam.
Akizungumzia Mradi wa Maji Safi na Salama kwa Wanafunzi uliowasilishwa na Action Aid katika Kikao Kazi hicho amesema ni Mradi Muhimu utakaowahakikishia Wanafunzi Upatikanaji wa maji Salama wakiwa Skuli pamoja na kuwalinda na Magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji Yasio salama
Ameihakikishia Action Aid Tanzania kuwa Zanzibar Maisha Bora Foundation iko tayari kushirikiana nao kufanya Kazi kwa Ukaribu zaidi kuyafikia Matarajio na Malengo ya Taasisi hizo ambayo yanafanana.
RAIS SAMIA ASHIRIKI KIKAO CHA ASASI YA ULINZI NA USALAMA YA (SADC - Organ)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ) Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akishiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kwa njia ya Mtandao pamoja na viongozi mbalimbali, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 13 Machi, 2025. Mkutano huo pamoja na mambo mengine unajadili hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
RC CHALAMILA MSINGI WA MALEZI BORA NA MAKUZI YA MTOTO NI MUHIMU KWA MASILAHI MAPANA YA TAIFA
-Amshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwa kinara katika kuhakikisha watoto wanapatata misingi bora ya makuzi, malezi na maendeleo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ameyasema hayo mapema Jana Machi 12,2025 wakati akifungua kikao cha Tathimini ya utekelezaji wa programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto-PJT MMMAM ( Naional Mult-sectoral Early Childhood Development Program) kwa kipindi cha Oktoba- Desemba 2024.
RC Chalamila amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata msingi bora wa Makuzi, Malezi, na maendeleo yao.
Aidha RC Chalamila amesema kikao hiki cha tathimini ya utekelezaji wa PJT-MMMAM ni fursa adhimu ya kutafakari maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha mienzi mitatu iliyopita, kujadili changamoto na kupanga mikakati ya kuboresha utekelezaji wa Programu kwa kipindi kinachofuata
Kwa upande wa Katibu Tawala wa Mkoa Dkt Toba Nguvila akimkaribisha Mkuu wa Mkoa amesema Programu hiyo ilizinduliwa Dec 13, 2021 ikiwa na lengo la kuhakikisha watoto wanakua na kufikia kiwango cha juu kabisa cha Maelezi, Makuzi na Maendeleo yao ya awali ambapo amesema Mkoa unaendelea kufanya vizuri katika masuala ya lishe bora ambapo hadi sasa Mkoa uko katika kiwango cha chini kabisa cha udumavu hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuondoa kabisa changamoto hiyo.
Vilevile Dkt Toba Nguvila amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa wabunifu, na kutumia mbinu mbalimbali zenye kulenga kuifikia jamii kwa ukubwa wake.
Hata hivyo RC Chalamila amesistiza lazima tuhakikishe kila mtoto anapata hiduma bora za Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya Awali ili aweze kufikia kilele cha maendeleo yake Kimwili, Kihisia, Kiroho na kijamii hii inawezekana kwa kuimarisha ushirikiano wetu, kuishirikisha jamii ipasavyo na kuhakikisha rasilimali za kutekeleza programu hii zinapatikana.
Mwisho kikao hicho muhimu kimehudhuriwa na Mganga Mkuu wa Mkoa, mratibu wa programu jumuishi, viongozi wa Dini, waratibu na wataalamu wa programu hii ngazi za Halmashauri, Watalaam kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na wadau wengine wa utekelezaji wa programu ya MMAM kutoka katika mashirika ya kimataifa, Kitaifa na Asasi za Kiraia.
MAJALIWA AZINDUA KITUO CHA MABASI NZEGA MJINI
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Machi 13, 2025 amezindua kituo kipya cha Mabasi cha Nzega mjini ambacho ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 4.327.
Akizungumza baada ya kuzindua kituo hicho ambacho utekelezaji wake umefikia asilimia 100, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza halmashauri hiyo kwa uamuzi wa ujenzi wa kituo hicho kwani kitaibua fursa za biashara kwa wakazi wa eneo hilo. “Kituo hiki ni kizuri na kimejengwa kwa ubora, kituo hiki kinatakiwa kianze kutumika ili wananchi waanze kunufaika nacho, Watumishi wa halmashauri ongozeni Wana-Nzega kunufaika na fursa katika eneo lenu”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa halmashauri hiyo kuongeza vibanda vya wafanyabiashara badala ya vichache ambavyo vimejengwa mpaka sasa. “Tunataka wananchi wengi zaidi wanufaike, ongezeni vibanda, huu ni ubunifu mzuri sana utasababisha wengi wanufaike, waleteni wajasiriamali hapa wapate rizki zao, mkifanya hivyo mtaongeza mzunguko wa fedha”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea na mpango kazi wake wa kuwahudumia watanzania wakati wote, “Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kukamilisha malengo yake katika kuwatumikia watanzania ninajua hatua tuliyoifikia”.
Katika hatua nyingine, Mhehimiwa Majaliwa ametoa wito kwa watumishi wa halmashauri nchini kuendelea kujielekeza katika kutatua changamoto za wananchi “Tumueni mapato yenu ya ndani kutekeleza miradi”
MAJALIWA: SERIKALI ITAENDELEZA MIKAKATI YA KUKUZA SEKTA YA MIFUGO
*Asisitiza kuwa mifugo ni uchumi, ajira na biashara
*Atoa wito kwa wakulima na wafugaji wawe wamoja
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha sekta ya mifugo inakuwa endelevu na yenye tija.
Amesema kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mara zote ameweka msisitizo katika kuiendeleza sekta hiyo kwa kuwa mifugo ni uchumi, ajira na ni biashara.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipozungumza na wananchi katika mikutano aliyoifanya jana Jumatano (Machi 12, 2025) Wilayani Igunga, mkoani Tabora ambapo yupo kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili.
“Tunawahamasisha wafugaji, fugeni mifugo ni uchumi, mifugo ni maisha na mifugo ni pesa na wakulima limeni tupate mazao mengi ya chakula na biashara na ni lazima wafugaji na wakulima tuelewane.”
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini kuweka mikakati ya kuhakikisha wanakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuzisimamia fursa zilipo kwenye maeneo yao ili kuwanufaisha wananchi. “Mkifanya hivyo mtakuwa mmewasaidia wananchi kujiendeleza kiuchumi.”
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye shule ya Sekondari ya Seif Gulamali, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka jamii kuweka nguvu za pamoja katika kumlinda mtoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mikakati iliyopo katika sekta ya elimu ili sekta hiyo iweze kuwanufaisha watanzania kwa kukuza ubora wa elimu nchini.
SEforALL KUIMARISHA USHIRIKIANO UPATIKANAJI NISHATI ENDELEVU



Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Viongozi mbalimbali wanaoshiriki mkutano wa kimataifa kuhusu matumizi ya nishati endelevu kwa watu wote unaofanyika nchini Barbados wameshauri kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuwezesha upatikanaji wa nishati endelevu kwa gharama nafuu.
Akizungumza katika mkutano huo unaofanyika jijini Bridgetown, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania kwa upande wake chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepanga kuwawezesha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Amesema, kupitia mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha megawati 2,115 utawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu kwa maendeleo na ustawi wa wananchi katika ngazi mbalimbali.
Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, utekelezaji wa lengo namba 7 katika mpango wa maendeleo ya milenia unahitaji ushirikiano miongoni mwa Serikali na sekta binafsi katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi ikiwa ni moja ya utatuzi wa changamoto zilizopo.
Amesema ni muhimu kwa mataifa kuwekeza katika miundombinu kwa ajili ya upatikanaji wa nishati safi sambamba na kuweka mifumo ya ubunifu na utashi katika kuwezesha upatikanaji wa nishati kwa usawa bila kuacha makundi mengine.
Naye, Waziri Mkuu wa Barbados, Mhe. Mia Mottley amesema ni wakati sasa wa kuweka mkakati wa kimataifa na kukubaliana kushirikiana kumaliza changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa wote.
Akizungumzia mkutano wa misheni 300 (M300) uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mia amesema inatia simanzi kuwa na watu zaidi ya milioni 600 barani Afrika wanaishi bila huduma ya umeme suala ambalo limesababisha changamoto katika nchi nyingi duniani.
“Tunahitaji kupata ufumbuzi wa changamoto zilizopo, uwe ufumbuzi wa ndani au kutoka katika nchi yoyote duniani,” amesema Mhe. Mottley.
Kwa upande wake, Rais wa Sierra Leone, Mhe. Julius Maada Bio amesema katika kipindi hiki ambapo nishati ni nyenzo muhimu katika upatikanaji wa maendeleo, ni muhimu kuwezesha watu na makundi yote kupata nishati hususani katika maeneo ya vijijini yanayokabiliwa na umasikini uliokithiri.
“Wanawake na watoto ambao wanatumia muda mwingi kutafuta nishati ambayo sio safi kwa ajili ya kupikia, wanatakiwa kuwezeshwa kupata nishati safi na hivyo kutumia muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo,” ameongeza.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mtendaji Mkuu SEforALL, Damilola Ogumbiyi, amesema zinahitajika ajenda madhubuti za kuwezesha kukabiliana na vitendo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo safi
“ Tumeshuhudia matokeo yanayosababishwa na ukosefu wa nishati safi kama vile uharibifu wa mazingira unaosababisha ukame na mafuriko ambayo kwa kupata nishati safi tunaweza kuondokana nayo,” amesema.
Mkutano huo wa kimataifa ni mwendelezo wa mikutano ya kikanda na kimataifa inayokusudia kupata suluhisho la changamoto zinazotokana na matumizi ya nishati chafu.
Mwezi Januari, 2025, viongozi na wakuu wa nchi mbalimbali barani Afrika na taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika walikutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta uwezekano wa kuwawezesha watu takribani milioni 300 barani Afrika kupata huduma ya nishati ya umeme.
SERIKALI: ELIMU YA FEDHA KUYAFIKIA MAKUNDI YOTE
Mkazi wa Manispaa ya Musoma, Bw. Athuman Khalid (mlemavu wa kusikia) akiishukuru Serikali kwa kuwafikia kundi la wasiosikia kuwapa elimu ya masuala ya fedha kwa kuwa itawakomboa kiuchumi wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi nyingine ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC, yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara, katika picha hiyo yupo pia Mkalimani Bi. Dainess Wilson, akitafsiri lugha ya alama.
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Elizabeth Mzava (kulia) na Afisa Mahusiano wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), wakimkabidhi zawadi ya fulana, Bi. Catheline Philipo, baada ya kujibu swali kuhusu maeneo salama ya kutunza fedha wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi nyingine ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC, yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Stanley Kibakaya, akitoa elimu kwa Bi. Juliana John kwa njia ya kipeperushi ambacho kina taarifa mbalimbali kuhusu uwekaji akiba, wakati wa mafunzo yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi nyingine ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC, yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Mkalimani, Bi. Dainess
Wilson, akitafsiri lugha ya alama mafunzo ya elimu ya fedha kwa kundi la
watu wenye ulemavu wa kusikia walioshiriki mafunzo hayo yaliyotolewa na
Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Kampuni ya
Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC
l, yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Baadhi ya watoa huduma
katika Taasisi za Fedha ikiwemo Benki ya NMB, CRDB, TCB, NBC pamoja na NSSF
wakifuatilia mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, pamoja
na Taasisi nyingine ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF, Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC yaliyofanyika katika ukumbi wa
Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha, kundi maalumu la watu wenye ulemavu wa kusikia wakifuatilia elimu iliyotolewa na Wizara ya Fedha, pamoja na Taasisi nyingine ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, NSSF, Benki Kuu ya Tanznaia (BoT), TCB, NMB, CRDB na NBC, yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
(Picha na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini WF, Mara)
.....................
Na. Josephine Majura WF, Mara
Serikali inatambua umuhimu wa kuhakikisha kwamba makundi yote maalumu, yakiwemo watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi), wanawake, vijana, na wazee, wanapata elimu ya fedha nchini ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Hayo yameelezwa na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya , wakati wa mafunzo kwa watu wenye ulemavu wa kusikia yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
“Elimu hii inalenga kuyawezesha makundi haya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kuwajenga uwezo wa kusimamia rasilimali zao, na kuboresha maisha yao kwa ujumla”, alisema Bw. Kibakaya.
Alisema kuwa katika utoaji wa elimu ya fedha katika makundi mbalimbali nchini, washiriki wamepewa elimu katika maeneo ya usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji akiba, mikopo, uwekezaji, bima, bima ya amana, kodi na kujipanga kwa maisha ya uzeeni.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Athuman Khalid (mlemavu wakusikia) alieleza furaha yake kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo ya elimu ya fedha.
“Kwa muda mrefu tulihisi kutengwa katika masuala ya fedha, lakini leo tumefikiwa na kupewa elimu kuhusu kupanga matumizi, kujiwekea akiba, kufanya uwekezaji na kutumia Taasisi rasmi kuchukua mikopo”, alisema Bw. Khalid.
Naye Mkalimani, Bi. Dainess Wilson, aliiomba Serikali kuendelea kutoa mafunzo endelevu kwa Wakalimani nchini ili kuboresha ujuzi na weledi wao katika kazi na kutoa huduma za utaalamu wa hali ya juu na kuongeza tija katika utendaji wao.
Wizara ya Fedha kwa kutambua umuhimu wa mchango wa Taasisi za Fedha Timu ya Wataalamu kutoka wizarani ambayo ipo mkoani Mara kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali imeambatana na Wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali, ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na NSSF, pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki ya Biashara Tanzania (TCB), CRDB, NMB, NBC.
MWISHO.