JSON Variables

Tuesday, April 8, 2025

RAIS MWINYI AWAKARIBISHA WAFANYABIASHARA WA UINGEREZA KUWEKEZA ZANZIBAR

........................

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha Wawekezaji kutoka Uingereza kuwekeza  Zanzibar katika fursa mbalimbali ikiwemo sekta ya Uchumi wa buluu, utalii,  usafiri wa baharini,  uvuvi , nishati na miundombinu ya kidijitali.


Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipojumuika kwenye chakula cha jioni na Wakurugenzi wa Taasisi mbalimbali za biashara na uchumi za Uingereza kilichoandaliwa na Taasisi ya Eastern Africa Association ya Uingereza katika Jiji la London, tarehe 7 Aprili 2025.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema katika kipindi cha Miaka 4 Uchumi wa Zanzibar unaendelea kukua zaidi  ya asilimia 7 kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta mbalimbali.

Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa  wawekezaji hao  kuwekeza katika zao la Mwani, ameeleza kuwa Zanzibar ndio  mzalishaji namba moja wa zao hilo Afrika ambalo soko lake linaendelea kukua zaidi.


 

MAWASILIANO SOMANGA- MTAMA YAANZA KUREJEA ABIRIA WASHUKURU


......................

Mawasiliano ya Barabara Somanga - Mtama yameanza kurejea kwa hatua katika barabara iendayo mikoa ya Kusini tangu leo alfajiri  baada ya wataalamu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana kurekebisha eneo la Somanga na Matandu lililoharibiwa na mvua na kufanya njia isipitike.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ambaye ameweka kambi katika eneo hilo tangu jana, amewaambia waandishi wa habari kwamba magari madogo 230, mabasi 10 na baadhi ya malori 30 yaliyobeba bidhaa mbalimbali ikiwemo mawe makubwa yamefanikiwa kuruhusiwa kupita katika eneo la Somanga Mtama na Matandu kuanzia leo kati ya saa 11:30 alfajiri hadi saa 12:00 asubuhi.

Ulega ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa ya awali akiwa mkoani Lindi wakati akiendelea kusimamia zoezi la urejeshaji wa maeneo yaliyokatika katika barabara kuu ya Dar es Salaam - Lindi linaofanywa na Timu ya  Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kushirikiana na Mkandarasi.

Baadhi ya abiria waliolazimika kusubiri usafiri usiku kucha wamezungumza na waandishi wa habari na kutoa shukrani kwa wataalamu waliofanikisha kazi hiyo kwa kufanya kazi usiku kucha.

“Tunaishukuru sana serikali hasa wataalamu wake na mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ambaye tumeshinda naye hapa kutwa nzima mpaka jioni na akatuahidi leo tutaondoka na neno lake limetimia,” alisema Shaaban Matwanga mkazi wa Lindi ambaye ameondoka kwenda Dar es Salaam leo.

Katika maelezo yake, Ulega alisema matengenezo zaidi katika maeneo ya Somanga Mtama na Matandu yanaendelea kuimarishwa kwa kuendelea kuwekwa mawe makubwa ili kuruhusu na magari mengine yaliyobakia kupita.

Ulega amewahakikishia Watanzania kuwa serikali ipo kazini usiku na mchana katika kuhakikisha miundombinu ya barabara hiyo inaimarishwa ili isiwe kikwazo kwa wasafiri.

MSD YAPELEKA MASHINE AKILI MNEMBA JKCI

.......................

Bohari ya Dawa (MSD), imenunua na kupeleka mashine za kisasa zenye Tekinolojia ya akili mnemba kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ili  kuiwezesha taasisi hiyo kutoa huduma za kisasa.

Mashine hizo ambazo baadhi tayari zimefungwa zinatarajia  kuanza kutoa huduma muda wowote kuanzia sasa.

Akizungumza baada ya kupokea mashine hizo   Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge ameipongeza MSD kwa juhudi zake za kuhakikisha huduma za moyo zinakuwa za kisasa kwenye hospitali hiyo. “

Dkt. Kisenge ameishukuru  MSD kwa kuleta mashine hizi ambazo zitasaidia kutoa huduma za moyo kwa ufanisi kwani mashine hizi zinauwezo wa kupiga picha sahihi kwa ajili ya matibabu lakini pia mashine hizi zinauwezo wa kutafsiri taarifa mbalimbali zenyewe kwa kutumia  tekinolojia za kisasa.

Kwa upande mwingine Dkt. Kisenge, ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa juhudi zake za kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa vya kisasa vya afya kwa haraka, jambo linaloimarisha huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo. "Tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na MSD katika kuhakikisha dawa na vifaa vya kisasa vinapatikana kwa haraka na kwa ufanisi," alisema Dkt. Kisenge. 

Amesema kuwa kwa sasa, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inahudumia zaidi ya wagonjwa elfu moja, na zaidi ya asilimia 95 ya wagonjwa hao  wanapata vipimo na matibabu kwa kutumia vifaa vya kisasa ambavyo MSD imevinunua na kuvisambaza. Vifaa hivi vikiwemo mashine za kisasa za ECG (Electrocardiogram),  na vifaa vya upasuaji wa moyo vinavyowezesha kutoa matibabu bora na ya haraka.

Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Bi. Betia Kaema amesema JKCI ni moja ya hospitali maalumu hivyo wanahakikisha huduma wanazowapa zinakuwa na ubora  wa hali ya juu na kwa haraka kuanzia pale wanapopokea maombi yao, kuwa na vikao endelevu na vya mara kwa mara ili  kuhakikisha huduma zinakuwepo muda wote na changamoto zote zinatatuliwa kwa wakati.

Vifaa hivyo ambavyo vimekabidhiwa vinagharimu jumla ya shilingi milioni 800

KIKWETE AWASILISHA UJUMBE MAALUM WA RAIS SAMIA KWA RAIS WA UGANDA


...............

Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amewasilisha Ujumbe Maalum wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Rais wa Jamhuri ya  Uganda, Mhe. Yoweri Museveni na kufanya naye mazungumzo kwenye Viwanja vya Ikulu ya Uganda. 

Akiwasilisha ujumbe huo, Mhe. Kikwete ameelezea  uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Uganda, na dhamira ya Mhe. Rais Samia ya kuimarisha zaidi ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.  

Kwa upande wake, Rais Museveni amepongeza uongozi thabiti wa Mhe. Rais Samia, si tu ndani ya Tanzania bali pia katika Bara la Afrika kwa ujumla. 

Ameeleza furaha yake kwa kumkaribisha Rais Mstaafu wa Tanzania katika Ikulu ya Uganda na kusisitiza kuwa Tanzania ni mfano bora wa uongozi wenye utulivu na demokrasia imara barani Afrika.

Monday, April 7, 2025

Watu 249 wachunguzwa na kutibiwa moyo Zanzibar


................

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

07/04/2025 Watu 249 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku nne katika uwanja wa Amaani uliopo Zanzibar.

Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aika Nnkya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi hiyo ya upimaji na matibabu ya moyo.

 

Dkt. Aika alisema kati ya watu 249 waliowafanyia uchunguzi watu 199 walikutwa na matatizo ya moyo hii ni sawa na asilimia 80 ya watu wote waliowaona ambapo watu 77 sawa na asilimia 31 hawakuwa wanajijua kuwa na matatizo ya moyo.

 

“Wagonjwa 22 ambao tumewakuta na matatizo ya moyo ya kuziba kwa mishipa ya damu, mfumo wa umeme wa moyo na valvu tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu ili tuwafanyie uchunguzi zaidi”.

“Ninatoa wito kwa wananchi zinapotokea nafasi za upimaji kama hizo wajitokeze  kwa wingi kupima afya zao kwa mfano katika kambi hii watu waliokutwa na matatizo  wametibiwa na kupewa dawa za kutumia mwezi mmoja bila malipo yoyote yale” alisema Dkt. Aika.

Kwa upande wake mratibu  wa kambi hiyo ya matibabu daktari bingwa wa moyo kutoka  hospitali ya Rufaa Lumumba Khamis Mustafa alishukuru kuwepo kwa kambi hiyo na kusema kuwa imesogeza kwa karibu huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.

“Ninazishukuru sana Idara za Habari maelezo kwa kuja na wazo hili katika mkutano wao kuwepo na huduma ya upimaji na matibabu kwa wananchi kwani wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) , Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wametoa huduma za matibabu ya magonjwa  mbalimbali”.

“Ninaomba kambi hii ya matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali ambayo inahusisha hospitali hizi kubwa tatu iwe endelevu kwani inawasaidia wananchi kupata huduma za matibabu ya kibingwa kwa wakati na bila gharama yoyote ile tofauti na ambavyo wangezifuata Dar es Salaam”, alisema Dkt. Ndiz.

Nao wananchi waliopata matibabu katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma walizozipata na kusema kuwa zimwewasaidia kufahamu hali za afya ya miili yao na wengine kupata matibabu kutokana na matatizo waliyokuwa nayo.

“Ninaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutuletea wataalamu hawa mimi nilikuwa nikilala moyo wangu unakwenda kasi sana baada ya kufanyiwa uchunguzi nimeambiwa moyo wangu unashida kidogo nimepewa dawa za kwenda kutumia”, alishukuru Halima Shaaban mkazi wa Mwera.

“Baada ya kusikia kuna huduma za matibabu nilikuja hapa kutibiwa kwani mimi ninatatizo la mgongo na presha , nimefanyiwa vipimo na kupewa dawa za kwenda kutumia ninashukuru sana na ninawaomba wananchi wenzangu wachangamkie fursa hii ya matibabu pindi inapotokea”, alisema Juma Abdala mkazi wa Makunduchi.

Huduma hiyo ya matibabu ilitolewa kwa wananchi za Zanzibar na washiriki wa kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kilichoandaliwa na Idara za Habari – Maelezo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mwisho


 

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI KUMBUKIZI YA MIAKA 53 YA KIFO CHA HAYATI KARUME


..................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameungana na Viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi katika Dua na  Kumbukizi ya Miaka 53 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hayati Sheikh Abeid Amani Karume iliyofanyika Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui Zanzibar leo tarehe 07 Aprili 2025.

Kumbukizi hiyo imeongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Zungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid, Marais Wastaafu wa Zanzibar Mhe. Ali Mohamed Shein na Mhe. Amani Abeid Karume, Mjane wa Hayati Abeid Karume Mama Fatma Karume pamoja na familia ya hayati Karume.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM - Bara Mhe. Stephen Wasira, Viongozi, Wanachama na Wazee wa Chama cha Mapinduzi Viongozi wa Mahakama, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Dini mbalimbali.

Sunday, April 6, 2025

UBUNIFU KATIKA TEKNOLOJIA ZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA NI MUHIMU-MGEJWA


 Nchi inashuhudia mageuzi makubwa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.


*Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kinara wa nishati safi ya kupikia.

*Ubunifu wa teknolojia za nishati safi ya kupikia kusaidia kupiga hatua.

NA MWANDISHI WETU 

Kaimu Mkurugenzi wa Nishati safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Ngereja Mgejwa amesema Nchi inashuhudia mageuzi makubwa katika Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini hii inasaidia katika kulinda afya, kutunza mazingira pamoja na ustawi wa jamii ambapo ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia Kinara wake ni Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mgejwa aliyasema hayo tarehe 05 Aprili, 2025 Alipotembelea Chuo cha VETA Moshi, Mkoani Kilimanjaro kuona ubunifu wao wa Majiko yayanayotumia gesi pamoja na kuhamasisisha matumizi ya nishati kupikia na aliwapongeza kwa ubunifu wao ambao utasaidia kupiga hatua katika suala la zima la Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Ziara hiyo, inatokana na maelekezo ya Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb.), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati alipokuwa Mgeni Rasmi katika 
Maadhimisho ya Wiki ya miaka 50 ya utoaji Elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini (VETA) iliyofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Machi 2025.

Aidha, Mgejwa alieleza kwamba lengo la Serikali ni kuona matumizi ya nishati safi ya kupikia yanapanda kufikia asilimia 80 ifikapo 2034.

Pia, alieleza matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia yanavyosababisha madhara ya kiafya, kimazingira na hata kiuchumi, huku akieleza takwimu ambazo zinaonyesha watu takribani 33,024 hupoteza maisha kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia. 

Kwa upande wa Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Moshi Mha. Lupakisio Mapamba amesema ubunifu wa Teknolojia ya jiko linalotumia gesi litasaidia kuondokana na uchafuzi wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti hovyo pamoja na kulinda afya kutokana na moshi pale unapotumia jiko la kawaida la mkaa au kuni.

Pia aliongeza kuwa majiko ya gesi yaliyobuniwa na Chuo Cha Ufundi VETA Moshi yataweza kuwarahisishia watumiaji kutumia bila kuchafua mazingira hasa katika suala la ukataji wa miti pamoja na kumkinga pale anapopika kwa kuwa jiko la gesi halitoi moshi hivyo hatuweza kudhurika kama atumiavyo majiko mengine”. Amesema Mapamba.

MAJALIWA: MEI MOSI INALENGA KUBORESHA USTAWI WA WAFANYAKAZI


_Achangisha zaidi ya sh. Bilioni 1.6 katika harambee ya Mei Mosi 2025_

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yana lengo la kuhamasisha utoaji wa haki za wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi na ustawi wa wafanyakazi kwa ujumla.


Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo jana usiku, Aprili 5, 2025 katika hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuchangisha fedha za kugharamia maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Singida. Hafla hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa Royal Village jijini Dodoma.


Amesema dhumuni jingine la maadhimisho hayo ni kutambua na kuenzi michango ya wafanyakazi katika maendeleo ya jamii na uchumi, Mei Mosi ni fursa ya kuonesha mshikamano kati ya wafanyakazi na kuhimiza usawa na haki katika maeneo ya kazi duniani kote.


Waziri Mkuu amesema mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Katika hafla hiyo jumla ya shilingi bilioni 1.62 zilikusanywa  zikiwa  ni ahadi na fedha taslimu, lengo lilikuwa ni kukusanya sh milioni 832.8.


Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete, rais wa TUCTA, Tumaini Nyamuhokya, Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Martha Mlata.