JSON Variables

Wednesday, April 9, 2025

FISI WAHARIBIFU WAZIDI KUDHIBITIWA, SIMIYU NA KONGWA.


..….....

Na Sixmund Begashe - Dodoma

Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuongeza jitihada zaidi za kukabiliana na Wanyamapori wakali na waharibifu hususani Fisi katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na usalama.

Akizungumzia jitihada hizo Jijini Dodoma, Mkurugenzi Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACC) Fidelis Kapalata, amesema Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi tangu imeunda kikosi kazi maalum cha kupambana na Wanyamapori wanaoleta usumbufu kwenye makazi ya watu, imesaidia kutatua changamoto hiyo hususani Mkoani Simiyu.

SACC. Kapalata amesema kuwa, katika kikosi kazi hicho chenye Askari wa Uhifadhi 27 kwa kushirikiana na serikali za Halmashauri za Wilaya katika Mkoa huo pamoja na wananchi, wameweza kudhibiti Fisi zaidi ya 25 ambao walikuwa kero kubwa kwa wananchi.

"Napenda kutoa shukrani na pongezi kwa askari wetu waliopo uwandani, wananchi na Serikali za Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu, kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika kuwakabili Wanyamapori hao waharibifu, niendele kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana askari wetu katika zoezi hili, ili tuweze kufikia malengo yanayokusudiwa". Amesema SACC. Kapalata

Aidha, SACC. Kapalata amesema kuwa hivi karibu kumeripotiwa uwepo na Fisi waharibifu katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, ambapo tayari Wizara imeshachukuwa hatua ya kupeleka kikosi kazi cha askari wake ambao wamesha weka kambi na kazi ya kuwasaka Fisi hao imeshaanza.

"Kuhusu taarifa ya uwepo wa Fisi hatarishi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Wilayani Kongwa, tumesha peleka askari wetu na tayari wameshaanza kazi ya kuwasaka Fisi hao ni imani yetu tutaitokomeza changamoto hiyo kwa mafanikio makubwa kama ilivyokuwa katika Mkoa wa Simiyu". Aliongeza SACC. Kapalata.

Ikumbukwe kuwa, uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii umeendelea kuunga mkono jitihata za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama bila kubughudhiwa na Wanyamapori wakali na waharibifu, kwa kuchukuwa hatua mbalimbali hususan za matumizi ya teknolojia ya kisasa, kuunda kikosi kazi maalum kutoka kwa askari wa Taasisi zote zinazounda Jeshi la Uhifadhi, kuongeza vitendwa kazi, kuelimisha umma, kushiriana na wananchi pamoja na uongozi wa maeneo husika.

TANZANIA, UINGEREZA ZAJADILI MPANGO WA KUONGEZA THAMANI MADINI MUHIMU, MKAKATI

*Dodoma*


Serikali ya Tanzania na Uingereza Aprili 8, 2025 zilikutana na kujadili kwa pamoja Taarifa ya Uchambuzi wa Kina iliyoonesha fursa za kuongeza thamani madini za muda Mfupi  na wa Kati wa Madini Muhimu na Mkakati ya Tanzania ambayo iliwasilishwa na Ujumbe kutoka Mpango wa Manufacturing Afrika unaofadhiliwa na  Uingereza.


Katika kikao hicho kilichoongozwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, ujumbe huo ukiongozwa na Mkuu wa Sehemu ya Diplomasia na Uchumi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini, Bi Tamsin Clayton, ulibainisha fursa zipatazo 13 za kuongeza thamani madini ya aina zipatazo 11 za madini muhimu na mkakati yanayopatikana nchini.


Uchambuzi huo unalingana na moja ya mikakati inayoandaliwa na Wizara ya Madini ambayo inatoa fursa kwa Tanzania kuzalisha mapato ya hadi Dola za Marekani bilioni 11 kwa mwaka huku ukitarajia  pia kuzalisha ajira hususan kwa vijana na wanawake.


Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde  aliushukuru ujumbe huo kwa mchango wao muhimu na kusisitiza kwamba taarifa hiyo iliyowasilishwa inakwenda sambamba na mkakati wa Serikali  ambao Wizara imeundaa kwa ajili ya kuwezesha  manufaa ya haraka  ya uongezaji thamani madini nchini.


Alisistiza kuhusu umuhimu wa kufanya utafiti wa kina wa madini ili kubaini kiwango cha madini muhimu na mkakati kilichopo nchini na kuongeza kwamba, shughuli za uongezaji thamani madini hayo kwa kiwango kikubwa kitategemea hali ya upatikanaji wa rasilimali hiyo.


Waziri pia alisisitiza haja ya kuwa na ushirikiano wa kitaifa, akitolea wito wa utekelezaji wa mpango wa Serikali kwa pamoja ili kufanikisha  kuzitumia fursa hizo, akirejelea ahadi ya Wizara yake kuongeza ushirikiano na taasisi na mashirika muhimu ya Serikali.


Mwisho, Waziri Mavunde alitoa shukrani kwa timu yake ya kiufundi ya Wizara kwa kwa karibu na kikamilifu katika utafiti huo na kubainisha dhamira yake ya kuendeleza ajenda ya kuongeza thamani ya madini nchini Tanzania.


*#InvestInTanzaniaMiningSector*


*#MadininiMaishanaUtajiri*

RAIS MWINYI:UCHUMI WA ZANZIBAR UMEKUA KWA ASILIMIA ZAIDI YA 7

 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema katika kipindi cha Miaka 4 Uchumi wa Zanzibar unaendelea kukua kwa kasi zaidi  ya asilimia 7 kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta mbalimbali.

Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipojumuika kwenye chakula cha jioni na Viongozi mbalimbali wa Wafanyabiashara wa Uingereza kilichoandaliwa na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) katika ukumbi wa Serikali ya Uingereza Jijini la London, tarehe 8 Aprili 2025.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amewakaribisha Wawekezaji kutoka Uingereza kuwekeza  Zanzibar katika fursa mbalimbali ikiwemo sekta ya Uchumi wa buluu, utalii,  usafiri wa baharini,  uvuvi , nishati na miundombinu ya kidijitali.

Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Uingereza wamehudhuria hafla hiyo akiwemo Alderman Professor Emma Edhen , Alderman City of London na Lord Malhard, House of Lords , na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Commonwealth, Lord Darroch wa House of Lords.

JELA MIAKA 60 KWA KUBAKA, KUMPA MIMBA MWANAFUNZI

 


Mwanza.Mkazi wa kijiji cha Kinamweli, wilaya ya Kwimba mkoa wa Mwanza, Iddy Renatus Makungu (30), amehukumiwa na mahakama ya wilaya hiyo kwenda jela miaka 60 kwa kosa la kubaka na kumsababishia ujauzito mwanafunzi (14).


Hukumu hiyo imesomwa leo tarehe 08.04.2025 na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Ndeko Dastan Ndeko ambapo amesema mshatakiwa huyo alitenda kosa kwa nyakati tofauti kati ya mwezi wa nne mwaka 2024 na mwezi wa tano mwaka 2024 huko katika kijiji cha Kinamweli wilaya ya Kwimba.


Kwa mujibu wa Hakimu Ndeko, mshtakiwa alitenda kosa hilo katika kesi ya jinai namba 31962 ya mwaka 2024 kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022. 


Mbele ya Hakimu Ndeko, Mwendesha mashtaka wa Serikali Juma Kiparo amesema kuwa Mshtakiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza Mahakamani hapo tarehe 11.11.2024 na kusomewa mashtaka ya kubaka na kumpa mimba binti huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, shule ya msingi Kinamweli, ambapo mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo yote mawili.


Upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano akiwemo mhanga na Mahakama kujiridhisha kwamba upande wa mashtaka umethibitisha makosa hayo pasi na kuacha Shaka dhidi ya mtuhumiwa.


Mshtakiwa katika utetezi wake alidai kwamba amesingiziwa makosa hayo kwani awali alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng'ombe kwa mjomba wa mhanga huyo.


" Mheshimiwa Hakimu., nimesingiziwa kesi baada ya kudai pesa zangu za mshahara nilizochunga  ng'ombe" alijitetea Makungu 


Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali utetezi huo kwa kukosa mashiko na kumhukumu mshtakiwa kwenda jela miaka 30 kwa kila kosa na kuelekeza kwamba adhabu hizo zitaenda kwa pamoja na hivyo mtuhumiwa atatumikia miaka 30.


*Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza*

Tuesday, April 8, 2025

JELA MIAKA 30 KWA KUBAKA KIZIWI

 



Mahakama ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza imemuhukumu Malimo Mathias Nguno kwa jina maarufu Gohe (41), kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumkuta na hatia ya kumbaka mtoto (13) mwenye ulemavu wa kusikia (kiziwi).

Hukumu hiyo imesomwa leo Aprili 08, 2025 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ndeko Dastan Ndeko.

Kwa mujibu wa hakimu Ndeko, mshtakiwa alitenda kosa hilo katika kesi hiyo ya jinai namba 2904/2025  kinyume na vifungu namba 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

“Baada ya kupitia vifungu vya sheria na kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ambao haukuaacha shaka lolote na hivyo mahakama hii imekukuta na hatia ya kumbaka kigori (13) ) (jina limehifadhiwa),” amesema Hakimu huyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshatakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 04.01.2025, katika Kijiji cha Nyambuyi kilichopo ndani ya wilaya ya Kwimba mkoa wa Mwanza kwa mwathiriwa ambaye ana ulemavu wa kusikia na kuongea maarufu kama Kiziwi.

Aidha, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kipalo, amesema mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza mbele ya Mahakama hiyo tarehe 04.02.2025 na kusomewa shtaka la kubaka ambapo mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo.

Upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano akiwemo mhanga chini ya usaidizi wa kutafsiri lugha za alama na ishara toka kwa mwalimu na mtaalam wa lugha za ishara.

Aidha, mshtakiwa baada ya kusomewa hukumu hiyo alitakwa na mahakama hiyo kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali, hali iliyopelekea mshatakiwa kuiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa umri wake ni mkubwa na kwamba kama atapewa adhabu kali ya miaka 30 atafia gerezani.

Hata hivyo, Hakimu Dastan Ndeko alitupilia mbali ombi hilo na kumhukumu kwenda jela miaka 30 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo.

MIRADI YA UTALII KULETA MAGEUZI



***********

Na Mwandishi wetu - Singida

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuimarisha Sekta ya Utalii, kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuchechemua ongezeko la watalii na kukuza pato la Taifa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Utalii (TDL).

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao kazi cha viongozi wa Taasisi za Wizara hiyo zinazotekeleza miradi kupitia mfuko huo, Mkoani Singida, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Abdullah Mvungi amesema kikao hicho kimelenga kupata uelewa wa pamoja wa uboreshaji wa mipango na mikakati ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati inayolenga kutoa matokeo chanya kwa jamii.

Bw. Mvungi amesema kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa vitendo kukuza utalii kupitia Mfuko huo hivyo ni vyema kwa Viongozi wa Taasisi zinazotekeleza miradi kupitia Mfuko huo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi itakayotekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.

Aidha, Bw. Mvungi ameongeza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo umelenga kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wale wa nje, kuongeza mapato ya fedha za ndani na za kigeni, kuongeza ajira pamoja na kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia Sekta ya Utalii.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. John Mapepele ameeleza kuwa Wizara itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya mafanikio yanayopatikana katika miradi.

Uongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi kuwapatia mafunzo wafanyakazi.


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema wakati umefika kwa Uongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi kuwapatia mafunzo wafanyakazi yatakayo wajengea uelewa wa kuzifahamu vizuri sheria za utumishi, haki, wajibu pamoja na kujua stahiki zao.


Ameyasema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa ZATUC uliofika Ofisini kwake Vuga kwa lengo la kujadili mambo mbali mbali yahusuyo Serikali na Vyama vya wafanya kazi.


Amesema umakini, usimamizi na utatuzi wa changamoto za wafanyakazi kwa Taasisi husika unahitajika ili kupunguza msururu wa malalamiko ambayo mengi yao yanakuwa tayari yameshasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikilipa kipaombele suala la stahiki zote muhimu za wafanyakazi kwa kusimamia, kufanya marekebisho na maboresho ya maslahi ya wafanyakazi wa Umma kama sheria za Utumishi Serikalini zinavyoelekeza.


Mhe. Hemed amevitaka vyama vya wafanyakazi kuwakumbusha wanachama wao suala la haki na wajibu wa mfanyakazi jambo ambalo litasaidia kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazowea na kutoa msukumko kwa kila mfanyakazi kuwajibika kwa nafasi yake kwa kuzingatia taratibu za kazi na miongozo ya utumishi serikalini.


Aidha Mhe.Hemed ameahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga Mkono jihudi zinazofanywa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi na kuwa tayari kukutana nao ili kujadili mambo mbali mbali ikiwemo malalamiko yanayohitaji marekebisho ya sheria katika utekelezaji wake ambayo yamekuwa yakichukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi kutokana na utatuzi wake unahitaji muda na umakini katika kufikia ufumbuzi wa malalamiko hayo.


Nae Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi(ZATUC) ndugu Khamis Mwinyi Mohd ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali zinazowakabili wafanyakazi na kuzipatia ufumbuzi jambo ambalo linazidi kuongeza ari na hamasa kwa wafanyakazi kufanya kazi zao kwa bìdii na uweledi mkubwa.


Katibu Khamis amesema ZATUC inekuwa na changamoto ya kukosa uhuru wa kujiunga pamoja jambo linalowakosesha fursa ya kufanya kazi zao pamoja na ushirikishwaji katiaka ngazi za maamuzi.

ULEGA: UJENZI WA DHARURA WA MADARAJA HAUTAATHIRI MIPANGO YA KUDUMU


........................

Serikali imefafanua kwamba kazi ya ujenzi wa madaraja matano kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam - Lindi zilikuwa zinaendelea na haitaathiriwa na juhudi za sasa za kukarabati maeneo yaliyoharibiwa na mafuriko ya mvua katika siku za karibuni. 

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, katika eneo la Somanga na Matandu mkoani Lindi ambapo anasimamia ukarabati wa dharura wa barabara iliyoharibiwa na mvua. 

Ulega alitumia fursa hiyo kutangaza pia kwamba serikali tayari imetenga fedha kwa ajili qpya ujenzi wa madaraja ya kudumu na ni kazi endelevu hadi itakapokamilika.

“Tutambue kuwa ujenzi wa madaraja sio suala la wakati mmoja ni la hatua kwa hatua. Niwatoe hofu Watanzania kwamba toka ilipotokea dharura mwaka jana ya kukatika maeneo hayo Serikali imechukua hatua madhubuti na kila mahali yupo Mkandarasi anafanya wajibu wake”, amesisitiza Ulega.

Aidha, Ulega amewahakikishia Watanzania kuwa huduma za usafiri na usafirishaji kwa mikoa ya kusini zimerejea  tangu alfajiri na zinaendelea kuimarika ambapo magari madogo, mabasi ya abiria na magari makubwa ya mizigo  yanaendelea kupita katika eneo la Somanga na Matandu ili wananchi waweze kuendelea na safari.

Hatahivyo, Ulega ametoa wito kwa wananchi waliosimama  kituo cha Mabasi yaendayo Mikoa ya Kusini cha Mbagala kutokana na hofu ya kushindwa kuvuka katika eneo la Somanga - Mtama kuendelea na safari kwani eneo hilo sasa ni salama  na linapitika.

Ulega amewashukuru wananchi wote waliokumbwa na changamoto hiyo kwa uvumilivu na subira pamoja na kuwapongeza Wakandarasi  na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kushiriki zoezi hilo usiku na mchana ili kuhakikisha mawasiliano yanarajea.